Facebook Comments Box

Monday, August 18, 2014

SHIBUDA AFICHUA SIRI ZA CHADEMA

SIKU moja baada ya Mbunge wa Maswa Magharibi, mkoani Simiyu,Bw. John Shibuda kutangaza kuachia ngazi ndani ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mbunge huyo ameibuka tena na kusema aliahidiwa kupewa helikopta mbili na uongozi wa chama hicho aweze kuzitumia katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010 lakini hakupewa.

Alisema uongozi wa chama hicho ukiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Wilbrod Slaa, ulimwahidi kumpa helikopta hizo kwenye kampeni zake na kumpigia debe Katibu huyo aliyekuwa akiwania nafasi ya urais.
Bw. Shibuda aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Malampaka, wilayani Maswa na kuongeza kuwa, alijitolea kutumia pesa zake katika uchaguzi huo na kuahidiwa kurudishiwa lakini mpaka sasa bado kurudishwa. "Katika kampeni za mwaka 2010, mbali ya kuahidiwa helikopta, pia nilikuwa chanzo kikubwa cha Dkt. Slaa kupata kura nyingi kwa mara ya kwanza na kuongoza kwenye Wilaya ya Maswa akimzidi mgombea mwenzake kutoka CCM, Rais Jakaya Kikwete. "Helikopta nilizoahidiwa, hata wakati wa kampeni sikupewa,
nilipouliza niliambiwa nitapewa...mimi ndiye chanzo kikubwa cha Rais Kikwete kupata kura ndogo katika jimbo langu, nilitumia gharama zangu kumfanyia kampeni Dkt. Slaa," alisema.
Wakati huo huo, Bw. Shibuda alisema msimamo wake ni Serikali mbili na kusisitiza hawezi kuwaunga mkono wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao msimamo wao ni Serikali tatu ambazo zitawaongezea mzigo wananchi wangu ambao ni wakulima na wafugaji.

Bw. Shibuda alisema wananchi wake hawataki kuongezewa mzigo wa Serikali; bali wanataka kutatuliwa kero walizonazo hasa zinazohusu kilimo cha pamba, migogoro ya wakulima na wafugaji. "Siko tayari kuunga mkono muundo wa Serikali tatu kwa sababu wakulima wa pamba wana matatizo makubwa katika bei ya zao hili
na pembejeo, pia katika wilaya yangu kuna migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji inayopaswa kutatuliwa kwa serikali hii
tuliyonayo," alisema Bw. Shibuda.
 
Katika mkutano huo, Bw. Shibuda alikwenda mbali zaidi akimfananisha Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mwanasheria wa chama hicho, Bw. Tundu Lissu na kundi la Interahamwe lililochochea ubaguzi wa kikabila uliosababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda akidai mbunge huyo amekuwa mchochezi wa vita ndani na nje ya chama.
"Tundu Lissu ni Interahamwe kwani amekuwa mtu mchochezi mwenye tabia ya kuwatukana wenzake, hana tofauti na kundi hili kama wenzake walivyosababisha mauaji nchini Rwanda," alisema.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU