MABINGWA wa
soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC wanatarajiwa kuondoka Desemba 28, mwaka
huu mjini Dar es Salaam, kwenda Uturuki kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa kwenda
kutetea taji lao hilo mjini Kigali, Rwanda.
Habari
kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba wiki hii mwalimu, Ernie Brandts ataamua
idadi na wachezaji wa kwenda ziara hiyo, ambayo ni maalum pia kujiandaa na
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Kocha huyo
Mholanzi, kwa wiki zaidi ya mbili amekuwa akikinoa kikosi chake kwenye Uwanja
wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam baada ya kumaliza likizo fupi ya baada ya
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Yanga, chini
ya Mwenyekiti wake, Alhaj Yussuf Manji imepania kurejesha utawala wake katika
soka ya Tanzania na kwa kuanzia inataka kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu kwa
kishindo mwishoni mwa msimu.
Yanga
inataka pia kutetea Kombe la Kagame Januari mwakani mjini Kigali, katika
michuano ambayo watakwenda na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
Yanga
ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa inaongoza kwa pointi zake 29, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 24, wakati Simba ni ya tatu kwa pointi
zake 23.