MWANAMUME mmoja katika
mtaa wa Mwanzo, Eldoret anauguza majeraha baada ya kupigwa na mkewe
kufuatia mzozo uliotokana na yeye kupatikana akitazama runinga kabla ya
kumaliza kazi ya nyumbani.
Kwa mujibu wa majirani mkewe mwanamume
huyo, alirejea nyumbani jioni kutoka kazini mnamo Jumatatu na kumkuta
akitazama televisheni. Mara moja, alimrukia na kumpiga vibaya.
Mwanaume
huyo aliokolewa na majirani waliofika kuitika kilio chake na kumkuta
akigaragara sebuleni kutokana na maumivu. Walimpeleka katika zahanati ya
kibinafsi alikotibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Majirani walisema wawili hao wamekuwa wakigombana mara kwa mara baada ya mwanamume huyo
kufutwa kazi miezi michache iliyopita.
Wakazi
wa Mwanzo sasa wanalitaka Shirika la Maendeleo ya Wanaume kuingilia
kati na kuokoa wanaume ambao wanadai wanadhulumiwa na kuchapwa na wake
zao kila siku. Wanasema visa hivyo vimeongezeka mtaani humo. Aidha,
wanataka wanaume hao wapewe ushauri wa kisheria kuwasaidia kutafuta
usaidizi.
Mmoja wa wakazi, Justus Mwaniki,
alisema wanaume wengi wanapigwa na wake zao kwa kuonekana kama mzigo
nyumbani hasa wanapokosa kazi: “Sisi huwatunza wake zetu, na kukidhi
mahitaji hao hata wakiwa hawana kazi na huleta nyumbani mapato yetu kwa
matumizi ya familia. Mbona wadhulumu wanaume ambao hawana kazi?”
alishangaa.
Majuzi, kiongozi wa Maendeleo
ya Wanaume Nderitu Njoka alijipata taabani baada ya kukaripiwa na
mwanamke mwenye nyumba kaunti ya Kiambu alipokuwa ameenda kumwoka
mwanamume aliyedai alikuwa akizuiliwa na kudhulumiwa nyumbani.