KIKAO cha kwanza cha Kamati mpya ya Utendaji ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) jana chini ya Rais, Jamal Emil Malinzi kimemuengua
Katibu Mkuu wa kuajiriwa, Angetile Osiah Malabeja.
Rais Malinzi, alifungua kikao kwa ajenda ya kumuengua Angetile na
Wajumbe wakaafiki, lakini wanamng’oa kistaarabu.
Angetile amepewa likizo ya hadi atakapomaliza Mkataba wake mwezi
ujao na kwa sasa, aliyekuwa Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface
Wambura Mgoyo atakatimu nafasi yake.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imemteua Bw. Boniface Wambura kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa TFF.
Uteuzi huo ni kuanzia Novemba 2 mwaka huu.
Aidha aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah ameagizwa aende
likizo ya malipo hadi atakapomaliza mkataba wake.
Kamati ya Utendaji inaviomba vilabu, vyama vya wilaya, vyama vya
mikoa, vyama shiriki na wadau wote kumpa ushirikiano Bw. Boniface
Wambura katika utekelezaji wa majukumu yake.
Jamal Malinzi
Rais, Dar es Salaam
Novemba 3, 2013
Sunday, November 3, 2013
ANGETILE OSIAH APEWA LIKIZO YA LAZIMA NA RAIS MPYA WA TFF MPAKA MWISHO WA MKATABA WAKE
ARSENAL YAIZABA LIVERPOOL KWA MABAO 2 KWA BILA NA KUJIKITA KILELENI
Timu ya Arsenal Imeibamiza Liverpool kwa jumla ya mabao 2 kwa bila katika Uwanja wa Emirates na kujikusanyia point zote tatu na kujikita kileleni na kuendelea kuongoza ligi hiyo ya Uingereza. Mabao yaliyoipa ushindi timu hiyo yaliwekwa kimiani na Santi Cazorla pamoja na Aaron Ramsey.
Arsenal walimiliki mpira mwanzo mpaka mwisho wa mchezo huo ambapo Washambuliaji wa Liverpool Luis Suarez na Dan Sturredge hawakufua dafu kwa mabeki wa watoto wa Jiji la London.
Vikosi vilikuwa kama ifuatavyo:
Arsenal:
Wojciech Szczęsny; Kieran Gibbs, Per Mertesacker, Laurent Koscielny, Bacary Sagna; Mikel Arteta, Aaron Ramsey; Santi Cazorla, Mesut Özil, Jack Wilshere; Olivier Giroud.
Liverpool:
Simon Mignolet; Mamadou Sakho, Martin Skrtel, Touré; Aly Cissokho, Steven Gerrard, Lucas Leiva, Jordan Henderson, Glen Johnson; Luis Suárez, Daniel Sturridge.
Par Metasacker akimuangalia Suarez pamoja na Sagna katika moja ya heka heka za mpambano huo.
Olivier Giroud akichanja mbuga huku Kolo Habib Toure akimfuata kwa karibu.
Ozil akimpongeza Aron Ramse kwa kuifungia Arsenal bao la Pili katika mchezo huo.
POS | LP | CLUB | P | W | D | L | GF | GA | GD | PTS | |
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
1 | (1) | Arsenal | 10 | 8 | 1 | 1 | 22 | 9 | 13 | 25 | |
2 | (2) | Chelsea | 10 | 6 | 2 | 2 | 16 | 8 | 8 | 20 | |
3 | (3) | Liverpool | 10 | 6 | 2 | 2 | 17 | 10 | 7 | 20 | |
4 | (7) | Manchester City | 10 | 6 | 1 | 3 | 28 | 11 | 17 | 19 | |
5 | (5) | Southampton | 10 | 5 | 4 | 1 | 11 | 4 | 7 | 19 | |
6 | (4) | Tottenham Hotspur | 9 | 6 | 1 | 2 | 9 | 5 | 4 | 19 | |
7 | (6) | Everton | 9 | 5 | 3 | 1 | 14 | 10 | 4 | 18 | |
8 | (8) | Manchester United | 10 | 5 | 2 | 3 | 17 | 13 | 4 | 17 | |
9 | (11) | Newcastle United | 10 | 4 | 2 | 4 | 14 | 16 | -2 | 14 | |
10 | (10) | Hull City | 10 | 4 | 2 | 4 | 8 | 10 | -2 | 14 | |
11 | (12) | West Bromwich Albion | 10 | 3 | 4 | 3 | 10 | 10 | 0 | 13 | |
12 | (9) | Swansea City | 9 | 3 | 2 | 4 | 12 | 11 | 1 | 11 | |
13 | (13) | Aston Villa | 10 | 3 | 2 | 5 | 9 | 12 | -3 | 11 | |
14 | (15) | West Ham United | 10 | 2 | 4 | 4 | 8 | 8 | 0 | 10 | |
15 | (14) | Fulham | 10 | 3 | 1 | 6 | 10 | 15 | -5 | 10 | |
16 | (17) | Stoke City | 10 | 2 | 3 | 5 | 7 | 11 | -4 | 9 | |
17 | (16) | Cardiff City | 9 | 2 | 3 | 4 | 8 | 13 | -5 | 9 | |
18 | (18) | Norwich City | 10 | 2 | 2 | 6 | 6 | 20 | -14 | 8 | |
19 | (19) | Sunderland | 10 | 1 | 1 | 8 | 7 | 22 | -15 | 4 | |
20 | (20) | Crystal Palace | 10 | 1 | 0 | 9 | 6 | 21 | -15 | 3 | |
POS | LP | CLUB | P | W | D | L | GF | GA | GD | PTS |
RAIS MPYA WA TFF JAMALI MALINZI AMEKABIDHIWA OFISI RASMI NA RAISI ALIYEMALIZA MUDA WAKE LEODGAR TENGA
Mheshimiwa Rais wa TFF,
Pongezi na Shukurani
1. Naomba nianze kwa kushukuru kwa
kukubali kufanyika kwa shughuli hii ya makabidhiano ya Ofisi. Utaratibu huu
haupo kikatiba wala katika kanuni zetu, lakini ni muhimu sana kwa vile unatoa
taswira ya uongozi endelevu na
ushirikiano unaostahili kuwepo baina ya uongozi mpya na ule wa zamani.
2. Aidha napenda, kwa mara nyingine,
kukupongeza kwa dhati wewe binafsi kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa
Shirikisho letu pamoja na kumpongeza Makamu wa Rais na Wajumbe wa Kamati ya
Utendaji kwa ushindi wao.
3. Tumeshuhudia mchakato wa uchaguzi
uliofanyika kwa uwazi, na ulio huru na wa haki. Ninawashuru sana na kuwapongeza
Wajumbe wa Kamati ya Uchanguzi kwa ueledi na kazi nzuri walioifanya. Kwa kiwango hicho hicho
ninawapongeza na kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wa
Kamati za Maadili – ngazi ya awali na ya rufani – kwa kutekeleza wajibu wao
kikamilifu na vyema.
4. Nawajibika kutoa pongezi kwa Wajumbe wa
Mkutano Mkuu kwa kukamilisha kazi muhimu ya kutuchagulia viongozi wetu kwa
utulivu mkubwa.
5. Utulivu wakati wa mchakato mzima wa
uchaguzi – kuanzia mwanzo hadi mwisho – ni kielelezo cha ukomavu wa uongozi wa
mchezo wa mpira wa miguu nchini. Natoa shukurani za dhati kwa wanachama na
wadau wote wa mpira wa miguu nchini kwa mchango wao wa hali na mali katika kufanikisha
zoezi hili muhimu kwa mustakabali wa mpira wa miguu nchini.
Dira
na Malengo ya Uongozi Uliopita
6. Dira ya uongozi uliopita ilikuwa ni
kujenga mazingira mazuri na endelevu ya maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu
nchini. Hii ilitokana na hali ya migogoro isiyoisha na malumbano ya mara kwa
mara yaliyokuwepo kabla ya kuingia madarakani.
7. Ili kufanikisha dira yetu, uongozi
uliopita ulidhamiria kujenga msingi bora wa uongozi wa mpira wa miguu nchini,
hivyo kujiwekea malengo yafuatayo:
· Kutengeneza Katiba mpya na Kanuni zitakazokidhi
mahitaji ya nchi yetu ya kudumisha demokrasia na utawala bora – uwazi,
uwajibikaji, na kadhalika.
· Kuhakikisha kuwa Katiba yetu na Kanuni zetu
zinazingatiwa na kuheshimiwa.
· Kuweka Kanuni za Fedha na kuchukua hatua za
kujenga uaminifu katika usimamizi wa ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya
fedha. Tuliazimia kuona hesabu za
Shirikisho zinakaguliwa na wakaguzi wenye sifa za kimataifa, na taarifa ya
ukaguzi kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu kila mwaka, bila ya kukosa.
· Kuwa na mfumo wa mashindano utakaongeza
ushindani na kuchochea uwekezaji. Azma ilikuwa ni kuongeza idadi ya mashindano
ili kutoa fursa kwa vipaji kuonekana na kuendelezwa.
· Kuweka jitihada katika mafunzo ya wataalamu wa
mpira wa miguu nchini kwa kuongeza idadi na kozi/semina za mafunzo ya uongozi,
uamuzi, ualimu na udaktari wa michezo.
· Kujenga mfumo mpya wa uongozi wa timu za taifa.
Lengo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa timu za taifa zinakuwa na uongozi wake chini
ya Mwalimu/Walimu wa timu ya taifa na kuzitofautisha na Idara ya Ufundi, pamoja
na kuhakikisha timu zetu za taifa zinashiriki michezo mingi iwezekanavyo ya
mashindano na ya kirafiki.
· Kujenga uhusiano mzuri na wadau na washirika
wetu, hususan wadau wetu wakuu ambao ni Serikali na vyombo zake; Mashirikisho
ya mpira tuliyojumuika nayo - FIFA, CAF, na CECAFA; Wadhimini na Wafadhili wetu
– kampuni, mashirikia ya umma na watu binafsi - wanaochangia maendeleo ya mpira
wa miguu nchini kwa hali na mali.
· Kuwa karibu na jamii na kuisaidia jamii. Nia ni
kutumia umaarufu wa mchezo wa mpira wa miguu nchini kuhamasisha maendeleo ya
jamii, hasa katika masuala ya afya ya jamii – kampeni ya malaria, ukimwi,
kupambana na madawa ya kulevya na kadhalika. Rais anayeondoka madarakani ni
Balozi wa Malaria nchini na Rais wetu mpya ni mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya
Kupambana na Malaria, chini ya Uenyekiti wa Waziri wetu wa Afya, Mheshimiwa Hussein
Mwinyi.
8. Utekelezaji wa Dira tuliyojiwekea na
malengo yetu ulifanyika kwa ushirikiano wa karibu na wanachama na wadau wetu. Yaliyofanyika
yanajulikana. Itoshe kusema kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa jitihada kubwa na
uadilifu mkubwa na kwamba malengo tuliyojiwekea yalifikiwa.
9. Katika hotuba niliyoitoa katika
Ufunguzi wa Mkutano Mkuu uliopita – Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2013, niliainisha
kwa kina nini kilifanyika katika kipindi cha uongozi uliopita pamoja na
mafanikio ya kazi iliyofanyika. Napenda kuimbatanisha hotuba hiyo kama sehemu
ya taarifa hii ya makabidhiano.
10. Matarajio yetu ni kuwa, baada ya jitihada
za kuweka msingi wa uongozi na wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini, nguvu itaelekezwa
katika kukuza kiwango cha mpira wa miguu nchini mwetu. Tulichokifanya ni
kutayarisha Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo ya Mpira Miguu Nchini – 2013
hadi 2016 (Long Term Technical Development Plan – 2013 to 2016), ambayo
umeambatanishwa kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.
11. Hivyo basi, uongozi mpya una kazi ya
kusimamia na kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo. Pia, ni matarajio yetu kuwa
uongozi mpya utayadumisha mambo ya msingi tuliyojiwekea na kuufanyia kazi
upungufu uliopo.
Shukurani
kwa Wanachama na Wadau wa TFF
12. Pamoja na kuwa nimeshatoa shukurani mara
kadhaa, napenda kwa mara nyingine tena kuwashukuru wote waliotusaidia kufika
hapa tulipo. Nawashukuru sana wanachama wetu, wadau wetu wote – Serikali yetu
na vyombo vyake vyote, wadhamini na wafadhili, waandishi na vyombo vya habari, wapenzi
wa mpira na wananchi kwa ujumla kwa mchango wao wa hali na mali. Bila yao
tusingefika hapa tulipofika.
13. Shukurani maalum zimwendee Mheshimiwa Rais
wetu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa mchango wake usiopimika. Alikuwa ni sehemu
mabadiliko haya tangu mwanzo, hata kabla ya uongozi wetu kuingia
madarakani. Ametusaidia kwa kiasi
kikubwa kuzijenga timu zetu za taifa siyo tu kwa uamuzi wake wa kulipia
mishahara ya walimu wa timu ya taifa, bali pia kwa kuwahamasisha vijana wetu
kwa hali na mali wafanye vizuri.
Sina hakika kuwa yupo Rais mwingine, popote
pale duniani, aliye karibu na mapenzi ya dhati kwa vijana wa timu zake za taifa
zaidi ya Rais wetu. Zaidi ya hayo, Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele
katika kuhamasisha utawala bora katika mpira wa miguu nchini na amefanya kila
aliloliweza kuona kuwa kiwango cha mchezo kinapanda na timu zetu zinafanya
vizuri. Napenda kutoa shukurani za dhati kwake kwa uongozi na msaada wake.
Wanachama,
Katiba na Kanuni, Wafanyakazi, Mali na Mikataba ya TFF
14. Wanachama
TFF ina jumla ya Wanachama 44 ambao
wote ni wanachama hai kama ifuatavyo:
·
Vyama vya Mikoa –
25
·
Vyama Shiriki
- 5
·
Vilabu vya Ligi Kuu - 14
15. Katiba na Kanuni
Hivi sasa TFF ina Katiba Mpya (ya
Mwaka 2013) iliyofanyiwa marekebisho ya mwisho na Mkutano Mkuu Maalum wa TFF tarehe
13 Julai 2013.
Pamoja na Katiba TFF ina kanuni
zifuatazo ambazo kwa mujibu wa Katiba ya TFF hupitishwa na kamati ya Utendaji:
· Kanuni za Fedha
· Kanuni za Mashindano kuanzia Ngazi ya Wilaya
hadi Ligi Kuu
· Kanuni za Utii
· Kanuni za Nidhamu
· Kanuni za Maadili
· Kanuni za Uchaguzi za Uchaguzi za TFF na za
Wanachama wa TFF
· Kanuni zinazosimamia Uendeshwaji wa Bodi ya Ligi
Kuu
· Kanuni za Mashindano mengine, kama vile Copa Coca
Cola, Uhai Cup, Super 8 na Taifa Cup. Ni vyema ikafahamika kuwa kila mashindano
lazima yawe na Kanuni zinazosimamia uendeshwaji wake.
TFF inalazimika kuzifanyia marekebisho
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wake kufuatia marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi
za TFF. Aidha, TFF inadeni la kutayarisha Kanuni za Chombo cha Usuluhishi
(Arbitration Tribunal) kama ilivyoainishwa katika Katiba. Hivi karibuni, TFF
imepokea Kanuni za Mfano kutoka FIFA ambayo ipo haja ya kazi hii kukamilishwa
na uongozi mpya.
16. Wafanyakazi wa TFF
Hivi sasa TFF ina jumla ya
wafanyakazi 29. Kati yao yupo/wapo:-
· Katibu Mkuu - 1
· Wakurugenzi / Maofisa Mwandamizi - 5
· Wafanyakazi wengine -
23
Katibu Mkuu na Wakurugenzi wapo
katika kipindi cha nyongeza cha miezi sita (6) cha mikataba yao, kinachoishia mwishoni
mwa mwezi Desemba 2013. Wafanyakazi wengine wapo katika mikataba ya
miaka minne yenye kipindi cha majaribio cha miezi sita kuanzia mwanzoni mwa
mwezi Septemba 2013. Hivyo basi, uongozi mpya una nafasi ya kufanya tathmini ya
mahitaji ya TFF kisha kufanya uamuzi juu ya ajira za Wafanyakazi waliopo kadiri
utakavyoona inafaa.
TFF ilichukua hatua ya kuingia kufanya
makubaliano ya hiari na wafanyakazi wake ili kuondokana na ajira za maisha (Permanent
Employment) na kubaki na ajira za mikataba (Contract Empoyment) kwa wafanyakazi
wake wote.
Wafanyakazi wa TFF wamekuwa
wakifanya kazi ngumu na saa nyingi kuliko kawaida. Ajira ya TFF haina saa za
ziada wala siku za mapumziko. Kutokana na dhana ya kujitolea na ukweli kwamba
shughuli nyingi za TFF, kama vile michezo na mikutano hufanyika siku za mwisho
wa wiki na sikukuu, ni dhahiri kuwa Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakilazimika
kufanya kazi siku hizo, na mara nyingi bila malipo ya saa za ziada. Aidha,
kutokana na kukosa uwezo, uongozi uliopita ulishindwa kupandisha mishahara yao
ipasavyo.
Napenda kuchukua nafasi hii
kuwapongeza na kuwashukuru kwa kuihudumia TFF na mpira wa miguu katika
mazingira magumu sana. Tunauomba uongozi mpya uliangalie suala hili kwa umakini,
kama moja ya hatua za kuongeza ufanisi wa Sekretariati.
17. Mali za
TFF
Hivi sasa
TFF ina mali zifuatazo:
· Kiwanja cha Karume Stadium, chenye hati namba 27026
iliyotolewa tarehe 10 Novemba 1981. Kiwanja cha Karume kina ukubwa wa ekari
8.26. Ombi la kuingezea muda hati hiyo limeshapelekwa na linafuatiliwa.
· Ndani ya Kiwanja hicho, kuna Jengo la ofisi ya
TFF, Jengo la Kituo cha Ufundi (Technical Centre) na Uwanja wa nyasi za bandia
wa Karume.
· Kiwanja cha Tanga chenye ukubwa wa hekta 7.6 (ekari
19) kilichopo katika eneo zuri sana mjini Tanga. Kiwanja hiki tayari
kimeshalipiwa na hivi sasa taratibu zinaendelea kukamilisha taratibu za
kukiandikisha na kupata hati.
· Magari sita (6) na Trekta moja (la kusafishia
uwanja wa nyasi bandia). Magari hayo ni: Bus kubwa aina ya Yutong, basi dogo
aina ya Coaster, magari ya aina 4WD Ford Everest, Rav 4, Suzuki Escudo na Honda
CVR. Mawili kati magari hayo - Suzuki Escudo na Honda CVR – yanatumika lakini hayapo katika hali nzuri. Ni
vyema uongozi mpya ukayafanyia tathmini magari hayo na kufanya maamuzi muafaka
kadiri utakavyoona inafaa.
· Fedha taslimu Shilingi 33,518,000 na US$ 1,390
zipo katika akaunti hivi sasa. Hii ni baada ya TFF kufanya malipo ya Shilingi
158,000,000 kwa ajili ya Mkutano Mkuu (uliofanyika wiki iliyopita) na malipo ya
Shilingi 56,240,000 yaliyofanyika kwa ajili matayarisho ya Timu ya Taifa ya Wanawake
U-20 na gharama za mchezo baina ya timu yetu ya Taifa na ile ya Msumbiji uliofanyika
wiki iliyopita. Hata hivyo, leo hii US$
415,000 (Shilingi 664,000,000) kimehamishwa kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda
kwenye Akaunti za TFF. Fedha hizo zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF ifikapo
Jumanne wiki ijayo. Malipo haya yalikuwa
yafanyike karibu miezi miwili iliyopita lakini yalicheleweshwa ili kutoa nafasi
kwa zoezi la ukaguzi wa fedha za udhamini wa TBL kufanyika. Zoezi limefanyika
vyema na kufikia ukingoni, ndiyo maana malipo yamefanyika. Malipo mengine
yanayofanana na hayo, ya US$ 420,000 (Shilingi 672,000,000) yanatarajiwa
kufanyika wiki mbili kutoka sasa - katikati ya mwezi huu wa Novemba 2013.
Hivyo
basi, uongozi unaoingia madarakani hautaanza kwa shida. Ni matarajio yetu kuwa
hatua ya awali itakuwa kurejesha fedha kwenye akaunti zilikoazimwa kinachofikia
US$ 166,509 - US$ 148,174 kutoka kwenya Akaunti za FAP na US$ 18,335 kutoka
kwenye Akaunti ya TRA - kwa ajili ya kugharimia Mkutano Mkuu na matumizi ya
Taifa Stars kwa ajili ya matayarisho na safari ya kwenda Gambia.
Ili kujiridhisha kuwa fedha za
udhamini zinatumika kama ilivyokubalika katika mikataba, TFF imetoa nafasi kwa
wadhamini kufanya ukaguzi wa fedha inazozitoa wakati wowote ule. Utamaduni huu
tumekuwa nao katika kipindi chote cha utawala wa uongozi wetu, ili kutoa imani
kwa wadhamini na kuhakikisha kuwa malengo ya udhamini husika yanafanikiwa. Huu
ni utaratibu mzuri na ni matumaini yetu kuwa utadumishwa.
Jengo la Kituo cha Ufundi ndiyo kwa
limekamilika kukarabatiwa na bado halijafunguliwa rasmi. Ukarabati huo
umefanikisha kutengenezwa kwa mfumo wa maji machafu unaojitegemea. Hivyo,
kutohitaji kutengemea mashimo ya Jengo la Ofisi za TFF. Hatuo ya mwisho ya kazi
hiyo ni kukamilisha ukaguzi wa matumizi yaliyofanyika katika ukarabati huo na
kuiwasilisha CAF mapema iwezekanavyo.
Hayo ndiyo makubaliana kuhusiana na msaada uliotolewa na CAF – unaojulikana kama
CAF FAP 2.
Ukarabati wa Kituo cha Ufundi
umefanywa, pamoja na sababu nyingine, ili kutoa fursa kwa Mradi wa Ujenzi wa
Karume kuendelea. Kama nilivyoeleza katika Mkutano Mkuu, dhamira ni kuwekeza
katika Mradi wa Ujenzi wa jengo / majengo yenye hadhi kubwa kwa ajili ya
kukodishwa kuzunguka uwanja huo. Jengo lililo karabatiwa na uwanja wa mpira
vitabaki na kuendelea kutumiwa kama Kituo cha Mafunzo. Jambo la muhimu ni kuhakikisha
kuwa uwekezaji katika mradi huo hauhitaji dhamana ya uwanja wetu na majengo
yetu. Ni imani yetu kuwa njia muafaka inapatikana, ikiwa ni pamoja na utaratibu
wa ‘Build, Operate and Transfer’ (BOT).
18. Hesabu za
TFF
Ripoti ya Ukaguzi wa hesabu za TFF hadi
kufikia Desemba 2012 iliwasilishwa katika Mkutano Mkuu uliopita. TFF ilipata
Hati Safi ya Ukaguzi wa hesabu zake na Mkutano Mkuu ukaikubali na kuipitisha
ripoti hiyo hesabu za mwaka 2012. Aidha, taarifa ya hesabu za TFF kwa kipindi cha
kuanzia tarehe 1 Januari hadi 30 Septemba 2013 kusambazwa kwa Wajumbe wa
Mkutano Mkuu.
Ifahamike kuwa TFF imekuwa ikipata
Hati Safi, kila mwaka katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Hatuna shaka
kuwa hali hii itaendelea.
19. Mikataba
ya Udhamini
TFF inayo
mikataba ifuatayo ya udhamini na Wadhamini wafuatayo:
· Vodacom – Udhamini wa Ligi Kuu
· TBL – Taifa Stars
· Coca Cola – Mashindano ya Copa Coca Cola
· SSB & Co – Mashindano ya Uhai
· Bank ABC – Super 8
· Azam Media – Haki za Matangazo ya Television kwa
Ligi Kuu
Aidha, baadhi ya vilabu kama vile
Yanga na Simba vinadhaminiwa na TBL,
Coastal Union inafadhiliwa na Tanga Cement na Azam FC inadhaminiwa na
Azam Cola.
Changamoto zinazoikabili TFF
20. Zipo changamoto nyingi zinazoikabili TFF lakini
kubwa kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu na ambazo uongozi mpya hauna
budi kuzishughulikia ni ulazima wa:
· Kuendeleza sola la vijana na watoto kwa kutoa
fursa kwa watoto/vijana wengi kupata malezi mazuri ya uchezaji wa mpira wa
miguu ili kupanua wigo wa kupata wachezaji wenye vipaji. Katika jambo hili bado
tuko nyuma sana. Tulididimia sana kutokana na kufutwa kwa michezo mashuleni.
Ipo haja ya uongozi mpya kushirikiana na Serikali kuhamisha michezo shuleni,
kama hatua ya wali ya kutatua tatizo la soka la vijana/watoto.
· Kuendeleza soka la wanawake. Matatizo ya soka la
wanawake yanafanana na ya soka la vijana. Tofauti ni ndogo sana. Kama ilivyo
kwa soka la vijana, hatua muhimu kufanyika kwa jitihada ya kuwahamasisha
wasichana wacheze mpira wa miguu shuleni.
· Kuhakikisha ueledi unazingatiwa katika uongozi
wa Vilabu na Vyama Wanachama wa TFF. Kinyume chake hatutaweza kushindana na
wenzetu ambao walishapiga hatua katika taaluma ya uongozi wa michezo. Vilabu vyetu ni lazima vihakikishe kuwa
vinatimiza masharti ya ‘Club Licencing’ kama yalivyotolewa na CAF, pamoja na
marekebisho yake. Huu ni mtihani kwetu. Ni lazima tufaulu kutimiza masharti
hayo, vinginevyo tutabaki nyuma. Ipo haja ya kuuangalia kwa mfumo wa uongozi wa
Vilabu vyetu na Vyama Vyetu kwa azma ya kubuni mfumo utakaotuletea ufanisi
zaidi wa kiungozi na uendeshaji kuliko ilivyo hivi sasa.
·
Kuhamasisha uwekezaji katika maendeleo ya mchezo
wa mpira wa miguu nchini. Tuna upungufu
mkubwa wa vifaa na viwanja vya kuchezea. Ni vigumu kuundeleza mchezo wa mpira
bila ya kuwa na viwanja vya kuchezea na vifaa. Aidha, zinahitajika raslimali
watu na fedha katika kulea na kuwaendeleza wachezaji na wataalamu wetu. Licha
ya hapo kiasi kikubwa cha fedha kinahitajika kwa ajili ya matumizi mengine ili
timu ifanye vizuri. Kwa maneno mengine tunahitaji kufanya kila jitihada
kuhamasisha watu binafsi, makampuni na Serikali iwekeze katika mpira, wadhamini
zaidi wajitokeze na wapenzi wengi zaidi wachangie timu zao – kwa njia
mbalimbali - ili kuongeza mapato ya vilabu na vyama husika. Vilabu vyetu na
Vyama Wanachama wa TFF vinakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za
uendeshaji. Mawazo au fikra kuwa kuna fedha
nyingi katika mpira wa miguu ni dhana isiyo na msingi na inayotokana na
kutofahamu gharama za uendeshaji wa vilabu na vyama vyetu. Pamoja na ongezeko
kubwa la mapato ya milangoni na mchango wa udhamini katika kipindi cha uongozi
uliopita, bado kinachopatikana hakikidhi hata theluthi moja ya mahitaji muhimu.
Haja ya kuongeza mapato ndiyo changamoto mama. Ikitatuliwa itasaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza makali ya changamoto nyingine.
· Ili kuvutia uwekezaji, udhamini na misaada
kwenye mpira wa miguu, ni lazima tuhakikishe kuwa tunaendelea na jitihada za
kujenga uaminifu wa utunzaji na matumizi ya fedha ndani ya TFF. Ipo haja ya
kuhakikisha kuwa Kanuni za Fedha zinazingatiwa na hesabu zetu zinakaguliwa mara
kwa mara. Mpango wa Tiketi za Elektroniki ni muhimu usimamiwe kwa nguvu zote
kwa vile sio tu utatuongezea mapato bali pia utatoa picha ya uaminifu na
ueledi.
Uhusiano na ZFA:
21. TFF haina budi kufanya kila
linalowezekana kudumisha uhusino mzuri baina yake na ZFA. TFF inatambulika na
FIFA kama msimamizi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini Tanzania. Lakini ukweli
ni kuwa mchezo wa mpira katika visiwa vya Unguja na Pemba unasimamiwa na ZFA.
Hakuna matarajio ya hali hiyo kubadilika. Kwa sababu hiyo, upo ulazima wa
kudumisha uhusiano uliopo na kuhakikisha kuwa ZFA inapata haki ya kupewa baadhi
ya miradi inayotokana na fedha za FIFA – FAP. Kwa vile fedha hizo hatolewa kwa
njia ya miradi, utaratibu tuliokubaliana ni kuhakikisha kuwa kila mwaka baadhi
ya miradi / semina zinafanyika visiwani.
Wakaguzi wa Hesabu za TFF
22. Hesabu za TFF zinakaguliwa makampuni ya
Ukaguzi wa Hesabu yafuatayo:-
·
TAC Associates – kwa hesabu zote za TFF
·
KPMG –
kwa fedha za FIFA
Bodi ya Wadhamini
23. Mkutano Mkuu wa Mwaka 2011 uliridhia
kuundwa kwa Bodi ya Wadhamini wa TFF na Mkutano Mkuu uliopita ulipitisha majina
ya Wajumbe wa Bodi ya Udhamini kama ifuatavyo:-
·
Said El Maamry –
Mwenyekiti
·
Mh. Joel
Bendera – Makamu
Mwenyekiti
·
Dr. Ramadhani Dau – Mjumbe
·
Steven Mashishanga – Mjumbe
·
Mohamed Abdulaziz - Mjumbe
Mheshimiwa Rais, napenda kukubidhi taarifa hii ya
makabidhiano leo hii tarehe 2 Novemba 2013 kwa ufahamu na kumbukumbu za TFF.
Tafadhali jisikie huru kuomba ufafanuzi wa jambo lolote lililomo katika taarifa
hii au kuomba taarifa juu ya jambo ambalo kwa bahati mbaya limesahauliwa. Sekretariati ya TFF inawajibika kutoa
ufafanuzi unaohitajika.
Tunakutakia wewe mwenyewe na uongozi wako kila la heri na
mafanikio katika kuingoza wa TFF kuelekea kule kunakotarajiwa na wapenzi wa
mpira wa miguu nchini. Wadau na wapenzi wote wa mpira wa miguu wanaoitakia heri
nchi yetu wapo nyuma yako.
Leodegar Tenga Angetile
Osiah
RAIS WA TFF KATIBU
MKUU WA TFF
TANZANIA FOOTBALL FEDERATION
HOTUBA YA RAIS WA
TFF KWENYE HAFLA YA MAKABIDHIANO
TAREHE 02 NOVEMBA
2013
Ndugu mgeni rasmi ……..…………………………………………….
Ndugu…………………………………. Mwakilishi
wa Wizara
Ndugu…………………………………. Mwakilishi
wa BMT
Ndugu…………………………………. Mwakilishi
wa wadhamini
Ndugu Leodegar Tenga
Rais aliyemaliza muda wake
Ndugu Said El Maamry Mwenyekiti mstaafu wa iliyokuwa FAT
Ndugu Muhidin Ndolanga Mwenyekiti
mstaafu wa
iliyokuwa
FAT
Wajumbe wa Baraza la Wadhamini
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji
Wafanyakazi wa TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kutuwezesha kuwa hapa leo.
Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kukupongeza Rais wetu uliyemaliza muda wako Ndugu Leodegar
Tenga na Kamati yako ya utendaji . Mliyoufanyia mpira wa Tanzania ni makubwa, historia
haitawasahau. Mmetujengea taasisi imara isiyotetereka, taasisi inayoheshimika
ndani na nje ya mipaka ya nchi hii, nawashukuru na kuwapongeza sana.
Uchaguzi umekwisha. Mchakato ulikuwa mrefu. Wapo walioshinda
na wapo ambao kura zao hazikutosha. Wote tuna kazi moja tu kujenga mpira. Kama
tulikwaruzana kwenye kampeni tusameheane, tuwe kitu kimoja, tuinyanyue soka yetu.
Makundi hayajengi yanabomoa, tuachane nayo.
Ndugu zangu, uongozi wetu ulioingia madarakani alfajiri ya
tarehe 28-11-2013 unakabiliwa na changamoto nyingi. Nitaelezea changamoto
chache zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
1.
Mashindano yanayotukabili.
Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali
ya kimataifa. Mfano ni mechi ya marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya Msumbiji
wiki ijayo, Mitoano ya mashindano ya Afrika wanawake mapema mwakani, Mashindano
ya Chalenji Novemba mwaka huu, na mashindano ya kufuzu AFCON 2015. Yote haya
yanahitaji maandalizi ya haraka.
2.
Programu ya vijana.
Ilani yangu ya uchaguzi ilielezea
azma ya Tanzania kuomba uenyeji wa fainali za vijana za Afrika U/17 mwaka 2019.
Jambo hili tutalizungumzia kwenye kikao chetu cha utendaji leo. Ili tuwe na
timu nzuri ya kucheza fainali hizo tukiwa wenyeji hatuna budi mwaka kesho
kuunda timu ya Taifa ya U/12 itakayokua pamoja kuelekea 2019. Programu yetu ya
vijana tutakayoiandaa sharti ijielekeze
kwenye ratiba hii.
3.
Udhamini wa timu za vijana na za
wanawake
Hii ni changamoto kubwa sana kwa TFF.
Timu zetu za Taifa kuanzia zile za wakubwa hadi za vijana ni brands, na kama ni
brands inabidi ziingizwe sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe wadhamini wa
hizo timu. Kitengo cha masoko lazima kiimarishwe ili kukabiliana na changamoto
hizi. Mdhamini ni mfanyabiashara, anapotoa pesa kudhamini brand fulani anategemea
matokeo mazuri kwake kwa njia ya kukuza biashara zake. Twende kwa wadhamini
tuwashawishi waone watafaidikia nini (leverage) kwa kudhamini timu zetu.
Tusisubiri waje tuwafuate sisi.
4.
Uwekezaji
Jitihada za haraka lazima zifanyike
kuiongezea TFF uwezo wa kiuchumi. Ni muhimu mtaalam mshauri (consultant)
atafutwe atufanyie mchanganuo wa uwekezaji katika ardhi yetu hii ya Karume ili
tuwekeze kitega uchumi kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano mkuu. Aidha bidhaa
zenye nembo yetu zianze kuuzwa kwa utaratibu maalum ili shirikisho lipate haki
yake.
Kabla sijamaliza kuzungumza, niongelee
suala la fujo viwanjani. Mpira ni dakika tisini. Katika kipindi hicho uamuzi wa
mwamuzi unakuwa ni wa mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu kwa kujificha
nyuma ya kivuli cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya makosa yawe ya
makusudi au ya bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo, mahakama ya waamuzi sio
mashabiki. Kitendo cha mashabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya mechi
ya mpira kamwe hakikubaliki mahali popote duniani.
Kanuni za FIFA, CAF na TFF ziko wazi na
adhabu zinajulikana. Moja ya adhabu hizi ni timu husika kucheza kwenye uwanja
mtupu usio na mashabiki kama ilivyowatokea Al Ahly na Zamalek huko Misri au
kucheza nje ya uwanja wako kama ilivyowatokea Senegal ambao baada ya vurugu
Dakar, Senegal waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani wachezee nje ya nchi na
wakachagua kuchezea Morocco.
Ndugu zangu yaliyotokea majuzi Mbeya
na Dar es salaam wote tumeyasikia na wengine miongoni mwetu hapa ni mashuhuda. Ninasema
iwe mara ya kwanza na y a mwisho. Kwenye masuala ya kutekeleza mahitaji ya
kanuni uongozi wangu hautaionea haya klabu yoyote, iwe mpya au kongwe kwenye
ligi yetu. Ni jukumu la viongozi wa klabu kudhibiti wanachama na wapenzi wao.
Tabia ya benchi la ufundi kutoa matamshi yanayoweza kuamsha hisia za mashabiki
ni kinyume na taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu jambo hili. Viongozi wa klabu
na mabenchi yao ya ufundi wakishindwa kutekeleza wajibu wao tusilaumiane.
Ndugu zangu ya kufanya ni mengi
katika kuiendeleza soka yetu. Tunashukuru Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na
changamoto hizi tunao na tuna ari na nia ya kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo ya mpira. Ombi langu kwenu nyote ninaomba ushirikiano wa wadau wote
kuanzia Serikali, Halmashauri, mashirika ya umma na binafsi na NGO’s, nina
imani tukishikamana tutaifikia ndoto yetu ya kuing’arisha Tanzania kimpira
kwenye anga za dunia.
Ahsanteni nawashukuru sana.
Subscribe to:
Posts (Atom)