Mchungaji Christopher Mtikila akifurahia ushindi baada ya kushinda kesi dhidi yake.
MWENYEKITI wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameshinda kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili.
Akizungumza
baada ya kushinda kesi hiyo, Mtikila amesema, "Ushindi huu niliutarajia
maana hata asubuhi kabla ya kuja mahakamani niliongea na Yesu na sasa
amenijibu".
Mara baada ya kushinda kesi hiyo lilizuka timbwili
lingine baada ya mtu mmoja kujitokeza akiwa na RB (Report Book)
akimtuhumu Mchungaji Mtikila kuwa alimtishia kumuua na ni mwizi wa
viwanja. Baada ya kutaka kukamatwa na polisi mmoja aliyekuwa na cheo cha
Koplo, Mchungaji alikataa kwa madai kuwa yeye ni kiongozi wa kitaifa
hivyo hawezi kukamatwa na polisi mwenye cheo cha Koplo, labda polisi
mwenye cheo cha SSP (Senior Superintendent of Police). Kwa kauli hiyo
polisi alishindwa kumtia nguvuni.
Mtikila
amkimsikiliza Koplo wa Polisi mwenye RB Namba : KMR/RB/10482 yenye
maelezo ya kutishia kuuwa kwa maneno na wizi wa viwanja iliyofunguliwa
na bwana Gotta Ndungulu.
*
"Hukumu dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher
Mtikila, iliyoahirishwa mara mbili kwa sababu ya hakimu kuwa na dharura,
ilisomwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu a Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Illivin Mugeta aliyeisikiliza kesi hiyo ya kutoa maneno ya
uchochezi.
Mtikila alikuwa akikabiliwa
na mashitaka ya kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya
Kikwete, kwamba anataka kuuangamiza Ukristo.
Mshitakiwa
Mtikila alifunga ushahidi kwa kuwa na mashahidi wawili wa utetezi,
akihofia kupoteza fedha za Serikali kwa kuwaleta mashahidi wengi ambao
hawana kitu tofauti na mashahidi wengine waliokuwa wamewasilisha
ushahidi wao mahakamani hapo.
Mtikila,
anadaiwa kwamba, Aprili, 2010 Dar es Salaam, alisambaza waraka aliokuwa
akidai ni wa kuunusuru Ukristo wenye lengo la kuangamizwa na Jihad ya
Rais Jakaya Kikwete na kwamba Wakristo wajitoe mhanga kukomesha ugaidi,
“Kikwete anaangamiza Ukristo, amekuwa jasiri wa kuingiza Uislamu katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alidai Mtikila katika waraka
wake huo.
Alidai waraka uliosambazwa
alisaini akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kuunusuru Ukristo na
walichapisha nakala 100,000, lakini aligoma kutaja mahali
walipochapishia nakala hizo. Maelezo yote hayo yalitolewa mahakamani
kama kielelezo na ofisa wa polisi, SSP, Ibeleze Mrema aliyemuhoji
Mtikila Aprili 14, 2010."