Facebook Comments Box

Thursday, October 25, 2012

TIMU YA PRISON YA MBEYA YAPATA AJALI

Timu ya prison ya Mbeya imepata ajali eneo la Hare mkoani Tanga,wachezaji Issa Mwantika,Lugano Mwangama,Khalidi Fungabreki,Daudi Masungwe wamepoteza fahamu na kukimbizwa hospitali ya Tanga, Kiungo wa Prisons Diego Magai akiongea na blog hii kutoka eneo la tukio amesema chanzo cha ajali iyo ni baada gari aina ya COaSter kuacha njia na kupinduka baada kupigwa na mwanga mkali wa taa za gari walilokua wanapishana nalo usiku huu,hadi saa tano na dk hamsini usiku huu majeruhi walikuwa wakikimbizwa hospitali teule ya Muheza.

POLISI WADAIWA KUTOROSHA MTUHUMIWA

MKAZI mmoja wa Kijiji cha Kogaja kata ya Goribe wilayani Rorya mkoani Mara Bw. Hamisi Omenda (33) amedaiwa kumuua kikatili mke wake Bi. Levina Hamisi (27) kwa kumkatakata kwa panga na kisha kutoroka, huku Polisi wakidaiwa kushiriki katika utoro huo kwa kuandaa mazingira ya kutoroka. Polisi wa kituo cha Kogaja wanadaiwa kuhusika na utoro huo kwa kile kilichodaiwa kuwa hawakumkamata mtuhumiwa licha kufika kituoni hapo kuchukua PF3 baada ya kufanya kitendo hicho. Hata hivyo, taarifa kutoka Kituo cha Polisi Kogaja zimedai kuwa Mtuhumiwa alitoa maelezo kuwa mkewe alikatwakatwa mapanga na watu wasiofahamika hivyo aliomba PF3 kwa ajili ya kumpeleka marehemu katika Hospitali ya Tarime mjini Tarime. Utetezi huo unadaiwa kuwa ni njama ya Polisi kwa kuwa wanayo mahusiano wa kibiashara na mtuhumiwa huyo. Akizungumza na waandishi wa habari, Mtendaji wa Kijiji cha Kogaja, Bw. Lukas Ambonya alikiri Bw. Omenda kuhusika katika tukio hilo na kwamba wakiwa njiani kwenda hospitalini mke wake alifariki na yeye kutokomea kusikojulikana hivyo hakuwepo hata wakati wa maziko. Kitendo hicho kiliwakasirisha ndugu wa marehemu ambapo juzi wakati wa maziko walitishia kuvamia kituo cha Polisi na kutaka kuchoma baadhi ya nyumba za ndugu wa mtuhumiwa kijijini hapo. Alisema chanzo cha mauaji hayo ni marehemu kutofautiana na Mumewe siku ya Jumamosi asubuhi, tarehe 20 Oktoba, 2012, (tofauti ambayo haijawekwa bayana), na marehemu baada ya kuhisi hali ya hatari alikimbia kutoka nyumbani hapo. Hata hivyo mume wake Bw. Omenda aliwatuma baadhi ya vijana kwa pikipiki waolifanikiwa kumkamata na kumrudidha nyumbani ambapo majira ya saa 4 asubuhi siku hiyo alimfungia ndani na kuanza kumkatakata kwa panga. “Sisi tunasema haya kwa sababu tunaishi kijijini hapa na Bwana huyu ana mahusiano makubwa na polisi hawa , ndio maana hawakutaka kumtia ndani badala yake walisaidia kuandaa njama za kutoroka kwake ..yeye alipeleka mke wake hospitalini akiwa marehemu” alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka kutaja jina. Marehemu hajaacha watoto. Polisi inawashikilia baadhi ya ndugu wa mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi.

WALIOGOMEA SHAHADA ZA ARDHI UNIVERSITY KUPEWA ZA UDSM


Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitakuwa na mahafali ya 42 tarehe 27 Oktoba 2012 na Novemba 3, 3012.

 Jumla ya wahitimu 3,643 watatunukiwa shahada na stashahada wakati wahitimu 902 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi (UCLAS) watatunukiwa shahada.

UCLAS kwa sasa ni sehemu ya UDSM.

Hayo yalisemwa na Makamu Mkuu wa wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala akitoa taarifa kwa umma kupitia waandishi wa habari.

“Tunapenda kuufahamisha umma pia kuwa, katika mahafali ya sasa wanafunzi wa UCLAS na wao watatunukiwa shahada kama wanafunzi wa UDSM, uamuzi huu umefuatia kumalizika kwa kesi Lello & Others Vs Ardhi University, University of Dar es Salaam and Attornry General, Misc.Civil Cause No. 69 of 2008, iliyofunguliwa na wanafunzi wa UCLAS wakipinga kupata shahada za UCLAS kwa madai kuwa udahili wao ulibaki wa UDSM, hivyo UDSM kinakubalina kwa dhati na uamuzi wa Mahakama Kuu,” alisema Prof Mukandala.

UDSM imekubali kuwatunuku shahada mbalimbali wahitimu hao 902 waliomaliza masomo yao UCLAS ambao awali waligoma kutunukiwa shahada zao na chuo hicho (UCLAS) katika Mahafali ya 42 kutokana na madai kuwa walipata udahili chini ya UDSM wakati UCLAS kilipopata hadhi ya kuwa chuo kikuu kinachojitegemea mwaka 2007 hivyo walistahili kutunukiwa shahada na chuo kilichowadahili. Wanafunzi hao ni wale waliohitimu masomo katika miaka ya 2007 hadi 2010.

Wanafunzi hao kwa kupinga suala hilo walifungua kesi mahakamani dhidi ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Sisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tumekubaliana kwa dhati na uamuzi huu wa mahakama na tumeamua kuwatunuku shahada wanafunzi hao kwa vile hakuna rufaa iliyokatwa dhidi ya uamuzi huo,” alisema Profesa Mukandala.

Kati ya watakaotunukiwa shahada mbalimbali, 28 watatunukiwa Shahada za Uzamivu, 671 Shahada ya Uzamili; 153 Stashahada za Uzamili na 2, 790 Shahada ya Kwanza.

Licha ya mahafali hayo, Profesa Mukandala alisema chuo hicho kitahitimisha maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwake kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo kufanya mkutano na wahitimu waliowahi kusoma chuoni hapo shughuli ambayo itafanyika Alhamisi.

Profesa Mukandala alisema wakati wa kuhitimisha sherehe hizo, shughuli zitakazofanyika ni kuweka jiwe la msingi la jengo la kituo cha wanafunzi, kuzindua Dira ya Chuo hicho (UDSM Vision 2061) na kutoa tuzo mbalimbali kwa watu na vikundi vilivyotoa mchango uliotukuka kwa chuo kikuu katika miaka 50 iliyopita.

Akizungumzia dira hiyo, alisema itakuwa ni ya nusu karne ijayo na malengo yake ni kufikia mwaka 2061 chuo kitakuwa katika nafasi za juu za viwango vya ubora vya kimataifa.



MAADHIMISHO YA MIAKA 67 YA UN

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Raphael Muhuga aliyemwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Tanzania katika sherehe za maadhimisho ya miaka 67 ya Umoja wa Mataifa tangu kuzaliwa kwake.
Mgeni rasmi Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Samwel Sitta akiwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam leo katika Kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Mataifa Tanzania kusheherekea miaka 67 tangu uanzishwe.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dkt. Alberic Kacou akimlaki na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Samwel Sitta kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaa leo.
Pichani Juu na Chini ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dkt. Alberic Kacou (katikati) akimtambulisha Mh. Samwel Sitta kwa baadhi ya Wakurugenzi wa Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa hapa nchini.
Waziri wa Afrika Mashariki Mh. Samuel Sitta akipokea heshima ya wimbo wa Taifa baada ya kuwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam leo kuhudhuria kilele cha maadhimisho ya wiki ya Umoja wa Mataifa baada ya kutimiza miaka 67 ya UN tangu kuanzishwa.
Mh. Samuel Sitta akikagua gwaride maalum katika kilele cha wiki ya maadhimisho ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Afrika Mashariki akishuhudia upandishwaji wa bendera ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni ishara ya kusheherekea miaka 67 ya Umoja huo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar leo.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dkt. Alberic Kacou, Mgeni rasmi Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Samwel Sitta na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meha Jenerali Raphael Muhuga wakiwa Meza kuu.
Pichani Juu na Chini ni viongozi wa Madhehebu ya Dini nchini wakiomba Dua kwa ajili ya kubariki sherehe za kutimiza miaka 67 ya Umoja wa Mataifa tangu kuanzishwa.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samwel Sitta akizungumza katika sherehe za kutimiza miaka 67 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN) katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Sitta aliipongeza Umoja wa Mataifa kwa kuisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ili kutokomeza umaskini.Waziri Sitta alisisitiza kwamba bado Umoja wa Mataifa unakabiliwa na changamoto nchini kama vile amani na usalama, tatizo la njaa, mabadiliko ya tabia nchi na uwepo wa silaha za maangamizi.Mh. Sitta alifafanua katika kilele cha sherehe hizo umuhimu wa kupitia na kusaidia nchi zinazoendelea kufikia malengo ya millennia.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dkt. Alberic Kacou akitoa nasaha zake wakati wa maadhimisho ya umoja huo katika viwanja vya Karimjee alisema matatizo ya njaa, kupanda kwa bei za mafuta na mtikisiko wa uchumi duniani ni kati ya changamoto kubwa ambazo Umoja wa Mataifa inakabiliana navyo katika dunia ya leo. Dtk Kacou pia aliipongeza Tanzania katika juhudi zake za kupunguza vifo vya wakinamama wakati wa kujifungua na watoto ili waweze kufikia malengo ya millennia itakapofika 2015.Mratibu Mkazi wa UN alisema Tanzania imepunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.
Katibu wa UNA Tanzania Fancy Nkuhi akizungumza kwenye hafla hiyo alisema umoja wa mataifa imefanya kazi kubwa katika kuwaunganisha vijana wa bara la Afrika. Nkuhi alisema kupitia YUNA walitoa elimu ya afya ya uzazi na ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana katika mikoa kumi hapa nchini Tanzania katika harakati ya kuelimisha vijana madhara ya ugonjwa huo na afya ya uzazi kwa vijana.
Wanafunzi kutoka shule ya mchepuo wa kiingereza ya Heritage (Heritage English Medium Schools) ambao walikuwa kivutio wakati wa maadhimisho ya miaka 67 ya wiki ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania wakiwa katika gwaride maalum kupamba sherehe hiyo.
Meza kuu ikifurahia jambo wakati wa gwaride la watoto wa shule ya Heritage baada ya kuonyesha mbwembwe katika kupamba sherehe hiyo.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Azania wakitoa burudani ya Wimbo maalum wa kuipongeza UN kutimiza miaka 67 ya kuzaliwa.
Wanafunzi kutoka shule ya mchepuo wa kiingereza ya Heritage (Heritage English Medium Schools) wakiimba wimbo maalum uliobeba ujumbe wa kuhimiza utunzaji wa amani miongoni mwa mataifa wakati wa maadhimisho ya miaka 67 ya Umoja wa Mataifa.
Pichani Juu na Chini ni baadhi ya Mabalozi, Wakurugenzi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Wafanyakazi wa UN na wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo.
Pichani ni baadhi ya maafisa wa Jeshi waliohudhuria sherehe hizo.
Waziri Sitta akiwa ameambatana na Mwenyeji wake Mratibu Mkazi wa UN Tanzania Dkt. Alberic Kacou (kushoto) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa wa Kitengo cha maafa UN Bw. Mdathiru Abubakar (wa pili kushoto) akielezea namna ya shirika la Umoja wa Mataifa linavyoshiriki pindi inapotokea maafa nchini. Kulia ni Judith Bihondwa wa UNICEF.
Afisa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa Tanzania Hoyce Temu (kulia) akifafanua utendaji wa kazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake 21 yanavyofanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Samuel Sitta (wa pili kushoto) aliyeambata na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dkt. Alberic Kacou.
Mwenyekiti wa Shirikisho la vijana la Umoja wa Mataifa nchini (YUNA) Bw. Lwidiko Edward akisalimiana na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Samwel Sitta kwenye banda la maonyesho la Umoja wa Mataifa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar.
Waziri Sitta katika banda la maonyesho la shirika linalohudumia wakimbizi nchini (UNHCR). Katikati ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dkt. Alberic Kacou na kushoto ni Afisa Habari kutoka kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) Stella Vuzo.
Afisa Itifaki na Uhusiano wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) Bw. Rodney Thadeus akimweleza Waziri Sitta jinsi ya kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) kinavyojipambanua kwa kupokea wageni mbalimbali wanaofanya mikutano katika kituo hicho na kutmia mwanya huo kutangaza Utalii na vivutio vya nchi.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Samwel Sitta na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Dkt. Alberic Kacou katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye banda la maonyesho katika wiki ya Umoja wa Mataifa.


POLISI AGOMBEA UONGOZI UVCCM-NEC

WAKATI Mkutano Mkuu wa Nane wa Uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM) ukimalizika, mmoja wa wagombea wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho nafasi sita Tanzania Bara, Stanley Mdoe, ametiwa mbaroni na Polisi akibainika kuwa askari Polisi.

Askari huyo mwenye namba F 7961 wa cheo cha Konstebo, anatoka kituo cha Polisi Mvomero, Morogoro ambaye alibainika jana akijihusisha na siasa hata kuingia kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa NEC kupitia Vijana.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana Morogoro, askari huyo alijitambulisha kwa baadhi ya wajumbe kuwa yeye ni mtoto wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, akijiita Stanley Bendera.

Wapambe waliofuatana naye kutoka Morogoro wakiwa Dodoma waliarifu kuwa mgombea huyo alikamatwa juzi jioni akiwa amevalia sare za chama hicho akiomba kura kwa wajumbe ili wamchague kwa nafasi hiyo.

Hata hivyo, ilielezwa na baadhi ya wanachama waliofuatana naye na wengine wanaotambua kazi yake uaskari, waliwajulisha maofisa usalama waliokuwa eneo hilo nao kufikisha taarifa hizo Polisi na kukamatwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, askari huyo alikuwa ameomba likizo isiyo na malipo, wakati wengine wakidai kuwa ameacha kazi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile akizungumzia tukio hilo alisema alipata taarifa ya kukamatwa kwa askari huyo Dodoma na kwamba wakati huo alikuwa akimtafuta kwa siku mbili kwa ajili ya shughuli za kikazi bila mafanikio.

“Sina uhakika kama askari huyu amejiingiza katika siasa ... nimetuma askari wengine kwenda Dodoma kufanya uchunguzi wa suala hilo,” alisema Kamanda Shilogile na kuongeza:

“Iwapo itabainika kuwa kweli, atachukuliwa hatua stahiki na kinidhamu kulingana na taratibu za kijeshi. Hata hivyo siwezi kuzungumzia suala la ugombeaji wake, sijathibitisha ukweli wake, isipokuwa hakuwa kazini kwa siku mbili na ni utovu wa nidhamu kwa Jeshi letu kutoonekana eneo la kazi,” alisema Kamanda Shilogile.

Kwa mujibu wa Kamanda, sheria za nchi na Katiba kuna vifungu vinavyohusu majeshi ya ulinzi na usalama vikitamka kuzuia na kupiga marufuku mwanajeshi kujihusisha na siasa.

Alisema iwapo jambo hilo litabainika, litakuwa limefanyika kinyume na kanuni na taratibu za kazi ya uaskari. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bendera, hakupatikana ofisini kwake wala kwa njia ya simu ya mkononi ili kufafanua kadhia hiyo.

Hata hivyo wasaidizi wake walidai kuwa yuko nje ya nchi kwa shughuli za kikazi.





KESI YA DECI: MCH MTARES AKIRI BOT WALIWAKATAZA KUPOKEA HELA

 
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kusimamia na Kuendesha Upatu (DECI), Mchungaji Jackson Mtares amekiri kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) iliwakataza kupokea fedha kutoka kwa mwanachama yeyote wa taaasisi hiyo.

Mtares alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kuendesha shughuli za upatu bila kibali inayomkabili pamoja na wakurugenzi wenzake wanne.

Akihojiwa na Wakili wa Serikali Prosper Mwangamila, Mtares alidai katika barua ya majibu ya kuomba leseni ya kufanya shughuli za taasisi hiyo, BOT iliwatakaza kupokea fedha kutoka kwa mwanachama yeyote iwe kwa hiari au kwa lazima.

Hata hivyo alipoendelea kuhojiwa na kupewa barua hiyo ambayo imepokelewa mahakamani hapo kama kielelezo cha upande wa mashitaka, Mtares alidai kuwa Mkurugenzi mwenziye ambaye pia ni mshitakiwa ndiye atakayetoa maelezo zaidi.

Awali Mtares aliwasilisha kielelezo ambacho ni barua ya maombi waliyoandika kwa Gavana wa Benki Kuu (BOT) kuomba leseni ya kufanya shughuli za taasisi ambazo ni kusaidia watu wenye kipato cha chini kujikimu kimaisha.

Akiongozwa na Wakili wake wa utetezi Hudson Ndusyepo, Mtares alidai hakuhusika kupokea fedha wala kutoa risiti kwa wanachama na hata katika ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashitaka hakuna shahidi aliyedai yeye alipokea fedha.

Mtares aliendelea kudai kuwa,  Benki ya Afrika (BOA) ilikataa kuhifadhi fedha za taasisi hiyo hivyo walizihamishia katika akaunti ya kanisa lake la Jesus Christ  deliverance iliyopo katika Benki ya Wananchi Dar es salaam (DCB) ambayo ilikutwa na zaidi ya Sh bilioni 1.3 baada ya shughuli za Deci kusimama.

Alipoulizwa sababu za benki hiyo kukataa kuhifadhi fedha hizo alidai hajui bali walipewa taarifa kuwa wanatakiwa watoe fedha hizo haraka ndipo bodi ya wakurugenzi ilipoamua fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti ya kanisa lake.

Aliendelea kudai kuwa wanachama walikuwa wanalipa kiingilio cha Sh 30,000 na baadaye wanaweka fedha na kupata uwezeshwaji (riba) ya asilimia 150 ya fedha ambayo mwanachama ameweka.

Alipobanwa kwa maswali na upande wa mashitaka, Mtares alidai fedha za riba  zilitokana na fedha walizokuwa wanaweka wanachama kwasababu Deci ilikuwa haijishughulishi na biashara yeyote zaidi ya kuwasaidia watu wenye kipato cha chini.

Hakimu Stewart Sanga aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8 mwaka huu, wakatakapoendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Wachungaji wa makanisa tofauti ya Pentecoste ni, Dominic Kigendi, Samuel Mtares, Timotheo Ole Loitingye na  Arbogast Francis.

Wanadaiwa katika tarehe tofauti mwaka  2007 na  Machi 2009 katika Makao Makuu ya Deci, Mabibo Dar es Salaam walikusanya fedha kutoka kwa wananchi  wakiwaahidi kuwa watapata faida ya riba kubwa, katika mpango huo waliouita kupanda na kuvuna pia walifanya shughuli hiyo bila leseni.


KIBONZO CHA LEO

Picture

 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU