Facebook Comments Box

Monday, August 11, 2014

TAMKO LA HISB UT TAHRIR JUU YA MAHAKAMA YA QADH ZANZIBAR.

Hizb ut –Tahrir Afrika Mashariki haina imani kabisa na mpango wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (GNU) kupeleka Muswada wa sheria wa kile kinachoitwa kuiboresha Mahkama ya Qadhi. Aidha, tunaonya kwa nguvu zote dhidi ya kudandiwa kwa kile kinachoitwa kuzifanyia marekebisho sheria za udhalilishaji wa
kijinsia ilhali ikidhamiriwa kuasisi sheria ya suala la mgao wa mali za wanandoa baada ya kuachana (division of matrimonial asset).

Jambo ambalo ni kinyume na Uislamu na kuingilia moja kwa moja mamlaka ya Mahkama ya Qadhi. Mchakato huu wa GNU kama ilivyo michakato ya sheria nyengine na hususan kama ulivyokuwa mchakato wa kuasisiwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2011 ni shinikizo la Madola ya nje (Gazeti la Mwananchi Juni 4, 2010. Uk 1&4). Pia likipigiwa tarumbeta na wakala wao wa ndani katika wanaoitwa wanaharakati na taasisi za kiraia zinazojinasibu na utetezi wa haki za wanawake ikiwemo Jumuiya ya ZAFELA. (Zanzibar Female Lawyers)

Tunatamka wazi kwamba licha ya malengo mengine, mchakato huu umedhamiria kukimaliza kichache kilichobakia katika sheria za Kiislamu katika miamala ya ndoa, urathi na matunzo ya watoto, kumega mamlaka ya Mahkama ya Qadhi kama si kuing’owa kamwe! Enyi Waislamu wa Zanzibar hususan Masheikh, Maimamu na Maustadhi: Mzazi mwenye uchungu hachoshi na ulezi wake , Sisi Hizb tunakukumbusheni tena kama tulivyokukumbusheni na kukuhadharisheni mwaka 2011 wakati harakati za kupitishwa Sheria ya Mtoto zilipopamba moto na hatimae kupitishwa.

Sheria thaqili na ovu ambayo itabakisha balaa na dhima kubwa katika historia ya visiwa hivi. Jee mnajuwa kuwa pamoja na mambo mengi mabaya ya sheria ile pia imetambuwa miongoni mwa vipimo vya kunasibishwa ubaba wa mtoto ni kwa kupitia vipimo vya vijinasaba (DNA test) au hata ndoa zilizo kinyume na Uislamu? Jee hatuoni kwamba hilo litawapa uwalii na urathi wasio na haki na kuendeleza dhulma mpaka siku ya Hesabu? Kampeni dhidi ya Mahkama ya Qadhi ni kampeni ya nje na inaendelea Kenya, Tanganyika na pia ni ajenda endelevu Zanzibar kwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo kuimarishwa wizara inayohusiana na masuala ya Wanawake na Watoto ili kuyaondoa majukumu hayo kwa maqadhi, kupitishwa sheria mbali mbali nk. 

Yote hayo hutendwa kwa kauli mbiu za ukombozi, uboreshaji, kuondoa udhalilishaji wa wanawake na watoto nk. Aidha, kwa ujanja mkubwa hupatilizwa kupitishwa sheria hizo wakati watu wameshughulishwa na mambo yasio na tija ikiwemo suala la katiba na mengineyo. Na vivi hivi ndivyo pia walivyopatiliza kuipitisha sheria ya Mtoto mwaka 2011 bila ya upinzani thabiti huku watu wakiwa wameshughulishwa na harakati za siasa batil za kidemokrasia.

Mwisho, Hizb inatoa mwito kwa Waislamu jumla wa Zanzibar hususan masheikh, maimamu maustadh kusimama kidete dhidi ya fitna hii na kuifedhehi waziwazi mipango na ajenda hii katika majukwaa na mimbar zetu ili kuonesha Ummah uone udhati wa uadui uliotuzunguuka. 

Aidha, tunawaonya katika wanaharakati, wanasisa na wanasheria wanaopiga debe kuingamiza Mahkama ya Qadhi kwa maslahi machache ya kidunia wazinduke na wasiendelee kujigubika guo la aibu, fedheha na uovu katika historia yao. Wao wametoka katika mifupa ya Kiislamu basi wamukhofu Mola wao wasihadaike na kichache cha kupita katika dunia hii kwa maangamizi ya kudumu milele.

ﻳَﺎﻗَﻮْﻡِ ﻟَﻜُﻢُ ﺍﻟْﻤُﻠْﻚُ ﺍﻟْﻴَﻮْﻡَ ﻇَﺎﻫِﺮِﻳﻦَ ﻓِﻲ ﺍﻷَﺭْﺽِ ﻓَﻤَﻦْ ﻳَﻨﺼُﺮُﻧَﺎ ﻣِﻦْ ﺑَﺄْﺱِ ﺍﻟﻠَّﻪِ ﺇِﻥْ َﻧَﺎ
Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika nchi; basi ni
nani atakayetusaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia? ( TMQ GHAFIR 29)).

Kumb: 18 / 1435 AH    12th Shawwal 1435 AH 08/08/2014 CE Masoud Msellem Naibu Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut Tahrir in East Africa.

Simu.: +255 778 8706 09
Pepe: jukwalakhilafah@gmail.com
Hizb ut Tahrir Official Website
www.hizb-ut-tahrir.org
Hizb ut Tahrir Media Office Website
www.hizb-ut-tahrir.info


MKE NA MUME WAZICHAPA KAVUKAVU MAHAKAMANI

Polisi wakimdhibiti mume.

TIMBWILI! Jamaa mmoja na mkewe ambao wote hawakujulikana majina mara moja wamezua varangati la aina yake mahakamani kisa kikiwa ni kufutiwa kesi na kushindwa kuheshimu amri za maafande.Tukio hilo la aina yake lililoshuhudiwa na mwanahabari wetu lilijiri kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar
baada ya mume huyo kufutiwa kesi iliyokuwa ikimkabili ya unyayasaji wa watoto wake wa kuwazaa. Jamaa huyo na mkewe walizua timbwili hilo wakati mtuhumiwa huyo akitolewa chumba cha mahakama kwenda kuweka sawa nyaraka ili awe huru. 

Huku akiwa na hasira, mwanaume huyo alianza kuzozana na polisi huku akiungwa mkono na mkewe wakikataa kutii amri ya askari aliyekuwa akiwaelekeza kwenda chumba kingine ili kukamilisha taratibu za kuwa huru.

Akiwa chini ya ulinzi wa polisi. Wawili hao walisikika wakitoa maneno makali kuwa wasisukumwe kwani hakimu alikuwa ameshamwachia mwanaume huyo huru, jambo ambalo liliwakera askari na kuwaambia kuwa wanatakiwa kutii sheria na taratibu za  mahakama. Katika sekeseke hilo huku askari wakilazimika kutumia nguvu, jamaa huyo alifanya mgomo baridi akipiga kelele na kufoka hivyo kusababisha watu kushangaa.

Hata hivyo, polisi hao walitumia mbinu ya kuwadhibiti kistaarabu ili kuhakikisha amani inakuwepo mahakamani hapo hivyo mambo yakawa shwari.

Mwanamke huyo akidhibitiwa. Habari ndani ya mahakama hiyo zilidai kwamba jamaa huyo alikuwa akikabiliwa na tuhuma hiyo ya unyanyasaji wa watoto wake ambao alizaa na mwanamke mwingine. Madai yalishushwa kwamba mwanaume huyo alikuwa akishirikiana na mkewe huyo mpya kuwafanyia manyanyaso kwa watoto wake hali ambayo iliyosababisha shirika moja la kutetea haki za  binadamu kumchukulia hatua ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani hapo.

Ilisemekana kwamba jamaa huyo alionywa na kupewa maelekezo kuwa  kama ikiwezekana watoto hao watafutiwe sehemu nyingine ya kuishi ikiwa ni pamoja na kupata mahitaji muhimu, jambo ambalo mwanaume huyo alilitekeleza na kumaliza ishu hiyo.


PUNGUZENI FURAHA WANA ARSENAL;HATA MWAKA JANA TULIANZA HIVI

Mabingwa wa ngao ya jamii
Habari wana Arsenal wenzangu, Mmeuchukuliaje ushindi wa jana dhidi ya Manchester City. Bado furaha ipo mpaka leo? Umekuwa hauna stori nzuri kuhadithia wenzako kazini zaidi ya mechi ya jana na bao zuri la Giroud?Bado ukiipamba stori yako na vijimaneno kama vile "kumbuka hawa ndio mabingwa wetu wa EPL msimu uliopita". Sitaki kusema ushindi wetu jana ulikuwa wa bahati, ule ni ushindi mjarabu katika wakati halisi.

Baadhi ya watu wasioipenda Arsenal wanasema Manchester City isingeweza kushinda kutokana na kikosi chao kutokuwa na baadhi ya wachezaji wao nyota huku wakisahau kuwa Arsenal nao hawakuwepo wachezaji nyota wengine katika mechi hiyo. Na kwa vile tumeshinda na Ngao tunayo sie hatunabudi sisi kuwa waongeaji na ikiwezekana kuwakejeli tutakavyo.

Kinachonirudisha nyuma hapa ni historia ya msimu uliopita. Kama una kumbukumbu nzuri mwaka jana wiki moja kabla ya ligi tulicheza mechi ya kirafiki na Manchester City tukawafunga tukawa na matumaini na kikosi chetu lakini kuingia kwenye ligi Manchester City wakawa mabingwa. Kwahiyo furaha yetu tusiendeleze mpaka kwenye ligi iishie pale huku tukiangalia mwenendo wetu katika ligi.

Msinichukie wala kunielewa vibaya sisemi kuwa Arsenal itafanya vibaya msimu huu maana mimi ndio niliandika kuwa msimu huu ndio kila mshabiki wa Arsenal atakuwa na furaha. Kusema itafanya vibaya itakuwa unafiki ila nnacho waambia tusihesabu kuku kwa mayai yaliyotagwa jana tuwe na subira na tusubiri yaanguliwe mayai.


NYUMBA YA MTUHUMIWA WA ULAWITI YACHOMWA MOTO

Wananchi wenye hasira, wameteketeza kwa moto nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Mwika Uuwo, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, wakimtuhumu kulawiti wanaume wenzake. Hasira za wananchi hao zilifikia kiwango kisichohimilika baada ya mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 42, kudaiwa kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12 kijijini hapo juzi.

Wananchi wa kijiji hicho wanamtuhumu mwanamume huyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa kwa sababu za kitaaluma, kuwa ana tabia ya kuwalawiti vijana kijijini hapo.Habari kutoka kijijini hapo zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, zilisema kuwa mbali na kuchoma moto nyumba hiyo, pia walifyeka ekari moja ya shamba la migomba la mtuhumiwa huyo.

Kamanda Boaz alisema jana kuwa tukio la kuchomwa moto kwa nyumba hiyo lilitokea saa 3:30 usiku na ilipofika saa 6:00 usiku wa kuamkia jana, nyumba hiyo ilikuwa imeteketea yote.

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, wakati wananchi wakiiteketeza nyumba hiyo na kufyeka shamba lake la migomba, mtuhumiwa huyo anayetafutwa na polisi hakuwepo ndani ya nyumba hiyo.

“Siyo jambo jema kuchukua sheria mkononi kwa sababu huyu ametenda kosa halafu mnaokwenda kuchoma nyumba yake, nanyi pia mnatenda kosa la jinai,” alisema Boaz.

“Kama walijua (wananchi) kuwa huyo mtuhumiwa amerudi na yuko ndani, wangemkamata na kumfikisha polisi siyo kuchoma nyumba. 

Nchi lazima iendeshwe kwa misingi ya kisheria,” alisisitiza. Kamanda Boaz alisema kuwa juzi polisi walifika kumtafuta mtuhumiwa huyo kwa lengo la kumkamata, lakini hawakuweza kumpata na inadaiwa alikuwa amekimbilia mahali kusikojulikana.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU