Young Africans imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya Coastal Union
kutoka mkoani Tanga kufuatia bao la kusawazisha la penati ya utata
dakika ya 90 ya mchezo la kiungo Jerry Santo baada ya Didier Kavumbagu
kuifungia Yanga bao la kwanza.
Coastal Union ambayo katika mchezo wake wa awali dhidi ya JKT Oljoro
ilipata ushindi wa bao 2-0, ilicheza mchezo mbovu tangu mwanzo mwa
mchezo hali iliyopelekea mwamuzi Martin Sanya ashindwe kulimudu pambano.
Yanga
iliuanza mchezo kwa kasi kwa lengo la kusaka bao la mapema lakini
kutokua makini kwa washambuliaji wake Jerson Tegete, Didier Kaumbagu na
Simon Msuva kuliifanya ishindwe kupata bao kwa dakika 45 za kipindi cha
kwanza.
Haruna Moshi 'Boban' na Said Nyosso walionyeshwa kadi za
njano katika kipindi cha kwanza kufuatia kuwachezea ndivyo sivyo
wachezaji wa Yanga, ambapo wachezaji hao wa Coastal walishindwa
kuonyesha soka la uungwana.
Kipindi cha pili cha mchezo kilianza
kwa Yanga kufanya mabadiliko kwa kuwaingiza Hussein Javu na Hamis Thabit
waliochukua nafasi za Jerson Tegete na Salum Telela aliyeumia katika
kipindi cha kwanza.
Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa timu ya
Yanga kwani katika dakika ya 69 mshambuliaji Didier Kavumbagu aliipatia
Young Africans bao la kwanza akimalizia pasi safi ya mlinzi wa pembeni
David Luhende aliyewazidi uwezo walinzi wa Coastal Union na kumpasia
mfungaji.
Baada ya kupata bao
hilo Yanga waliendelea kufanya mashambulizi kupitia kwa washambuliaji
wake Hussein Javu na Didier Kavumbagu lakini walinzi wa waliendelea
kucheza ndivyo sivyo kwa wachezaji wa Yanga kana kwamba wanacheza mchezo
wa mateke na ngumi.
Katika hali iliyowastaabisha wengi
mwamuzi alimpatia kadi nyekundu Saimon Msuva baada ya kuchezewa vibaya
na mlinzi wa Coastal Abdi Banda, huku watu wakisubiria mwamuzi amuadhibu
Banda alimpatia kadi Msuva na kiungo wa Coastal Crispin Odula.
Dakika
ya 90 mwamuzi Martin Sanya aliipatia Coastal Union penati ya utata
kufuatia kiungo Haruna Moshi 'Boban' kumdanganya mwamuzi kuwa mlinzi
Nadir Haroub 'Cannavaro' ameunawa mpira ndani ya eneo la hatari na
penati hiyo ilipigwa na Jerry Santo na kuwapatia bao la kusawzisha.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Young Africans 1 - 1 Coastal Union.
Mara
baada ya mchezo kocha mkuu wa Yanga Ernie Brandts amemtupia lawama
mwamuzi wa mchezo Martin Sanya kwa kushindwa kuumudu mchezo na kusema
katika mchezo wa amekuwa mchezaji bora baada ya kushindwa kulimudu
pambano.
Young Africans: 1.Ally Mustapha
'Barthez', 2.Juma Abdul, 3.David Luhende, 4.Nadir Haroub 'Cannavaro'
5.Mbuyu Twite, 6.Salum TelelaHamis Thabit , 7.Saimon Msuva, 8.Frank
Domayo, 9.Didier Kavumbagu, 10.Jerson Tegete/Hussein Javu, 11.Haruna
Niyonzima.
Coastal Union: 1.Shaban Hassan 'Kado',
2.Juma Hamada, 3.Abdi Banda, 4.Marcus Ndehele, 5.Juma Nyosso, 6.Jerry
Santo, 7.Uhuru Seleman/Seleman Kassim, 8.Haruna Moshi 'Boban', 9.Lutimba
Yayo/Kenneth Masumbuko, 10.Crispin Odula, 11.Danny Lyanga/Razack
Khalfani