Facebook Comments Box

Wednesday, September 11, 2013

OPERESHENI YA KUSAKA WAHAMIAJI HARAMU YASABABISHA MNYARWANDA KUJINYONGA

Raia wa Rwanda amejinyonga kwa kamba chumbani kwake, tukio linalohusishwa na zoezi linaloendelea hivi sasa nchini la kuwasaka wahamiaji haramu na kuwarejesha makwao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, marehemu anatajwa kuwa ni Francis Mathias (75), ambaye alikuwa mkazi wa kitongoji Kikukuru kata Kikukuru, tarafa Mabira wilayani Kyerwa mkoani Kagera.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kikukuru, Joseph Leo, jana alilithibitishia NIPASHE kutokea kwa tukio hilo na kuwa alipata taarifa hizo kutoka kwa binti wa marehemu juzi saa 3:00 asubuhi.

“Baada ya kupata hizo taarifa niliongozana na mgambo, tulipofika mlango wa chumba chake ulikuwa umefungwa kwa ndani, tukafanikiwa kuuvunja tukaingia ndani na kukuta amejitundika kwa kamba,” alisema Leo na kuongeza kuwa marehemu alikuwa mfugaji na mkulima.

Alisema kuwa kabla ya kujiua, mzee huyo alichana fedha za Kitanzania zinazokadiriwa kufikia Shilingi
milioni saba zikiwamo noti za Sh. 5,000 na za Sh. 10,000, ambazo zilikutwa ndani ya chumba chake.

Leo alisema baada kushuhudia alipiga simu kwa Ofisa Mtendaji wa Kata Kikukuru ambaye alifika na kupiga ngoma na watu walikusanyika kushuhudia kilichotokea na baadaye kwenda kutoa taarifa  katika kituo cha Polisi.

Alipotakiwa na NIPASHE kuthibitisha kama kweli mwananchi wake aliyejinyonga alikuwa raia wa Rwanda, Leo alithibitisha na kufafanua kuwa tayari alikwisha kumuorodhesha kwa lengo la kurejeshwa kwao katika opereshani iliyoanza Jumamosi ya kuwarejesha makwao wahamiaji haramu wanaoishi mkoani Kagera.
Aliongeza kuwa aliwahi kumhoji marehemu Mathias ambaye alimweleza kuwa alikuja Tanzania kutoka Rwanda tangu mwaka mwaka 1976.

Naye Ofisa Tarafa ya Mabira, Nicolaus Rugemalira, alisema uchunguzi wa awali wa kimazingira umeonyesha kuwa kulikuwa na mgogoro wa familia baada ya marehemu kutaka wauze mali zao zote warudi Rwanda, lakini familia yake haikukubaliana naye kutokana na mkewe kuwa raia wa Tanzania.

“Mke wake ni Mtanzania, inaonekana baada ya familia yake kukataa uamuzi wake wa kuuza mali zote ili waondoke, aliamua kuchukua uamuzi huo,” alisema Rugemalira.

Akizungumzia tukio hilo, binti wa marehemu, Melania Francis, alithibitisha kuwapo ugomvi kati ya baba yake na mama yake hali iliyosababisha mama yao kuondoka bila kufahamika alikoelekea.

Alisema siku ya tukio aliamka na kuwaandaa wadogo zake kwenda shuleni na baada ya hapo alikwenda shambani kuona kama vibarua wameanza kazi ya kulima, lakini aliporudi nyumbani alishangaa kuona mlango wa chumba cha baba yake bado umefungwa wakati haikuwa kawaida yake kulala hadi saa moja.

Melania alisema alibisha hodi bila majibu, akajaribu kufungua ikashindikana na alipochungulia aliona fedha nyingi zimetapakaa ndipo alipokimbia kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji.

“Nafahamu baba alikuwa na uwezo wa kumiliki fedha hizo, lakini sikufahamu anazihifadhi wapi,” alisema binti huyo wa marehemu.

Alisema wamezaliwa watoto watano katika familia hiyo na kwamba ndugu zake wawili walitoweka na kubakia watatu na kuongeza kuwa kuwa anatambua kuwa baba yake alikuwa raia wa Rwanda.

Alipotakiwa kueleza kama anafahamu alikoelekea mama yake, binti huyo alidai kuwa hafahamu ingawa anafahamu kuwa ni mzaliwa wa Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.

Kutokana na kutoweka kwa mama huyo pamoja na wanafamilia wengine, uongozi wa eneo hilo unaendelea na ufuatiliaji ili kujua wanafamilia wengine wamekwenda wapi.
--- via gazeti la NIPASHE


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU