KWA
mara ya kwanza, kiungo Amri Ramadhani Kiemba ameibuka na kukanusha
kusaini Yanga SC, ingawa amesema yeye bado mchezaji huru, kwa kuwa hadi
sasa hajasaini timu yoyote baada ya kumaliza Mkataba wake Simba SC.
Akizungumza Kiemba alisema kwamba hajasaini timu yoyote hadi sasa na anajitambua kama mchezaji huru.
Alipoulizwa
kuhusu mustakabali wake, Kiemba alisema kwa sasa akili yake ipo kwenye
kuisaidia timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iweze kukata
tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia.
“Sasa
hivi ukiniuliza mambo ya klabu, utakuwa unanionea tu. Nipo katika kambi
ya timu ya taifa, fikra zangu ni majukumu yangu ya kitaifa. Nadhani
baada ya hapa, nitazungumzia hayo mambo,”alisema Kiemba.
Kiemba
aliibua wasiwasi mkubwa kwa wapenzi wa Simba SC, baada ya kuvuma kwa
habari amesaini Yanga SC, huku Mkataba wake ukiwa umemalizika Msimbazi.
Na anaonekana mtu asiye na wasiwasi kabisa kuhusu mustakabali wake- pengine inatokana na kiwango chake cha juu hivi sasa.
Stars inashika nafasi ya pili
katika Kundi C, kuwania tiketi ya Kombe la Dunia mwakani Brazil, ikiwa
na pointi sita nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, ambayo kesho
itakuwa ugenini ikimenyana na Gambia katika mchezo mwingine wa kundi
hilo.
Stars
ilitua hapa Jumatatu ikitokea Ethiopia ambako iliweka kambi ya wiki
moja na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan, ulioisha kwa sare ya
bila mabao.
Kabla
ya kuja hapa, Stars iliweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya
Tansoma, Dar es Salaam ikijifua Uwanja wa Karume na siku chache kabla ya
kuondoka ilialikwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, aliyewapa hamasa kwa
hotuba nzuri.
SOURSE: BIN ZUBEIRY