Facebook Comments Box

Saturday, October 11, 2014

WATU SABA WACHOMWA MOTO KWA TUHUMA ZA UCHAWI


Moja ya nyumba zilizoteketezwa katika Kijiji cha Murufiti ambapo watu saba waliuawa kwa kuchomwa moto. Picha na Diana Rubanguka.
Na Diana Rubanguka na Antony Kayanda, Mwananchi

Kigoma. Watu saba wameuawa kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba katika tukio ambalo nyumba 18 ziliteketezwa na mbili kubomolewa na wananchi waliodai wanawaua wachawi katika Kijiji cha Murufiti, Kasulu, mkoani Kigoma.
Polisi wameeleza kuwa tayari watu 17 wamekamatwa kwa kuhusika kwenye tukio hilo.Miongoni mwa waliouawa katika tukio hilo lililotokea

Jumatatu iliyopita ni John Mavumba (68) na mkewe Elizabeth Kaje 55 ambao pamoja na wenzao walikuwa wakituhumiwa kuwa ni washirikina.Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Josephat John ambaye ni mtoto wa Mavumba, alisema wazazi wake walichomwa moto na kundi la vijana waliokuwa wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.

Alisema vijana walikuwa wamebeba mapanga, marungu na kupita katika nyumba mbalimbali wakifanya mauaji wakisema maneno kwa kurudiarudia kwamba watawamaliza wachawi kwa kuwaua, ndipo yeye na wenzake walikimbia usiku huo wakihofia kuuawa.

“Niliporudi alfajiri niliukuta mwili wa mama ukiwa umbali wa mita 10 kutoka ilipo nyumba yetu ukiwa umeungua na mwili wa baba ukiwa umeungua ndani ya nyumba,” alisema John.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohamed alisema mauaji hayo yalitokea Oktoba 6 kuanzia saa 4:00 usiku katika kijiji hicho. John alisema baada ya tukio hilo wanaume wengi wameyakimbia makazi yao wakihofia kuuawa na kundi la vijana hao. “Kijiji kimebaki na wanawake tu, wanaume wamezikimbia nyumba zao wanahofia kuuawa,” alisema.

Mohamed alisema mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina.

Aliwataja waliouawa kuwa ni John Muvumba (68), Elizabeth Kaje (55), Dyaba Kitwe (55), Vincent Ntiyaba (42), Herman Ndabiloye (78), Redempta Mdogo (60) na Ramadhan Kalaliza (70) wote wakazi wa kijiji hicho.

Alisema nyumba zilizochomwa moto ni 18, mbili zilibomolewa na kufanya jumla ya nyumba 20 zilizoharibika kabisa.Wakazi wa kijiji hicho, Zablon Andrew na Eveline Enock walisema kwa nyakati tofauti kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mganga wa jadi aliyefika kijijini hapo na kupiga ramli akiwataja watu waliouawa kuwa ni wachawi.Andrew alisema baada ya mganga huyo kuwataja, vijana walikusanyana na kuanza kuwateketeza watu bila huruma.

“Kitendo hiki kimeturudisha nyuma kimaendeleo kwa sababu nyumba zetu zimechomwa moto na mazao yetu yameharibiwa,” alisema Andrew.

Hali ilivyo kijijini

Mmoja wa watu aliyechomewa nyumba, Evelyne Msilu alisema sasa kijiji hicho kina askari wengi wanaofanya doria. “Hali inasikitisha, tumepoteza ndugu zetu waliouawa, wanaume
wengi wamekikimbia kijiji kwa hofu ya kuuawa na vijana wengine wamekimbia
wakiogopa kukamatwa,” alisema.

Kwa nini ipigwe ramli?

Akisimulia, Enock alisema kuna kijana mmoja katika kijiji hicho ambaye kazi yake ni kufyatua matofali aliwaomba vijana wanzake kuwa siku inayofuata wamsaidie kuyapanga katika tanuru. Alisema jambo la ajabu ni kwamba walipoamka asubuhi walikuta matofali yamekwishapangwa na haikujulikana aliyefanya kazi hiyo.

Alisema kijana huyo na wenzake waliamini kwamba waliofanya kazi hiyo ni wachawi. Akisimulia kisa kingine, Enock alisema siku chache zilizopita kuna msiba ulitokea kijijini hapo na baada ya mazishi, siku iliyofuata walikuta msalaba umeng’olewa na haujulikani ulipo, jambo ambalo pia
lilihusishwa na ushirikina.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Ogen Gasper aliyeomba Serikali kujenga kituo cha polisi kijijini hapo, alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo alifanya jitihada kubwa kuwapata askari, lakini hawakufika kwa kilichodaiwa ni kukosa usafiri.

Gasper alisema hilo ni tukio la tatu kwa watu kuuawa kwa kutuhumiwa kuwa ni wachawi, la kwanza likiwa limetokea mwaka 1996.


CHANZO: MWANANCHI

TIMES FM WATOZWA FAINI KWA WATANGAZAJI WAKE KUTUMIA MANENO YASIYO NA STAHA

Kituo cha Redio cha Times FM kimetozwa faini ya kulipa kiasi cha Shilingi milioni moja na kupewa onyo kali kutokana na kukiuka vifungu vya maadili na kanuni za utangazaji, vilivyopo katika leseni ya utangazaji inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Akisoma hukumu hiyo jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya TCRA, Margareth Munyagi, alisema ‘Times FM’ imepewa adhabu hiyo baada ya watangazaji wake kwa nyakati tofauti kupitia kipindi chake cha ‘Hatua Tatu’ kinachosikika saa 3 hadi saa 5 asubuhi na ‘Mitikisiko ya Pwani’, kilichosikika mchana wa Agosti 29, 2014, watangazaji wa vipindi hivyo walisikika wakizungumzia dondoo zilizolenga kuhamasisha ngono, na kukiuka maadili ya utangazaji..

Alisema kiutaratibu muda ambao dondoo hizo kutolewa unapaswa kuanzia saa 3 usiku hadi saa 11 alfajiri lakini kinyume chake, zilitangazwa muda ambao vipindi hivyo vingeweza kusikilizwa pia na watoto.

Aidha alisema utetezi uliotolewa na Mkurugenzi wa Redio hiyo, Leule Nyaulawa haukidhi haja mbali na kulipokea shitaka lililotolewa dhidi yao. Nyaulawa alisema suala la kupata watangazaji wazuri Tanzania bado ni changamoto kutokana na vyuo vingi kuzalisha watangazaji wasio na uwezo mzuri. 

Pia alisema kupitia kwa utetezi wake watakwenda kulifanyia kazi suala hilo ili kuepusha kurudiwa kwa kosa kama hilo na mengine yaliyopo katika leseni za utangazaji huku kamati hiyo ikitoa muda wa mwezi mmoja kwa Times Fm kulipa faini hiyo au kukata rufaa kama haikuridhika na uamuzi uliotolewa dhidi yao.


BENIN WATUA NCHINI TAYARI KUIKABILI STARS




BENIN YATUA NCHINI TAYARI KUUMANA NA TAIFA STARS JUMAPILI HII
Kikosi cha wachezaji 18 na viongozi 11 wa timu ya Taifa ya Benin, kimetua jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi ya Kalenda ya FIFA dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumapili (Oktoba 12 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji wa timu ya Benin ambayo imefikia hoteli ya JB Belmont waliwasili jana (Oktoba 9 mwaka huu) Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa nyakati tofauti.

Kikosi hicho kitafanya mazoezi yake ya kwanza leo (Oktoba 10 mwaka huu) saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Gymkhana. Benin watafanya mazoezi yao ya mwisho kesho (Oktoba 11 mwaka huu) saa 10 jioni Uwanja wa Taifa.

Wachezaji walioko kwenye kikosi cha Benin ni Stephane Sessegnon (West Bromwich Albion, Uingereza), Didier Sossa (USS Krake, Benin), Abdel Fadel Suanon (Etoile Sportive du Sahel, Tunisia), Jodel Dossou (Red Bull Salzburg, Austria), Sessi D'almeida (FC Girondis Bordeaux, Ufaransa), Mohamed Aoudou (JS Saoura, Algeria) na Saturnin Allagbe (Niort, Ufaransa). 


(P.T)Steve Mounie (Montpellier, Ufaransa), Farnolle Fabien (Clermont Foot Auvergne 63, Ufaransa), Jordan Adeoti (Caen, Ufaransa), Michael Pote (Omonia Nikosia, Cyprus), David Djigla (FC Girondis Bordeaux, Ufaransa) na Seidou Baraze (Kawkab Marrakech, Morocco).

Jean Ogouchi, Centre Mberie Sportif Club, Gabon), Nafiou Badarou (ASO Chlef, Algeria), Eric Tossavi (Avrankou Omnisport, Benin), Fortune Ore (USS Krake, Benin) na Seibou Mama (Aspac, Benin).

Nayo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager leo (Oktoba 10 mwaka huu) itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10 jioni.

Wakati huo huo, makocha wa Taifa Stars, Mart Nooij na wa Benin Didier Nicolle Olle watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (Oktoba 11 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika Jengo la PPF Tower.

Chanzo:Shaffihdauda.com


CBA YAFANYA VIZURI IKISHIRIKIANA NA VODACOM

Huduma ya M-PAWA inayotolewa na Benki ya Biashara ya Afrika (CBA) imetoa mikopo ya shilingi milioni 200 katika kipindi cha miezi mitatu tangu ianzishwe.

Pamoja na fedha hizo huduma hiyo imewezesha kuwepo na amana za shilingi bilioni 6 kutoka kwa wateja laki 7 ambao wanapata huduma ya M-Pawa,Taarifa hiyo ya mafanikio imetolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa benki hiyo Julius Mcharo akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya Huduma kwa Wateja iliyofanyika Kariakoo.
 

Mcharo alisema huduma hiyo inayotolewa kwa ushirikiano kati ya benki hiyo na Vodacom imepata muitikio kutokana na watanzania kuweza kufungua akaunti za huduma hiyo mahali popote pale walipo kwa kutumia mtandao.

Alisema huduma hiyo ambayo pia inawezesha kupatikana kwa mikopo na kupokea na kulipa huduma mbalimbali kwa m-pesa imerahisisha maisha ya wananchi wengi na kusema kwamba itaendelea kuboreshwa na kutanuliwa.

Akizungumzia wiki ya huduma kwa wateja alisema kwamba watendaji wote wa benki hiyo wanakwenda katika matawi yapatayo 11 nchini kote kutoa huduma kwa karibu zaidi na wateja wao kwa lengo la kufahamu changamoto zao.

Alisema changamoto hizo zitawawezesha kutambua mahitaji halisi ya wateja na kutengeneza bidhaa zinazolingana na mahitaji yao.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), Julius Mcharo watatu kutoka kushoto akiwa na wafanyakazi wa Benki hiyo tawi la k.koo




 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU