Facebook Comments Box

Tuesday, May 6, 2014

MSIBA WA USTAADH ILUNGA WAINGIA KATIKA HISTORIA YA TANZANIA

Katikati ni Sheikh Ilunga na pembeni ni.Salum Ally Mkangwa na nyuma ni Mohamed Said picha ilipingwa CBE mwaka 1988.
Sheikh Ilunga Hassan Kapungu kaingia katika historia ya Dar es
Salaam katika kifo chake. Bahari ya watu walijazana Msikiti wa
Kichangani kuja kuswalia jeneza lake na kisha kulifata nyuma jeneza
hilo hadi Makaburi ya Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa. Sheikh
Ilunga ni mgeni katika mji wa Dar es Salaam kwa maana ya kuwa
hakuzaliwa Dar es Salaam wala hakuwahi kuishi Dar es Salaam.
Alikuwa akija na kuondoka zamani akirejea kwao Tabora na baadae
baada ya kuhamia Mwanza, akija Dar es Salaam na kurejea
Mwanza. Iweje leo mji mzima wa Dar es Salaam usimame na utoke
kuja kumzika Sheikh Ilunga Hassan Kapungu? Hakika hili ni swali
linalotaka majibu ya kuridhisha. Jibu ni dogo na rahisi sana. Hivi
ndivyo Waislam wa Dar es Salaam wanavyofanya kila wanapofiwa
na kipenzi chao. Labda linaweza kuja swali jingine, ''kipenzi?''
Sheikh Ilunga kawaje kuwa kipenzi cha Waislam? Naam Sheikh
Ilunga Hassan Kapungu juu ya udogo wake wa umri alikuwa kipenzi
cha Waislam si Waislam wa Dar es Salaam peke yake. Sheikh Ilunga
Hassan Kapungu alikuwa kipenzi cha Waislam wa Tanzania nzima.
Kibla cha kila msikiti wa Waislam katika Tanzania kilikuwa
kinamkaribisha kama si kuwaidhi basi angalau asimame awasalimie
nduguze Waislam. Sheikh Ilinga Hassan Kapunga hakuwa katika lile
kundi la mesheikh ambao wao wenyewe kwa hofu tu kuna baadhi ya
misikiti wanaogopa si kuingia kuswali, bali hata kupita nje. Sheikh
Ilunga hakuwa katika lile kundi la masheikh wenyeji katika futari za
serikali ''misikiti ya wakubwa'' na shughuli zinazohusiana na mambo
kama hayo lakini wageni katika misikiti ya ndugu zao Waislam.
Kubwa Sheikh Ilunga hakukosa usingizi kwa kukosa kualikwa futari
Ikulu au kualikwa katika dhifa za serikali akapigwa picha na
waheshiwa na kutokea katika runinga na magazeti siku ya pili
ukurasa wa mbele. Sheikh Ilunga Hassan Kapungu
hakushughuliswa na hayo. Yeye alishughulishwa na kuliweka juu
jina la Allah Subhana Wataala. Hili ndilo lililokuwa likimshughulisha
mpaka siku Allah alipomfisha. Sheikh Ilunga kaweka historia katika
historia ya mazishi makubwa Dar es Salaam, historia inayokwenda
nyuma kiasi miaka takriban 100 ukianzia mazishi ya Sheikh
Mwinyikheri Akida sheikh aliyeasisi Msikiti wa Mwinyikheri Akida,
Kitumbini unakuja kwa Sheikh Idrissa bin Saad Khalifa wa Tariqa
Askariyya, kisha Sheikh Kaluta Amri Abeid, halafu Abdulwahid
Sykes, kisha Sheikh Kassim bin Juma, halafu Prof. Kighoma Ali
Malima unaishia kwa Mzee Kitwana Dau baba yake Dk. Ramadhani
Dau. Iweje Ilunga kijana mdogo mno aungane na majina ya watu
maarufu kama hawa na katika hao wote walikuwa katika umri
mkubwa ukimtoa Abdul Sykes? Kitu kimoja ndicho
kilichompandisha daraja Ilunga katika jamii ya Kiislam Tanzania.
Ilunga alikuwa mtumishi wa Waislam. Wakimtuma Ilunga kila kazi
na akiifanya kwa moyo mkunjufu, kuanzia kujenga madras na shule
kisha akawasomeshea na watoto wao hadi siku aliposimama
Ukumbi wa Diamond kuitahadharisha serikali kuwa kuna
''Mfumokrsisto'' nchini unaotawala na kudhulumu haki za Waislam.
Hii ilikuwa mwaka 2012. Nilikuwa mmojawapo wa Waislam
waliokuwa pale ukumbini kushuhudia kitendo kile cha kihistoria.
Kwa nini nakiita kitendo cha kihistoria kwa kuwa kwa takriban miaka
40 Waislam walikuwa wanasemea pembeni. Wakati ulikuwa umefika
Waislam wakasimama kuitahadharisha serikali kuhusu kujiachia dini
moja ikahodhi fursa zote za nchi kwa hila na Radio Imaan na TV
yake vilikuwapo na Radio Imaan ilirusha hafla ile na mubashara,
yaani ''live.'' Kote Radio Imaan ilikosikika Waislam walimsikia Sheikh
Ilunga akieleza nini Waislam walifanya katika Tanganyika wakati wa
kupigania uhuru kuuondoa dhulma na kuleta haki kwa kila
mwananchi. Hili lilikuwa jambo kubwa na zito kwa serikali yoyote ile
kuwa inashutumiwa kwa kulea udini ndani ya serikali. nchi nyingi
Afrika zimeangamia kwa ugonjwa huu. Vyombo vyote vya habari
ukitoa vile vya Kiislam viligoma kabisa kuitaarifu jamii kuhusu
kongamano hili la Waislam. Ikawa kama vile hapajapatapo kutokea
kitu chochote. Kuanzia siku ile Sheikh Ilunga alitembea nchi nzima
na kufanya mikutano ya hadhara kuitahadharisha kwanza serikali
kuhusu Mfumokristo na pili Waislam ili wajue nini kilikuwa
kinawatafuna.

Profesa Lipumba akisali nje baada ya kukosa sehemu ya kusali ndani ya msikiti
Mohamed Said anaelezea alivyomjua Ustaadh Ilunga
Nilimfahamu vipi Sheikh Ilunga Hassan Kapungu? Nilianza kuzisikia
sifa zake katika miaka ya 1980 kabla sijauona uso wake. Wkati ule
Sheikh Ilunga alikuwa kijana mdogo sana na mdogo kwangu kwa
miaka kadhaa. Wakati naingia kusoma Chuo Kikuu Cha Dar es
Salaam Ilunga alikuwa maarufu pale chuoni msikiti wa Muslim
Students Association of the University of Dar es Salaam (MSAUD)
kiasi unaweza ukadhani kuwa na yeye ni mwanafunzi. Ilikuwa Ilunga
na wenzake ndiyo walioleta ''documents'' za Mzee Bilali Rehani
Waikela MSAUD. Hizi ''documents'' zilikuwa zimefichwa Tabora kwa
karibu miaka 20. Katika ''documents hizi,'' kulikuwa na kisa kizima
cha kile kilichokuja kujulikana kama ''Mgogoro wa East African
Muslim Welfare Society (EAMWS),'' Ndani ya jalada lililofikishwa
MSAUD kulikuwa na ''minutes,'' za mikutano ya EAMWS, taarifa ya
Kamati ya Upatanishi iliyokuwa inajaribu kupatanisha kati ya kundi
la Adam Nasibu na wenzake waliokuwa wanaipiga vita EAMWS,
kulikuwa na ''cuttings'' ya magazeti ya ''Uhuru,'' ''Nationalists'' na
''Tanganyika Standard,'' magazeti makubwa ya zama zile yaliyokuwa
yakifuatilia kwa karibu sana mgogoro ule. Nyaraka hizi za Mzee Bilal
Rehani Waikela zilikuwa hazina kubwa. Kutokana na nyaraka hizi
ndipo ukweli wa nini na nani alikuwa nyuma ya kuvunjwa EAMWS na
kuundwa kwa BAKWATA. Lakini kubwa zaidi waliokabidhiwa
Nyaraka za Waikela walizileta zikiwa na maelezo ili maelezo yale
yaenda na kile kitakachosomwa ndani ya jalada. Ilunga alikuwa
kijana wa Mzee Waikela. Katika hali ya unyonge sana walikuwa
wakiendesha shule ya Nujum katika juhudi za Waislam kujitoa katika
dhulma ya elimu. Mzee Waikela alimsomesha vyema Ilunga kuhusu
fitna na chuki ya Nyerere kwa Uislam na Waislam na mbinu
zinazotumika kuudhalilisha Uislam. Bilali Rehani Waikela alikuwa
mmoja wa waasisi wa TANU Western Province mwaka wa 1955 na
ni yeye na wenzake ndiyo waliomleta Nyerere Nyerere na Bi. Titi
Mohamed kuja kuitia nguvu TANU Western Province. Mzee Waikela
vilevile alikuwa Katibu wa EAMWS Western Province. Mzee Waikela
alikuwa mfano na kigezo kikubwa kwa Ilunga katika maisha yake ya
kuwatumikia Waislam.
msikiti ulijaa hadi nje wakati wa Sala ya jeneza




 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU