Facebook Comments Box

Saturday, August 17, 2013

VIDEO: LADY JAY DEE - YAHAYA




HII NDIO YANGA: YAIPIGA AZAM NA KUCHUKUA NGAO YA JAMII

BAO pekee la kiungo Salum Abdul Telela jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeipa Yanga SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC na kutwaa Ngao ya Jamii. 
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Oden Mbaga, aliyesaidiwa na Hamisi Chang’walu na Omar Kambangwa wote wa Dar es Salaam, hadi mapumziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Yanga ilipata bao hilo mapema tu dakika ya pili, mfungaji kiungo Salum Abdula Telela aliyeunganisha pasi ya Didier Kavumbangu.
John Bocco wa Azam akienda chini baada ya kuchezewa rafu na Nadir Haroub 'Cannavaro' wa Yanga kushoto. Mwingine kulia ni Haruna Niyonzima.

Baada ya bao hilo, Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Azam na kipa Aishi Manula alifanya kazi ya ziada kuokoa.
Dakika ya 11, Yanga ilipata pigo baada ya beki wake Kevin Yondan kuumia kufuatia kugongana na mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco ‘Aedebayor’. Yondan alitibiwa kwa dakika nne, lakini akashindwa kurejea uwanjani na nafasi yake ikachukuliwa na Mbuyu Twite dakika ya 15.
Dakika tano baadaye Yanga ikapata pigo lingine baada ya kipa wake, Ally Mustafa ‘Barthez’ kuumia kufuatia kugongana na Kipre Tchetche.
Barthez ‘alijitoa muhanga’ kuutokea mpira miguuni mwa mshambuliaji huyo wa Ivory Coast baada ya kuwatoka mabeki wake, Juma Abdul na Nadir Haroub ‘Cannavaro’- hivyo kugongwa kifuani na mguu wa Kipre.
Salum Telela kushoto akikimbia na Jerry Tegete baada ya kufunga. Mwingine kushoto ni Haruna Niyonzima 

Barthez alitibiwa kwa dakika nne kabla ya kumpisha Deo Munishi ‘Dida’.  Azam waliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Yanga na dakika ya 30 Kipre Tchetche alifumua shuti kali likagonga mwamba na kutoka nje akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi ya Bocco.   
Aishi Manula alikuwa majaribuni tena dakika ya 30 baada ya krosi maridadi ya Simon Msuva kumponyoka kabla ya kuondoshwa hatarini na Erasto Nyoni.
Dakika ya 38 Dida alidaka shuti kali la mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita Kipre Tchetche kutoka umbali wa mita 17 na kupigiwa makofi na mashabiki.
Kipindi cha pili, Yanga SC waliendelea kucheza vizuri na kukosa mabao zaidi, huku sifa zaidi akistahili kipa chipukizi Aishi Manula.
Dakika ya 67 Telela alikarbia kufunga tena baada ya kuunganishia nje krosi nzuri ya Haruna Niyonzima.
Dakika ya 81 Niyonzima alikaribia kufunga mwenyewe kwa mpira wa adhabu, lakini shuti lake liligonga mwamba wa juu na kudondokea chini kabla ya beki Aggrey Morris kuondosha katika hatari.  
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’/Deo Munishi ‘Dida’ dk15, Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan/Mbuyu Twite dk15, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Salum Telela, Jerry Tegete/Hussein Javu68, Didier Kavumbangu na Haruna Niyonzima. 
Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni/Joackins Atudo dk46, Waziri Salum, David Mwantika, Aggrey Morris, Himid Mao, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’/Gaudence Mwaikimba dk74, Kipre Balou/Ibrahim Mwaipopo dk62 na Khamis Mcha
CHANZO: BIN ZUBEIRY

WANANCHI WAMZUI WAZIRI MKUU ASIONDOKE


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameonja joto baada ya wananchi wa maeneo ya Mloganzira na Kwembe Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kulala barabarani kama njia ya kushikiniza kutekelezewa madai yao. Pinda alikwenda Kwembe kutuliza mgogoro uliotokana na wananchi kudai fidia za viwanja vyao vilivyochukuliwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili (MUHAS), ambapo majengo ya kisasa yanatarajiwa kujengwa katika eneo hilo. 
Chuo hicho kinatarajiwa kujengwa mpakani katika eneo hilo la mpakani kati ya Mlogazira (Pwani) na eneo la Kwembe lililopo Wilaya ya Kiondoni Mkoa wa Dar es Salaam. 
Mbali na Pinda viongozi wengine waliokumbwa na dhahama hiyo ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ambaye alikuwa ameandamana na maofisa kutoka MUHAS.
Licha ya askari polisi kufanya kazi kubwa ya kutuliza ghasia lakini juhudi hizo ziligonga mwamba kutokana na wananchi hao kuendelea kukaa na wengine kulala barabarani.Pinda ambaye alifika katika eneo hilo saa saba mchana alikuta viongozi kadhaa waliotangulia katika eneo hilo wamezuiwa na wananchi hao ambao walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali.Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alijaribu kuwasihi wakazi hao wapishe viongozi lakini waligoma kuondoka wakipaza sauti za kumtaka waziri mkuu.Hali hiyo ilimlazimu Pinda kushuka katika gari na kuwahisi wananchi hao waende katika eneo la mkutano ili kuweza kuzungumza kero zao badala ya kulala barabarani.Kauli hiyo ya Pinda ilionyesha kushusha jazba za wananchi hao ambao waliamua kutii ushauri huo na kwenda katika eneo la mkutano.Akizungumza katika mkutano huo, mjumbe wa kamati ya madai Frederick Chole, alisema jumla ya wakazi 2,335 walipewa fidia ya awali lakini haikukidhi mahitaji huku watu 93 wakiwa hawajalipwa fedha zao. 
“Tuliweza kwenda Ofisi ya waziri ya ardhi na kupewa mchanganuo ambao ulikuwa unaeleza juu ya fidia ya ardhi na mazao yote yalipo juu ya mashamba na nyumba lakini wakati wa malipo tulikwazwa na malipo kiduchu,” alisema Chole. 
“Zoezi zima la ulipaji fidia katika eneo hili lilizungukwa na uchakachuaji katika ofisi ya Manispaa ya Kinondoni na MUHAS (Chuo cha Afya Muimbili),” alisema Chole. 
Naye Abasi Tamimu, alimtaka waziri mkuu kuangalia suala hilo kwa kina kwani wananchi wa maeneo hayo wamegeuzwa kafara katika mradi huo. 
Akijibu hoja hizo waziri mkuu Pinda, alisema kuwa Serikali imesikia kilio chao hivyo itaanza kulipa fidia kwa kuwalipa watu 93 ambao hapo awali walikuwa hawajalipwa. 
“Tutawalipa hawa wasiopewa chochote kwanza na nyie mliolipwa Serikali haiwezi kuwafidia mara mbili labda tuangalie utaratibu wakulifanyia kazi ombi lenu hilo la kupewa viwanja hivyo ngoja nikae na watendaji wangu kisha nitawaletea jibu,”alisema Pinda. 
Aliongeza kuwa katika hilo serikali itamua kutumia ubinadamu hili kuweza kupunguza matatizo ya wakazi hao na kuhahidi kushughulikia madai ya uchakachuzi wa fedha kwa wale wote wenye vielelezo. 
Hata hivyo wananchi hao waliridhishwa na majibu ya waziri mkuu, wakisema kuwa hawana jambo jingine zaidi ya kusibiri utekelezaji wa kauli ya Pinda kwa kuwa ni kiongizi wa juu serikalini. 
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick.


SWALI LA MASANJA KWA VODAKOMU




YANGA KUWEKA REKODI LEO IKIIFUNGA AZAM NA KUIPOTEZEA MBALI SIMBA


YANGA SC itaweka rekodi ya kuwa timu iliyotwaa mara nyingi zaidi Ngao ya Jamii, iwapo itaifunga Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- hivyo kuwapiku wapinzani wao wa jadi, Simba SC. Hadi sasa, vigogo hao wa soka nchini, kila mmoja ametwaa Ngao mara mbili, wakati timu nyingine zaidi ya hizo iliyowahi kutwaa ubao huo ni Mtibwa Sugar ya Morogoro. Yanga SC ndio washindi wa kwanza wa Ngao mwaka 2001 walipoifunga mabao 2-1 Simba SC, enzi hizo Ligi Kuu inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager. 
Baada ya hapo, haikuchezwa tena mechi ya Ngao hadi mwaka 2009 wakati Mtibwa Sugar ilipoilaza 1-0 Yanga SC.
Mwaka 2010 Yanga walirejesha Ngao kwenye himaya yao, baada ya kuwachapa tena wapinzani wa jadi, Simba kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.
Simba SC walitwaa mara mbili mfululizo Ngao na kufikia rekodi ya watani, kwanza 2011 walipoifunga 2-0 Yanga na mwaka jana walipotoka nyuma kwa 2-0 na kuilaza Azam 3-2.
Katika mchezo wa leo, Kocha Mholanzi, Ernie Brandts atamkosa mshambuliaji wake Mrisho Khalfan Ngassa ambaye amefungiwa mechi sita na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kamati hiyo baada ya kupitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom jana, ilimuidhinisha Ngassa kuchezea Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngassa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.


Kwa sababu hiyo, Simon Msuva anaweza kurejea uwanjani leo katika nafasi ya Ngassa, huku wachezaji wapya wanaotarajiwa kucheza leo Yanga sana ni Hussein Javu.
Kocha Muingereza wa Azam, Stewart John Hall atatakiwa kutorudia makosa mawili makuu aliyoyafanya msimu uliopita hata yakachangia kumkosesha ubingwa.
Alifungwa na Yanga SC 1-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu kwa sababu siku hiyo alimjaribu kiungo Kipre Michael Balou katika beki ya kulia, badala ya kupanga beki halisi.
Akafungwa na Simba SC katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu pia msimu uliopita kwa kosa la kujaribu mfumo ambao wachezaji hawakuwa wamuelewa vyema na hizo ndizo pointi sita zilizowapa Yanga ubingwa.
Burudani inatarajiwa kuwa nzuri katika mchezo leo, kutokana na ukweli kwamba pande zote zina mafundi na wataonyeshana kazi uwanjani.
Upande wa Azam, langoni anaweza kusimama Aishi Manula badala ya Mwadini Ally, kulia Erasto Nyoni, kushoto Waziri Salum na katikati Aggrey Morris na Joackins Atudo. Himid Mao anaweza kuanza katika kiungo cha chini badala ya Balou na juu yake bila shaka atacheza Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Kulia anaweza kucheza Kipre Tchetche, kushoto Khamis Mcha ‘Vialli’ na John Bocco ‘Adebayor’ akaanza katika ushambuliaji na Ibrahim Mwaipopo.
Gaudence Mwaikimba ni mchezaji anayetarajiwa sana kutokea benchi leo kipindi cha pili kuja kujaribu kuisulubu timu yake ya zamani, Yanga SC.
Yanga SC hapana shaka Ally Mustafa ‘Barthez’ ataendelea kusimama langoni, Juma Abdul atacheza kulia badala ya Mbuyu Twite, kushoto David Luhende badala ya Oscar Joshua, katikati kama kawaida Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’- Athumani Iddi ‘Chuji’ ataanza badala ya majeruhi Frank Domayo na juu yake anaweza kucheza Haruna Niyonzima.
Kwa kuwa washambuliai ni wengi kwa sasa Yanga, kiungo kulia na kushoto wanaweza kuenea wao tu. Kulia anaweza kucheza Simon Msuva na kushoto Hamisi Kiiza, wakati washambuliaji wanaweza kuanza Didier Kavumbangu na Jerry Tegete, Javu akianzia benchi. 

MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
Mwaka Mshindi            Matokeo     
2001: Yanga SC 2-1 Simba
2009: Mtibwa Sugar 1-0 Yanga SC
2010: Yanga SC 0-0 Simba (3-1penalti)
2011: Simba SC   2-0 Yanga
2012: Simba SC 3-2 Azam FC

CHANZO: BIN ZUBEIRY 

ABAKWA, ATOBOLEWA MACHO NA KUINGIZWA VITU SEHEMU ZA SIRI

Picture
Mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 30 amekutwa amekufa katika makaburi ya Majengo katika soko la mjini Kahama mkoani Shinyanga huku mwili wake ukiwa ametobolewa macho na kuonesha kupigwa na kitu kizito usoni.

Mwanamke huyo ambaye hajatambulika jina lake wala anakotoka, alikuwa amevaa blauzi nyeusi yenye madoa meupe, viatu vyenye urembo wa rangi ya fedha, ni mnene kiasi, mweusi na mwenye nywele ndefu.

Mwili wa Mwanamke huyo amegunguliwa leo majira ya saa sita mchana baada ya watu waliokuwa wanachimba kaburi kuuona mwili huo pembeni ya eneo hilo na kutoa taarifa kwa Polisi.

Majirani wanaoishi eneo la makaburi hayo wanahisi unyama huo umefanyika usiku wa kuamkia jana huku, baadhi ya akina mama wakikiri kusikia sauti ya mwanamke akipiga yowe katika eneo la mnadani.

Jeshi la Polisi wilayani Kahama limethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku mrakibu msaidizi wa Polisi Aziz Mayunga akitoa wito kwa wananchi kufika katika chumba cha kuhifadhia maiti ili kuutambua mwili huo.

--- kitongoni blog haina ujasiri wa kuweka picha za marehemu ila kwa anayetaka kuziona tafadhali bofya  hapa uende mwenyewe kwenye chanzo cha taarifa hii blogu ya Bundala William Kijukuu cha Bibi "KJ" kuzitizama!


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU