Facebook Comments Box

Sunday, August 11, 2013

TAMKO LA UMOJA WA WANAZUONI WA KIISLAM TANZANIA KUHUSU TUKIO LA SHEIKH PONDA

Sheikh Suleiman Amran Kilemile
TAMKO LA UMOJA WA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA KUHUSU TUKIO LA SHEIKH PONDA

Sisi, Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay – atul Ulamaa), tumepokea kwa masikitiko makubwa habari za kushambuliwa na kujeruhiwa kwa silaha za moto, Sheikh Ponda Isa Ponda, huko Morogoro, Jumamosi Agosti 10, 2013.

Hay-atul Ulamaa, imesitushwa na tukio hili linalo uma na linaloumiza na kuleta mshtuko na fazaa katika jamii kama ilivyoshtushwa na matukio mengine kama hili hapa nchini. Hili ni tukio ambalo linaashiria kuwa walio litenda hawaitakii mema na amani nchi yetu.

Tunalaani vikali kitendo hicho na tunaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua hatua kali na za haraka dhidi ya wale wote walio husika katika tukio hili lenye kuumiza nyoyo za wengi.

Aidha tunawasihi Waislamu na jamii kwa ujumla kuwa watulivu, wenye subira na wenye kunyenyekea kwa Mola wao katika jambo hili zito, wakati tunasubiri vyombo vya dola vichukue hatua zinazo stahiki dhidi ya wahusika wa tukio hili.

Tunamuombea Sheikh Ponda Isa Ponda Allah Amponye haraka na Am,pe baraka katika umri wake. Amin

Sheikh Suleiman Amran Kilemile

Mwenyekiti

Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.

11/August/2013


TAARIFA YA JESHI LA POLISI KUHUSU SHEIKH PONDA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI



AGOSTI 10, 2013.
JESHI LA POLISI TANZANIA
DAR ES SALAAM 
1.  MNAMO TAREHE 10, AGOSTI ,2013 MAJIRA YA SAA 8 MCHANA, MAENEO YA SHULE YA MSINGI KIWANJA CHA NDEGE MANISPAA YA MOROGORO, KULIFANYIKA KONGAMANO LA BARAZA LA EID LILILOANDALIWA NA UMOJA WA WAHADHILI MKOANI MOROGORO. DAKIKA KUMI KABLA YA KONGAMANO HILO KUMALIZIKA  ALIFIKA SHEKHE PONDA ISSA PONDA AMBAYE ALIZUNGUMZA KWA MUDA MFUPI.

2. KONGAMANO HILO LILIFUNGWA  MAJIRA YA SAA 12:05 JIONI AMBAPO WATU WALIANZA KUTAWANYIKA, BAADHI YAO WAKIWA WAMEZINGIRA GARI DOGO ALILOKUWA AMEPANDA SHEKHE PONDA. BAADA YA KUTOKA KATIKA  ENEO HILO, ASKARI WA JESHI LA POLISI WALIZUIA GARI HILO KWA MBELE KWA NIA YA KUTAKA 
KUMKAMATA SHEKHE PONDA AMBAYE MPAKA SASA ANATUHUMIWA KWA KOSA LA KUTOA MANENO YA UCHOCHEZI SEHEMU MBALIMBALI HAPA NCHINI YENYE MLENGO WA KUSABABISHA UVUNJIVU WA AMANI.

3. BAAADA YA ASKARI KUTAKA KUMKAMATA, WAFUASI WAKE WALIZUIA UKAMATAJI HUO KWA KUWARUSHIA  MAWE ASKARI.  KUFUATIA PURUKUSHANI HIYO, ASKARI WALIPIGA RISASI HEWANI KAMA ONYO LA KUWATAWANYA.

4. KATIKA VURUGU HIZO, WAFUASI HAO WALIFANIKIWA KUMTOROSHA MTUHUMIWA.  HIVI SASA IMETHIBITIKA KUWA SHEKHE PONDA YUKO KATIKA HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI AKITIBIWA JERAHA KATIKA BEGA LA MKONO WA KULIA LINALODAIWA ALILIPATA KATIKA PURUKUSHANI HIZO.

5. KUFUATIA TUKIO HILO, TIMU INAYOSHIRIKISHA WAJUMBE KUTOKA JUKWAA LA HAKI JINAI IKIONGOZWA NA KAMISHINA WA JESHI LA POLISI  CP ISSAYA MNGULU IMEANZA KUFANYA UCHUNGUZI WA TUKIO HILO.

6. AIDHA, JESHI LA POLISI LINATOA  WITO KWA  WANANCHI KUWA WATULIVU WAKATI SUALA HILI LINASHUGHULIKIWA KISHERIA.

Imetolewa na:-
Advera Senso- SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.


VIDEO: SHEIKH PONDA AKIPOKELEWA MUHIMBILI (MOI) LEO




YANGA WAITANDIKA SC VILLA 4 KWA 1 TAIFA LEO

Mrisho  Khalfan Ngassa

YANGA SC imetuma salamu Johannesrbug, Afrika Kusini ambako Azam FC wameweka kambi kujiandaa na msimu mpya- kufuatia ushindi wa mabao 4-1 leo katika mchezo wa kirafiki dhidi SC Villa ya Uganda, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga na Azam zitamenyana Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa, katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, kuashiria ujio wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Azam imeweka kambi Afrika Kusini kujiandaa na mechi hiyo ya kufungua msimu na Yanga wanaendelea na maandalizi yao Dar es Salaam, wakitarajiwa kuingia kambini baada ya mechi ya leo kisiwani Pemba, au Bagamoyo, Pwani.

 
Washabiki wa Yanga wakishangilia goli lao la pili
Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa 3-1, mabao yake yakifungwa na Mrisho Ngassa dakika ya saba, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 27 na Didier Kavumbangu dakika ya 30, wakati la nne lilifungwa kipindi cha pili na Haruna Niyonzima dakika ya 62.
Bao la kufutia machozi la Villa ambayo jana ilifungwa 4-1 pia na Simba Uwanja huo huo wa Taifa, lilifungwa na Moses Ndaula dakika ya 18.  
Katika mechi zake za awali za kujiandaa na msimu, Yanga SC ilitoa sare ya 2-2 na URA ya Uganda kabla ya kuzifunga 3-1 Mtibwa Sugar na 3Pillars ya Nigeria 1-0.
Azam nayo imekwishacheza mechi tatu za kujipima nguvu Afrika Kusini, imeshinda moja tu dhidi ya Mamelodi Sundwons 1-0, imefungwa mbili, 3-0 na Kaizer Chiefs na 2-1 na Orlando Pirates na kesho itacheza mechi ya mwisho na Moroka Swallows kabla ya kurejea nyumbani keshokutwa.
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, David Luhende/Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan/Rajab Zahir, Athumani Iddi ‘Chuji’/Bakari Masoud, Mrisho Ngassa, Salum Telela, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete/Hussein Javu na Haruna Niyonzima/Said Bahanuzi.


TAARIFA YA KIKAO MSIKITI WA MTAMBANI LEO KUELEZEA HALI YA SHEIKH PONDA

Amir Kundecha
 
Bismillahir Rahmanir Rahiim 
TAARIFA
Taarifa rasmi kuhusu hali ya Sheikh Issa Ponda itatolewa leo (Jumapili) Al'asiri msikiti wa mtambani, jijini Dar-es-salaam. Pamoja na taarifa hiyo, Amiri wa Baraza Kuu, Sheikh Mussa Kundecha atazungumza na vyombo vya habari Insha-Allah muda na mahali hapo hapo.

Wabillah Taufiiq
11 Agosti, 2013


SERIKALI YADHIBITI UAGIZAJI NA USAMBAZAJI WA TINDIKALI

Kutokana na kukithiri kwa matukio ya uhalifu kwa kutumia tindikali, Serikali imeamua kudhibiti uingizaji, usambazaji na uuzaji wa rejareja wa tindikali zinazotumika viwandani, katika maabara na vyombo vya usafiri.

Kwa kuanzia, wameanza kutoa leseni maalumu kwa watumiaji halali kwa kuwasajili katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali huku wakipeleka mrejesho wa mauzo katika ofisi hiyo kila mwezi.

Hayo yalisemwa jana na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manywele alipozungumza na waandishi wa habari akiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi.

Alisema kwa kuanzia, vibali vya kuagiza kemikali hizo lazima kuombwa upya ili kusimamia na kudhibiti huku takwimu za mauzo na jina la mnunuzi, tarehe aliyonunua, kiasi na ukali wa tindikali vikioneshwa.

Alisema taarifa hizo zitakuwa zikitumwa kwa Mkemia Mkuu kila mwezi kuanzia mwezi huu huku wauzaji wa rejareja wakipewa miezi mitatu kujisajili kwenye ofisi hizo: "Pia wauzaji wanatakiwa kuwa na kumbukumbu za mauzo na alizonunua, namba ya leseni, kiasi na
tarehe huku watumiaji katika vyombo vya usafiri wakitakiwa watoe malipo ya huduma kwani hawatatakiwa kununua na kuondoka na tindikali," alisema Manywele.

Aliongeza kuwa huduma hizo zitatolewa kwa wauzaji wa rejareja waliosajiliwa ambapo tindikali zitakuwa katika ujazo wa lita tano na kuendelea na kuanzia sasa hairuhusiwi kuuzwa chini ya ujazo huo.

Mkemia huyo alisisitiza kuwa wanajiandaa kuongeza uelewa kwa wauzaji wa tindikali nchini  huku wakitarajia kuanzisha kituo maalumu cha kuratibu matumizi ya sumu.

"Katika kituo hicho tutahakikisha taarifa zinapelekwa kwa Mkemia haraka na kufanyiwa uchunguzi haraka ili kuhakikisha tunakabiliana na majanga haya ya matumizi mabaya ya tindikali," alisema.

Mwema alisema katika kudhibiti tindikali kutumika kama silaha, itatumika sheria  iliyopo kudhibiti aina hiyo mpya ya uhalifu na kutaka wananchi kusaidia kutoa taarifa mapema ili kupata ushahidi.

Alisema kwa kutumia mikakati iliyopo ya ofisi ya Mkemia Mkuu, aliagiza makamanda wote mikoani kufuatilia waagizaji, wasambazaji, wauzaji wa rejareja na watumiaji kwa kushirikiana na jamii ili kutokomeza uhalifu huo.

Feleshi alisema changamoto iliyopo katika kukabiliana na uhalifu huo mpya ni pamoja na usimamiaji kesi kwa kufuata sheria inayoagiza ushahidi, lakini unakosekana.

Aliomba wananchi kushirikiana na kuacha matumizi ya tindikali kutumika kama ugaidi, kwani kwa sheria ya ugaidi ya mwaka 2002 inategemea jinsi uhalifu wa kigaidi unavyotendeka.

Hivyo aliomba wanajamii kutoa taarifa, kwani si hiari na ikibainika mtu alijua sehemu ya uhalifu na lakini akaficha naye atakuwa sehemu ya uhalifu huo.

Feleshi alisema kwa mujibu wa sheria, wahalifu wa makosa hayo ya tindikali wakibainika iwapo mwathirika ameumizwa kiasi cha kupata ulemavu atahukumiwa kifungo cha maisha jela, na kama mwathirika atakuwa ameumia kidogo basi kifungo kitakuwa ni miaka saba jela. (Taarifa via gazeti la HABARI LEO)


HALI ILIVYOKUWA KATIKA KONGAMANO LA SHEIKH PONDA

 Kutambulishwa jukwaani Shekh Ponda.
 Askari wa FFU wakijisongeza kati kati ya uwanja mara baada ya muda wa kongamano kumalizika.
 Kikosi cha FFU uwanjani
 Shekh Ponda akikaribishwa kwenye jukwaa kuu baada ya kuwasili kwenye viwanja vya shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege , mjini Morogoro
 Shekh Ponda akisalimiana na Mhadhiri wa Mihadhara nchini, Ustaadhi Abubakari
 Shekh Ponda akisisistiza jambo mbele ya waumini wa Dini ya Kiislamu kwenye Kongamano , Augosti 10, mwaka huu mjini Morogoro
 Shekh Ponda akiteta jambo na baadhi ya Viongozi wa umoja wa Wahadhiri wa Dini ya Kiislamu Mkoa wa Morogoro
 Shekhe Ponda akiwa meza kuu kwenye kongamano hilo
 Shekhe Ponda akiwa amezingirwa na waumini
 Umati wa waumini wa Kiislamu wakimsikiliza Shekh Ponda
Waumini wa Dini ya Kiislamu wa mjini Morogoro wakimsikiliza Shekh Ponda
Waumini wa Kiislamu wakitawanyika uwanjani baada ya muda wa kongamano kufikia tamati,


POST YA MH ZITTO KABWE KUHUSU SHEIKH PONDA KUPIGWA RISASI




 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU