INNA LI LAHI WA INNA ILAIHI RAJIUUN
Pichani juu, nahodha John Bocco, Khamis Mcha na Humphrey Mieno wakimpongeza Kipre Tchetche baada ya kufunga goli la tatu
Timu ya Azam FC imezidi kusonga mbele kwenye ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuichapa Tanzania Prisons 3-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Azam FC imepata ushindi huo wa nyumbani huku mshambuliaji wake Kipre Tchetche akijiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa kiatu cha dhahabu kwa kufikisha magoli 12 tofauti na wafungaji wengine kwenye ligi kuu.
Katika mchezo huo Azam FC walipata goli la kwanza katika dakika ya 17 kupitia kwa Kipre Tchteche aliyecheza vizuri crosi iliyopigwa na Khamis Mcha, shuti la Kipre lilimbabatiza kipa wa Prisons David Burhan na kutinga wavuni, matokeo yakawa Azam FC 1-0 Prisons.
Goli hilo lilidumu hadi mapumziko huku Azam FC wakiwa wameutawala mchezo kwa kutengeneza nafasi nyingi dk 23 John Bocco alishindwa kumalizia krosi ya Tchetche na mpira ukatoka nje, dk 34 Tchetche alipiga shuti likatoka nje na kupeleka timu zote mapumziko Azam FC ikiwa mbele kwa 1-0 dhidi ya Prisons.
Kipindi cha pili timu zilirejea uwanjani kwa kasi kila moja ikisaka bao la kumalizia mchezo, Kipre tena alipiga shuti likadakwa na kipa David wa Prisons, Humphrey Mieno naye alipiga shuti likaenda nje, huku Prisons dk 58 Elias Maguli alijaribu kufunga lakini shuti lake likatoka nje.
Wakipata nafasi nyingi na kukosa magoli ya wazi, dk 75 mshambuliaji mahiri wa Azam FC, John Bocco aliandika bao la pili kwa timu yake baada ya kuachia shuti la mbali lililongonga mwamba wa chini na kutinga wavuni, Bocco alibadili matokeo na kuwa Azam FC 2-0 Prisons.
Tchetche alizidi kulisakama lango la Prisons na dakika ya 84 alihitimisha kalamu ya magoli kwa kuandika bao la tatu akimalizia kazi nzuri ya Seif Abdalah ‘Karihe’, na kuipa Azam FC ushindi wa 3-0 dhidi ya TZ Prisons.
Katika mchezo huo Azam FC walifanya mabadiliko dk 65 alitoka Khamis Mcha akaingia Seif Abdalah ‘Karihe’, dk 70 akaingia Abdi Kassim ‘Babi’ kuchukua nafasi ya Humphrey Mieno na dk 73 Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alipumzika nafasi yake ikachukuliwa na Ibrahim Mwaipopo, mabadiliko hayo yaliimarisha kikosi hicho na kucheza kandanda safi muda wote wa mchezo.
Prisons waliwatoa Nurdin Iss na Aziz Sibo nafasi zao zikachukuliwa na Peter Kazengele na Henry Mwalugala, mabadiliko yaliimarisha safu ya ushambuliaji lakini hayakuweza kubadilisha matokeo ya mchezo huo na kuicha Azam FC kupata ushindi huo mnono wa 3-0.
Kocha msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala amefurahishwa na matokeo hayo na kiwango cha timu yake, amesema kilichopo sasa ni kuhakikisha hawapotezi hata mechi moja katika michezo iliyobaki ya ligi kuu.
Azam FC kesho itaingia kambini kwa maandalizi ya kucheza dhidi ya Ruvu Shooting, mechi itakayopigwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Azam FC, Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, Luckson Kakolaki, Jockins Atudo, Michael Bolou, Tchetche Kipre, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Ibrahim Mwaipopo 73’, John Bocco, Khamis Mcha/Seif Abdalah ‘Karihe’ 65’ na Humphrey Mieno/Abdi Kassim ‘Babi’ 70’.
SOURCE:AZAMFC.CO.TZ