Facebook Comments Box

Tuesday, May 7, 2013

RUGE HAJAJIBU SHUTUMA ZA LADY JAY DEE

 
Imewasilishwa na Jacob Buberwa --

Boss wa Clouds FM  Bw. Ruge Mutahaba katika maamuzi ya "hasira za mkizi" kashindwa kujibu shutuma za comando Lady Jay Dee

Wasanii amkeni kujua nani mchawi wa kazi zenu

Watanzania tulimsikiliza mkurugenzi wa utafiti wa redio Clouds FM Bw. Ruge Mutahaba katika mahojiano na redio yake ya Clouds FM, mahojiano ambayo tulikua tukitegemea boss Ruge ajibu shutuma dhidi yake za kumtilia kauzibe katika kupata riziki mwanamuziki Lady Jay Dee bint machozi.

Katika mahojiano hayo ambayo sisi wasikilizaji tunayafananisha sawa na "Kesi ya Nyani na mwamuzi awe Ngedere", tulichokua tunakitegemea ni majibu ya shutuma lakini cha kushangaza Ruge kashindwa kabisa kujibu shutuma zinazomkabili, baadala yake akawa anarusha maneno na kuhusisha mifano ya wasanii walioshuka na kupanda.

Ruge alikwenda nje ya hoja ya msingi na mwisho wa mahojiano alikurupuka kwa kauli za kuamrisha kuwa ni maarufu kupiga nyimbo za kizazi kipya (Bongo Fleva) kwa muda wa siku nzima katika kituo cha Clouds FM.

Watanzania tunajiuliza, hivi redio ya Clouds FM au Redio ya Ruge na wasanii pamoja na sisi wananchi nani ni muhimu?

Kwa karne hii ambayo Taifa lina vituo vya redio zaidi ya 80?

Kwani wasanii wanamuhitaji sana Ruge na mshirika wake Bw. Kusaga, yaani wao ndiyo tuseme miungu ya wasanii?

Wananchi walio wengi wanamuunga mkono Lady Jay Dee kwa kutokukubali afanywe ngazi au kitendea kazi cha kuwanufaisha wanyonyaji katika soko la muziki, na kaamua kujitegemea. Maamuzi hayo ya Jay Dee ndiyo yanamfanya Jide atake kugeuzwa  "Kondoo wa Sadaka."

MRADI WA RUGE MUTAHABWA KATIKA SEKTA HII YA MUZIKI NI KUUA MUZIKI WA DANSI NA TAARABU NA KUJENGA MSINGI WA UTAMADUNI NA MZIKI WA KIZAZI KIPYA.

Ukisikiliza sana maelezo ya Ruge katika mahojiano utagundua wazi kuwa alijenga au alijaribu kujenga mtandao wa
kuwamiliki na kuwajenga wanamuziki wa kizazi kipya kwa manufaa yake, yaani mwanamuziki asipoingizwa katika
mtandao huu basi hatojulikana na kazi zake hazitotambulika.

Mtandao ambao pia unampendekeza msanii gani
akubalike kupewa tuzo hata kama si msanii mzuri.

Mtandao huu pia unatumika kama sururu la kuuchimbia kaburi
muziki wa dansi na muziki wa taarabu.

Mtandao huu pia unawalazimisha Watanzania walio wengi muziki gani wa kusikiliza, na mara nyingine kuwalazimisha wanamuziki nini cha kupiga (beat) n.k.

Leo Ruge anamsema Lady Jay Dee ampe kijiti mwingine. Lady Jay Dee alisema atapiga muziki kwa maisha yake na kuwaridhisha washabiki wake. Hakuna haja ya kupokezana vijiti katika gemu la muziki. Mfumo huu kupokezana vijiti ni mfumo unaoitwa "Ruge Mtahaba System" na wasananii wameshaushitukia kuwa si mfumo mzuri.

Je, wanamuziki wapo tayari kufanywa kete za kuchezea bao au chess?

Lazima wasanii wapate pumzi ya uhai kutoka katika mtandao wa Ruge?

Hivi wasanii hawezi kusimama kidete na kuungana kwa pamoja wakajipigania na kukataa kufanya wapagazi katika sekta hii?

Ruge kaonyesha kiburi kwa kusema muziki wa bongo flava usipigwe kwa siku nzima redioni Clouds, sasa wasanii na ninyi onyesheni mshikamano na msimamo wenu dhidi ya Ruge, kuwa nanyi ni muhimu kwa jamii ya Watanzania.

Je, nani mchawi wa kazi za wasanii na muziki wa Tanzania?

Watanzania na serikali ya Tanzania imeshuhudia kuangushwa kwa makusudi muziki wa dansi wa Tanzania na kuchimbiwa kaburi utamaduni na sanaa za maonyesho wa Watanzania, hujuma ambazo zinafanywa na mtandao ya siri ya wajanja wanaohujumu utamaduni na muziki wa Watanzania. Wanamtandao ambao wanaangaliwa macho bila ya kufanywa chochote na Watanzania au kuchukuliwa hatua zozote
na Serikali kupitia idara husika.

Leo Watanzania tunajiuliza, hivi hawa akina Ruge Mutahaba wanaijua historia, misingi ya
miziki ya Tanzania, na wale waliojitoa muhanga katika kujenga misingi hiyo imara? Mbona nchi za wenzetu
wanaendeleza misingi na miziki yao ya awali? Inakuwaje leo  baadhi ya wajanja wasiojua hata historia ya muziki wa Tanzania watuchagulia nini cha kusikiliza?

 "JOTO HASIRA"  KUNA HAJA YA KUWAFUKUZA KAZI NA KUVUNJA MTANDAO HUU UNAOHUJUMU UTAMADUNI, MUZIKI NA WASANII WATANZANIA!
 
SOURSE:WAVUTI


JINSI BILIONI 876 ZITAKAVYOTATUA FOLENI ZA DAR ES SALAAM

 
SERIKALI imesema   inatekeleza miradi ya kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam yenye thamani ya sh. bilioni 876.336   katika barabara ya Al Hassan Mwinyi ambapo watumiaji wa barabara hiyo hutumia takribani saa moja na nusu kufika Osterbay polisi hadi daraja la Selander hususani mida ya asubuhi saa moja hadi saa tatu.

Hayo  yalisemwa jana Bungeni na  Naibu Waziri wa Ujenzi   Gerson  Lwenge Naibu  wakati    akijibu swali  Mbunge  wa Jimbo la  Temeke  Abasi Zuberi Mtemvu  lililouliza kuwa  Je, Serikali inaweza kutoa ufafanuzi juu ya ufumbuzi wa tatizo la msongamano huo?

Alisema   kuwa  inayolenga kutatua tatizo hilo ,ikiwemo miradi ya kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo ambayo ni  kama ifuatavyo;

Barabara ya Kimara –Kivukoni (Fire), Fire-Kariakoo na Magomeni –Morocco (Sh.  bilioni 240), Karakana na vituo vya mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) pamoja na kuhamisha nguzo za umeme (Sh. bilioni 47.90).

Nyingine ni  Barabara ya Mwenge – Tegeta(sh.  bilioni 88.00), Barabara ya Kilwa (Kilwa Road) Bendera Tatu-Mbagala Rangi Tatu, (Sh.  bilioni 35.16), Daraja la Kigamboni (sh. 214.64). Flyover ya TAZARA, Serikali ya Japani imetoa msaada wa fedha kwa ajili ya usanifu.

Barabara ya Gerezani (Bendera –Tatu-KAMATA), Serikali ya Japani imetoa  msaada wa fedha kwa  ajili ya ujenzi.

Barabara ya Mandela (Sh. bilioni 61.25) na barabara ya  Wazo Hill –Bagamoyo-Msata (Sh. bilioni 89.61).

Waziri  huyo  alisema  ujenzi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) kutoka Morocco kwenda Magomeni hadi Kivukoni na Kimara yatapunguza msongamano wa magari kati ya Oysterbay Polisi na Daraja la Selander.

Aliongeza kuwa katika mipango ya baadae, Serikali itaangalia uwezekano na kujenga barabara ya juu  (viaduct) pande zote za daraja, kujenga daraja lingine pembeni mwa daraja la Selander au kujenga njia mbadala (Selander Bridge Bypass) kutokea Kenyatta Drive kuunganisha na Ocean Road.



TCU YAIFUNGIA KIU KUTOA SHAHADA YA UZAMILI NA SHAHADA YA UZAMIFU



 
Tume ya VyuoVikuu Tanzania (TCU) hivi punde imekitaka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) kusimamisha mara moja kufundisha au kutoa mafunzo ya Shahada ya Juu (Postgraduate), Shahada ya Uzamili (Masters) na Shahada za Uzamivu (PhD) katika kampasi ya Dar es Salaam, Tanzania.
KIU imeamriwa kusimamisha kutoa shahada hizo kuanzia LEO hawana wahadhiri wa kutosha wenye sifa stahili jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.
Taarifa imetolewa na Katibu Mtendaji wa TCU, pia KIU imeamriwa kuzungumza na kushirikiana vizuri na wanafunzi wote waliodahiliwa katika kozi zilizotajwa hapo juu ili wahamie kwenye  vyuo  vingine vyenye  idhibati ya kutoa  mafunzo  hayo.
“Tume haitatambua shahada yeyote ya uzamili au uzamivu itakayotolewa na chuo hicho ambao watasoma katika kampasi ya Dar es Salaam, Tanzania.
“Chuo cha KIU Kampasi ya Dar es Salaam kina ithibati na kitaendelea kutoa mafunzo ya shahada ya kwanza (Bachelors), Diploma au vyeti zilizopitishwa na TCU kwa mujibu wa Ithibati husika tuu,” imesema sehemu ya taarifa iliotolewa na Katibu Mtendaji wa TCU.
Uamuzi huo umefikiwa  na tume hiyo katika mkutano wake wa hivi karibuni uliofanyika jijini Dar es Salaam.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU