Facebook Comments Box

Wednesday, February 27, 2013

KIWANDA CHA NGUO CHA MAZAVA CHANUSURIKA KUUNGUA KWA MOTO


Picture
Suma na Asha wakiwa hoi baada ya kufikishwa wodi namba 3 hospitali ya mkoa wa Morogoro (picha: Dunstan Shekidele)
Imeripotiwa kuwa Kiwanda cha nguo cha Mazava kinachomilikiwa na wawekezaji kutonga  nje ya nchi, kilichopo Msamvu mkoani Morogoro kimepata hitilafu ya umeme majira ya saa nne wafanyakazi wakiwa ndani wakishona nguo.

Hali ya hewa iliyobadilika kutokana na moshi ndani ya jengo hilo imesababisha baadhi ya wafanyakazi wanaokadiriwa kuwa 30, kuanguka na wengine kupoteza fahamu  na hivyo kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu zaidi.

Waandishi wa habari, Wafanyakazi wa shirika la umeme - TANESCO na Wafanyakazi wa zima-moto waliofika hapo kwa ajili ya kusaidia uokozi na kupata raarifa, walizuiwa kuingia ndani ya kiwanda hicho na wamiliki ambao ni raia wa China wakidai hakuna tukio lolote kubwa linalohitaji huduma ya uokozi hadi kuingia ndani.
Mwandishi wa habari Dunstan Shekidele anasema kumbukumbu za matukio zinaonyesha kuwa  hili ni tukio la tatu.

Akiwahoji baadhi ya wafanyakazi wa kituo hicho, amefahamishwa kwamba hali hiyo huenda hali hiyo inatokana na hujuma za baadhi ya wafanyazi wanaolalamika kufanya kazi kwa saa 12 na kulipwa mashahara ya shilingi elfu 80/=.
Picture
(picha: Dunstan Shekidele)
Picture
Bi, Subira Juma Athumani [kushoto] akiwa na majeruhi wenzake. (picha: Dunstan Shekidele)



MUFT SIMBA ATENGUA NAFASI YA SHEIKH MKUU SEMWALI WA MOROGORO


  Sheikh Mkuu na Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, ametengua nafasi ya Shekhe Mkuu mkoani Morogoro, Yahya Semwali akidaiwa kushindwa kusimamia maendeleo ya Waislamu mkoani humo.

Katika barua yake kwa Shekhe Semwali yenye namba MK/BR/UL/03/04/79 ya Februari 19 mwaka huu, Mufti Simba alisema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha Baraza la Ulamaa Taifa hivyo anatakiwa kukabidhi ofisi.

Kutokana na uamuzi wa baraza hilo, Mufti Simba amemteua Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Shaaban kukaimu nafasi hiyo kwa barua yenye namba MK/BR/UL/03/04/81 ya Februari 20 mwaka huu na kusisitiza kuwa, nafsi hiyo inapaswa kujazwa ndani ya siku 90 kwa kufanya uchaguzi mwingine.

“Waumini wa Kiislamu mkoani Morogoro wapewe fursa ya kuchagua Sheikh mwingine wa Mkoa,” ilisema barua hiyo.

Uamuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti na viongozi mbalimbali wa BAKWATA mkoani humo akiwemo Sheikh
Semwali aliyeondolewa madrakani ambaye alisema madai yaliyotolewa dhidi yake si sahihi na yameegemea upande
mmoja yakisukumwa na hisia zaidi.

Alisema kuondolewa kwake katika nafasi hiyo kunatokana na hisia za kuunga mkono msimamo wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda jambo ambalohalina ukweli.

Sheikh Semwali alisema:
Hisia nyingine zilizojionesha ni kitendo cha mimi kwenda ibada ya Hijja kupitia taasisi nyingine tofauti na Baraza la Waislamu nchini (BAKWATA), pamoja na uamuzi wangu wa kutengua uchaguzi wa baraza hili ngazi ya kata, wilayani Gairo.

Uchaguzi huu ulifanyika kinyime na utaratibu bila ya ngazi husika kama BAKWATA Wilaya na Mkoa kuwa na taarifa, hili ndio lililomsukuma Mufti Simba kufikia maamuzi haya japo baraza hili Mkoa lina taarifa za ukikukwaji husika lakini bado aliendelea kukaa kimya.
Kuhusu madai ya kushindwa kusimamia maendeleo ya Waislamu, Sheikh Semwali alisema hivi sasa katika Wilaya zote kuna miradi ya maendeleo kama ule wa Wilaya ya Ulanga ambako kuna ujenzi wa vyumba vya maduka 14.

Pia kuna mchakato wa upatikanaji ekari 20 kwa ajili ya upandaji miti ya matunda ambapo hivi sasa walikuwa kwenye hatua za mwisho kupata ekari nyingine 600.

Alisema Wilaya ya Morogoro Vijijini kuna vyumba vitano vya maduka, Mvomero vyumba vinne vya madrasa na Kilombero vyumba vitano vya biashara ambapo maendeleo hayo  yametokana na juhudi zake.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baraza la Masheikh mkoani humo, ambalo lilikaa hivi karibuni kupitia maamuzi hayo, Sheikh Shaaban Nyoni, alisema uamuzi wa Mufti Simba amekiuka Katiba ya BAKWATA.
Shekhe Semwali alichaguliwa hakuteuliwa hivuyo kama alikuwa na tatizo, wao kama baraza ndio waliopaswa kuwasilisha tatizo lao kwa Mufti Simba si vinginevyo.

Halmashauri ya BAKWATA Mkoa inatarajia kukutana kesho (leo), ili kujadili uamuzi huu na baadaye kikao cha Mashekhe wote wa Wilaya na Mkoa, watakaa kujadili na kutoa msimamo.
Imam wa Msikiti wa Al Aqswaa wa Mazimbu, mkoani humo, Sheikh Mohamed Msoma ambaye ni mjumbe wa Baraza la Masheikh, alisema si sahihi Mufti Simba kumuondoa Sheikh Semwali katika nafasi yake.



KAGERA SUGAR WAPELEKWA PUTA MPAKA WAOMBA POO KWA YANGA: WAMEPIGWA KAMOJA TU

Niyonzima akiwapungia mikono mashabiki baada ya mechi

Na Mahmoud Zubeiry
KWA mara ya pili mfululizo, kiungo Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima leo tena amekuwa shujaa wa timu yake, Yanga SC baada ya kuifungia bao pekee la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Niyonzima alijikuta akituzwa fedha na mashabiki wa timu yake baada ya mechi hiyo, iliyokuwa ngumu kwa Wana Jangwani, kutokana na kuibeba timu hiyo mara mbili mfululizo kwa kufunga mabao ya juhudi binafsi, ikiwemo mechi iliyopita dhidi ya Azam FC. 
Didier Kavumbangu akipiga shuti langoni mwa Kagera mbele ya mabeki wa Kagera
Ushindi huo unaifanya Yanga ifikishe pointi 42, baada ya kucheza mechi 18, hivyo kujitanua kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi Azam FC kwa pointi sita, ambayo inashika nafasi ya pili kwa pointi zake 36, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao 31.
Kagera inabaki na pointi zake 28 katika nafasi ya tano, baada ya kucheza mechi 19, chini ya Coastal Union ya Tanga inayoshika nafasi ya nne kwa pointi zake 30.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Simon Mberwa kutoka Pwani, aliyesaidiwa na Milambo Tshikungu wa Mbeya na Said Tibabimale kutoka Mwanza, hadi mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.
Hata hivyo, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu aliikosesha timu yake bao, baada ya kupiga juu ya lango mkwaju wake wa penalti dakika ya 44.
Refa Mberwa, alitoa penalti hiyo baada ya Kavumbangu mwenyewe kudakwa miguu kwenye eneo la hatari na kipa wa Kagera, Mganda Hannington Kalyesebula.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko, Yanga inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts ikiwatoa Kavumbangu na Bahanuzi na kuwaingiza Jerry Tegete na Mganda Hamisi Kiiza, wakati Kagera inayofundishwa na mzalendo, Abdallah Kibadeni, iliwatoa Mnigeria Darlington Enyinna na Julius Mrope na kuwaingiza Paul Ngway na Themi Felix.
Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa kila upande na kuongeza kasi na ladha ya mchezo, lakini bahati hii leo ilikuwa kwa wana Jangwani, kutokana na kupata bao pekee la ushindi lililofungwa na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Niyonzima.   
Niyonzima alifunga bao hilo dakika ya 65, baada ya kumhadaa kiungo wa Kagera, George Kavilla na kufumua shuti kali akiwa umbali wa mita 25, lililomshinda kipa wa Kagera, Kalyesebula.
Halikuwa na tofauti sana na bao pekee la ushindi alilofunga kwenye mchezo uliopita wa timu yake dhidi ya Azam FC, Uwanja huo huo wa Taifa, Jumamosi iliyopita.   
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Shijja Mkinna alikosa bao la wazi dakika ya 89, baada ya kupewa pasi nzuri na Paul Ngway, lakini akapiga juu ya lango.
Hiyo ilikuwa nafasi pekee ya kujutia kwa Kagera ambao leo iliitoa jasho Yanga.  Jerry Tegete naye alikosa bao la wazi dakika ya 87, akishindwa kuunganisha krosi ya Simon Msuva. 
Kwa ushindi huo, Yanga imelipa kisasi cha kufungwa 1-0 na Kagera katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo, mwishoni mwa mwaka jana mjini Bukoba.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbangu/Hamisi Kiiza dk67, Said Bahanuzi/Jerry Tegete dk 67 na Haruna Niyonzima.
Kagera Sugar; Hannington Kalyesebula, Benjamin Asukile, Martin Muganyizi, Malegesi Mwangwa, Amandus Nesta, Gaorge Kavilla, Julius Mrope/Paul Ngway dk 62, Juma Nade, Darlington Enyinna/Themi Felix dk 69, Shijja Mkinna na Daudi Jumanne.    

SOURCE: BIN ZUBEIRY

ALIYEKUWA MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI KENYA SAMWEL KIVUITU AMEAGA DUNIA


336544_319369068086667_163569676999941_1031123_336563521_o

Wakili aliyekuwa mwenyekiti  wa tume ya uchaguzi ya Kenya,  ECK ndugu Samuel Kivuitu ameaga dunia
Taarifa zilizotolewa na familia ya Kivuitu zinasema kuwa marehemu aliaga dunia jana usiku mwendo wa saa nne katika hospitali ya MP Shah iliyopo jijini Nairobi, alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya saratani.
Kivuitu alikuwa akisumbuliwa na saratani ya  koo ambapo alikuwa akipelekwa katika hospitali hiyo mara kwa mara kwa muda wa miaka miwili.

Marehemu Kivuitu alivuma sana mwaka 2007 baada ya matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini Kenya yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya wakati huo ECK yeye akiwa Mwenyekiti, matokeo ambayo yalipokelewa kwa hisia tofauti na kuwa sababu hasa ya kuchochea machafuko makubwa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Kenya ambapo watu 1,133 waliuawa na wengine laki sita na nusu kuachwa bila ya makazi.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU