WAKATI mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa,
akimtuhumu Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki,
kuibeba kampuni ya uwindaji ya Leopard Tours Ltd, mwenyewe amejibu
mapigo akidai mbunge huyo hajafanya utafiti.
Msigwa aliwaambia
waandishi wa habari jana mjini Dodoma kuwa Kagasheki alitumia nafasi
yake kuiarifu kampuni hiyo kuipatia ekari tano kwa gharama ya dola za
Kimarekani 30,000 nusu ya gharama za kawaida dola 60,000 kwa ekari kumi.
Mbunge
huyo ambaye pia ni msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa wizara hiyo,
alisema kuwa Kagasheki anaendesha wizara kwa kukiuka sheria na taratibu
akitumia mamlaka vibaya.
Msigwa alisema kuwa Kagasheki tangu
alipoingia madarakani na kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA), sasa hifadhi inaendeshwa bila bodi jambo ambalo ni
kinyume.
Alidai kuwa waziri huyo alifanya maamuzi hayo ya kuibeba
kampuni hiyo ya uwindaji bila kuzingatia sheria na kanuni za ugawaji wa
vitalu na kwamba alivunja sheria kwa kufanya uamuzi wa moja kwa moja na
Leopard Tours wa kushusha viwango vilivyowekwa kisheria bila kutoa
tangazo la serikali.
Msigwa pia aliibua tuhuma nyingine akidai kuwa Kagasheki ama kwa makusudi au kutokujua kuwa ana
maslahi binafsi
ya mahusiano na mbunge wa viti Maalumu wa Mkoa wa Arusha, Catherine
Magige (CCM), na kumkingia kifua ili taasisi yake ya Catherine
Foundation ipate msaada wa sh milioni 10 kutoka NCAA.
“Msaada
huo si tu ulikiuka kanuni za msaada ambao unaelekezwa katika shughuli
za msaada wa kijamii kupewa kiasi kisichozidi sh milioni 2 lakini mradi
huo wa Catherine ulipewa fedha hizo huku dokezo la maombi ya msaada huo
likionyesha watendaji wa NCAA wakilalamika. Walitoa mapendekezo mara
mbili, kwanza kwa kupitia meneja wa maendeleo ya jamii kuwa hakuna
bajeti ya kusaidia msaada huo kutoka idara ya maendeleo ya jamii labda
wafikiriwe kupitia fungu la donesheni,” alieleza Msigwa.
Aliongeza kuwa nyaraka zinaonyesha kwamba kaimu mhifadhi wa Ngorongoro, alimjibu meneja maendeleo ya jamii kuwa fungu la donesheni halina fedha za kutosha, hivyo ni bora Magige ajibiwe na asubiri mpaka mwaka wa fedha ujao.
Msigwa
alifafanua kuwa dokezo hilo lilisainiwa Desemba 14 mwaka jana: “Jambo
la kushangaza na kutia walakini ni kuwa kaimu mhifadhi kwa shinikizo
alimuelekeza mhasibu kuilipa Catherine Foundation kiasi cha milioni 10
kwa ajili ya ununuzi wa madawati 18 Juni, mwaka huu, ukiwa ni mwaka wa
fedha wa 2012/13 kinyume na mapendekezo yake ya awali.”
Alisema
kuwa wanataka kujua kaimu mhifadhi alitumia kigezo gani kuilipa taasisi
hiyo fedha hizo za msaada wa ununuzi wa madawati tofauti na kiwango
kilichowekwa cha sh milioni 2.
Kagasheki ajibu
Akijibu
tuhuma hizo, Kagasheki alisema kuwa anamfahamu Msigwa kwa vile hiyo si
mara yake ya kwanza kutoa tuhuma za uongo dhidi yake: “Msigwa alishawahi
kusema nijiuzulu kwamba nimeshindwa kushughulikia ujangili kwa kuwa eti
nashughulika na watu wadogo (dagaa) na kuwaacha mapapa (viongozi),”
alisema.
Kagasheki alifafanua kuwa
tatizo analoliona kwa Msigwa ni kukurupuka bila kufanya utafiti wa kina
na kuanza kutuhumu watu kwa sababu binafsi anazozijua yeye: “Msigwa ana
chuki na mimi na hii ilitokana na yeye kuondolewa kwenye Kamati ya Bunge
ya Ardhi, Maliasili na Mazingira; anadhani nilishawishi aondolewe kumbe
yalikuwa matakwa ya Spika,” alisema.
Alisisitiza
kuwa kwa vile Msigwa amejitokeza kuisemea Ngorongoro ni dhahiri sasa
anaamini tetesi zilizopo dhidi yake kuwa anatumika kuwatetea vigogo
walioondolewa kwa tuhuma za ufisadi: “Ngorongoro kuna ufisadi wa
kutisha, subirini kidogo ripoti yake inakamilika mtajionea hao watu
anaowatetea walifanya nini huko,” alisema.
Kuhusu
madai ya kuibeba kampuni ya uwindaji, Kagasheki alisema kuwa mwindaji
huyo amekuwa nchini akifanya kazi zake kihalali na kutoa ajira kwa
wazawa na kwamba uamuzi wake ulikuwa wa busara kwani NCAA walitaka
kumchakachua: “Huyu aliomba eneo kujenga kambi lakini lililopatikana
halikufikia hata nusu sasa wakawa wanataka kumuuzia kila kilomita kwa
dola 60,000 ndipo nikaagiza auziwe kwa nusu yake. Hapa nilifanya kosa
gani wakati nilidhibiti ufisadi?” alihoji.
Alisisitiza
kuwa tayari anazo taarifa za Msigwa kutumiwa na kundi linalompiga vita
ndani ya wizara hiyo na kaapa kwamba kamwe hawatashinda.
Kuhudu
madai ya kuishinikiza NCAA kumpa msaada Magige, waziri huyo alisema
maneno hayo ni ya kitoto zaidi kwani kama angetumia wadhifa wake
kumkingia kifua asingepewa fedha kidogo kiasi hicho: “Ni kweli Magige
ana taasisi yake na wamekuwa wakiomba fedha maeneo mengi kusadia yatima
na wahitaji wengine lakini sina taarifa kama hata aliomba fedha NCAA;
Msigwa ana ajenda yake,” alisema.
Magige awaka
Akizungumzia
tuhuma hizo, Magige alisema taasisi hiyo ni kama zingine na hivyo
kumshangaa Msigwa kuihusisha na mahusiano binafsi ya watu.
Alikiri
kuomba msaada NCAA na kupewa kiasi hicho cha sh milioni 10 lakini
akasema huo ni uamuzi wao kwani hawakuwapangia kiwango.
“Tuliandika
barua ya maombi tukapeleka; ikakaa muda mrefu lakini baadaye wakatuita
na kutupa msaada huo. Mimi nadhani kungelikuwa na shinikizo la waziri
ningepewa fedha nyingi zaidi ya hizo! Msigwa ni mchungaji, sisi
tunapaswa kujifunza ukweli kutoka kwake sasa iweje anasingizia watu na
kuwazulia mambo ya uongo jamani? Amekumbwa na nini?” alihoji Magige.
Source:
wavuti