Facebook Comments Box

Tuesday, July 9, 2013

TAARIFA YA KESI YA MUME WA JOYCE KIRIA (KILEO)

Picture
Wakielekea na kutoka chumba cha mahakama (picha: Tumaini Makene)
Picture
Wakili, Kibarala akizungumza na waandishi wa habari, baada ya shauri kortini. (picha: Tumaini Makene)
HATIMA ya kesi ya ugaidi inayowakabili makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), sasa ipo mikononi mwa Mahakama Kuu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora ilikofunguliwa kusema haina uwezo wa kusikiliza kesi ya ugaidi.

Wakati Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Tabora, Issa Magoli, akiisukumia Mahakama Kuu kesi hiyo, wakili wa watuhumiwa hao, Peter Kibatala, aliliambia Tanzania Daima kuwa wameshafanya utaratibu wa kupeleka shauri lao Mahakama Kuu baada ya kupewa nakala ya uamuzi huo.

Makada hao wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi ni Katibu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo, Evodius Justinian, Oscar Kaijage , Seif Kabuta na Rajab Daniel, wanaotuhumiwa kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mwaka 2011.

Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Magoli alisema mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza kesi hiyo,
 hivyo akaiahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, mwaka huu.

Hakimu Magoli kabla ya kuahirisha shauri hilo aliwashauri mawakili wa upande wa utetezi wawasilishe hoja zao Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo watapatiwa ufumbuzi wa kisheria.

Akizungumza kwa simu na gazeti hili, wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala, saa chache baada ya uamuzi huo, alisema wameshapeleka Mahakama Kuu Kanda ya Tabora maombi kwa hati ya dharura ya kutaka iipitie upya kesi hiyo ya ugaidi.

Aliongeza kuwa maombi hayo yamepokewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na wanasubiri kupangiwa tarehe nyingine na Mahakama Kuu ili kesi hiyo isikilizwe.

Alisema katika maombi yao wameomba Mahakama Kuu ipitie shauri hilo, pia kuona kama ni halali kisheria kwa washtakiwa hao kufunguliwa kesi hiyo baada ya awali watuhumiwa wanne (isipokuwa Kilewo), mashtaka yao yaliondolewa na kisha kukamatwa na kufunguliwa mashitaka mapya.

Kwa mara ya kwanza watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi Juni 24, mwaka huu, wakidaiwa walimteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.

Awali kabla ya kusomewa shitaka la ugaidi ambalo kwa sasa mahakama inasema haina uwezo wa kusikiliza, mwanzoni walifunguliwa shitaka la kushambulia na kudhuru mwili, ambapo Mahakama ya Wilaya ya Igunga iliwaona hawana hatia, hivyo kuwaachia huru lakini walikamatwa tena.

Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mjini. Jocktan Rushwera, ndiye aliyesikiliza hoja za mawakili wa utetezi, waliomtaka kuifuta kesi hiyo. Hata hivyo haijulikani kwanini kesi ilisikilizwa halafu baada ya kubadilisha hakimu, kwa kesi hiyo hiyo mwingine akasema mahakama hiyo haina uwezo wa kuisikiliza.

Upande wa serikali uliwakilishwa na Wakili Juma Massanja na Ildefons Mukandara.

Awali watuhumiwa hao waliposomewa shitaka, jopo la mawakili wa utetezi, Abdalah Safari na Peter Kibatala, liliomba mahakama hiyo iyafute mashitaka hayo kwa sababu ya kutokuwa na uhai.

Mawakili hao wa utetezi walidai kuwa mashitaka hayo hayana uhai kwa sababu yamefunguliwa bila ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Pia mawakili hao walidai kuwa sheria za uendeshaji wa makosa kama hayo hapa nchini zinadai kuwa mashitaka kama hayo yanapofunguliwa ni lazima ridhaa ya DPP iwepo, lakini ridhaa hiyo haipo, hivyo yatupwe.

Waliongeza sababu ya pili kuwa maelezo hayaoneshi kosa husika ni la kigaidi, tofauti na makosa mengine ya kawaida kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hivyo waliomba yafutwe au yafunguliwe kama kosa la kawaida.

Upande huo wa utetezi pia ulidai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, inaelekeza kuwa mshitakiwa ashitakiwe katika mahakama yenye mamlaka na hadhi kama ile waliyopelekwa katika maeneo yale walikokamatwa.

Hivyo mawakili waliiomba mahakama itupilie mbali shitaka, kwani washitakiwa kama walikuwa na hatia walipaswa kushitakiwa katika maeneo yao walipokamatwa.

Upelelezi wa Lwakatare bado

Wakati huo huo, mkoani Dar es Salaam, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kesi ya kula njama na kutaka kumuua kwa sumu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky, inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.

Hakimu Mkazi, Alocye, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, mwaka huu kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.

Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Ponsia Lukosi, aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Lwakatare yupo nje kwa dhamana, Ludovick bado yupo gerezani baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika kisheria ambapo kila mdhamini atatakiwa asaini bondi ya sh milioni 10 pamoja na washitakiwa wenyewe.

Pia mshitakiwa anatakiwa kusalimisha hati yake ya kusafiria mahakamani na kutotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama.

Taarifa hii imeandaliwa na Happiness Katabazi (Dar), Thomas Murugwa na Josephat Isango (Tabora).

---
Picha via JamiiForums.com
Maandishi via TanzaniaDaima


NYATI MWEUPE AZUA TAFRANI NGORONGORO


WAHIFADHI watafiti na wataalamu kadhaa, wako katika harakati za kumsaka Nyati wa ajabu anayedaiwa kuwa na rangi ya maziwa, ambaye hivi karibuni ameonekana katika mwambao wa bonde kuu la Ngorongoro (Kreta) na kusababisha tafrani kubwa.
Kwa mujibu wa mtalaam wa ikolojia katika mamlaka hiyo, Patrice Mattay, uwepo wa nyati (mbogo) huyo wa aina yake hifadhini hapo, kumeibua suala jipya katika utafiti wa wanyama pori, kwani hakujawahi kuwepo Nyati mwenye rangi nyeupe popote duniani. Kwa kawaida Nyati huwa anangozi yenye rangi nyeusi.
Nyati huyo mweupe aligundulika kwa mara ya kwanza na maafisa wa polisi wanaofanya kazi katika kituo cha polisi kilichopo ndani ya hifadhi hiyo, ambao wanasema mnyama huyo hupita katika maeneo ya kituo hicho majira ya asubuhi akiwa miongoni mwa mbogo wengine takribani 20. Ngorongoro ina nyati wapatao 350.


“Ni kweli hata mimi binafsi nimemshuhudia Nyati huyo mweupe akikatiza katika sehemu mbalimbali za hifadhi ya Ngorongoro majira ya asubuhi akiwa katika kundi la mbogo wengine,” alisema mkuu wa kituo cha Ngorongoro Afisa wa Polisi, JJ Paul.

Hadi sasa ni maaskari wanaofanya doria katika maeneo ya hifadhi hiyo, hususan nyakati za asubuhi, ndio wanaothibitisha kwa kiwango kikubwa kumuona Nyati huyo wa ajabu ambaye sasa anatarajiwa kuwa atakuwa kivutio kipya cha utalii nchini.

Meneja Uhifadhi katika mamlaka ya Ngorongoro, Amiyo T. Amiyo amesema tayari shirika lake limekwisha tuma askari wake kadhaa kumsaka Nyati huyo wa ajabu, ili kubaini eneo ambalo anapatikana kwa ajili ya kuwezesha utafiti zaidi.

“Na kwa mtu yeyote mwenye kutuletea taarifa kuhusu Nyati huyo mweupe zitakazotuwezesha kumpata mnyama huyo, basi naye pia atazawadiwa ipasavyo,” alisema Amiyo.

Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ndiyo inayoongoza kwa kupata watalii wengi nchini na kwa mujibu wa Ofisa Utalii wa Shirika hilo, Asantaeli Melita, zaidi ya wageni 585,000 hutembelea eneo hilo, na hasa Kreta, kila mwaka.

Idadi ya wanyamapori walioko Ngorongoro kwa sasa inafikia 300,000 wengi wao wakiwa ndani ya bonde lenyewe huku baadhi na hasa twiga wakiishi nje ya Kreta.

Mbali na Mbogo wa jabu aliyegunduliwa hivi karibuni, eneo la Ngorongoro pia lina maajabu mengine kadhaa, ukiwemo kilima cha mchanga unaotembea bila kusambaratika, idadi kubwa ya Kakakuona, mnyama anayedaiwa kuwa na uwezo wa kutabiri, pamoja na idadi kubwa ya wanyama adimu kama Mbwa-mwitu na Faru.


TAARIFA YA MWEZI WA RAMADHAAN


Assalaamu 'alaykum wa Rahmatullaahi wa Barakaatuh,
Tumefuatilizia sana kila pahali taarifa za mwezi, na hatujapata taarifa zozote za mwezi kuonekana popote duniani jana Jumatatu 29 Sha'baan 1434H (8 Julai 2013M). Hivyo, leo Jumanne tunakamilisha siku thalathini za Sha'abaan  In shaa Allaah, na Jumatano (10 Julai 2013M) itakuwa ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhaan.
KITONGONI inawaombea Ramadhaan ya kheri na baraka nyingi, mchume thawabu tele, Swawm zikubaliwe, dhambi zighufuriwe, na Allaah Atutakabalie 'amali zetu.  Tusiache kuwaombea du’aa ndugu zetu Waislam popote walipo ulimwenguni walio katika dhiki za ukandamizwaji,
vita, njaa na machafuko. Na pia tukumbukane kwa du’aa kwani Mtume Swalla-Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam amesema katika Hadiyth kutoka kwa Ummu Dardaa (Radhiya-Allaahu ‘anhaa): ((Atakayemuombea ndugu yake kwa siri Malaika aliyewakilishwa kwake husema: “Aamiyn nawe pia upate mfano wake)) (wa kama unayomuombea) [Muslim]
Kwa Munaasabah wa kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhaan, Alhidaaya imewaekea tayari  mafundisho mbalimbali yenye manufaa katika kuongeza elimu na kuimarisha 'ibaadah zenu ili muweze kuchuma mema mengi na muweze kufikia kuipata taqwaa ambayo ndio lengo kuu la Swawm.

 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU