Utajiri, safari zake nje ya nchi vyatiliwa shaka
*Ahusishwa na mtandao hatari wa Masogange
KWA mara ya kwanza tangu lilipoibuka sakata la watu maarufu kujihusisha
ama na utumiaji au usafirishaji wa dawa za kulevya, jina la
mwanamuziki anayeaminika kuwa na ukwasi mkubwa kwa sasa hapa nchini,
Nasseeb Abdulmaliki, maarufu zaidi kwa jina la Diamond, limeanza
kutajwa kuwa ni miongoni mwa vigogo wa dawa hizo.
Tayari mjadala mkubwa wa chini chini umeibuka kwa watu mbalimbali
wakiwemo mashabiki wake, na taarifa ambazo zimelifikia MTANZANIA
Jumatano kutoka vyanzo mbalimbali zimedai kuwa, mwenendo wa maisha ya
Diamond sasa unachunguzwa na baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola vya
ulinzi na usalama.
Kutajwa kwa jina la Diamond katika sakata hili, kunatiwa nguvu zaidi na
mwenendo binafsi wa maisha wa msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi
kipya, unaokwenda sambamba na ukwasi mkubwa alioupata katika kipindi
kifupi.
Kama hiyo haitoshi, safari za nje ya nchi za mwanamuziki huyo
unaohusisha ziara zake nchini Afrika Kusini na Uingereza, pia ni mambo
ambayo yamechochea wingu la mashaka lililofikia hatua ya jina lake
kuingizwa katika mtandao huo ambao katika siku za karibuni, umewagusa
pia baadhi ya watu wenye majina makubwa katika jamii.
Kuhusu ziara hizo, kilicholeta mshtuko na dukuduku dhidi yake ni kuwapo
kwa taarifa kwamba, katika moja ya ziara hizo za nje ya nchi, Diamond
alifikia hatua ya kusafiri akitumia chumba kinachotumiwa na wageni
mashuhuri (VIP), badala ya njia ya wasafiri wa kawaida.
Mbali na hilo, taarifa nyingine zinaeleza kwamba, mizigo ya msanii huyo
ambaye mara kadhaa amekuwa akisafiri na kundi la wacheza shoo wake,
imekuwa ikipita pasipo kupitishwa katika hatua za ukaguzi kwa namna ile
ile ilivyokuwa kwa mabinti wawili wa Kitanzania walionaswa nchini
Afrika Kusini baada ya kuruka mfumo wa ukaguzi wa JNIA.
Aidha, ukaribu wa kimahusiano kati ya Diamond na baadhi ya Watanzania
wanaoishi nchini Afrika Kusini na ambao majina yao pia yameanza
kuhusishwa na biashara hiyo ya mihadarati, ni jambo jingine ambalo
limechochea harakati za kufuatiliwa kwa karibu kwa nyendo za Diamond.
Taarifa zaidi kutoka JNIA zinaeleza kwamba, miongoni mwa watu wanaoweza
wakawa wamemponza Diamond ni wale ambao walionekana kuwa karibu na
Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), siku walipokuwa
wakisafiri kwenda Afrika Kusini kabla hawajanaswa katika uwanja wa
Ndege wa Oliver Thambo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini,
wakiwa na shehena ya dawa za kulevya.
Mwenendo wa watu hao unatiliwa shaka kuwa huenda ni miongoni mwa
wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wenye maskani yao nchini
Afrika Kusini, kwa sababu mbali na ukaribu na wasichana hao, pia
walihusika kwa karibu kuusafirisha mwili wa mwanamuziki Albert
Mangwair, aliyefia huko huko Afrika Kusini ambaye taarifa za kufa kwake
ziligumbikwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Alipoulizwa jana na MTANZANIA Jumatano kupitia simu yake ya kiganjani
kuhusu taarifa hizo na iwapo amekwishahojiwa na vyombo vya dola baada
ya jina lake kuanza kutajwa kuwa miongoni mwa orodha ya wasanii wa
muziki wanaosafirisha dawa za kulevya, Diamond alikiri kuwa na pesa za
kutosha kuishi maisha anayoyataka, lakini akakana kujihusisha na
biashara hiyo.
Akifafanua tuhuma moja baada ya nyingine kwa mpangilio aliokuwa
akiulizwa na gazeti hili, Diamond alisema katika maisha yake, hajawahi
kujihusisha na utumiaji au usafirishaji dawa za kulevya, lakini madai
hayo yamekuwa yakitolewa dhidi yake na watu ambao hawajui siri ya
mafanikio yake.
“Kazi ngumu siku zote inalipa, sasa napata matunda ambayo yanatokana na
kile nilichokifanya, iweje watu wanitilie mashaka, Watanzania ni
mashahidi wangu wananiona navyochumia juani, nitaendelea kulia kivulini
tu kwani nakula kwa jasho langu.
“Siyo kweli kwamba mizigo yangu haikukaguliwa na kama haikukaguliwa na
ingekuwa na kasoro, basi Uingereza wangenitia hatiani, nilipita na
nilikaguliwa.” Alisema Diamond.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za kuwa mwanamtandao wa kundi la Masogange,
pia alikanusha kwa kueleza kuwa hata siku aliyosafiri kwenda Afrika
Kusini alikwenda peke yake uwanja wa ndege na kuongeza kuwa alikwenda
huko kwa shughuli za kimuziki, ambapo safari nzima iligharimu zaidi ya
Dola 30,000 za Kimarekani.
“Afrika Kusini nimekwenda kufanya kazi zangu na safari hiyo
imenigharimu zaidi ya Dola 30,000, nilikwenda kurekodi nyimbo yangu
mpya inayoitwa namba moja ambayo itaanza kusikika hivi karibuni.
“Unajua Watanzania sasa hivi wanajua mtu hawezi kufanikiwa au kupata
maendeleo bila kuuza ‘unga’, hili si sawa juhudi za mtu ndizo
zinamfikisha alipo, na mimi juhudi zangu ndio zinanifikisha hapa, watu
waache kunijadili vibaya.” Alisema Diamond.
Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja ikiwa ni takribani miezi miwili sasa
tangu Watanzania wawili, Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa
Edward (24), waliokuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya wanamuziki
maarufu hapa nchini, kukamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na dawa za
kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh bilioni
6.8.
Mbali na kuwa na uhusiano wa karibu na wanamuziki, Edward anadaiwa kuwa
alikuwa mfanyakazi katika mgahawa mmoja maarufu jijini Dar es Salaam,
unaomilikiwa na mmoja wa vijana matajiri hapa nchini ambaye hata
hivyo gazeti hili halijafanikiwa kumpata ili kufanya naye mahojiano.
Wakati huo huo, tayari hatua za kinidhamu zimekwishaanza kuchukuliwa
dhidi ya wafanyakazi wa JNIA waliohusika kupitisha kilo 150 za dawa za
kulevya, ambao Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametaja
majina yao hivi karibuni na kuonyesha kwa waandishi wa habari ushahidi
wa kuhusika kwao.
CHANZO:
JAMII FORUMS