Facebook Comments Box

Sunday, September 14, 2014

YANGA WAIFUNZA ADABU AZAM: YAITANDIKA TATU MTUNGI

Jaja akishangilia goli lake na Ngassa na Msuva
Zile kelele za timu ya waoka mikate wa Azam za kuwa wao ndio timu bora zimenyamazishwa leo baada ya kupokea kipigo cha mwana ukome kutoka kwa Young Africans Sports Club.
Kelele za Azam zikikuwa zikiwaaminisha watanzania wengi kuwa wao ni timu bora na watakao shinda mechi hiyo.

Wakitumia vyombo vyao vya habari,kurasa za mitandao ya kijamii na vipindi vyake katika luninga mbalimbali walionesha kuwa wao wapo vizuri na watashinda lakini hali haikuwa hivyo mbele ya Yanga baada ya kuoneshwa kuwa mpira ni uwanjani na sio mdomoni. 
Mshabiki wa Azam Steve kulia lia akiangalia Azam wakifanyiwa sio uungwana na Yanga

Mshambuliaji wa Kibrazil, Genilson Santana Santos ‘Jaja’ alifunga mabao mawili katika mchezo huo, wakati Simon Msuva alifunga la tatu, yote kipindi cha pili. Mabao hayo yalitosha kuipa Yanga ngao ya jamii kwa mara pili mfululizo.
Washabiki wa Yanga walijaza uwanja

Dakika 45 za kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na timu zote zilishambuliana kwa zamu.

Yanga walionesha makali baada ya kocha Marcio Maximo kumpumzisha chipukizi Said ‘Kizota’ Juma na kumuingiza Hassan Dilunga aliyekwenda kufanya kazi nzuri.

Safu ya ulinzi ya Yanga SC leo ilicheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kufanikiwa kuwadhibiti washambuliaji wa Azam FC, akina Leonel Saint Preux, Didier Kavumbangu na Kipre Herman Tchetche. Winga Simon Msuva aliyeingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya Nizar Khalfan ndiye aliyekwenda kuimaliza Azam FC.

 Msuva aliseti bao moja na kufunga moja kwanza akitia krosi ambayo ilimbabatiza beki wa Azam na kumkuta Jaja aliyefunga dakika ya 56 na baadaye akafunga mwenyewe bao la tatu. Lakini kabla ya Msuva kufunga la tatu, Jaja alifunga tena baada ya kupokea pasi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa na kumchambua vizuri kipa Mwadini Ali dakika ya 65. Washabiki wengi wa mpira wakilisema kuwa ni goli zuri kuwahi kutokea hapa nchini.

Msuva alifunga bao la tatu baada ya kupokea pasi ndefu ya Hussein Javu na kukutana na kipa Mwadini Ali aliyetoka langoni ambaye alimlamba chenga na kwenda kuukwamisha mpira nyavuni dakika ya 87.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Meckysadick alimkabidhi Nahodha wa Yanga SC Ngao baada ya mechi hiyo na baada ya hapo, wachezaji, viongozi na makocha wa timu hiyo wakaanza kushangilia.

Hii ni mara ya pili mfululizo Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii,baada ya mwaka jana pia kuifunga Azam FC 1-0, bao pekee la Salum Telela.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa;
Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Said ‘Kizota’ Juma/Hassan Dilunga dk37, Haruna Niyonzima/Hussein Javu dk79, Genilson Santana ‘Jaja’/Hamisi Kiiza dk79,
Mrisho Ngassa/Omega Seme dk72 na Nizar Khlafan/Simon Msuva dk46.

Azam FC; 
Mwadini Ali, Erasto Nyoni/Gardiel Michael dk74, Shomary Kapombe, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao/Kevin Friday dk62, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Didier Kavumbangu, Kipre Tchetche/Ismaila Diara dk83 na Leonel Saint- Preux/Khamis Mcha dk62.


UKICHANGIA DAMU UTAINGIA BURE KUONA YANGA VS AZAM

Kwa watanzania wapenda mpira na wanaopenda kusaidia watanzania wenye magonjwa mbalimbali,waliopata ajali na wamama wajawazito kuepushwa na umauti kwa ukosefu wa damu wataingia uwanjani bure kwa kuchangia damu tu.

Huduma hii ni pale nje ya uwanja wa taifa kabla ya mechi.
Shime tujitokeze kuchangia damu.



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU