Facebook Comments Box

Tuesday, August 6, 2013

VILABU 13 VYA LIGI KUU TANZANIA BARA VYAISHUKIA YANGA KUHUSU UDHAMINI WA AZAM TV

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo na mjadala kuhusiana na hatua ya klabu ya Yanga kupinga udhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania unaotarajiwa kufanywa na Azam Media.
 
Tumeona ni vema tukatoa msimamo wetu wa pamoja kuhusiana na hatua hiyo ya wenzetu kwa lengo la kuweka rekodi sawa. Tunataraji hatua hii ya vilabu hivi 13 itafunga mjadala huu na tungependa wana habari, kama mtaamua kuuendeleza, basi muundeleze katika mlengo ambao wadau, yaani sisi vilabu vinavyoshiriki mashindano hayo, zimeamua kuufuata.
 
Tunapenda kukumbusha kwamba kwa muda mrefu, kilio cha vilabu vya Ligi Kuu ya Tanzania kilikuwa ni ukosefu wa wadhamini na kwa bahati nzuri kuna dalili kwamba Mungu ameanza kukisikia kilio hicho msimu huu. 

Kwa faida ya umma, tungependa kutoa takwimu za nchi jirani zinazotuzunguka. Kenya, kila klabu hupata Sh milioni saba za Kenya (sawa na Sh milioni 125 za Kitanzania) kwa mwaka –fedha ambazo zimeifanya ligi ya Kenya kuwa na uwiano na ushindani wa kweli (fedha hizo ni mjumuisho wa gharama za matangazo ya televisheni na udhamini wa bia ya Tusker). 

Tanzania leo tunajivunia kuwazidi Kenya kutokana na udhamini wa Azam ambapo kwa mwaka huu, kila klabu itapata zaidi ya Sh milioni 170 (Jumla kutoka milioni 100 za Azam na milioni 70 za Vodacom).  

Hatuna sababu ya kutaja viwango vya udhamini kwa nchi nyingine jirani kama Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia nk kwa vile zote zina udhamini wa chini kuliko Kenya. SuperSport, ambao wanaliliwa na baadhi yetu, udhamini wao kwa ligi ya Uganda ni dola 350,000 ambazo ni pungufu kulinganisha na dola milioni moja zilizotolewa na Azam Media hapa nchini.  

Ni imani yetu kwamba udhamini huu utaifanya ligi ya Tanzania kuwa bora kuliko zote za Afrika Mashariki. Hili litasaidia kutengeneza timu bora ya Taifa ya Tanzania. Tungependa kutoa ufafanuzi wa masuala machache ambayo yaliongelewa na wenzetu wa Yanga kama sababu za kupinga udhamini huu. 

BODI YA TPL
Kwa mujibu wa Katiba za FIFA, CAF na TFF, Haki za Televisheni zipo chini ya FA ya nchi husika. TFF iliamua kukasimu shughuli ya majadiliano kwa Kamati ya Ligi ambayo ilishirikisha vilabu vyote 14, ikiwamo Yanga na wawakilishi wake walihudhuria mchakato mzima hadi mwisho.
 
Hoja ya Yanga kuwa bodi haina nguvu/Mamlaka kisheria kwa kuwa ni ya mpito inakosa mashiko kwa sababu kimsingi ni TFF ndiyo iliyoingia mkataba kwa sababu ndiyo iliyopewa mrejesho na Kamati ya Ligi kwamba mchakato umekwenda sawasawa. 

Hoya ya kuwa Bodi ya TPL iliyoko sasa hivi haina mjumbe hata mmoja aliyeteuliwa kutoka YANGA. Hili si kweli hata kidogo. Mmoja wa wajumbe wa TPL ni Seif Ahmed almaarufu Seif Magari; ambaye vyeo vyake ndani ya Yanga vinajulikana.  

Kama alikuwa hahudhurii vikao vya TPL, hilo ni suala la Wanayanga wenyewe kumuhoji kwanini alikuwa hahudhurii hivyo na hivyo kuinyima klabu yake ushiriki katika mijadala muhimu kwa maslahi ya soka hapa nchini. Ifahamike pia kwamba TPL haikuhodhi mchakato huu bali ilitoa fursa kwa vilabu vyote vya Ligi Kuu kushiriki ambapo Yanga ilikuwa ikiwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Clement Sanga na Katibu Mkuu, Lawrance Mwalusako.  

Hii maana yake ni kwamba hoja kuwa Yanga haikushirikishwa ni mfu. Yanga walitumia neno UTARATIBU WA DUNIA NZIMA wakisema eti hakuna mahala duniani ambapo kampuni yenye klabu inayocheza ligi husika kupewa mkataba wa udhamini au urushwaji wa matangazo. 

Inaonekana Yanga hawakufanya utafiti kwani ligi ya Afrika ya kusini ina timu inayoitwa Super Sports United na inarushwa na kituo cha TV chaSupersports. Pia majirani zetu Kenya wana timu inayoitwa Tusker FC huku ligi hiyo ikidhaminiwa na bia ya Tusker.  

Tunawashauri Yanga kuwa ni vema kufanya utafiti kabla ya kuibuka na hoja za namna hii ili kuepuka kuwapotosha wanachama wao. Yanga pia katika hoja zao wamepinga utaratibu wa kugawana mapato sawa. Hoja hii ni ya msingi na majadiliano yetu yalilitazama hili kwa kina lakini tukaona kwa mazingira ya Tanzania na uchanga wa ligi yenyewe kwa sasa ni heri kugawana sawa ili pesa kwa usawa ili itoke kwa wakati na kusaidia vilabu kujiendesha. 

Yanga wanakosea wanaposema eti wao wanastahili kupewa zaidi kwa sababu ni klabu kubwa na yenye mashabiki wengi kwa kuwa sababu hii haitumiki sehemu yoyote duniani. 
 
Tuchukulie mfano wa nchi ya England ambako ingawa Liverpool ina washabiki wengi kuliko Manchester City na Chelsea, imezidiwa kwenye mapato ya televisheni na timu hizo. 

Hii ni sababu kinachoamu mapato mwisho wa siku ni kiasi cha mechi za timu ambazo zimeonyeshwa na televisheni kwenye msimu husika na nafasi ya timu kwenye msimamo wa ligi. 

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba nchini England, malipo haya hufanyika baada ya msimu kumalizika na hapo ndipo watu hukaa chini na kupigiana hesabu za nini kilipatikana. Sasa ukitumia mfumo huu, ina maada timu zitalazimika kusubiri ligi iishe ili kuangalia msimamo ya ligi kisha kugawana mapato. Sote tunajua jinsi timu zinavyoteseka kwa kukosa nauli, posho, mishahara, pesa za kambi nk.  

Kwa mazingira yetu ya Tanzania kwa sasa, mfumo kama huu haufai. Hii ni kwa sababu timu zinahitaji fedha kuanzia kwenye maandalizi ya mechi ya kwanza na hazikopesheki fedha kwenye mabenki. Tanzania inachohitaji kwa sasa ni ligi yenye ushindani tofauti na sasa ambapo ushindani uko kwa timu chache zenye uwezo wa kifedha.  

Tukizijengea uwezo timu zote taifa litakuwa na ligi nzuri na hatimaye timu nzuri ya taifa. Pia itawezesha wadhamini wengi zaidi kuingia kwenye mpira na hivyo timu nyingi zaidi kufaidika. 
Tukifikia huko, tunaweza kukaa chini na kutazama mfumo wa kugawana mapato utakaokuwa bora zaidi wakati huo.
 
Mambo ya Kuzingatia.Tangu ligi ianze hapa nchini takribani miaka 50 iliyopita, hakuna timu iliyowahi kulalamikia mfumo wa kugawana mapato sawa kwa kila mechi ambao umekuwa ukitumika. Mfano mapato ya mlangoni tumekuwa tukigawana sawa na Yanga haijawahi kulalamika, Pesa za udhamini wa Vodacom tangia ilipokuwa ikidhaminiwa na TBL hadi leo hii  tumekuwa tukigawana sawa na Yanga haijawahi kulalamika kutaka kupata zaidi kwa kuwa eti ina mashabiki wengi, pia hata pesa za haki ya matangazo ya Televisheni zilizowahi kutolewa huko nyuma nailiyokuwa ikiitwa GTV, na Star TV kwa nyakati tofauti pesa ziligawiwa sawa kwa kila timu.
 
Hii ni kwa sababu kikanuni, timu zote zinazoshiriki kwenye ligi ni sawa na zote zinaweza kuwa bingwa au kushuka daraja. Ni mdudu gani huyu aliyeingia kwenye soka ya Tanzania na kuanza kuleta siasa za kubaguana? Baba wa Taifa alipata kutuasa kwamba dhambi ya ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu. Ikianza, haitaishia kwenye ligi pekee na itakwenda hadi mahali tusipotaka. 

MGOGORO WA MASLAHI. 
 Yanga imekuwa ikilalamikia uwepo wa kiongozi mwandamizi wa makampuni ya Bakhresa kwenye bodi ya Ligi na kusema inaleta mgongano wa maslahi.  Sisi vilabu tunaamini kwamba uwepo wa kiongozi huyu ndiyo umesaidia makampuni yake kuwekeza fedha kwenye mpira. Na mifano ipo hai tukianzia na michuano ya Vijana ya Uhai Cup, ujenzi wa kituo cha michezo cha Chamazi ambacho kinatumiwa na timu nyingi za Tanzania.  

Na sasa tunafaidika na udhamini huu mnono ambao haujapata kutokea katika historia ya Tanzania. Tungependa viongozi wengi zaidi wa makampuni yanayoheshimika hapa nchini wakijitokeza kuongoza mpira badala ya kuanza kuwapinga. Kwa mfano tungependa kuona Mkurugenzi wa Benki ya CRDB akiwa kiongozi wa Ashanti, bosi wa Barrick akiongoza Mbeya City na Mkurugenzi wa Tanga Cement akiongoza Coastal Union.  

Hivi ndivyo namna mpira unavyoweza kuvutia wawekezaji. Ndiyo maana tulifurahi wakati Yusuf Manji, alipoomba uongozi Yanga. 
Bado tunataraji kwamba naye atajitosa kuingiza fedha zake kwenye ligi ya Tanzania (mpira) kama alivyofanya Bakhresa ambaye pamoja na kutumia fedha zake Azam FC, bado ameamua kusaidia na timu nyingine kwa ujumla. Tunapenda kumuahidi Yusuf Manji kwamba iwapo naye atataka kudhamini Ligi Kuu iwe kibiashara au kiufadhili, sisi tutamuunga mkono na hatutajali suala la mgongano wa maslahi. 

UPOTEVU WA MAPATO 
Wenzetu Yanga wamedai kwamba kwa kuonyesha mechi kwenye televisheni, mapato yake ya mlangoni yatapungua. 
Hili pia halikufanyiwa utafiti wa kutosha. Katika siku za karibuni, mechi zilizoingiza mapato makubwa zaidi ya milangoni ni zile ambazo zilionyeshwa Live kwenye televisheni za ndani na nje ya nchi. Mifano ni mechi za watani wa jadi msimu uliopita zilizoonyeshwa Live na SuperSport na mechi za Kombe la Kagame zilizoonyeshwa wakati huo.  

Hata mechi ya Taifa Stars na Ivory Coast iliyoonyeshwa Live pia, ilijaza uwanja. Ulaya ambako karibu kila familia inamiliki televisheni na umeme wa uhakika, bado watu wanajaa katika viwanja vya soka. Mpira kuonyeshwa kwenye televisheni unaufanya utangazike zaidi na watu watake kuona. Kuna faida nyingi za mpira kuonyeshwa kwenye televisheni kuliko hasara moja ya kufikirika ambayo Yanga wanaiona. 

Ingekuwa vema iwapo Yanga wangetoa takwimu za kuonyesha ni kwa namna gani mechi kuonyeshwa kwenye televisheni kuliwahi kupunguza mapato ya milangoni. Kwa faida ya umma, mpira kuwa kwenye televisheni kuna faida zifuatazo; jezi kuongezeka thamani na hivyo kuvutia makampuni makubwa kutaka kudhamini klabu wakitumia fursa ya kutangaza bidhaa zao, matangazo ya viwanjani (touchline fence) kuwa na thamani zaidi ambapo kwa sasa vilabu havipati chochote, kuchochea michezo ya kubahatisha, kutabiri matokeo na kupata habari kupitia simu za mkononi na hivyo vilabu vitaanza kutengeneza fedha za kutosha. 

Ulaya wamesonga mbele kutokana na televisheni. Anayekataa mpira kuonyeshwa kwenye televisheni ni sawa na mtu anayegoma kutumia mfumo wa digitali katika ulimwengu wa leo.

UWAZI KWENYE MCHAKATO WA KUUZWA KWA HAKI ZA MATANGAZO
Yanga wameandika kwenye taarifa yao rasmi eti hakukuwa na uwazi kwenye mchakato wa kuipata kampuni ya kurusha matangazo ya Televisheni.
Sote tunajua kuwa vituo vya televisheni vilivyopo nchini kama Star TV ambayo iliwahi kurusha mechi kadhaa msimu uliopita vilikuwa vikijua kuwa kuna nafasi hiyo na TFF mara kadhaa wamekuwa wakitangaza hilo kupitia idara ya Habari ya TFF.  

TFF kwa mfano walikwenda mbali kwa kuialika Supersports kuja kuonesha mechi bure kwa kilichokuwa kikiitwa Super Week ili kuwashawishi waje kuwekeza na mara ya mwisho ni Yanga hawa hawa walioongoza harakati za kuikataa Supersports kuonesha mechi bure wakisema kuwa kama ni kuwavutia inatosha. Katika mazingira kama haya tunastaajabishwa na ukigeugeu wa Yanga leo kusema eti tenda haikuwekwa wazi. Sote tunajua kuwa ni Super Sports pekee tuliokuwa tukiwategemea na kuwashawishi ambao hawakuonesha kuhitaji kuja kuwekeza. Kwa nini leo tuikatae Azam TV?  

Yanga wanaposema eti TFF/Kamati ya Ligi imeipa haki za matangazo kampuni ambayo haina ofisi wala kituo cha televisheni kilicho hewani kwa sasa wanasahau kuwa huko nyuma TFF iliwahi kuwapa haki za matangazo GTV ambao hawakuwa na ofisi wala kituo cha TV na baada ya miezi michache walifungua ofisi zao na kuleta vingamuzi na kuaza kurusha mechi zetu.  

Vilabu vilifaidi udhamini ule kabla ya ile kampuni kufilisika. Kwa hiyo hii si mara ya kwanza kwa jambo hili kufanyika na kama Azam TV hawataonesha mechi za ligi hiyo sisi kama vilabu haituhusu kwani ni hasara yao.  

 Tunachowaomba Azam Media sisi kama vilabu ni kuhakikisha wanatulipa pesa zetu kwa haraka ili zitusaidie kwenye maandalizi,Tunawaomba Yanga wasichafue hali ya hewa kwa kuwa wao hawana shida ya Pesa.  

Sisi Umoja wa Vilabu 13 vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania tunapinga, kwa nguvu zote, madai ya Yanga kwamba hatukushirikishwa kama vilabu kwenye mchakato huu. Mfumo wa ugawanyaji wa mapato tuliouchagua, tuliuchagua wenyewe bila kushurutishwa na yeyote na tunadhani ndiyo mfumo unaotufaa kwa sasa hadi hapo ligi yetu itakapokuwa na nguvu maana kwa sasa inaruhusiwa klabu kupata fedha mwanzoni kulingana na hali halisi ya vilabu vyetu. 

Tunawashauri wenzetu wa Yanga waanze kuamini kwenye kitu kinachoitwa Uwajibikaji wa Pamoja (Collective Responsibility). Mambo yanayoamuliwa kwenye vikao hayapaswi kupingwa nje ya vikao. Kama hoja ililetwa kwenye vikao na ikazidiwa nguvu na hoja nyingine, hakuna sababu ya kuikataa kwa sababu tu hukubaliani nayo. Mfumo wa kidemokrasia una kanuni moja kuu; Wengi Wape.

Imetolewa na
Vilabu 13 vya Ligi Kuu ya Tanzania
 
Simba SC, Azam FC, Ashanti United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, Mgambo JKT, JKT Oljoro, Rhino Rangers, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Kagera Sugar.
 
MWISHO

RAIS KIKWETE AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI LEO


8E9U1937Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza kikao cha baraza la Mawaziri kilichofanyika ikulu jijini Da es Salaam leo.Wapili Kulia ni Makamu wa Rais Dkt.Mohamed Gharib Bilal na watu kulia ni Katibu mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue


POLISI, RAIA 2 JELA MIAKA 7 KWA KUIBA MILIONI 33O ZA JESHI LA POLISI

WATU watatu akiwemo aliyekuwa Polisi, Edna Kadogo wamehukumumiwa kifungo cha miaka saba jela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam baada ya kupatikana na hatia ya kula njama na kuiba Sh milioni 330 mali ya Jeshi la Polisi.

Hakimu Gene Dudu alitoa hukumu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa mashitaka.

Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama, kughushi na wizi wa kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti namba 2011000015 inayoitwa Police Retention Collection kwenye benki ya NMB Meatu.

Akisoma hukumu hiyo , Hakimu Dudu alisema upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka mashitaka mawili dhidi ya washitakiwa watatu na mahakama imewaona wana hatia.

Alisema katika mashitaka ya kula njama watatumikia kifungo cha miaka miwili jela na wizi wa Sh milioni 330 watatumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Adhabu hizo zitakwenda pamoja ambayo ni sawa na kifungo cha miaka mitano. Mbali na Kadogo, washitakiwa wengine waliotiwa hatiani ni mfanyabiashara Joshua Aseno na Mfanyakazi wa Benki, Adelina Lwekoramu.

Baada ya kutoa hukumu hiyo, Hakimu Dudu alimuaru, Aseno arudishe Sh milioni 30 na nyingine zilizoingizwa kwenye akaunti yake kutoka katika akaunti ya polisi na Kadogo anatakiwa kurudishwa milioni 10.

Aidha mahakama imewaachia huru washitakiwa Vedastus Mafuru, Kennedy Achayo, Luciana Limbu, Agnes Maro, Mkika Nyasebwa, Amos Hangaya. kwa kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Kesi hiyo ilikuwa ikikabili washitakiwa 11 lakini Fortunatus Biseko na Deogratias Lumato waliachiwa huru baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu na hivyo wakabaki tisa

Source: WAVUTI


TANGAZO: KUITWA KWENYE USAILI MUHIMBILI NATIONAL HOSPITAL



MWINYI KAZIMOTO: NIMEILIPA SIMBA DOLLAR 40,000 ILI NICHEZE SOKA QATAR

Wiki kadhaa baada ya kutoroka nchini na kukimbilia nchini Qatar kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio ya soka la kulipwa, leo hii kiungo wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba Mwinyi Kazimoto amezungumza rasmi na mtandao huu na kutoa taarifa nzima ya kuhusu sakata lake la kutoroka.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Doha Qatar na Shaffih Dauda, Mwinyi Kazimoto kwanza amekiri kwamba alitoroka kwenda Qatar kwa nia ya kwenda kufanya majaribio, "Safari yangu ya kuja huku Qatar ilibidi iwe kabla hata sijacheza mechi ya marudiano na Ivory Coast, lakini kwa sababu nilikuwa na majukumu nilivumilia nikabaki mpaka nilipocheza mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda, wakati tukiwa kambini kwa ajili ya mchezo wa pili ikabidi niondoke kwa sababu siku zilikuwa zinaenda na muda wangu wa kufanya majaribio ukawa unaisha," anazungumza Kazimoto
Alipoulizwa kama tayari ameshafuzu majaribio aliyoenda kufanya kiungo huyo wa zamani wa JKT Ruvu alisema: "Mwanzoni nilipata vilabu viwili vinavyoshiriki ligi daraja la kwanza ya huku, lakini nikachelewa majaribio na hivyo nikakosa nafasi. Baada ya hapo ndipo ikajitokeza timu ya Al-Markhiya Sports Club - inayoshiriki ligi ya daraja la pili na ikavutiwa nami na ikafanya mipango ya kunisajili."

Taarifa nchini zimeenea kwamba klabu ya Simba imepokea kiasi cha $35,000 kwa ajili ya kumuuza kiungo huyo, Je Kazimoto anasemaje juu ya hili? "Ni kweli kutokana na kwamba nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Simba ilibidi nitoe kiasi cha fedha ($40,000 na sio $35,000 kama inavyoripotiwa) kutoka kwenye ada ya usajili wangu kuununua mkataba wangu uliobakia na Simba.

"Sasa hivi nimefanikiwa tayari kupata timu hii lakini ndoto yangu ni kujitahidi na kuweza kucheza ligi ya juu kabisa hapa. Vilevile ningependa kuwaomba radhi watanzania wote na klabu yangu ya Simba kwa kitendo cha kutoroka wakati nikiwa nahitajika. Nafasi ya kucheza soka la kulipwa ilikuwa ni muhimu kwa maisha yangu na sikutaka niipoteze hivyo naomba wanielewe na kunisamehe."
 
 
 
SOURSE: SHAFFIH DAUDA


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU