Facebook Comments Box

Wednesday, October 17, 2012

KILICHOMUUWA KAMANDA BARLOW CHAHUSISHWA NA KISASI CHA MAPENZI

MWELEKEO wa upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow umebadilika na sasa tukio hilo linahusishwa na kisasi cha mapenzi na tayari mtu mmoja anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi Mwalimu Dorothy Moses kutiwa mbaroni na polisi.Awali, ilidaiwa kwamba Kamanda Barlow ambaye aliuawa kwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi muda mfupi baada ya kumfikisha mwalimu huyo nyumbani kwake, alivamiwa na majambazi. Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI, Robert Manumba alithibitisha jana kukamatwa kwa mtu huyo (jina tulihifadhi) akisema: “Ni kweli mtu mmoja amekamatwa, lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia kwa kina kuhusu suala hilo kwa sababu bado tunamhoji na tunaendelea na uchunguzi. Tutakapokamilisha, tutatoa taarifa.” Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola pia alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, alisema amesikia habari hizo kwa kuwa yuko safarini kwenda mkoani Kilimanjaro kwenye mazishi ya kamanda huyo... “Hayo nimesikia, lakini kwa sasa sipo Mwanza hivyo siwezi kuzungumzia lolote.” Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinaeleza kwamba upelelezi wa mauaji hayo umefanikiwa kwa hatua kubwa na kwamba mtu huyo alikamatwa Dar es Salaam baada ya kuwekewa mtego na makachero waliopo katika timu ya uchunguzi na alisafirishwa hadi Mwanza ambako anashikiliwa na jeshi hilo. Ilielezwa kuwa mtu huyo alikamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa za siri za kiitelejensia kutoka kwa watu mbalimbali. “Kuna hali imefunguka na imesaidia sana. Inaonyesha kwamba Dorothy alikuwa na uhusiano na mtu huyu ambaye alikuwa akifika nyumbani kwake, kama mumewe na watu wanajua jambo hili,” alieleza mmoja wa askari polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini. Alisema kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba uamuzi wa mwalimu huyo kusitisha uhusiano wa mapenzi na mtu huyo huenda ndicho chanzo cha mauaji hayo lengo likiwa ni kumshawishi Dorothy kurejesha uhusiano. “Mimi natambua kwamba huyu jamaa na Dorothy walikuwa na uhusiano na inajulikana mjini kuwa hata mke wa mtuhumiwa anatambua jambo hilo kwani walishagombana siku moja mjini na hata katika msiba nyumbani kwao na mtuhumiwa,” alisema mama mmoja (jina tunalo), aliyejitambulisha kama mmoja wa marafiki wa karibu wa Dorothy. Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri (jina tunalo), anasema amekuwa akimfahamu mtuhumiwa aliyekamatwa kama baba mwenye nyumba hiyo na kila mara amekuwa akimkuta hapo nyumbani wakati wa kujisomea na wanafunzi wenzake. “Mimi ninamfahamu kama baba wa rafiki yangu na nimewahi kumkuta wakati wa kujisomea hapo nyumbani na watoto wa nyumba hiyo.” Dorothy ambaye ametajwa kuwa mjane, ni Mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamagana na tangu kufariki kwa mumewe Ofisa wa zamani wa TRA, Modest Lyimo mwaka 1997. “Watu wote wanajua kwamba mtuhumiwa alikuwa akitembea na huyo mwalimu, wameonekana mara nyingi wakiwa muziki,” alieleza mmoja wa ndugu wa karibu wa mke wa mtuhumiwa. Hili ni tukio la tatu mkoani Mwanza kutokea kwa ofisa wa polisi kuuawa. Katika tukio la awali lililotokea mwaka 1987, askari aliyetambulika kwa jina la Inspekta Gamba aliuawa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi eneo la Nyakato na katika tukio la pili mwaka 1997, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Kati ASP Mahende aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la Bugando saa nne usiku alipokuwa akifuatilia majambazi waliokuwa wakijitayarisha kuvamia. Dar wamuaga Kamanda Barlow Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliongoza waombolezaji waliofika kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Barlow nyumbani kwake, Ukonga Dar es Salaam jana. Mwili wa Kamanda Barlow ambao unasafirishwa leo kwenda mkoani Kilimanjaro kwa mazishi, uliwasili nyumbani kwake saa 6.45 kabla ya kupelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Ukonga kwa ajili ya ibada na kutoa heshima za mwisho. Akitoa salamu za Serikali, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima alisema kifo cha Kamanda Barlow ni pengo kwa taifa... “Tutahakikisha watuhumiwa wanapatikana kwa mikono yote miwili na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.” Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema alisema juhudi za kuwasaka watuhumiwa zinaendelea kwa ushirikianao wa wananchi. “Kifo cha Kamanda Barlow kimeacha pengo kwani hivi sasa askari mmoja analinda watu 1,300 hivyo kwa kifo chake unaweza kuona ni pengo la aina gani na ukilinganisha yeye alikuwa kamanda wa mkoa mzima,” alisema IGP Mwema. Alisema jeshi lake litaendelea kulinda amani ya wananchi na kifo cha Kamanda Barlow kinalifanya liongeze nguvu. Akitoa mahubiri, Padri Veri Urio alisema kila jambo hutokea kwa wakati na kifo cha Kamanda Barlow kimesababishwa na watu. Alisema mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa mtu ni Mungu pekee hivyo waliosababisha kifo chake siku ikifika, watajibu kwa nini walifanya hivyo. IGP Mstaafu, Omary Mahita alisema atamkumbuka Kamanda Barlow kwa uchapaji wake kazi tangu akiwa polisi Interpol (polisi kimataifa)alifanya kazi kwa weledi uliotukuka. “Daima nitamkumbuka kwani nimefanya naye kazi sehemu tofauti na askari waliobaki waige mfano wake wa uwajibikaji” alisema Mahita. Mbali ya Dk Bilal, viongozi wengine walioshiriki katika ibada hiyo jana ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), makamanda wa polisi, viongozi wa Serikali na vyama vya siasa na wananchi.

 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU