Facebook Comments Box

Sunday, May 12, 2013

MANCIN ATIMULIWA KAZI MANCHESTER CITY



Roberto Mancini sasa si kocha mkuu tena wa Manchester City, imeelezwa.
Nafasi ya Muitaliano huyo itachukuliwa na kocha wa Malaga, Manuel Pellegrini.

Bado haijajulikana rasmi ataondoka leo usiku, kesho au keshokutwa lakini inaonekana hakuna uhakika kama atakuwepo kwenye benchi kesho wakati City watakapokuwa wakiivaa Reading.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Man City zinaeleza, uamuzi wa kumtimua Mancini ulichukuliwa katika kikao cha pamoja kilichowajumuisha mabosi wawili Ferran Soriano, Txiki Begiristain na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Khaldoon Al Mubarak ikiwa ni siku moja tu baada ya City kuchapwa bao 1-0 katika mechi ya fainali ya Kombe la FA.


 The Sun la Uingereza lilifanya juhudi za kumnasa Mancini ili azungumzie suala hilo lakini haikuwezekana lakini kumekuwa na taarifa amebanwa kwa kuwa anashughulikia suala la malipo ya fedha zake baada ya mkataba wake kusitishwa.
 
Ingawa yeye alisema jana amebakiza miaka minne na City, lakini taarifa zinaeleza ana miaka mitatu iliyosalia na alisaini baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England.

Jana, Mancini aliushambulia uongozi wa City kwa madai haukuonyesha juhudi za kukanusha kwamba ulikutana na wakala wa Pellegrin na aliyehusishwa kufanya naye mazungumzo ni Txiki.

Taarifa za Txiki kukutana na wakala wa Pellegrini zilianza kuchukua nafasi tokea wiki iliyopita na uongozi wa City ulionekana kuwa kimya kabisa kuhusiana na suala hilo.

Pamoja na kuipa City ubingwa wa Ligi Kuu England, Mancini aliibebesha Kombe la FA msimu huu.

Kwa kifupi, msimu huu pamoja na kushika nafasi ya pili, wamevulikuwa makombe yote waliyokuwa nayo msimu huu na uliopita.



TAMKO LA WATETEZI WA HAKI ZA BINAADAMU DHIDI YA VURUGU NA KUTISHWA KWA WANAHABARI

TAMKO LA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU DHINI YA AGENDA ZA KUVURUGA AMANI YA NCHI NA VITISHO KWA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU NCHINI TAREHE 11 MACHI, DOUBLE VIEW HOTEL SINZA, DAR ES SALAAM 
Watetezi kutoka mikoani ambao ni wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini (THRD-Coalition), waliokutana kwa siku tatu jijini Dar es Salaam, pamoja na kupata mafunzo adhimu ya usalama kwa watetezi yatolewayo na THRD-Coalition, pia walifanya tathmini ya hali ya usalama kwa watetezi nchini; asasi za haki za binadamu, waandishi wa habari na watu wanaojitolea katika eneo la msaada wa kutetea wenzao yaani (volunteers). Tathmini imeonyesha kwamba yapo mambo kadhaa yanayosababisha kukosekana kwa usalama kwa watetezi nchini na kupotea kwa amani.

1. Utendaji wa Vyomba Serikali na Vuguvugu la Kisiasa

Serikali ndicho chombo chenye jukumu la kuwalinda watetezi wa haki za binadamu na watu wengine waliomo ndani ya mipaka ya nchi yetu, wao na mali zao. Vitendo vya watu kujichukulia sheria mikononi mwao, kuteka, kutesa, kung’oa meno, na macho, kukata vidole na hata kuwarushia bomu waamini wakiwa katika maeneo ya maombi ni ishara ya dhahiri ya serikali iliyoshindwa kutimiza majukumu yake. Vitendo vya baadhi ya viongozi nchini hasa katika ngazi za Serikali za Mitaa kuwakandamiza watetezi wa haki za binadamu kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwafungulia kesi za kubambikiza vimefikia kiwango cha kutovumilika. Matamko mengi yanayotolewa na viongozi wa juu wakiwamo mawaziri dhidi ya watetezi na asasi za haki za binadamu nchini yanaonyesha kuwa ni viashiria vya vitisho vya kiusalama wazi wazi kwa watetezi nchini. Pia watetezi wamekuwa wakishutumiwa kuwa ni wapinzani kwa sababu kazi zao zimekuwa zikilinganishwa na kazi za vyama vya upinzani na za kiuchochezi.
Kuwa mtetezi ni kiungo muhimu katika kuibua na kufichua maovu ili kujenga utawala unaoheshimu haki za binadamu, lakini siku zote tumejikuta tukihatarisha maisha yetu. Katika mazingira ya aina hiyo watetezi hawawezi kujiweka katika kundi salama hata kidogo, bali kwamba usalama wao umo hatarini kwa sababu kazi nyingi wanazozifanya huwalazimisha kuikosoa serikali pale inapokuwa haitimizi wajibu wake kuhusiana na kulinda haki za msingi za binadamu na haki nyinginezo stahiki. Mifano halisi ya migongano kati ya asasi na serikali ni kesi za kugombea ardhi Pugu, Loliondo, Bagamoyo na migogoro isiyoisha katika migodi mkoani Mara.

2. Wamiliki wa vyombo vya habari

Katika kudadisi ni kwa nini wanahabari wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama iligundulika kwamba wamiliki wa vyombo hawana mikakati mizuri juu ya suala zima la usalama kwa waandishi wao. Pia malipo finyu kwa wanahabari ilionekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa sababu baadhi yao hawapati malipo ya uhakika wala mikataba. Hali hiyo husababisha waandishi waishi maisha ya kubahatisha na wakati mwingine hujikuta wakishawishika kuingia katika makundi ya kisiasa ili kuanza kuvitumikia ‘vyanzo vyao’ jambo ambalo husababisha wakiuke maadili ya kazi zao na mwisho hushambuliwa na wale wanaoguswa na habari za aina hiyo. Aidha watetezi wanawasihi wamiliki kuanza kuweka mikakati ya kiusalama kwa waandishi na kuboresha mishahara kwa waandishi ili wafanye kazi kwa uhakika zaidi.

3. Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi wawe makini na matumizi ya silaha za moto na nguvu za ziada ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu wa kudumu. Katika purukashani nyingi za kisiasa jeshi hilo limeshindwa kabisa kuonyesha kwamba linafanya kazi ya kuutumia umma wa Watanzania wote na badala yake limekuwa likichukua mwelekeo wa kuwatumikia wanasiasa au chama fulani. Aidha askari polisi wanakumbushwa kwamba wao ni sehemu ya jamii na hao wanaowatesa ni ndugu zao wa karibu wadogo zao mama zao n.k. Jeshi la Polisi litambue kuwa kazi za watetezi wa haki za binadamu ni kazi halali zinazolindwa kisheria na wanajukumu la kuweka mazingira mazuri ya watetezi kufanya kazi zao bila kutekwa, kuteswa ama kungo’lewa macho, meno, kucha n.k. Mfano halisi wa mapungufu ya jeshi hilo ni kukamatwa kwa askari hivi karibuni waliokuwa na fuvu la kichwa cha mtu mkoani Morogoro kwa lengo la kumbambika mtu kesi ya jinai. Tunaisihi Serikali na Jeshi la Polisi kuanza kutekeleza Tamko la Umoja wa Mataifa la tarehe 15 Machi 2013 linalotaka mataifa yote kutambua umuhimu na uhalali wa majukumu ya watetezi wa haki za binadamu katika kutetea haki za binadamu demokrasia, utawala wa sheria, kama nyenzo la kuhakikisha usalama wao ikiwa ni pamoja na kuheshimu uhuru wa asasi zao na kuepuka kunyanyapaa shughuli za asasi za kiraia.

4. Wanaharakati na Watetezi wa Haki za Binadamu

Wanaharakati wote na watetezi wa haki za binadamu wasichukue upande wowote katika masuala ya itikadi za kisiasa kwani wao ni watu wa kati. Pia wanaharakati wasijiingize katika matumizi ya nguvu au kupambana na Jeshi la Polisi. Aidha wanaharakati wametakiwa kuwa waelimishaji wa umma na kujizuia kujiingiza katika mambo yaliyopandikizwa na watu wasioitakia mema nchi yetu kama vile udini na migogoro isiyoisha ya kugombea ardhi, maeneo ya malisho, ukabila n.k.

5. Vurugu za Udini

Kwa miaka mingi Tanzania haikuwahi kupata misukosuko ya udini kama inayotokea sasa. Lakini kwa miaka ya hivi karibuni uhasama wa kidini umezidi kushamiri. Watetezi kwa umoja wetu tunaamini Tanzania hatuna udini bali kinachoendelea ni ajenda za watu fulani kwa maslahi binafsi ama ya kifedha, kidini au kisiasa. Kwa sasa nchi inaweza kutumbukia katika machafuko ya kidini endapo viongozi wa dini zote, wanasiasa na serikali hawatachukua hatua za makusudi kuwakomesha wachache hao ambao wanataka kuondoa amani ya nchi. Katika mazingira haya pia mtetezi wa haki za binadamu hawezi kubakia salama na ndio maana tunakemea kwa nguvu zote vitendo hivi viovu.

6. Watanzania Wote Kwa Ujumla

Watanzania katika ujumla wao wameaswa kuwa makini hususani wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Wapo watu wanaochomekea ajenda zao kwa malengo wanaoyafahamu wao wenyewe na hivyo kuligawa taifa katika misingi ya udini na mambo mengine kama hayo yasiyo na tija wala manufaa kwa nchi yetu. Aidha Watanzania wameshauriwa kuirejea kazi nzuri ya kuwaunganisha ambayo iliifanya nchi hii ifahamike kama kisiwa cha amani miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.

Mwisho tunaungana na watanzania wengine kulaani kitendo cha kutupa mabomu katika mikusanyiko ya watu kama ilivyotekea kule Arusha. Tunawapa pole wafiwa na majeruhi wote. Na kutaka watanzania wote bila kujadili itikadi zao kuendelea kulaani vitendo hivi vya kinyama.

TAMKO HILI LIMEANDALIWA NA WATETEZI 30 WA HAKI ZA BINADAMU TOKA MIKOA MBALIMBALI KWA NIABA YA WENZAO KATIKA AZIMIO LA KUIREJESHA NCHI HII KATIKA HALI YA AMANI NA UTULIVU



MAJESHI YA TANZANIA YAFIKA DRC CONGO

 
Umoja wa Mataifa (UN) umearifu kwamba kundi la kwanza la wanajeshi (TANZBATT 1-DRC) 100 kutoka nchini Tanzania limewasili Jumamosi hii katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mpango wa amani wa UN wa kukabiliana na makundi ya waasi.

Tanzania inatarajia kupeleka jumla ya wanajeshi wake 1,280 katika mpango huo.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa azimio la Machi 28 lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC wa kuunda brigedi maalumu ya kupambana na waasi katika eneo la mashariki mwa DRC.

Msemaji wa mpango huo Felix Basse amesema Tanzania imekuwa ni nchi ya kwanza kupeleka wanajeshi wake katika eneo hilo, wanajeshi zaidi toka Malawi na Afrika Kusini wanaarajiwa kujiunga na kikosi hicho wakati wowote kuanzia hivi sasa.

Wanajeshi zaidi ya 3,000 watadhibiti makundi ya waasi zaidi ya 25 katika mkoa wa Kivu pekee. Tayari kundi la waasi la M23 limeripotiwa kujiandaa ili kujibu mashambulizi yatakayoelekezwa kwao na vikosi hivyo.

Jeshi la DRC kwa muda mrefu limeshindwa kutokomeza makundi la waasi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo, hata hivyo mamlaka za nchi hiyo zinatarajia mpango wa sasa wa UN huenda ukazaa matunda mema kwa usalama wa nchi hiyo.



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU