Picha ikionesha heliKopta ikiwa
inapeleka chakula na maji kwa waanga walioshindwa kushuka kwa kutumia
miamvuli maalum katika mlima kilimanjaro
Marubani waliopanda mlima
Kilimanjaro kwa ajili ya kuruka kutoka kileleni kwa kutumia miamvuli
maalum wanaendelea kusota baada ya hali mbaya ya hewa kuwazuia
kutekeleza azma yao.
Wakiwa wametimiza siku 11 sasa
tangu waanze safari yao mlimani, inaripotiwa kuwa hivi sasa wameanza
kuishiwa akiba ya chakula na helikopta iliyosheheni maji na shehena
nyingine ya vyakula imeruka kwenda kileleni siku ya Jumatano ili
kuvidondosha kwa wahanga hao.
Marubani hao zaidi ya 100
walikuwa wanatarajiwa kuruka kutoka kilele cha Mlima Kilimanjaro kwa
kutumia miamvuli maalum (Paragliding)na kutua eneo la Kibosho siku ya
Jumanne, lakini hadi leo hii (Alhamisi) bado wako mlimani.
Mkuu wa Hifadhi ya Mlima
Kilimanjaro Erastus Lufungulo amesema hali ya hewa mlimani hapo bado
inaendelea kuchafuka kwa upepo mkali na mawingu mazito.
Marubani hao wa kimataifa,
wanatoka nchi mbalimbali duniani, walitarajiwa kuwa binadamu wa kwanza
kabisa kuruka kutoka kilele hicho kirefu zaidi barani Afrika.
Helikopta maalum ilitumwa mara
kadhaa kuzunguka mlimani kwa siku mbili mfululizo ili kujaribu kuona
marubani hao 100 wakiwemo wanawake 30 watakuwa wamefika wapi. Na siku ya
jumanne usiku, watu 15 waliokuwa kwenye timu hiyo walirudishwa chini na
kukimbizwa hospitali baada ya kuugua.
“Ni kweli zoezi limeshindikana
hadi sasa ila hatuna wasiwasi na usalama wa watalii hao kwani tumekwisha
kujiandaa kwa huduma zote za uokoaji,” alisema Afisa Habari wa Shirika
la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Paschal Shelutete.
Shelutete amesema hii ni mara ya
kwanza kabisa tukio hili la kuruka kutoka kilele cha Kilimanjaro kwa
kutumia miamvuli kufanyika nchini na kwamba likifanikiwa litajumuishwa
kuwa miongoni mwa vivutio vipya vya utalii.
Marubani hao walianza kupanda
mlima tarehe 27 Januari na ilitarajiwa kuwa wangeruka kutoka kilele cha
Uhuru siku ya tarehe 5, wakielea kutumia miamvuli hiyo maalum, ikiwa ni
tukio la kwanza kabisa kufanyika nchini.
Mratibu wa taasisi ya ‘Wings of
Kilimanjaro,’ ya Australia, inayoratibu zoezi hilo, Bi Paula McRae
amesema zoezi hilo pia litasaidia kuchangia fedha kiasi cha dola
millioni moja za kimarekani kwa ajili ya kusaidia jamii zinazounguka
mlima huo mrefu zaidi barani Afrika.
Picha ikionysha mwanamama aliyekuwa katika hali mbaya na kuamua kulala chini huku akimhofia mumewe alipanda mlima mara baada ya kupata taarika kuwa hali ya mlima huo bado ni tete
Hapa ni baada ya heliKopta kurudi chini ambapo kamera ilifungwa na baadae kuleta hali halisi ya mlima huo …..hapa ndugu jamaa na marafiki wa marubani wakiwa wanaangalia video ya tukio hilo
Kikosi kazi cha waandishi wa habari walioweka kambi maalum kuwasubiri watalii kushuka kutoka mlima Kilimanjaro kwa kutimia miamvuli,zoezi ambalo halikuzaa matunda(picha zote na jamiiblog.co.tz)