Facebook Comments Box

Tuesday, August 20, 2013

YANGA YABURUZA MKIA KATIKA MSIMAMO WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA:

Kabla ya kuanza kwa Msimu wa ligi ya Vodacom Tanzania Bara msimamo huwa kama unavyoonekana hapo pichani, timu zimepangwa kwa kufuata mtiririko wa majina (Alphabetic Order) kwamba timu zenye herufi 'A' huwa zakwanza kama wanavyo onekana ASHANTI ya Ilala wakiwa juu kabisa ya msimamo huo wakati Mabingwa wa mwaka jana 2012 / 2013 YANGA wao wakiwa wanaburuza mkia.

Lakini mambo hugeuka pindi mtanange huo unaotarajiwa kuanza rasmi siku ya Jumamosi ya tarehe 24/08/2013 ambapo Ratiba ya siku hiyo timu zote 14 zitakuwa uwanjani kama ifuatavyo:-

YANGA vs ASHANT(U/Taifa), MTIBWA vs AZAM(Manungu), JKT OLJORO vs COASTAL UNION(Sh. Amri Abeid), MGAMBO JKT vs JKT RUVU(Mkwakwani), R.RANGERS vs SIMBA(Ally H.Mwinyi), MBEYA CITY vs KAGERA SUGAR(Sokoine), R.SHOOTING vs PRISONS(Mabatini).  





HALI SI SHWARI MISRI WAFUASI WA MORSI 38 WAUAWA GEREZANI



Kiongozi mmoja wa usalama nchini Misri ametangaza kuwa, wanachama 38 wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin wameuawa, katika tukio la mapigano kati ya askari polisi na watu waliokuwa na silaha, waliotaka kuwatorosha watu hao kutoka gerezani. 
 
Habari zinasema kuwa, mapigano hayo yalitokea karibu na jela ya Abu Zaabal katika mkoa wa al-Qalyubiyah. Aidha wafungwa hao walikuwa wamemteka polisi mmoja katika mapambano hayo.
 
 Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Misri imetangaza kuwa, polisi walifanikiwa kumuokoa polisi huyo ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya. Jana wafuasi wa Ikhwanul Muslimin walisitisha maandamano mjini Cairo kwa kile walichosema kuwa ni kuepusha umwagikaji damu zaidi dhidi yao.  
 
Ripoti iliyotolewa na harakati hiyo, ilisema kuwa, Ikhwan wameamua kusitisha maandamano yao, kutokana na kuwepo hali tete nchini humo. Kabla ya hapo, ilikuwa imepangwa kufanyika maandamano ya nchi nzima, kwa ajili ya kutaka kurejeshwa Muhammad Mursi, Rais halali wa Misri aliyepinduliwa na jeshi la nchi hiyo.




SAFARI NZIMA YA SHEIKH PONDA NA YALIYOJIRI

Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda alisafirishwa jana kwa helikopta kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa kujibu mashtaka yanayomkabili.

Ponda jana alianza kwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu asubuhi na kufutiwa mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili baada ya kusomewa mara ya kwanza Agosti 14, mwaka huu akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kumshtaki.

Alidaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.

Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi na baadaye alipandishwa kizimbani na kufutiwa kesi hiyo, baada ya Wakili Kweka kuwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Hata hivyo, baada ya kufutiwa mashtaka hayo, aliendelea kushikiliwa na kisha akachukuliwa na kupelekwa Morogoro ambako pia alisomewa mashtaka ya uchochezi.

Kuwasili Moro

Sheikh Ponda aliwasili kwa helikopta ya polisi na kutua kwenye Uwanja wa Gofu, Morogoro akiwa chini ya ulinzi wa polisi na alipakiwa kwenye gari maalumu ambalo liliongozana na magari mengine matatu ya polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama ukiwajumuisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), askari wa upelelezi, Usalama wa Taifa pamoja na mbwa wa polisi na kusababisha shughuli za kazi katika Mahakama hiyo na ofisi za jirani kusimama kwa muda.

Baada ya kufika mahakamani saa tano asubuhi, magari yalisimama kwa takriban dakika 30 kabla ya kumtoa na kumwongoza kwenye Mahakama ya wazi ambayo tayari ilikuwa umejaa watu.

Baada ya kumalizika kusomwa kwa kesi hiyo, msafara uleule ulimrejesha Uwanja wa Gofu saa sita mchana na kupandishwa kwenye helikopta kurejea Dar es Salaam.

Mahakamani Morogoro

Ponda alisafirishwa kwa helikopta ya polisi hadi Morogoro na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi akiwa chini ya ulinzi mkali.

Wafuasi wa Ponda wapiga kambi Segerea

Mara baada ya kumfikisha katika Mahakama hiyo iliyofurika mamia ya waumini na wafuasi wake, Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alimsomea mashtaka matatu yanayomkabili.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate alisema: “Agosti 10, mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro Ponda Issa Ponda, aliwaambia wafuasi wake.

“Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watakuja kwenu na watajitambulisha kwamba wao ni Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana.”

Kongola alisema kauli hiyo ilikuwa ikiumiza imani za watu wengine na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lililotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, mwaka huu ikimtaka kuhubiri amani ndani ya mwaka mmoja na kwenda kinyume na kifungu cha Sheria namba 124 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Ponda alikana.

Katika shtaka la pili, Ponda anadaiwa Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro aliwaambia Waislamu kuwa Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.

Alisema Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo na kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine jambo ambalo ni kinyume cha Kifungu cha Sheria 129 cha mwaka 2002, shtaka ambalo pia alikana.

Shtaka la tatu linafanana na lile la pili lakini na upande wa mashtaka ulieleza kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha Kifungu 390 cha Sheria na Kanuni ya Adhabu namba 35 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Sheikh Ponda alilikana. Baada ya kusomwa kwa mashtaka yote matatu, wakili wa Serikali aliiambia Mahakama kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na kupanga kesi kuanza kusikilizwa Septemba 2 mwaka huu. Upande wa utetezi uliomba Mahakama kupanga kuanza kusikilizwa kwa kesi Agosti 26, mwaka huu.

Hakimu Kabate aliwapa mawakili kujadiliana na baadaye kuomba kesi hiyo ianze kusikilizwa Agosti 28 mwaka huu.

Wakili alalamika

Akizungumza Dar es Salaam jana, Wakili wa Ponda, Juma Nassoro alilaani kitendo cha kuondolewa kwa mteja wake gerezani na kwenda kusomewa mashtaka mapya Morogoro bila taarifa.

Alidai kuwa polisi wanaendelea kukiuka taratibu za kumshikilia kiongozi huyo kutokana na kufanya mambo kinyume na sheria kwa lengo la kutaka waumini kufanya vurugu ili waendelee kumshikilia kiongozi huyo.
“Kitendo cha kumuondoa mteja wangu gerezani na kwenda kumsomea shtaka jingine Morogoro nimelilaani. Sijalipenda. Polisi hawakuwa na nia nzuri na Ponda kwa sababu sheria zinajulikana na kila mtu ana haki ya kutetewa,” alisema Nassoro.

Akizungumzia kufutiwa kesi Mahakama ya Kisutu, Nassoro alisema Serikali imeamua kufuta kesi kabla ya kusikilizwa baada ya kuona imeelemewa kwani alishapeleka maombi ya kuirudisha Mahakama Kuu kutoka Kisutu kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na maombi hayo yalipewa namba 11/2013.

Msemaji wa familia, Isihaka Rashidi alisema: “Hawa jamaa wamempeleka Morogoro kwa siri kwa sababu jana (juzi) tulikwenda Segerea hakukuwa na hizo taarifa. Tumekuja kushtuka asubuhi baada ya mke wake kwenda kumpelekea chai na kuambiwa ameondolewa na kupelekwa Morogoro.”

Alisema baada ya kupata taarifa hizo iliwalazimu kuwasiliana na ndugu zao waliopo Morogoro kwa ajili ya kwenda mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

*Imeandikwa na Lilian Lucas na Hamida Sharrif (Morogoro), James Magai, Aziza Masoud na Aidan Mhando, Dar. (Gazeti la Mwananchi)



PROF WARIOBA ATEULIWA NA RAIS KUWA MKURUGENZI WA TSN



UDA YAPELEKA MABASI MIKOANI KWA AJILI YA WANAFUNZI: YAWEKA PIA MABASI KWA AJILI YA WANAWAKE NA WALEMAVU

Wanafunzi wa mikoa mbalimbali nchini wataondokana na kero ya usafiri wa daladala baada ya kampuni ya UDA kuingiza magari 10 kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi ili kuwahi masomo.

Aidha, wanawake, wanaume na watu wenye ulemavu watakuwa na mabasi maalumu ambayo yatatoa huduma mikoani. 

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Ofisa Rasilimaliwatu wa UDA, Cyprian Malekela alipozungumza na waandishi wa habari jinsi kampuni hiyo inavyopambana na changamoto za usafiri ukiwamo uboreshaji wa huduma za usafiri mikoani.

Alisema kampuni hiyo kwa kuanzia, itatoa mabasi 10 ya wanafunzi kila mkoa na itaanza na Mwanza, Dodoma, Iringa, Mbeya na Arusha na sasa iko katika hatua ya mwisho ya mazungumzo na walimu wakuu wa shule za
msingi na sekondari ili kujua vituo watakavyopandia wanafunzi na muda wa kuwachukua na kuwarudisha.

Malekela alisema kampuni hiyo itakuwa na magari mengine 15 ya wanawake ambao hawawezi kugombania magari, 10 kwa ajili ya wanaume huku mengine sita yakiwa ni maalumu kwa watu wenye ulemavu.

"Kampuni imedhamiria kuboresha huduma zake kwa kuongeza idadi ya magari kwa ajili ya wanafunzi, wanawake, walemavu na wanaume lengo ni kutoa huduma za usafiri kila mkoa ili kuboresha huduma ya usafiri na kuondoa kero kwa wananchi wanaohitaji usafiri wa uhakika," alisema.

Aliongeza kusema kwamba awali kampuni hiyo kabla haijabinafsishwa ilikuwa ikimilikiwa na Serikali huku ikiwa na magari saba, lakini sasa iko mikononi mwa Mtanzania ambaye ameongeza idadi ya magari hadi 40.

Alisisitiza kuwa UDA imedhamiria kuboresha huduma za usafiri kila mkoa na kutoa rai kwa wamiliki wa kampuni na taasisi nchini kukodisha magari hayo ili yatoe huduma na hata madereva na wahudumu wa mabasi ya UDA wamepewa mafunzo maalumu ya kuhudumia abiria. -- HabariLeo



PICHA: KWA UCHACHE MAANDAMANO YA CHADEMA MWANZA

Chini ni picha kwa uchache maandamano ya wafuasi wa chadema jijini Mwanza kwa ajili ya kumng'oa meya wa jiji hilo.  Wafuasi hao wanadai hana uhalali wa kuwa madarakani



PICHA: WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YA SKOL WAKIFANYAKAZI BILA VIFAA MAALUMU VYA KAZI

Picha chini ni wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya Skol ambao kwa sasa wanatengeneza barabara ya tabata wakiwa wanasafisha barabara eneo la tabata posta bila vifaa vya kuzuia vumbi puani mwao.



PICHA: CHADEMA MKOANI KAGERA KATIKA KUJADILI KATIBA MPYA

Picha chini zikionesha viongozi wa ngazi za juu wa chama cha demokrasianna maendeleo chadema walivyofika mkoanI Kagera katika kujadili kuhusu mabaraza ya katiba mpya na katiba mpya kwa ujumla.



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU