Mabehewa Mapya yakishushwa bandarini baada ya kuwasili nchini tayari kwa safari.
Moja wapo ya behewa jipya kama linavyoonekana kwa ndani hapo ni kitanda katika behewa la kulala.
Moja wapo ya behewa jipya kama linavyoonekana kwa ndani sehemu ya kukaa abiria
Moja wapo ya behewa la zamani katika muonekano wa ndani abiria wakiwa wamekaa tayari kwa safari.
Treni ya Zamani ikiwa ndo inaanza safari yake ya kwenda Kigoma, Tabora na Mwanza.
Mamlaka ya huduma za usafiri wa nchi kavu na majini SUMATRA imekutana na wadau wa usafiri wa reli mjini Dar es salaam, lengo likiwa ni kupokea na kujadili mapendekezo ya nauli ya huduma mpya ya usafiri huo, unaotarajiwa kuanza katikati ya mwezi Januari 2015, baada ya shirika la reli TRA kupokea mabehewa mapya na vichwa ambapo itafanya safari zake kutoka Dar es salaam, Mwanza na Kigoma.
Usafiri huo mpya utakuwa katika madaraja matatu(3) ambapo behewa la daraja la pili likiwemo lenye vitanda litakuwa na vyumba 6 kila behewa ambapo kila chumba kitakuwa na abiria 6 na kufanya jumla ya abiria katika behewa moja kuwa 36.
Aidha daraja la pili lingine litakuwa na mabehewa yenye viti ambavyo vitachukuwa abiria 60 na daraja la tatu litakuwa na mabehewa yenye uwezo wa kuchukuwa abiria 80 kila behewa wakiwa wamekaa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa (SUMATRA) Giriad Gewe, amesema mapendekezo hayo yatazingatia vigezo muhimu ambavyo vitalinda maslahi ya pande zote mbili (Mtoa huduma na Mtumiaji).
Zikiwemo gharama za uwendeshaji na viwango vya ushindani na kuahidi kuwa baada ya siku 14 SUMATRA itakuwa na maamuzi ambayo yameridhiwa.
Nae Mkuu wa Masoko wa TRL Bwana Charles Ndege amesema kuanzishwa kwa huduma kutaimarisha uwezo katika utendaji wa shirika hilo kwa kuongeza utoaji wa huduma hadi kufikia mara tatu kwa wiki ikilinganishwa na awali ambapo imekuwa ikitoa huduma mara mbili kwa wiki.
Aidha huduma hiyo itaendana na wakati kwa kuwapunguzia safari ndefu wasafiri hususan wafanya biashara kwa kuwa na vituo 14 kwa safari nzima badala ya 54 vya awali.
Bwana Ndege amesema Nauli ya kutoka Dar es salaam mpaka Mwanza itakuwa ni 76,400/= kwa daraja la pili kulala, na Shilingi 44,400/= kwa daraja la pili kukaa, huku shilingi 38,100/= kwa daraja la tatu kukaa.
Treni hiyo ambayo haitaruhusu abiria kusimama itakuwa na uwezo wa kubeba abiria wapatao 800 daraja la tatu, 360 daraja la pili kukaa na abiria 200 wa daraja la pili kulala na itakuwa na behewa moja kwa ajili ya maakuli na viburudisho.
Baadhi ya wadau wameelezea kutoridhishwa na viwango hivyo vya nauli kwa madai kwamba vipo juu na kuboresha huduma ya mabehewa na vichwa haitakuwa na maana endapo miundo mbinu yake bado itakuwa ni ya zamani na isiyokuwa na uhakika kwa usafiri.
Afisa elimu wa SUMATRA Bwana Nicolas Kinyariri alitoa maoni kwa niaba ya SUMATRA kuwa:
- Nauli zilizo wasilishwa hazija zingatia hali halisi ya usafiri wa Tanzania ya leo na Tanzania ya kesho,Nauli za Treni za abiria zinapaswa kuwa nafuu sana zikilinganishwa na usafiri wa mabasi.
- Baraza linashauriwa kwamba TRL waendelee na nauli zilizopo ambazo zinaweza kuhimili ushindani na nauli za mabasi japo kwa miezi siat (6) kushawishi abiria kuwa huduma zimebadilika
Nae Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA Bwana Giriad Gewe amesema nauli hizo zinaweza kubadilika kutokana na maoni ya wadau hivyo amepongeza ujio mpya wa TRL kwani utaweza kuleta mabadiliko katika sekta ya usafirishaji ikiwemo kupunguza ajali za barabarani zinazo sababishwa na mabasi.