BAADA ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DDP) kulitaka Jeshi la Polisi kumwachia mtuhumiwa Mussa Omar Makame kutokana na ushahidi kutojitosheleza, jeshi hilo sasa limeingia kwenye mkorogano.
Katika mahojiano, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa A. Mussa, alikanusha jeshi la polisi kushirikiana na kikosi cha upelelezi cha Marekani (FBI) ili kumkamata Makame.
Kauli yake inakinzana na ile aliyoitoa Machi 23, mwaka huu aliposema uchunguzi huo ulikuwa ukifanywa na makachero wa polisi kwa kushirikiana na wapelelezi kutoka Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kufanikisha kumkamata mtuhumiwa huyo.
Katika mkorogano huo wa taarifa kuhusu Makame, tamko rasmi la Jeshi la Polisi nchini lililotumwa kwa vyombo vya habari halikumtaja mtuhumiwa kwa jina likidai uchunguzi unaendelea lakini Kamishna Mussa alimtaja kuwa ni Mussa Omar Makame.
Kamishna Mussa jana alilieleza kuwa licha ya DPP kusema Makame hana hatia, wataendelea kumshikilia kwa uchunguzi zaidi.
“Sisi tutaendelea kumshikilia hata kama DPP hakuridhika na upelelezi tuliofanya, tuna taratibu mbalimbali ambazo si lazima kuzitaja kwa sasa,” alisema.
Alipotakiwa kufafanua kama ni kweli FBI hawakushirikiana nao katika uchunguzi huo, kamishna huyo aliomba apigiwe simu baadaye kwa madai kuwa alikuwa na kazi, lakini alipotafutwa tena hakupokea simu.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Isaya Mungulu, alipotakiwa kuzungumzia mkorogano huo wa kauli, alidai apigiwe Kamishna wa Zanzibar ndiye anayejua vizuri.