Facebook Comments Box

Tuesday, October 21, 2014

MAPATO YA MECHI YA YANGA VS SIMBA TAIFA ILIYOCHEZWA JUMAMOSI



Y

VIKOSI VYA YANGA NA SIMBA VIKIINGIA UWANJANI KATIKA MPAMBANO HUO AMBAPO HAKUKUWA NA MBABE BAADA YA KUTOKA 0-0.

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba iliyochezwa juzi (Oktoba 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 427,271,000.

Washabiki 49,542 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambapo viingilio vilikuwa sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 20,000 na sh. 30,000. Asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 65,176,932 wakati asilimia 5 ya gharama ya tiketi kwa CRDB ni sh. 21,363,550.

Kwa upande wa Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) ambayo ni sh. 1,000 kwa kila tiketi, timu mwenyeji Yanga imepata sh. 17,339,700, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 7,431,300 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 24,771,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni Uwanja sh. 43,678,277.67, gharama za mchezo sh. 24,751,024.01, Bodi ya Ligi sh. 23,295,081.42, TFF sh. 17,471,311.07, DRFA sh. 10,191,598.12, timu mwenyeji Yanga sh. 100,460,038.64 na timu ngeni Simba sh. 71,341,186.86.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA.


KUHAMISHIA DALADALA KITUO CHA SIMU 2000 (NYUMA YA MAWASILIANO TOWERS) KUANZIA ALHAMIS TAREHE 23.10.2014

Baada ya kituo cha Simu 2000 kukamilika SUMATRA kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni na Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Kinondoni tumekubaliana kufungua kituo hiki tarehe 23.10.2014 asubuhi, kwa daladala ambazo zilikuwa zinaishia au kuanza safari katika kituo cha daladala Ubungo.

Kila dereva anatakiwa kufuata utaratibu ulioelekezwa hapa chini ili kuondoa usumbufu usio na tija.

1. DALADALA ZINAZOTOKA MASAKI

zikifika barabara ya Shekilango zitaingia kulia kwa kutumia barabara ya TANESCO inayokwenda moja kwa moja kituoni simu 2000 na zitarudi barabara ya Shekilango kwa kutumia njia hiyo hiyo ya TANESCO.

2. DALADALA ZINAZOTOKA KARIAKOO, POSTA na KIVUKONI

zikifika mataa ya Ubungo zitaingia kulia (barabara ya Sam Nujoma) kwenda kituoni Simu 2000, zitarejea zilikotoka kwa kutumia barabara hiyo hiyo

3. DALADALA ZINAZOTOKEA BARABARA YA MANDELA

zitavuka mataa ya Ubungo (kwa kutumia barabara ya Sam Nujuma) na kwenda kituoni Simu 2000, zitarejea zilikotoka kwa kutumia barabara hiyo hiyo.

4. DALADALA ZINAZOTOKEA MWENGE

zikikaribia jengo la Mawasiliano Towers zitachepukia kushoto kwa kutumia service road inayopita mbele ya Mawasiliano Towers hadi kituoni simu 2000, zitarejea zilikotoka kwa kutumia barabara ya Sam Nujoma (sio servive road).

5. DALADALA ZINAZOTOKEA KIMARA NA MBEZI

zikifika mataa ya Ubungo zitaingia kushoto kwenda kituoni simu 2000. zitarejea zilikotoka kwa kutumia barabara hiyo hiyo.

Conrad Shio
Afisa Mfawidhi SUMATRA –DSM
0755 660 016


DIAMOND KUSIMAMA KIZIMBANI??


 Naseeb Abdulmaliki (Diamond Platnum) akiwa na sare za Jeshi
Hapa akiwa jukwaani

Msanii nyota wa muziki wa Bongo Flava nchini, Naseeb Abdulmaliki (Diamond Platnum) huenda akaingia matatani baada ya kupanda jukwaani kutumbuiza katika Tamasha la Fiesta 2014 akiwa amevaa sare ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kinyume cha sheria.

Tangu msanii huyo afanye hivyo, mjadala umeibuka kwa wengi wao kujiuliza nini maana yake na kama alifanya hivyo kwa kibali maalumu au la, hasa ikizingatiwa ni hivi karibuni Jeshi hilo lilitoa onyo kwa wasanii na wengineo kutotumia mavazi hayo.

Mbali ya Diamond, hata vijana wake nao walishambulia jukwaa wakiwa katika mavazi hayo, akiwemo msanii aliyemshirikisha katika moja ya nyimbo zake, Ney wa Mitego.

Wakati shoo hiyo ikiendelea, baadhi ya mashabiki walianza kumzomea kila alipoimba kabla ya video kubwa ambazo zilikuwa mbele ya jukwaa hilo kuanza kuonyesha picha za mnato na video za mwanamuziki huyo akiwa amevaa mavazi hayo huku akiwa kama askari ‘anayekoki’ risasi katika bastola na baadaye katika bunduki ya kivita.

Kitendo hicho, kilionekana kuwakera zaidi maelfu ya wapenzi na mashabiki wa muziki waliokuwa katika viwanja vya Leaders, huku kila mmoja akiwa na tafsiri yake.

Kwa upande wake Diamond, alitoa taarifa ndefu katika ukurasa wake wa Facebook na Instagram, akiishia kuelezea ni kwa nini alizomewa katika shoo hiyo.

Tanzania Daima ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura juu ya kitendo cha msanii huyo, alisema alikuwa hajui chochote na kuahidi kulifanyia kazi kama atapelekewa taarifa na wasaidizi wake.

Alipotafutwa Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Msanja, simu yake iliita bila kupokelewa na alipotafutwa msaidizi wake, alikiri kupata taarifa na kujionea kupitia shoo hiyo, huku akisisitiza bosi wake anaweza kulizungumzia hilo.

Tukio hilo limefanyika ikiwa ni siku chache tu tangu kijana mmoja aliyekuwa amevalia mavazi ya kijeshi maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kuvuliwa na kupewa adhabu ya kuogelea katika dimbwi la maji machafu yaliyotuama.

Chanzo: Tanzania Daima


MREMA AWAFUKUZA MADIWANI WAKE WAWILI KWA KUMUUNGA MKONO MBATIA


Augustin Lyatonga Mrema (MB) wa jimbo la Vunjo.
Joseph Mbatia (MB) ambae ametangaza kugombea jimbo la Vunjo.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amekunjua  makucha yake yaliyowahi kurarua viongozi wenzake akiwa katika NCCR-Mageuzi na TLP, na sasa amewafukuza madiwani wawili wa chama chake waliounga mkono nia ya Mbunge wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye ametangaza kugombea ubunge wa Vunjo.

Mrema amewavua uanachama wa TLP, Meja Mstaafu Jesse Makundi, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya Mrema; na Yorolanda Lyimo, Diwani wa Kilema Kaskazini.

Jimbo hilo linawakilishwa na Mrema tangu 2010, na amesema mara kadhaa kwamba hataki kusikia mtu akitaka ubunge katika jimbo lake. Tayari amemlalamikia Mbatia kwa Rais na katika Bunge Maalumu la Katiba.

Kilichowaponza Makundi na Lyimo ni kushiriki harambee iliyoongozwa na Mbatia ya ujenzi wa maabara na mabweni katika shule za Sekondari za Pakula, Kiluani na Mwika, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika harambee hiyo, Makundi alisema anatambua uwezo wa Mbatia na kwamba, kwa sababu hiyo, anamuunga mkono katika azima yake ya kuwa mbunge mwakani.

Alisema kwa kuwa alipokea tochi ya kumulikia wana Vunjo kutoka kwa Mbatia, ameona ni busara kuirudisha kwa yule aliyemkabidhi tochi hiyo.

“Leo nimefikia uamuzi ambao naamini ndio hitaji la wana Vunjo, kwa kuwa Jimbo hili nililipokea kutoka kwa Mbatia na kwa kuwa yeye ndiye aliyenikabidhi hii Tochi, natamka hadharani kuwa Mbatia ndiye chaguo langu, yeye ndiye atakayemulika wana Vunjo,” alisema Makundi.

Yorolanda naye alidai kuwa uamuzi wa kumuunga mkono Mbatia ni wa Mungu.

“Tunamuomba Mungu amuinue aweze kuwa Mbunge wetu. Mimi ni Diwani wa TLP, nina Mbunge wangu, namuheshimu sana (Mrema), lakini namuomba Mungu amteue Mbatia chaguo letu Wana Vunjo. Nafahamu wapo watakaonukuu maneno yangu lakini kama mbaya acha iwe mbaya,” alisema.

Mrema amekerwa na kauli hizo, akawavua uanachama akidai wameonyesha utovu wa nidhamu na wamekiuka katiba ya chama chao kuunga mkono mtia nia wa ubunge wa chama kingine, katika jimbo lake ambalo naye ameshatangaza kuwania nafasi hiyo tena mwakani.

Alikuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Mwanjeni, Kata ya Mwika Kusini.

Hata hivyo, Makundi amesema uamuzi wa Mrema ni batili, kwani mwenyekiti wake huyo hana mamlaka hayo.

Mrema amekuwa analalamikia hatua ya Mbatia kutaka ubunge wa Vunjo, akisema kinachomtia kiburi ni ubunge wa kuteuliwa aliopewa na Rais Jakaya Kikwete.

Analaumu pia vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambavyo vimetangaza kuweka mgombea mmoja mmoja kila jimbo kwa ushirikiano.

Hata hivyo, UKAWA haijatangaza mgombea wa Vunjo. Licha ya Mbatia, yupo mtia nia mwingine kutoka CHADEMA, John Mrema, ambaye naye ameshatangaza kugombea ubunge huo, akisubiri uamuzi wa mwisho wa UKAWA.

Lakini Mrema amekuwa anamshambulia Mbatia kwa kuwa ndiye amekuwa anafanya mikutano ya mara kwa mara.

“Siko tayari kujibizana na mtu. Kuna kazi kubwa mbele yetu. Tuelekeze nguvu zetu kuwatumikia Wana Vunjo. Mkutano wa Septemba ndio unaomtesa. Nyinyi ni mashahidi. Tangu Septemba 6, sijafanya mkutano wowote. Kulalamika kwake ni sawa na kulalamikia kivuli. Kivuli chake kinamuhukumu. Mimi siko tayari kumjibu,” alisema Mbatia.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU