Facebook Comments Box

Thursday, October 4, 2012

BAADA YA RAFU MBAYA YA BOBAN, YONDANI AANZA MATIBABU MUHIMBILI (MOI)



Mlinzi wa kati ya timu ya Young Africans, Kelvin Yondani
























Mlinzi wa kati wa kutumainiwa wa klabu ya Young Africans na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Kelvin Yondani anaendelea vizuri mara baada ya kuanza kupata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha mifupa MOI jijini Dar es salaam.
Daktari wa timu ya Young Africans Dokta Suphian Juma, amesema Yondani alipata mshtuko katika mfupa wake mkubwa, baada ya kuchezewa vibaya na kiungo wa timu ya Simba Haruna Moshi 'Boban'.
Dr Suphian anatoa wasi wasi wapenzi na washabiki wa Young Africans, kwamba Yondani anaendelea vzuri na anatazamiwa kurudi dimbani baada ya wiki mbili. 'Unajua Yondani baada ya kukanygwa na Boban alipata mshituko katika mfupa wake mkubwa mguuni, hivyo anapata matibabu ya kumrejesha katika hali yake ya kawaida.
Katika hali ya kushangaza mwamuzi wa mchezo huo wa watani wa jadi, Mathew Akrama alishindwa kumonyesha kadi nyekundu Boban kwa mchezo mbaya uliopelekea Yondani kutolewa nje na kushidwa kuendelea na mchezo.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyowakutanisha watani wa jadi wakongwe Afrika Mashariki iliishia kwa sare ya mabao 1-1, mabao yaliyofungwa na Amri Kiemba Simba dakika ya 4 na Said Bahanunzi aliyesawazisha kwa upande wa Young Africans dakika ya 67.
Young Africans leo imeendelea na mazoezi katik uwanja wa shule ya sekeondari ya Loyola kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya timu ya Kagera Sugar, mchezo utakaofanyika siku ya jumapili katika uwanja wa kaitaba mjini Bukoba.

RAFU MBAYA YA BOBAN YAMPELEKA YONDANI HOSPITALI


Yondan wa pili kutoka kulia waliosimama katika kikosi cha Yanga jana
BEKI Kevin Yondan wa Yanga hajaamka mazoezini leo, kutokana na kuumizwa vibaya na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga wapo Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo hivi sasa wakifanya mazoezi, lakini Yondan anajiandaa kwenda hospitali kufanyiwa uchunguzi wa maumivu yake.
Habari kutoka Yanga, zimesema kwamba tangu jana beki huyo anasikia maumivu makali na hatima yake itajulikana baada ya vipimo hivyo.
Yanga jana ilitoka nyuma na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
Habari kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba wachezaji waliahidiwa asilimia ya 60 ya mgawo wa timu kutokana na mapato ya milangoni na asilimia 20 ya kiwango hicho kuongezwa na Friends of Simba, lakini kwa sare hiyo, ahadi hiyo imeota mbawa.
Hata hivyo, uongozi wa Simba unafikiria kuwapa ‘kifuta jasho’ wachezaji wake kwa angalau kulinda hadhi ya klabu kwa kutokubali kufungwa na wapinzani wao hao wa jadi jana.
Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri Kiemba.  
Hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba dakika ya pili.
Simba walicheza vizuri kipindi chote cha kwanza wakigongeana pasi za uhakika na kuwazidi kasi uwanjani wapinzani wao, wakati Yanga pamoja na kuzinduka baada ya kufungwa bao, lakini makosa yalikuwa mengi.
Pasi zao zilikuwa nyingi hazifiki, walikuwa wanapokonyeka mipira kirahisi, wanazidiwa nguvu na wapinzani wao katika kugombea mipira na hata mashambulizi yao hayakuwa ya mpangilio, zaidi ya kuonekana kubahatisha zaidi.
Katika kubahatisha huko, Mbuyu Twite alifumua shuti zuri dakika ya 38 kutoka wingi ya kulia, ambalo lilitoka nje sentimita chache.    
Kabla hata ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika, kocha Mholanzi Ernie Brandts alimtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Frank Domayo ili kuimarisha safu ya kiungo, ambayo ilionekana kuzidiwa na Simba inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick.
Kipindi cha pili, Yanga walianza na mabadiliko, kocha Ernie Brandts akimtoa kiungo Nizar Khalfan na kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu, ambaye alikwenda kuongeza nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Angalau, kipindi cha pili Yanga walionekana kucheza vizuri na kupeleka mashambulizi yenye uhai langoni mwa Simba, ingawa safu imara ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ilikuwa kikwazo.
Katika dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika harakati za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Katika dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’. Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na hasira za kitoto.
Pamoja na Yanga kubaki pungufu, waliendelea kucheza vema na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili. Refa Akrama alishindwa kuumudu mchezo na maamuzi yake mengi yalikuwa chungu kwa Yanga, mfano Haruna Moshi ‘Boban’ alipomchezea rafu mbaya beki Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Abdul alimpoza kwa kadi ya njano.
Hakumchukulia hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
Alipingia Abdul alikwenda kucheza beki ya kulia na Mbuyu Twite akahamia katikati kucheza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Simba, Milovan alisema kwamba ulikuwa mchezo mzuri na Yanga walicheza vizuri, lakini timu yake ilicheza vizuri na anajivunia. Alisema Yanga imeimarika tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba hizo ni dalili Ligi Kuu msimu huu itakuwa ngumu.
Kwa upande wake, kocha wa Yanga, mwanzoni hawakucheza vizuri, lakini baadaye walitulia na kucheza vizuri. “Hii ni mechi ya kweli ya upinzani, unaweza kuona rafu na kadi nyingi,”alisema Brandts.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 13, ndani ya mechi tano na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, wakati Yanga imefikisha pointi nane na kubaki nafasi ya tano, kwani Coastal Union imetoa sare ya 2-2 na JKT Oljoro mjini Arusha na kufikisha pointi tisa.   
SIMBA: Juma Kaseja, Nassor Chollo, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Shomary Kapombe, Jonas Mkude/Haruna Moshi, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Edward Christopher/Daniel Akuffo na Mrisho Ngassa.
YANGA: Yaw Berko, Mbuyu Twite, Stefano Mwasyika, Nadir Cannavaro, Kevin Yondan/Juma Abdul, Athumani Iddi, Simon  Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza/Frank Domayo na Nizar Khalfan/Didier Kavumbangu.


KIBONZO CHA LEO




HUU NDIO UDHAIFU MWINGINE WA TFF

Pichani ni sehemu ya paa la chumba cha habari cha chama cha mpira wa miguu Tanzania (TFF),ambacho kinatumika kukutana na Wanahabari wa vyombo mbalimbali kuhusiana tasnia ya michezo kwa madhumuni ya kuihabarisha jamii.Kwa wanahabari za Michezo naamini kabisa mtakubaliana na mimi kuhusiana na hali iliyopo ndani ya ofisi hiyo,ambayo kimsingi nayo una umuhimu wake mkubwa,lakini imetelekezwa kama hivyo.
Chombo cha kutoa ubaridi ambacho kiliwekwa angalau kupunguza joto la Daslam ofisini humo,lakini kwa sasa ndege wamepata mahala pa kujipumzikia na kuzaliana,lakini sio ishu.
Taa nazo ziko hoi zinaning'inia tu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa watu.
Baadhi ya Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakisubiri wahusika wa TFF, kukutana na Wanahabari hao kwa ajili ya kuwapa taarifa mbalimbali za michezo, ili jamii ihabarishwe.
Dude la kuwekea Maji ya Kunywa ambalo sijui kwa mara ya mwisho lilitumika lini,kwani limejaa vumbi, haliangaliwi tena.



HII NDIO MBINU MPYA YA KUTOROSHA MADINI

WIZARA ya Nishati na Madini imegundua ‘madudu’ katika sekta ya madini, ikiwamo utoroshaji wa madini ya tanzanite kwa punda na ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na kampuni za migodi nchini.

Kutokana na hilo, imefanya marekebisho ya mifumo ya ulipaji kodi iliyowezesha kulipwa kwa baadhi ya madeni na imetangaza Mtanzania yeyote, ikiwamo mfanyakazi wa mgodi atakayetoa taarifa za utoroshaji wa madini, atapewa asilimia 30 ya thamani ya mzigo utakaokuwa umetoroshwa.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza katika uzinduzi wa Kitabu cha Ripoti inayohusu Haki za Binadamu katika Kazi, Biashara, Mazingira, Ardhi, Ulinzi na Haki ya Mlaji.

Hafla hiyo iliandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na yeye alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza kabla ya uzinduzi wa ripoti hiyo iliyoelezea ukiukwaji mkubwa wa haki za wafanyakazi katika kampuni za madini nchini na uharibifu wa mazingira uliobainika, Masele alikubaliana nayo na kueleza jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na kadhia hiyo.

“Kuna ‘madudu’ mengi na makubwa yanafanyika, rasilimali za nchi hii zinatoroshwa na kuyeyuka, tumegundua kule Manyara madini pekee yanayopatikana Tanzania tu ulimwenguni kote-tanzanite yanatoroshwa kwa punda, hii haiwezekani kukaa kimya, wezi wa mali zetu ni Watanzania wenyewe, tubadilike,” alisema Masele na kuongeza: “Kuna watu wanapewa asilimia 10 ya madini yanayotoroshwa, tumegundua hilo pia sasa tumesema mwananchi au mfanyakazi atakayegundua utoroshaji na kutoa taarifa kwetu, tutampa asilimia 30 ya fedha ambayo ni thamani ya mali aliyookoa”.

Akisisitiza ukwepaji kodi, alisema: “Tena nitoe onyo kwa kampuni zinazokwepa kodi na kukiuka haki za binadamu hasa katika sekta inayosimamiwa na wizara yetu, waache mara moja maana kuna mapinduzi makubwa yanafanyika sasa na hatutasita kuyafutia leseni mara moja”.

Masele alisema walibaini kampuni zote za madini nchini zikikwepa baadhi ya kodi kupitia uandikaji wa nyaraka zao na sasa wamezibaini na kuanza kulipa madeni hayo.

Alitoa mfano kampuni ya Barrick katika ukokotoaji wa hesabu, ilibainika kuwa na deni la zaidi ya Sh bilioni 5.6 na hadi sasa imelipa Sh bilioni 2.3; nyingine ni TanzaniteOne inayodaiwa zaidi ya dola za Marekani milioni 2.5.

“Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) ilikuwa inadaiwa zaidi ya dola milioni 1.4 ambazo sasa imeanza kuilipa Halmashauri ya Geita, niseme tu kuna mapinduzi makubwa na tunaamini Watanzania wako nyuma yetu hatuogopi,” alisema Masele.

Kuhusu TanzaniteOne, alisema leseni yake imekwisha tangu Agosti na Serikali imesitisha kuipa leseni nyingine mpaka mpango wa kurejesha asilimia 50 ya hisa serikalini ili kuondoa umiliki binafsi uliopo sasa na masuala mengine ya utendaji vitakapokaa vizuri.

Alisema katika kuhakikisha kuna usimamizi mzuri wa kodi na rasilimali za madini, mafuta na gesi nchini, Wizara inafanya mapinduzi makubwa katika taasisi zake kwa kufumua Bodi, kupanga mifumo na kuongeza nguvu ya kiutendaji ya rasilimali watu.

Masele alisema miongoni mwa Bodi zitakazofumuliwa ni pamoja na ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ili kuongeza usimamizi katika sekta ya madini, pia itafanya marekebisho makubwa ya utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC).

Alisema lengo la wizara ni kutekeleza malengo ya kiuchumi ya mwaka 2020 hadi 2025 ya nchi kuwa katika uchumi wa kati kwa kutumia rasilimali zake hasa madini, gesi na mafuta na kusisitiza kuwa hawataacha kuwachukulia hatua wezi wa rasilimali, waharibifu wa mazingira na ardhi.

Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wanaharakati wa haki za binadamu, kwamba Serikali inawatambua na haipingi kukosolewa, lakini kwenye pongezi ipewe, huku akiwahakikishia kuwa utafiti wao ni moja ya zana za kuendeleza utendaji unaoendelea hivi sasa katika sekta mbalimbali.

Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa kuonesha matumaini mapya kwa wananchi, hasa usalama wao katika maeneo ya kazi kwenye migodi na kampuni za uwekezaji.

Kuhusu ripoti ya utafiti, Kijo- Bisimba alisema utafiti ulifanyika nchi nzima na kugundua ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wafanyakazi wa migodini, ujira mdogo na usalama kazini, uharibifu wa mazingira na ardhi.

“Ilizoeleka katika nchi nyingi, kwamba walaumiwa wa ukiukaji wa haki za binadamu ni Dola, lakini sasa hali hiyo imebadilika, sekta binafsi inashiriki katika ukiukaji wa haki za binadamu kupitia mifumo yao ya utendaji na kukwepa kulipa kodi,” alisema Dk Kijo-Bisimba.

Akitoa takwimu, Wakili na Mratibu wa Uwajibikaji wa Kampuni na Mazingira wa LHRC, Flaviana Charles alisema wafanyakazi asilimia 15.77 waliohojiwa walikiri kuwapo na ukiukwaji wa haki za binadamu migodini na ujira mdogo, hakuna haki ya kujumuika (kuwa na vyama vya wafanyakazi).

“Pia asilimia 28.22 ya kampuni hazina sera ya kuzuia ajira kwa watoto na asilimia 4.62 ya kampuni hazishirikishi wananchi kuchukua ardhi ya uwekezaji, pia watu hawajui haki zao wanapouziwa bidhaa bandia,” alisema Charles.

LHRC waliiomba Serikali kuhakikisha pia kuwa familia 20 zinazoishi katika mahema Geita zilizopisha mradi wa GGM, zinajengewa nyumba. Naibu Waziri Masele alisema tayari GGM imekubali kujenga nyumba hizo.

Kwa mujibu wa LHRC, utafiti huo ni wa kwanza wao kuufanya nchini kuhusu masuala ya haki za wafanyakazi, mlaji, ardhi, mazingira na ulinzi.



PINI JIPYA LA LINNAH




VODACOM WAZINDUA HUDUMA YA BIMA KWA NJIA YA SIMU

.
.
.
.
Taarifa kwa vyombo vya habari.
Watanzania sasa kupata Bima kupitia huduma ya M–Pesa.
  • Ni ushirikiano kati ya Vodacom na Heritage Tanzania kuzindua bima ya Faraja, Bima ya mazishi na ajali.
  • Wateja kununua na kulipia Bima kupitia M-Pesa.
  • Huduma ya bure kutolewa kwa wateja watakaolipia huduma mara kumi kwa Mwezi.
Dar-es salaam, Octoba 3, 2012 … Huduma ya Vodacom ya M-Pesa imezidi kupiga hatua baada ya kuwawezesha Watanzania kufanya malipo yao ya bima kupitia huduma hiyo.
Hii inafuatia ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania na Heritage Tanzania kuzindua Bima ya Faraja, ambayo ni Bima ya mazishi ambayo inamuwezesha mlengwa kulipwa fedha taslim za mazishi kwa muhusika mwenye bima. Bidhaa mbalimbali ziko katika mpango huo ili kukidhi mahitaji ya wateja na bajeti ya malipo ya kila mwezi kuanzia shilingi 20000/= fadi 9800/= kwa Mwezi.
Mteja ana chaguo la kuongeza malipo kwa kuongeza huduma ya vifo vinavyotokana na ajali kulingana na faida na sera zao. Ongezeko hili la ziada litaongeza kiasi cha faida mara tatu kwa ongezeko dogo la malipo.
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, amesema wateja wa Vodacom wanaotumia M-Pesa, wataweza kujipatia bima ya bure kwa mwezi.
“Wateja wetu wote ambao watafanikiwa kutuma pesa walau mara 10 kwa Mwezi watapata  bima ya bure ya kiasi cha Shilingi laki mbili kwa mwezi unaofuata,” amesema Meza.
Suala la kipekee katika huduma hii ni kwamba hakuna haja ya kujaza fomu ili kujiunga na bima hii. Mteja atajiunga kwa njia rahisi kwa kupiga *150*00# na kuchagua kipengele cha bima. Vodacom inahakikisha kuwa wateja wote wa M-pesa wanaweza kupata huduma hii ili kuwa na amani ndani ya familia zao.
 “Ni muhimu kuthibitisha kuwa taarifa zako ni sahihi, na kuthibitisha kuwa unaelewa vigezo na masharti. Taarifa zako zitatumwa moja kwa moja kwenda Heritage Tanzania,” alisema Meza na kuongeza kuwa, “Unaweza kuchagua aina ya bima ambayo inakidhi mahitaji na bajeti yako,”
Bima hii ya Faraja pia itawawezesha kila mmoja kubadili au kuongeza kiwango chake kwa ile yenye faida zaidi kulingana na mahitaji yao na mabadiliko ya bajeti katika maisha yao.
Kwa taarifa zaidi kuhusiana na huduma mteja atapiga 0764 300001 bure au vipeperushi kutoka kwa wakala wa M-Pesa nchini.

 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU