Timu ya Yanga ya Jijini Dar es Salaam imegawana point na Polisi ya Dar es Salaam pia pale zilipotoka suluhu bin suluhu katika mtanange wa kirafiki uliofanyika leo asubuhi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola ambao ndiyo uwanja wa mazoezi wa timu ya Yanga.
Mpambano huo uliokuwa mzuri na wa kasi kutokana na timu zote mbili kutumia sana viungo ambapo kwa upande wa wenyeji Yanga Mrisho Ngassa na Coutinho waling'ara sana.
Coutinho
katika dakika ya 14 tu ya mchezo, mshambuliaji wa timu ya Polisi alikosa goli la wazi akiwa ana kwa ana na mlinda mlango wa Yanga Juma Kaseja ambaye aliucheza mpira huo kwa mguu.
Mpira huo uliingia dosari katika dakika ya 20 ya mchezo wakati Coutinho alipoumia na kutolewa nje na kuzua hofu kubwa kwa Viongozi, wachezaji pamoja na mashabiki wa timu hiyo kuona kuwa anaweza kukosa mchezo wa ufunguzi wa Ligi kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Azam ambao unataraji kufanyika tarehe 14 septemba, 2014 siku ya jumapili.
Kwani hata kuondoka kwake hapo uwanjani mchezaji huyo alipewa msaada mkubwa na Daktari wa timu yake aliyekuwa amemshikilia begani na kuacha maswali mengi hasa kuhusu mchezo huo.