RIPOTI MAALUMU ya gazeti la JAMHURI
Kipindi
cha uwindaji kinachoruhusiwa kisheria kinachoanza Julai hadi Desemba
kila mwaka kimekwisha. Hii haina maana kwamba ulaji wanyamapori umekoma.
Nipo
njiani naelekea mkoani Iringa. Kilometa 40 hivi kutoka mjini Morogoro,
tunafika katika eneo linaloitwa Lugano. Hapa kunachomwa nyama za kila
aina, lakini zinazotawala zaidi ni za mbuzi na swala. Kwa kutambua kuwa
naweza kupata nyama ya swala, najenga urafiki na wauza nyama hawa. Nao,
bila hiyana wanakuwa wachangamfu kwangu.
Swali
langu la kwanza kwao ni, “Naweza kupata nyama ya swala?” Mmoja wa
vijana hawa anajibu, “Sema jingine kaka, nyama umepata.” Nauliza swali
la pili, “Naweza kupata nyama ya nyati au aina nyingine tofauti na
swala?” Najibiwa, “Hapa nyati hupati, labda uende Mkata. Mkata ndiyo
kwenye kila kitu.”
Naelekezwa
kwamba kutoka hapa Lugano hadi Mkata ni mwendo kama wa kilometa 10 na
ushei hivi. Maneno ya vijana hawa ya kwamba Mkata ndiyo kila kitu,
yananifanya niwe na shauku ya kufika katika kijiji hicho. Kweli, napanda
basi tayari kuelekea Iringa. Punde si punde, kwa msaada wa kondakta na
kibao cha utambulisho, napaona Mkata. Naendelea na safari yangu hadi
Iringa, lakini akili yangu inanisukuma niandae siku maalumu kwa ajili ya
kufuatilia taarifa hizi.
Nasukumwa
na ukweli kwamba vijiji kama Lugano, Mkata na Doma vipo jirani kabisa
na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Vijiji hivi vinapitiwa na barabara kuu ya
Morogoro-Iringa. Wakubwa wanapita hapa kila siku. Kama hivyo ndivyo,
iweje ujangili ushamiri kwa kiasi hiki cha kutisha?
Mwishoni
mwa Desemba naamua kufunga safari kutoka Dar es Salaam kwenda Mkata na
Doma. Kabla ya safari nampigia simu Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na
Ujangili katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Faustine Masalu.
“Kamanda
naelekea mkoani Morogoro kufuatilia taarifa za ujangili. Nakupa taarifa
hizi kwa sababu huko naweza kukutana na mambo yasiyokuwa ya kawaida.
Lakini kubwa itanipasa niweze kushiriki kununua nyamapori na hata
kusafiri nayo bila kibali, kisheria nikikamatwa naweza kushitakiwa.
Nakupa taarifa hii kama kinga kwa linaloweza kunipata,” huu ndiyo
uliokuwa ujumbe wangu kwa Masalu, kabla ya kuanza safari kwa kutumia
gari langu.
Muda ni
saa tano asubuhi. Naanza safari ya kwenda Morogoro. Kwa kutambua ugumu
wa kazi ninayokwenda kuifanya, namchukua mwandishi mwenzangu, Edmund
Mihale.
Tunakwenda
hadi Lugano. Hapa tunaegesha gari pembeni kwa ajili ya kuanza kazi. Mvua
kubwa inanyesha. Majiko ya nyama ni mengi. Tunaomba tuuziwe nyamapori,
lakini kwa hadaa, baadhi ya wauzaji wanatupatia nyama ya mbuzi. Wote
tunashituka. Kuona hivyo, mmoja anatuelekeza kwenye jiko lake.
Kweli,
tunakula nyama yenye ladha na sifa zote za swala. Kazi imeanza.
Nakumbuka kwamba nilishaelezwa na hawa hawa vijana kwamba nyama za kila
aina zinapatikana Mkata, mahali ambako sifa zake zinafanana na Mkata ya
Handeni, mkoani Tanga, ambako kunauzwa nyama nyingi za mbuzi, lakini si
swala na wanyamapori wengine.
Tunaanza
safari kwenda Mkata. Si mbali. Baada ya kilometa tano hivi, tunakuta
gari la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aina ya Land
Rover likiwa limepinduka na kuwaumiza askari na raia waliokuwamo. Ni
mali ya Kikosi cha 401.
Wanajeshi
hawa walikuwa wakitoka kumzika mwenzao Kigamboni, Dar es Salaam, na
sasa walikuwa njiani kurejea Songea. Kama ilivyo ada, tunashiriki kutoa
huduma kwa wapiganaji na makamanda hawa. Magari mengi yanafika,
yanasimama na kuuliza aina ya msaada unaotakiwa. Mwisho, majeruhi wote,
isipokuwa mmoja, wanapelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
Kuona
hivyo, tunashawishika kuendelea na safari yetu. Vijana wawili wanaomba
lifti. Nawauliza wanakokwenda. Wanajibu kwamba wao ni wakazi wa Mkata.
Kusikia hivyo, haraka haraka nawakaribisha waingine katika gari. Njiani
naanza kuwauliza kama wana uwezo wa kuniwezesha kupata nyama ya swala.
Mmoja anajibu, “Sisi hatuuzi swala, lakini tunaweza kukupeleka kwa
wanaouza.” Namwuliza kama naweza kupata aina nyingine ya wanyamapori.
“Hapo
kila kitu utapata, hakuna wasiwasi,” anajibu kwa lafudhi ya Kimaasai.
Baada ya kilometa kama saba hivi, tunafika Mkata. Nashangaa kuona magari
mengi yakiwa yameegeshwa kando ya barabara. Nauliza kama kuna sherehe
mahali hapa. Mmoja wa vijana hawa anajibu, “Siyo sherehe, watu wanakuja
wote kula nyama hapa.”
Tunakwenda
moja kwa moja hadi mahali kunakouzwa. Wenyeji wetu hapa hawana
wasiwasi, pengine kutokana na hawa vijana wawili wenyeji waliotufikisha
hapa. Tunawakuta wateja wengi wakila nyama. Jiko limejengwa ndani ya
nyumba mbovu ya miti na kuezekwa kwa nyasi.
Anayechoma
nyama hapa ni maarufu kwa jina la Mangi. Baadaye tunamwuliza jina lake
halisi na anajitambulisha kuwa anaitwa Mrosso Anthony. Kuna nyama ya
nyati, swala na pofu. Pande linauzwa kuanzia Sh 10,000. Mimi nasita
kuchukua nyama kubwa, naomba atutengee ya Sh 5,000. Wateja wote
tuliokutana hapa ni kama vile tulishaonana siku nyingi, maana wengine
wanakata "kilaji" (bia). Wanatukaribisha tunywe. Ni katika mazingira
ambayo watembezi huyaita “adventure”.
Upande
wa pili wa nyumba hii, kuna nyama mbichi iliyotundikwa. Inavutia kweli
kweli. Inavuja damu mbichi kabisa. Kuna miguu na mikono. Pembeni mwa
hiyo nyama, kuna kijana mmoja mwenye uso uliojaa makovu. Anaitwa Pengo.
Sijui kwanini anaitwa Pengo, pengine ni kutokana na kutokuwa na meno
mengi mdomoni. Namwuliza; “Pengo, vipi bwana, mbona uso umeharibika,
wewe ni mgomvi au ulikuwa ukipambana na nyati?” Anajibu kwa tabasamu,
“Siyo nyati mkuu, hii kitu ndiyo imefanya yote haya,” anasema huku
akinionesha pikipiki.
Wageni
wanazidi kumiminika hapa, na nyama zinauzwa kwa kasi. Ghafla, Pengo na
Mangi wanaonekana kuhamaki baada ya kuwaona wateja wengine wawili
wasiowajua wakija mahali tulipo. “Wale nani?" Anahoji Mangi. Pengo
anajibu, “Ni wateja tu, siyo watu wabaya.”
Nyama
tuliyoilipia ipo tayari. Tunaanza kula, lakini ni ngumu. Yaelekea ni ya
upande wa shingo. Nimeshindwa kutelemka na kamera yangu kubwa. Hali
hii inalilazimu nitumie kamera maalumu kupata picha za hapa na pale.
Ili
nisiweze kushitukiwa, nauliza bei ya mguu wa pofu. Naambiwa kuwa bei
yake ni Sh 120,000. Naomba niuziwe kipande cha Sh 20,000. Pengo
anachukua mguu wa pofu. Anaupeleka nje kwenye gogo maalumu. Anakata.
Kuona hivyo, walaji wenzetu nao wanaanza kununua. Wanakatiwa kadiri ya
fedha zao. Wengine wanaingia wakiwa na bia zao kabisa. Nyama ni nyingi
na hakuna mwenye wasiwasi.
Mwisho,
nikiwa nimeshajiridhisha kuwa nyama inayouzwa ni ya pori, namwuliza
Pengo wapi wanakopata nyama. “Hii nyama tunanunua kwa Waarabu wa
Morogoro wanaokuja kuwinda huku.” Namwuliza, “Mbona muda wa kuwinda
umekwisha?” Anakosa jibu.
Tumeshajiridhisha
pasi na shaka kuwa hapa ni kwenye mnada wa wanyamapori. Tunaaga, lakini
kabla ya kuondoka, Mangi anatupatia namba yake ya simu. “Chukua namba
yangu ya simu, ukiwa unahitaji kabla ya kufika hapa wewe piga simu
kabisa tukuandalie. Namba yangu ni
0655 093795. Karibu sana,” anasema.
Ingawa
mwanzoni alinieleza kwamba jina lake ni Mrosso Anthony, usajili wa
namba hii unaonesha kuwa ni ya Christian Joseph. Hii inazidi kunipa
shaka.
Baada ya hapo
naanza uchunguzi wa hapa na pale. Najiridhisha kuwa pikipiki iliyopo
hapa ni moja ya zana zinazotumika kusafirisha nyama. Naelezwa na mmoja
wa vijana kwamba pamoja na kuwapo kundi la vijana wanaoendesha ujangili,
baadhi ya nyama wanazipata kutoka kwa askari wanyamapori wa Mikumi.
Wiki
ijayo naendelea kueleza vituo vingine vya uuzaji wanyamapori. Ushiriki
wa maofisa na askari wanyamapori katika biashara hii haramu. Je,
Mkurugenzi na mwenye dhamana ya kupambana na ujangili nchini, Paul
Sarakikya; Kamanda Masalu, Mkuu wa KDU (Kikosi Dhidi ya Ujangili), Majid
Lalu; Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi; Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya
Mvomero, Sarah Limuna; Ofisa Wanyamapori Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa.
Nao,
Askari Wanyamapori Wilaya ya Mvomero aliyepewa dhima ya kusimamia
wanyamapori eneo la Doma, Peter Mayapila; Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya
Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete; wanasemaje? Je,
kuwapo kwa huduma za mitandao ya simu hifadhini na katika mapori pamoja
na kuruhusu matumizi ya bodaboda kunachangiaje wimbi la ujangili
nchini?
...Usikose toleo lijalo la gazeti JAMHURI.