Facebook Comments Box

Tuesday, September 18, 2012

RAIS KIKWETE AZINDUA UJENZI WA BARABARA YA MSATA-BAGAMOYO

Picture
Rais Dk Jakaya Kikwete (katikati) akiweka jiwe la msingi kuzindua rasmi ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo - Msata uliofanyika katika kijiji cha Kiwangwa wilayani Bagamoyo leo mchana. Wengine katika picha kutoka (kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi, Kaimu Mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik (wa pili kushoto), Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli (wanne kushoto) na kulia ni Waziri wa Mazingira Mh Terezya Huviza. (Picha: Freddy Maro/IKULU)


                                TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndoto ya miaka mingi ya kujengwa kwa barabara ya Msata-Bagamoyo kwa kiwango cha lami imetimia leo, Jumanne, Septemba 18, 2012, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara hiyo katika sherehe kubwa iliyofanyika eneo la Kiwangwa.

Barabara hiyo ya kilomita 64 inajengwa na mkandarasi wa ndani ya nchi, Estim Construction, na inagharimiwa asilimia mia na Serikali ya Tanzania bila msaada kutoka kwa mfadhili yoyote.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania, Injinia Patrick L. Mfugale amesema kuwa barabara hiyo inayogharimu kiasi cha Sh. bilioni 94, ikiwa ni pamoja na fedha za fidia na kumlipa mkandarasi mshauri, itakamilika Juni mwakani.

Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais ameweka jiwe la msingi kwenye barabara hiyo, Injinia Mfugale amesema kuwa mkandarasi wa sasa alianza ujenzi tokea 2010 baada ya usanifu wa barabara hiyo kukamilika na baada ya Serikali kumtimua mkandarasi wa mwanzo wa barabara hiyo, TACOPA, Novemba 13, mwaka 2009.

Amesema kuwa mpaka sasa barabara hiyo imekamilika kwa asilimia 65, yaani kwamba kiasi cha kilomita 36.7 tayari zimewekwa lami na kuwa ni kilomita 23 zilizosalia na ambazo zitamalizika katika miezi tisa ijayo.

Injinia Mfugale amesema kuwa mpaka sasa Serikali imekwishakulipa kiasi cha Sh. bilioni 56.8 ikiwa ni pamoja na fedha iliyolipwa kama fidia kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.

Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo hautahusisha ujenzi wa daraja kwenye Mto Ruvu kwa sababu usanifu wa daraja hilo ulichelewa kidogo kukamilika hata kama tayari sasa umekamilishwa.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John P. Magufuli amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya ujenzi wa kilomita 11,154 za barabara za lami zinazojengwa na Serikali ya Mheshimiwa Kikwete.

“Nataka muelewe vizuri maana ya kilomita hizi. Wakati wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, tulikuwa na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,330. Kati ya Uhuru na mwaka 2005, tulijenga barabara zenye urefu wa kilomita 6,500 na kati ya 2005 na sasa tunajenga barabara zenye urefu wa kilomita 11,154,” amesema Waziri Magufuli.

Waziri huyo amerudia msimamo wake kuwa kamwe Serikali haitawaachia watu wanaojenga ama kufanya shughuli katika eneo la hifadhi ya barabara bila kuwachukulia hatua.

Naye Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi walioshiriki katika sherehe hizo kuwa barabara ndiyo mishipa ya damu ya uchumi wa nchi yoyote na ndiyo maana Serikali inatenga kiasi kikubwa katika Bajeti yake kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Amesema kuwa katika Bajeti ya sasa, barabara zimetengewa kiasi cha Sh. trilioni 2.2 ambacho ni kiasi kikubwa cha pili baada ya Bajeti ya elimu.

Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na faida zake kubwa na nyingi, barabara hiyo itakuwa na changamoto zake ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ajali za barabara, kuongeza urahisi wa kusambaa kwa ugonjwa wa ukimwi na hata kuvutia watu wenye lengo la kununua ardhi kubwa ya wanavijiji ambako inapita barabara hiyo.

Rais pia ameungana na Waziri Magufuli kwa kuonya: “Kama alivyosema Waziri, wanaoifuata barabara watavunjiwa nyumba zao na hawatalipwa, lakini wale ambao barabara inawafuata watalipwa hata wakivunjiwa.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

18 Septemba, 2012
Picture
Sehemu ya Barabara ya Bagamoyo - Msata iliyojengwa kwa kiwango cha lami ambayo ujenzi wake ulizinduliwa rasmi leo na Rais Dk Jakaya Kikwete, huko Kiwangwa, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani. (Picha: Freddy Maro/IKULU)


RAIS OBAMA AJIBU BARUA YA MWANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI YA UGANDA


Kijana Christopher Kule na babake Dasiel Raul
Kama kuna rais ambaye watu wengi Uganda wangetaka kukutana naye ni rais wa Marekani Barack Obama.
Kijana Christopher Kule, mwenye umri wa miaka kumi na ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi wilayani Kasese, nchini Uganda, hajaachwa nyuma katika ndoto hiyo.
Bila shaka wengi watasema yuko hatua nyingi mbele ya wale walio na ndoto ya kumuona Obama. Hii ni baada ya Kule kupokea majibu ya barua aliyomwandikia Rais Barack Obama kutoka kwa Obama mwenyewe.
Kijana huyo anaamini kuwa baada ya kuandikiana barua na Rais Obama, kuna matumaini kwamba siku moja atakutana naye.
Yote haya yanatokana na zoezi la kuandika barua ambalo Kule na wanafunzi wenzake walikuwa wanafanya darasani, baada ya kuagizwa na mwalimu wamwandikie barua mtu yeyote wakiomba msaada kwa jamii yao.
Barua ya Kule bila shaka ilimtia hamasa mwalimu wake wa kigeni kutoka Marekani ambaye alikuwa anafunza shuleni humo kwa muda.
Mwalimu huyo alisema kuwa nyanyake ni rafiki wa mmoja wa wasaidizi katika ikulu ya rais na kuahidi kuhakikisha kuwa ujumbe huo utamfikia rais Obama na bila shaka ahadi ikatimizwa , kwani barua ilimfikia rais Obama.
Kule alisema kuwa katika barua yake, alimwomba Obama kusaidia Uganda kuangamiza uasi na kuhamasisha amani.
Katika majibu yake kwa Kule, rais Obama alisema kuwa Marekani imejitolea kuangazia maswala kadhaa muhimu kote duniani kama haki za binadamu kwa sababu Marekani inapinga vikali ghasia na ukandamizaji dhidi ya watu wote. Pia alimtumia kijana huyo picha yake aliyokuwa ametia saini.

TAMKO LA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA

KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA JUU YA UTEKELEZAJI WA MADAI YA MADAKTARI NCHINI TAREHE 18.09.2012


Kamati ya Jumuiya ya Madaktari Nchini , kwanza inapenda kutoa pole kwa Wanahabari wote nchini kwa kitendo cha kinyama ambacho Mwanaharakati na Mwandishi wa habari, Marehemu David Mwangosi alifanyiwa, hii ni ishara kuwa Jeshi la Polisi wameamua kutumia njia ya kuua raia ili kujenga hofu na woga miongoni mwa wapenda demokrasia na maendeleo nchini.

Pia tunapenda kulaani kitendo cha Serikali kupitia Wizara ya Michezo, Habari na Utamaduni kulifungia gezeti makini la Mwanahalisi kwa sababu ya kutoa taarifa za ukweli juu ya waliotaka kukatiza uhai wa Dr.Ulimboka Stephen, Jamii ya Madaktari na watanzania wengi bado wanaamini kuwa waliotajwa na gazeti la Mwanahalisi ni miongoni mwa waliohusika na kutekwa, kuteswa na kutelekezwa kwake na si yule anayesemekana kuwa na matatizo ya akili aliyedaiwa kukamatwa na Suleimani Kova. Hivyo tunalitaka Jeshi la Polisi litoe ripoti yake ya Uchunguzi ili kubaini ukweli wa taarifa hii.

Pia, tunachukua nafasi hii kupongeza mshikamano ambao Madaktari wameendelea kuuonyesha licha ya changamoto nyingi tunazopitia, ni vema ikafaamika kuwa ni katika kipindi hiki ambacho Mwenyekiti wa MAT na MAT imefunguliwa kesi 2 mahakamani, Ni katika kipindi hiki ambacho zaidi ya interns 300 wanasubiri kuitwa kuhojiwa na MCT bila kujua ni lini hilo litafanyika, Ni katika kipindi hiki ambacho Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari anapata mapumziko baada ya kutoka katika Matibabu nchini Afrika Kusini, lakini ni katika kipindi hiki ambacho mpaka sasa hakuna hata hoja moja ya Madaktari imefanyiwa kazi na Serikali.

Tunapenda ieleweke kuwa suala la madai ya Madaktari si tukio, ni mchakato ambao utaendelea kwa vizazi vya sasa na vijavyo, ndio maana tumeshuhudia migomo hii katika nyakati tofauti pamoja na kujitokeza kikundi au mtu kutumiwa kuomba msamaha kwa lengo la kudhalilisha taaluma na kurudisha nyuma jitihada za kuboresha hali ya afya nchini na maslai ya watumishi kwa ujumla.

Kuhusu suala la interns, Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 10, Julai 2012, Baraza la Madaktari Nchini lilitoa taarifa kwa umma kuwa imesitisha leseni za muda kwa Madaktari waliochini ya mafunzo kwa vitendo, pia waliahidi kuwaita kwa nia ya kuwahoji mmoja mmoja pindi wakatapokamilisha uchunguzi wao, cha kushangaza ni kwamba miezi 2 sasa imepita bila hilo kufanyika.

Katika vikao mbalimbali ambavyo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Naibu wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, na Kaimu Katibu Mkuu wameshiriki, wamekuwa wakisisitiza kuwa hili lipo kisheria na interns wasuburi kuitwa kwa ajili ya kuhojiwa. Hivyo tunapenda kutumia nafasi hii kuitaka MCT itekeleze kwa haraka majukumu yake kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa haki.

Hivyo basi Kamati ya Jumuiya ya Madaktari imejiandaa vya kutosha na taratibu za kisheria na itahakikisha inaweka wakili pale interns watakapoanza kuhojiwa kwa kuwa sheria inayounda MCT inatoa hiyo nafasi.

Mwisho kabisa tunapenda kutoa wito kwa interns kutumia hekima na busara katika kipindi hiki kigumu, waepuke kutumiwa na kikundi cha watu ambao wanatumika au wanajitumia kwa maslai ya kustarehesha watawala.

                           IMETOLEWA NA; KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA.



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU