Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea
kuchukizwa kwake na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani
vilivyotokea hivi karibuni visiwani Zanzibar.
Amesema
vitendo hivyo vimeigharimu Zanzibar katika Nyanja mbali mbali zikiwemo
za kiuchumi, kisiasa na kijamii, sambamba na kuitia doa katika jamii ya
kimataifa.
Akihutubia mkutano wa
hadhara wa chama hicho katika viwanja vya demokrasia Kibandamaiti mjini
Zanzibar, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
amevilaumu vyombo vya dola kwa kutochukuwa hatua zinazostahiki katika
kudhibiti vitendo hivyo.
Amesema hatua
zilizochukuliwa katika kurejesha amani baada ya kutokea kwa vurugu hizo
hazikuwa muafaka, kwani zimekuwa zikiwadhalilisha na kuwanyanyasa
wananchi wasiokuwa na hatia pamoja na kuhujumu mali zao.
Amesema
yeye binafsi amechukizwa na kitendo cha kuuliwa kwa askari polisi
katika eneo la Bububu, Koplo Said Abrahmani lakini bado serikali na
vyombo vya dola vina jukumu la kulinda haki za raia kwa kuwasaka
wanaohusika na tukio hilo, na sio kuwanyanyasa raia wasiokuwa na hatia.
“Nazungumza
haya kwa unyonge sana leo, sikufikiria kuwa vitendo hivi vingetokea
Zanzibar katika wakati huu tunaotekeleza maridhiano ndani ya serikali ya
umoja wa kitaifa”, alieleza Maalim Seif na kuongeza: “Sipendi kuisema
serikali yangu na Rais wangu hadharani, lakini inanibidi niseme ‘Rais
wangu Dkt Shein unatuangusha’ kwa kuwa wewe ndiye mwenye jukumu kubwa
zaidi la kulinda amani ya nchi hii” alieleza.
Ametahadharisha
kuwa huenda vitendo hivyo vimepangwa kuvuruga umoja wa Wazanzibari
ambao umeiletea sifa kubwa Zanzibar, na kuwataka wananchi kutokubali
kuingizwa katika mtego utakaopelekea kuvunjika kwa umoja na mshikamano
uliopo miongoni mwa wananchi.
Katibu
Mkuu huyo wa CUF alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa vikundi
vinavyolalamikiwa kufanya vurugu vikiwemo vya ‘Ubaya ubaya, Mbwa mwitu
na Janjawid vilikuwepo kabla ya tukio hilo na kwamba vimetokana na kundi
kubwa la vijana la JANJAWID lililoahidiwa kupewa ajira na Serikali.
Katika
hatua nyengine Maalim Seif ameitaka Tume ya mabadiliko ya katiba
kufanya kazi kwa uadilifu na kuheshimu mawazo ya wananchi wanayoyatoa
bila ya kuonyesha upendeleo kwa baadhi ya watu au makundi fulani.
“Tume
hii inaonekana kuanza kuwa na ‘bias’ kwa baadhi ya watu na makundi
fulani, lakini tunamwambia Jaji Warioba tume yake iheshimu mawazo ya
wananchi”, alitanabahisha.
Katika
risala ya wanachama wa chama hicho kwa wilaya sita za Unguja iliyosomwa
na Katibu Mtendaji wa vijana CUF taifa Khalifa Abdallah walitahadharisha
juu ya uwezekano wa kuwepo kwa ajenda ya siri ya kuvuruga Serikali ya
Umoja wa Kitaifa.
Amesisitiza kuwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa bado inahitajika katika kupata ukombozi wa
kweli wa Zanzibar, sambamba na kuendeleza umoja na mshikamano wa
Wazanzibari.
Naye Kaimu wa Kaimu Naibu
Katibu Mkuu wa CUF Bw. Salim Bimani amewasisitiza wananchi kuendelea
kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao juu ya mabadiliko ya katiba, na
kuiomba Tume inayohusika na ukusanyaji wa maoni kuwapa fursa wananchi
kutoa maoni yao kwa uwazi.
“Wananchi msikubali kuchokozeka, nendeni mkatoe maoni kwani hii ni fursa pekee ya kupata katiba tuitakayo” alisisitiza Bimani.