Facebook Comments Box

Thursday, November 6, 2014

RAIS AFANYA UTEUZI WA MAKATIBU WA KUU WA WIZARA

Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu wa Wizara kwa kuteua Makatibu Wakuu wanne wapya na kuhamisha mmoja, uteuzi uliomuondoa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Charles Pallangyo.

Pallangyo sasa anakua Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, nafasi ambayo inatafsriwa kuwa adhabu, siku chache baada ya vyombo vya habari ikiwamo FikraPevu kuibua kashfa ya uhaba wa dawa katika hospitali kubwa za serikali. Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa.

Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa walioteuliwa ni pamoja na Dkt. Donan Mmbando ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuchukua nafasi ya Pallangyo.

Katika uteuzi huo Dkt. Yohana Budeba anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Mbogo Futakamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Dkt. Adelhelm James Meru ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Maliasili.

Kabla ya uteuzi wake, Dkt Mmbando alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Budeba alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Mhandisi Futakamba alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Dkt. Meru alikuwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje(EPZA).

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Rais Kikwete amemhamisha Bibi Maimuna Tarishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Adoh Steven Mapunda, Mkurugenzi Mtendaji, Manispaa ya Bukoba amepanda na kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Severine Kahitwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na Dkt. Faisal Issa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro anahamishiwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa
wa Mwanza. Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Kanali (Mst) Joseph Simbakalia, Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa EPZA kuchukua nafasi ya Dkt. Meru.

Uteuzi huo unaanza leo na Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014, Ikulu, Dar es Salaam. Wakati huohuo, Rais Kikwete amefanya
uteuzi wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine watatu watapangiwa kazi nyingine. Mabadiliko hayo yanampumzisha

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Fabian Massawe na kuwahamisha wakuu wa mikoa ya Arusha Magessa Mulongo na Fatma Mwasa wa Tabora. Taarifa ya Balozi Sefue inawataja Wakuu
wapya wa Mikoa ni Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John
Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Taarifa inasema kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya
ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Bwana Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha. Taarifa hiyo inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho,
Alhamisi, Novemba 6, 2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na Kanali
Joseph Simbakalia wa Mtwara.

Wakuu wa Mikoa ambao wamehamishwavituo vya kazi ni Bwana  Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza
kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma, Bwana Ludovick John Mwananzila
anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist
Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.

Wengine waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dkt.
Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.

Taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa,
Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa. Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa
Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi. Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya
kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU