Facebook Comments Box

Monday, November 11, 2013

ALICHOSEMA ZITO KABWE KUHUSU TAARIFA YA SIRI YA CHADEMA

NILIPOKUWA katika ziara ya bara la
Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka Novemba
2 mwaka huu (2013), nilipokea kwa njia
ya barua pepe ripoti inayoitwa "Taarifa
ya Siri ya Chadema" ambayo pia ilikuwa
imesambazwa katika mitandao
mbalimbali ya kijamii.
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba
chama hicho (chama changu) kilikuwa
kimechunguza mwenendo wangu tangu
mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa
mimi napokea fedha kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga
Chadema.
Ripoti hiyo ilinihusisha pia na
mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea
Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti
hiyo, alinisaidia kupokea na kuhifadhi
kiasi cha dola 250,000 za Marekani
kupitia kwenye akaunti yake binafsi.
Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa uongo
wa kiwango cha kutisha,
imenifadhaisha, kunisikitisha na
kunikasirisha.
Taarifa hii iliibuliwa katika kipindi
ambacho nilikuwa safarini kutetea haki
za Watanzania na Waafrika ambao
utajiri wao wa rasilimali unafaidiwa na
watu wachache waliohifadhi mali katika
nje za nje na pia kupigania makampuni
ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki
katika nchi zetu.
Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni
kutaka kunipoteza kutoka katika nia na
dhamira yangu ya dhati ya kutaka
Watanzania wafaidike na utajiri wao.
Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo
waliamua kutoa taarifa yao unazua
maswali mengi kuliko majibu.
Nafahamu kwamba mimi ni mwanasiasa
ambaye nimekuwa mlengwa (target) wa
mashambulizi kutoka kwa makundi
mbalimbali ya wanasiasa na vikundi
vyao. Kama mwanasiasa, niko tayari
kupokea changamoto zozote zinazokuja
na uanasiasa wangu.
Hata hivyo, ambacho sitakubali ni kwa
watu kutumia jina langu na uanasiasa
wangu kunichafua mimi binafsi na watu
wengine wasiohusika kwa sababu ya
kutaka kutimiza malengo yao ya
kidhalimu.
Raia huyo wa Kijerumani tayari
amekana kuhifadhi fedha zangu. Kwa
maelezo yake kwa baadhi ya viongozi
wa Chadema amekana kuwa na akaunti
inayotajwa na amekana pia kuwepo
nchini Ujerumani katika siku na wakati
uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imemtaja pia mtu kama Dk.
Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya CRDB ikidai kwamba nilikutana
naye na alishiriki kwenye igizo hilo la
kunipa fedha.
Niseme mapema kwamba tangu kuzaliwa
kwangu sijawahi hata mara moja
kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani
au nje ya nchi. Kumuingiza mtu ambaye
amejenga jina lake kwenye taaluma ya
kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la
kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si
uungwana bali ni unyama.
Kutokana na uchafuzi huu wa wazi dhidi
ya taswira yangu binafsi na watu
wengine walioingizwa kwenye mkumbo
huu, nimeandika rasmi kwa Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa
kumwomba athibitishe kwamba
kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema
ni kweli ni taarifa ya chama au
kiikanushe ili niweze kuchukua hatua za
kisheria dhidi ya waandishi wa hekaya
hiyo.
Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa
kutishiwa maisha kutoka kwa mtu
anayejiita Theo Mutahaba na kuahidiwa
KUPOTEZWA endapo nitaendelea na
jitihada zangu za kupambana na ufisadi
na kutafuta haki kwa Watanzania wote
pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi,
kikanda, kikabila na kidini.
Natarajia kuchukua hatua kali za
kisheria dhidi ya wote ambao
wamehusika na utungaji na uenezi wa
taarifa hii. Nitahakikisha kwamba
wahusika wanatafutwa na kufunguliwa
mashitaka stahiki ya upotoshaji na
kuchafuana.
Ni matarajio yangu kwamba wale wenye
mapenzi mema na Tanzania, mimi
binafsi na utawala wa sheria,
wataelewa nia yangu ya kutafuta haki
katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa
ajili ya Watanzania na kama alivyopata
kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini,
Nelson Mandela; “Struggle Is My Life.”
Forward Ever, Backward Never- Kwame
Nkrumah
Zitto Kabwe (Mb)



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU