BAO
pekee la Haroun Athumani Chanongo dakika ya 57 limetosha kuipa Tanzania
Bara, Kilimanjaro Stars ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Somalia
mchana wa leo katika mchezo wa Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Kwa
matokeo hayo, Stars imetimiza pointi nne baada ya awali kutoa sare ya
1-1 na Zambia katika mchezo wake wa kwanza na mustakabali wake wa
kuingia Robo Fainali utategemea matokeo ya mechi za mwisho za kundi
hilo.
Katika
mchezo wa leo, Stars ilikuwa inaanza vizuri kutokea nyuma, lakini
wanapofika kwenye eneo la wapinzani wanaharibu, ama kwa kupeana pasi
mbovu au kupokonywa mipira kirahisi.
Na
hakukuwa na uelewano kabisa baina ya washambuliaji wa Stars, Elias
Maguri, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa hali ambayo ilifanya mabeki wa
Somalia wacheze kwa uhuru zaidi.
Somalia
walicheza vizuri kipindi cha kwanza na kukosa mabao mawili ya wazi,
kutokana na juhudi za kipa Ivo Mapunda kuokoa hatari zote.
Kipindi
cha pili, kocha Mdenmark Kim Poulsen alianza na mabadiliko, akiwatoa
Kiemba na Maguri na kuwaingiza washambuliaji wawili a Simba SC,
Ramadhani Singano na Haroun Chanongo ambao walibadilisha mchezo.
Pasi nzuri ya Singano ‘Messi’ iliunganishwa nyavuni na Chanongo dakika ya 57 kuipatia Stars bao hilo pekee.
Baada
ya bao hilo, Stars iliendelea kushambulia kupitia kwa Singano na
Chanongo, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi. Somalia nayo iliendelea
kushambulia lango la Stars na kuishia kukosa mabao mawili ya wazi, sifa
zimuendee Ivo Mapunda.
Kim
Poulsen alimtoa Mrisho Ngassa dakika ya 79 na kumuingiza Farid Mussa,
lakini mabadiliko hayo hayakuleta jipya upande wa Stars.
Kikosi
cha Stars leo kilikuwa; Ivo Mapunda, Himid Mao, Erasto Nyoni, Said
Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar, Athumani Iddi
‘Chuji’, Elias Maguri/Haroun Chanongo dk46, Amri Kiemba/Ramadhani
Singano ‘Messi’ dk46 na Mrisho Ngassa/Farid Mussa dk79.
Somalia;
Mohamed Sherif, Hassan Ali Roble, Mohammed Tahlil Shidane, Aden Hussein
Ibrahim, Hassan Hussein Mohamed, Daud Abdullah Hassan, Sidi Mohamed
Omer, Mohamed Abdi Hayow/Mahmoud Adi Mohamed dk63, Jabril Hassan
Mohamed, Mohamed saleh Hussein na Sadaq Abdulkadir Mohamed/Deki Abdullah
Nur dk88.
CHANZO: BIN ZUBEIRY