Facebook Comments Box

Thursday, March 14, 2013

DOWNLOAD WIMBO MPYA WA NAY WA MITEGO NA DIAMOND HAPA




WAZIRI MEMBE ARUKA KIMANGA KUHUSIKA NA SAKATA LA KIBANDA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika gazeti la Mtanzania toleo namba 7255 la tarehe 13 Machi, 2013 ilitolewa taarifa yenye kichwa cha habari “SAKATA LA KUTESWA KWA KIBANDA: Membe atajwa” na kwamba eti mimi ninahusika na vitendo vya kikatili na unyama alivyofanyiwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa kampuni ya New Habari, Bw. Absalom Kibanda.

Nimeshangazwa na kusikitishwa sana na habari hizo na ningependa kuwahakikishia Watanzania wenzangu kwamba sijahusika, sihusiki na sina sababu ya kuhusika kwa namna yoyote ile. Sina nia, genge wala fedha za kufanya shughuli kama hiyo. Katika maisha yangu yote, sijawahi kugombana naye na hajawahi kunifanyia ubaya wowote. Kwa kifupi, sina uhasama na Bw. Absalom KIbanda.

Taarifa iliyotolewa na Mtanzania ni taarifa ya uongo, ni habari za kuunga-unga maneno na habari za kughshi. kwa vyovyote vile, mwandishi wa habari hii na wenzake wana malengo ya kisiasa anayoyajua yeye na wenzake wanaomtumia. Huu ni mwendelezo wa mkakati wa kisiasa wa kunichafua ambao umekuwa ukiendelezwa na wale wasionitakia mwema. Wanajaribu kuwaondoa Watanzania katika kiu yao ya kutaka kufahamu ukweli wa jambo hili.

Nawashukuru sana wananchi wenzangu, jamaa na marafiki walioniletea salamu za kunitia moyo. Naungana nao katika kujiuliza, hivi kiburi hiki, dhihaha hii na ujsriri huu wa kusema uongo hadharani wanautoa wapi!? Jeuri na kiburi cha nmana hii hakiwezi kutokana na sheria za nchi, haki ya kikatiba wala hofu ya Mwenyezi Mungu. Naomba Watanzania wenzangu mnisaidie kutegua kitendawili hiki. Naamini kwa dhati kwamba ukweli kuhusu suala hili utajulikana na yeyote mwenye ushahidi wa kweli aonyeshe uzalendo wake kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.

Mwisho, wakati nashauriana na wanasheria wangu kuona hatua ya kuchukua dhidi ya kuchafuliwa huku, nawaomba Watanzania wenzangu tuvute subira na tuache vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi zake ili Watanzania hatimaye wajue ukweli wa kilichotokea.

Bernard Kamillius Membe (Mb)

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


RAIS KIKWETE AKIWA CHUO KIKUU CHA KIISLAM CHA MOROGORO (MUM) NA HOTUBA YAKE

Picture
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipunga mkono kuaga wanafunzi na wafanyakazi baada ya kuzindua rasmi jengo la Kitivo cha Sayansi la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro leo Machi 14, 2013 mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Mama Mwantumu Malale.
Picture
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mmoja wa wahadhiri Profesa Juma Mikidadi Mtupa (aliyeketi) Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Mama Mwantumu Malale, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Hamza Mustafa Njozi na wadau baada ya kuzindua rasmi jengo la Kitivo cha Sayansi la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro leo Machi 14, 2013 mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Mama Mwantumu Malale.
HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA UFUNGUZI RASMI WA JENGO LA KITIVO CHA  SAYANSI KATIKA CHUO KIKUU CHA WAISLAMU CHA  MOROGORO (MUM), TAREHE 14 MACHI, 2013, MOROGORO



Mzee Kitwana Suleiman Kondo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF);

Mheshimiwa Joel Bendera, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;

Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro;

Profesa Hamza Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro;

Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na Jumuiya mliohudhuria;

Wageni waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Niruhusuni niungane na wenzangu walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa.  Nakushukuru sana Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro na viongozi wenzako kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya ufunguzi wa jengo la Kitivo cha Sayansi katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro. Mmenipa heshima kubwa ya kuwa sehemu ya historia ya Chuo hiki.  Kwa kweli, nimefarijika sana kuona Chuo chetu kinazidi kupata mafanikio ya kutia moyo hasa ukizingatia ukweli kwamba kina muda mfupi tu tangu kuanzishwa kwake.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Natoa pongezi nyingi kwako, Makamu Mkuu wa Chuo na wale wote walioshiriki kubuni wazo la kuwa na jengo la Kitivo cha Sayansi na kufanikisha ujenzi wake.  Juhudi zao na moyo wao wa kupenda maendeleo ndio umetufanya sisi kujumuika hapa leo kushuhudia mafanikio haya. Hakika ni jambo la kujivunia. Pia, nawapongeza sana Wajenzi na 
Mhandisi Mshauri kwa kazi nzuri waliyofanya ya ujenzi wa jengo hili.  Sote tunaliona jengo lilivyojengwa vizuri na kwa namna yake linapendezesha mandhari ya Chuo.

Kwa namna ya pekee napenda kwa niaba yenu nitoe shukrani zangu za moyoni kwa taasisi ya Al-Barakah kwa kufadhili ujenzi wa jengo hili.  Asanteni sana kwa ukarimu wenu na upendo mkubwa mliouonesha kwa nchi yetu na watu wake. Naomba taasisi nyingine na watu binafsi waige mfano huu mzuri wa kusaidia miradi mbalimbali inayonufaisha jamii.  Tukumbuke ule msemo wa wahenga kuwa “kutoa ni moyo, usambe si utajiri”.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Mabibi na Mabwana;

Kwa miaka mingi madhehebu ya dini  na mashirika ya dini yamekuwa washirika muhimu sana wa Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.  Yamekuwa yanajihusisha na kutoa huduma kwa jamii kama vile afya, elimu na nyinginezo. Kwa ajili hiyo watu wengi sana nchini wamenufaika na wanaendelea kunufaika na huduma zinazotolewa na mashirika ya dini.

Kwa miaka mingi  mashirika na  taasisi za madhehebu ya dini ya Kikristo ndiyo yaliyokuwa yakionekana kutoa huduma hizo. Kwa upande wa Waislamu, ukiacha Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, mchango umekuwa mdogo sana. Ni jambo la faraja kubwa kuona Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF) ikionyesha njia.  Kwa kumiliki na kuendesha Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro kwa ufanisi, MDF inatoa mchango muhimu katika kuendeleza elimu ya juu na maendeleo nchini.  Idadi kubwa ya wanafunzi waliofuzu masomo yao na waliopo katika Chuo hiki tangu kilipoanzishwa mwaka 2005 ni ushahidi tosha wa kazi nzuri inayofanywa na MDF.  Hongereni sana.  Tunawaombea kwa Mola mpate mafanikio makubwa zaidi miaka ya usoni kwa upande wa elimu na huduma nyingine muhimu.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Katika kipindi cha miaka saba sasa, Serikali yetu imeongeza sana uwekezaji katika upanuzi wa elimu  tangu ya awali hadi elimu ya juu.  Tumeamua kufanya hivyo kwa sababu vijana wengi waliokuwa wanastahili kupata elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwahawapati. Tanzania ni kubwa kuliko Kenya na Uganda kwa eneo na idadi ya watu lakini ndiyo tuliokuwa na idadi ndogo ya wanafunzi kwa ngazi zote hizo.  Kwa mfano, mwaka 2005 idadi ya wanafunzi waliokuwa Chuo Kikuu nchini Kenya ilikuwa 108,407, Uganda 88,360 na kwa baadhi ya nchi za SADC kama vile Afrika Kusini idadi hiyo ilikuwa 717,973. Wakati wenzetu wakiwa na idadi hiyo, sisi tulikuwa na wanafunzi 40,719 tu katika vyuo vikuu nchini.  Hali ilikuwa hivyo pia kwa elimu ya sekondari.  Kenya ilikuwa na wanafunzi 925,341, Uganda 619,519 na Afrika Kusini4,186,882 wakati Tanzania ilikuwa na wanafunzi 524,325 tu waliokuwa katika shule za sekondari.

Tuliona hali hii haikubaliki hivyo tukaamua hatuwezi kuiacha iendelee.  Tukaamua kudhibiti. Tukachukua hatua tulizochukua za kupanua elimu katika ngazi zote.  Matokeo ya uamuzi huo ni kwamba vijana wanaopata fursa ya kupata elimu katika ngazi zote wamekuwa wengi kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu, tumewafikia na kuwapita majirani zetu. Kazi kubwa tunayoendelea nayo sasa ni kuwekeza katika kuimarisha ubora wa elimu waipatayo vijana wetu kwa kuongeza walimu, vifaa vya kufundishia, vitabu na huduma nyinginezo. Inshallah hata kwa dhamira yetu, hii njema Mola atatuwezesha. Mwanzo mgumu lakini hatma itakuwa nzuri.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kufuatia juhudi hizo, idadi ya wanafunzi waliopo kwenye vyuo vikuu nchini imeongezeka sana, kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi wanafunzi 166,484 mwaka 2012. Kwa upande wa sekondari mwaka 2011 tulikuwa na wanafunzi milioni 1.79 na wenzetu wa Kenya walikuwa na wanafunzi milioni 1.77. Haya ni mafanikio makubwa.

Serikali itaendelea kuwekeza  kwenye upanuzi wa fursa za elimu na ubora wake. Hata hivyo ushiriki wa wadau wengine kuunga mkono juhudi za serikali ni jambo muhimu sana.  Tumeweka  mazingira mazuri kwa wadau hao kufanya hivyo na mafanikio yanaonekana wazi. Kama nilivyokwishasema awali, mashirika ya dini yamekuwa wadau wa kutumainiwa na mchango wao uko wazi. Unajieleza wenyewe. Kwa mfano, katika vyuo vikuu 49 vilivyopo nchini, vinavyomilikiwa na umma ni 14 tu. Vyuo vikuu 24 vinamilikiwa na mashirika ya dini na 11 na sekta binafsi.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa na muhimu unaotolewa na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na sekta binafsi.  Ninyi mmekuwa washirika wazuri na wa uhakika katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu katika nchi yetu.  Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nanyi ili kuwawezesha vijana na Watanzania wengi zaidi waweze kupata elimu. Uamuzi wa kufanya utaratibu wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu uhusishe wanafunzi wa vyuo visivyokuwa vya umma ni moja ya mambo mengi muhimu yanayofanywa na Serikali kuthibitisha usemi wangu huo.

Tulipoingia madarakani mwaka 2005 tulifanya mambo mawili muhimu kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.  Kwanza uamuzi kwamba, mikopo itolewe kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma na vile visivyokuwa vya serikali. Kabla ya hapo ilihusu vyuo vya umma pekee. Pili kwamba, kila mwaka tuongeze fedha zinazotengwa  kwa ajili ya Mfuko huo ili idadi ya wanafunzi wanaonufaika iongezeke. Tulikuta Mfuko ukiwa na  shillingi billioni 56.1 unanufaisha wanafunzi 16,345 mwaka 2005. Tukaongeza kila mwaka na katika mwaka huu wa fedha (2012/13) tumetenga shillingi bilioni 345 zinazowanufaisha wanafunzi 98,772.

Tutaendelea kuongeza fedha katika Mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na hata ifikie siku moja tuweze kuwakopesha wote bila ya kujali sifa ya uwezo wa wazazi au walezi kulipa ada.  Kwa kasi tuliyonayo na kwa jinsi tunavyozidi kufanikiwa katika kukusanya mapato ya serikali, naamini miaka michache ijayo tunaweza kufikia lengo hilo. Nawasihi Bodi ya Mikopo iwekeze katika  kuimarisha uwezo wa kuwafuatilia waliokopeshwa kulipa mikopo waliyopewa. Matamanio yangu ni kuwa fedha zilizotolewa zizunguke ili tupunguze kiasi kinachotolewa na bajeti ya serikali kila mwaka.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Mabibi na Mabwana;

Niruhusuni nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Mkuu wa Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo, Wahadhiri  na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu hiki  kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo ya kuendeleza na kuboresha Chuo. Tumeshuhudia ujenzi wa jengo nililolifungua leo. Tumeona mafanikio kwa upande wa ongezeko la idadi ya wanafunzi, walimu, wafanyakazi na fani zinazofundishwa katika kipindi hiki kifupi cha uhai wa Chuo hiki.

Nimefurahishwa na kufarijika sana  kusikia kuwa ubora wa elimu inayotolewa hapa chuoni ni jambo linalopewa kipaumbele cha kwanza.  Jambo hili ni muhimu sana kulisisitiza kwani tunataka wahitimu wa Chuo hiki wafanane na wahitimu wa Chuo chochote kizuri nchini na hata duniani.  Ningependa kuona wahitimu wa Chuo hiki wanagombewa katika soko la ajira.  Hili ni jambo linalowezekana.  Kinachotakiwa  ni uamuzi wa Baraza na Seneti kuwa iwe hivyo na kuchukua hatua zipasazo.  Sina shaka kuwa mnaweza kufanya hivyo.  Hakika mnaweza, na sote kwa umoja wetu tunaweza.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Nimefurahi sana, pia, kusikia kuwa Chuo kinatoa mafunzo ya ualimu. Bila ya shaka mnaelewa kwa nini nafurahi. Tuna uhaba mkubwa wa walimu nchini hivyo Chuo cho chote kinachotoa mafunzo ya ualimu hunifurahisha.  Endeleeni kuimarisha mafunzo hayo ili Chuo chenu kitambulike na kukubalika nchini kwa sifa ya kutoa walimu wazuri.  Walimu wa kutoka Chuo hiki wawe wale wanaojua vyema masomo wanayofundisha, mahiri kufundisha na waadilifu.  Naomba pia mtoe kipaumbele cha juu kwa mafunzo ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati.  Mkifanya hivyo, mtakuwa mnatoa mchango mkubwa katika jitihada za kupunguza uhaba wa walimu wa masomo hayo nchini.  Naamini kitendo cha kuzindua Jengo la Kitivo cha Sayansi, kilichofanyika muda mfupi uliopita kinatoa matumaini ya Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro kuchangia katika jitihada za kupunguza pengo la walimu wa sayansi nchini.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Nimewasikia mkieleza kwa ufasaha changamoto kubwa na ndogo ambazo Chuo inakabiliana nazo.  Nawapongeza kwa dhati, wewe na viongozi wenzako kwa ubunifu wenu na hatua mnazochukua kuzikabili changamoto hizo.  Nawaahidi msaada na ushirikiano wangu na wa serikali kwa yale yaliyoko kwenye uwezo wangu na wa serikali katika kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zinazowakabili.

Nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kutafuta vyuo vikuu rafiki vilivyoko katika nchi mbalimbali duniani mnavyoweza kushirikiana navyo.  Endeleeni kufanya hivyo kwani vyuo vikuu vingi duniani hufanya hivyo.  Hamtakuwa wa kwanza na wala hamtakuwa mnafanya jambo la kustaajabisha. Mnaweza,        mkipenda, kuwaomba Mabalozi wetu waliopo katika nchi mbalimbali duniani wawasaidie. Ni wajibu wao kufanya hivyo kwani kusaidia kusukuma maendeleo ya hapa nchini kutoka huko waliko ndilo jukumu lao la msingi. Vile vile, nimefurahishwa na mipango yenu ya baadaye ya kuwa na matawi katika mikoa mbalimbali nchini.  Hongereni kwa uamuzi wenu wa busara. Lazima Chuo kitanuke kwa maana ya kuwa kikubwa zaidi, makao makuu na kwa kuwa na vyuo vishiriki na shule au  vitivo sehemu mbalimbali nchini.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kazi iliyo mbele yenu ni kubwa, hivyo ni vyema kuweka mikakati mizuri na mipango thabiti ya utekelezaji na ufuatiliaji wa dhamira yenu hiyo njema.  Rai yangu kwenu ni kuwaomba muwe wabunifu zaidi hasa katika kutafuta vyanzo vingine vya mapato vitakavyosaidia Chuo kujiendesha bila kutegemea ada peke yake.  Chuo kiangalie uwezekano wa kufanya shughuli zitakazowaingizia mapato kama vile kufanya shughuli za kutoa ushauri. Pia muangalie uwezekano wa kuwekeza wenyewe kwenye miradi ya kiuchumi au kwa kushirikiana na wawekezaji katika baadhi ya maeneo.

Kuhusu nafasi mbili za ufadhili nilizopewa na Chuo kikuu cha Tun Abdul Razak cha Malaysia, nitafuatilia kujua  kilichoendelea na kinachoendelea. Je, nafasi hizo bado zipo?  Zikiwepo, nitawasiliana na wahusika waangalie uwezekano wa kuwapeni. Kama zimeshagawiwa basi tusubiri safari ijayo. Kwa  masuala ya ardhi na maombi mengine nimeyasikia, yaleteni tuangalie namna ya kusaidiana.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo, na

Wafanyakazi wote wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;

           Napenda kuwakumbusha kuwa mnayo dhamana kubwa na wajibu mkubwa na wa kihistoria. Ule ukweli kwamba ni mara ya kwanza kwa Taasisi ya Waislamu wazawa kuwa na Chuo Kikuu inawapeni wajibu maalum wa kuhakikisha Chuo kinafanikiwa. Ni mtihani na changamoto ya aina yake kuthibitisha kuwa Waislamu nao wanaweza kuwa na Chuo kizuri na chenye kutoa elimu ya ubora wa hali ya juu.  Kwa sababu hiyo hamna budi kuhakikisha kuwa mna mipango mizuri ya kujenga Chuo cha hadhi na ubora wa hali ya juu.  Ihakikishwe kuwa mipango hiyo inatekelezwa kwa ukamilifu.

           Aidha jumuiya yote inao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, maarifa na weledi ili dhima hiyo ya Chuo iweze kutimizwa kwa ukamilifu. Timizeni wajibu wenu ipasavyo ili jina la Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro likue haraka. Sifa yake isambae na kuvuma kote nchini. Chuo kifanye vizuri ili wanafunzi waone fahari kuwa wahitimu wa Chuo hiki. Chuo ambacho, wazazi wapende kuleta vijana wao kuja kusoma hapa. Kwa jinsi Mkuu wa Chuo alivyoeleza, mimi nina imani mnaweza, fanyeni kweli.

Ndugu Wanafunzi wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;

Naomba wote muone fahari ya kuwa wanafunzi katika Chuo cha kihistoria hapa nchini.  Nawasihi mjitume kwa kadri ya uwezo na vipaji mlivyopewa na Mwenyezi Mungu mfanikishe kile kilichowaleta.  Jifunzeni kwa bidii mfaulu vizuri ili mkihitimu muwe kielelezo kizuri cha mafanikio na ubora wa  Chuo  Kikuu Cha Waislamu cha Morogoro.  Muwe Mabalozi na kioo cha ufanisi wa Chuo hiki. Nawasihi mjiepushe na mambo yatakayowapunguzia muda au kuwaondoa katika shughuli ya msingi iliyowaleta hapa ya kujifunza mpate digrii katika fani mliyochagua mwenyewe kuisomea.  Vishawishi ni vingi na wapo watu wengi wanaopanga kuwashawishi mtumie muda wenu adhimu kufanya wanayoyataka wao ambayo mkishiriki huwatoa kwenye malengo na kutekeleza yao. Mambo ya dunia ya nje ya Chuo ni mengi huna budi kutambua lipi ufanye na lipi usifanye na kwa wakati gani!

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu ni mtu mzima, si mtoto. Lazima ujue kuwa unawajibika kwa kila unaloamua na kutenda.  Amua kuwajibika vizuri. Fikiri kabla ya kutenda, changanua lipi ni lipi kabla ya kufanya uamuzi wa kile unachotaka kufanya.  Wakati wote uongozwe na busara na hekima na siyo jazba na ushabiki wa matakwa ya kundi.  Kama ni jema fanya na kama si jema usifanye.  Kwanza tambua wewe ni nani na uko hapa kwa ajili gani. Lazima ujue kuwa hatma ya yote uko peke yako.  Utafaulu au kufeli wewe.  Utapata shahada wewe na si mtu mwingine.  Hakuna ubia wa kufaulu au kufeli au kiwango cha kufaulu. It will always remain personal. Katika masomo unanufaika wewe.  Shirikiana na wengi lakini usisahau kujali maslahi yako.  Maslahi ya wengi yasiyojumuisha yako, yahoji vizuri kabla ya kuamua kushiriki au kufanya. Vinginevyo labda kama umeamua kujitoa muhanga, uwe shujaa. Hata kwa hilo, sijui utakuwa shujaa wa nani.

Mabibi na Mabwana;

Kabla ya kumaliza napenda kutambua na kumshukuru Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa na viongozi wa MDF kwa juhudi zao za pamoja zilizowezesha Chuo hiki kuwepo.  Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru wananchi wanaokizunguka Chuo kwa ujirani mwema na wakazi wa Morogoro kwa ujumla kwa kukipokea vizuri na kuishi na wanajumuiya wa Chuo hiki kwa upendo mkubwa. Naomba muendelee na moyo na ushirikiano huo.

Baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunialika. Nawatakia kila la heri na mafanikio tele.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Picture
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifunua pazia kuzindua rasmi jengo la Kitivo cha Sayansi la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro leo Machi 14, 2013 mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Mama Mwantumu Malale.
Picture
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifunua pazia kuzindua rasmi jengo la Kitivo cha Sayansi la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro leo Machi 14, 2013 mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Mama Mwantumu Malale.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo juu ya ujenzi wa jengo la kitivo cha Teknohama toka kwa Bw. Hamza Mustafa Njozi kabla ya kuzindua rasmi jengo la Kitivo cha Sayansi la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro leo Machi 14, 2013 mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Mama Mwantumu Malale.



KIBONZO CHA LEO: KUHUSU KUONGEZA MAUMBO




HIVI NI KWELI HII NI OFISI YENU?




MOURINHO KURUDI CHELSEA? ABRAMOVICH AMPA BONGE LA ZAWADI

Mourinho na Abramovich
Tajiri wa Chelsea Abramovich amezidi kuimarisha uhusiano wake na Kocha wa Real Madrid Morinho baada ya kumnunulia zawadi ya saa yenye thamani ya fedha za kiingereza Paund 350,000 ambazo ni sawa na Dollar za kimarekani 400,000 ambazo ni sawa na fedha zetu za kitanzania Tsh 875,000,000 ( Milioni Mia nane na sabini na tano)

Kipindi cha Televisheni cha Kihispania kinachoitwa  Punto Pelota kimeripoti kuwa Morinho ataachana na Real Madrid mwisho wa msimu na kujiunga na Chelsea. Pia kituo hicho kimeripoti kuwa wachezaji wakongwe wa Chelsea wanajua kuwa viongozi wa kilabu hicho wanafanya mawasiliano na Morinho na atakuja kuchukua nafasi ya kocha aliopo sasa ambae ni Benitez.



BAADA YA VIDEO YAKE KUVUJA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII; HATIMAYE LWAKATARE AKAMATWA

Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Chadema,Wilfred Lwakatare 



Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Chadema,Wilfred Lwakatare jana alikamatwa, akahojiwa na kupekuliwa na polisi kwa tuhuma za uchochezi wa uvunjifu wa amani.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso aliliambia Mwananchi jana kuwa Lwakatare alikamatwa kutokana na taarifa zilizopatikana kutoka katika video kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha akiwahamasisha watu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani au uhalifu. Alipoulizwa mahali na lini alikamatwa Lwakatare, Senso alisema hilo halijalishi, lakini jambo la msingi ni kwamba wako naye kwa ajili ya uchunguzi na hakutaka kuweka bayana ni lini wangemwachia.

Siku nzima ya jana mitandao ilikuwa imetawaliwa na habari ya picha ya video ikimwonyesha Lwakatare akidaiwa kupanga mikakati ya kumteka Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky. Lwakatare alionekana akitoa maelekezo kwa watu, ambao sura zao hazikuonekana, akiwataka kufuatilia nyendo za Msacky.

Alionyeshwa akiwataka watu hao kumkamata bila ya kumdhuru Msacky, lakini wamtupe mbali kama njia ya kumnyamazisha. Alikuwa anamtuhumu Msacky kama alikuwa anashirikiana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ili kukihujumu chama chao.

“Inabidi mfahamu nyendo za mtu huyu, kama anapenda vitu kama kutembea usiku au kinywaji anachokunywa,” alinukuliwa kwenye mtandao huo.

Pia anaonekana kwenye video hiyo akitoa mbinu mbalimbali za namna ya kufanya utekaji nyara.

Wakili wa Lwakatare alonga

Wakati akihojiwa na kupekuliwa, Lwakatare aliongozana na wakili wa kujitegemea, Nyaronyo Kicheere, ambaye alilieleza Mwananchi kuwa mteja wake alichukuliwa kutoka ofisini kwake kwenye Makao Makuu ya Chadema yaliyoko Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kicheere alidai kuwa hakuwa na uhakika kuwa Lwakatare alikamatwa muda gani ofisini kwake kwani yeye aliitwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi saa 9.00 alasiri.Mwananchi, hata hivyo, lina taarifa kuwa Lwakatare alikamatwa na askari wanne saa 7.00 mchana na kupelekwa Makao Makuu ya Polisi.

Lwakatare, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini kupitia CUF na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alipokamatwa alifuatana na maofisa kadhaa wa Chadema akiwamo Ofisa wa Ulinzi wa chama hicho, Hemed Sabula na Ofisa wa Mawasiliano aliyejulikana kwa jina moja tu la Karungebe.

Alichukuliwa ndani ya gari aina ya Land Cruiser na kupelekwa moja kwa moja Makao Makuu ya Jeshi la Polisi katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Mahojiano
Kicheere alisema Lwakatare alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi ingawa alidai polisi hawakubainisha ni uchochezi upi.
Mahojiano hayo kwa Lwakatare yaliongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Obadia Jonas.
“Lwakatare alihojiwa kuanzia saa 9.00 alasiri hadi 9.55 jioni na tuhuma zilizomkabili ni uchochezi. Ila askari hawakuniambia ni uchochezi upi,” alieleza Kicheere. Alisema kuwa baada ya mahojiano yale waliamriwa kwenda nyumbani kwa Lwakatare kwa ajili ya upekuzi.

Upekuzi
Lwakatare, ambaye anaishi eneo la Kimara King’ong’o jijini Dar es Salaam, alisindikizwa na askari saba walioongozwa na ACP Jonas. Katika msafara huo wa kwenda kupekua nyumbani kwake, maofisa wa Chadema walizuiwa kuongozana naye, isipokuwa mwanasheria wake, Kicheere, ndiye aliruhusiwa kuongozana naye.

“Tunavyoongea na wewe hivi sasa ni kwamba upekuzi unaendelea katika vyumba vya nyumba . Kwa sasa tuko ndani ya chumba chake cha kulala,” alieleza Kicheere.

Kicheere alisema upekuzi huo ulianza saa 10.30 jioni na ulilenga katika kutafuta nyaraka ambazo zingeweza kutumika kama ushahidi wa tuhuma hizo. Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa upekuzi kilichokuwa kinatakiwa kufuata ni kuandikisha maelezo katika Kituo cha Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

“Hawa jamaa wanaendelea na upekuzi na hawajapata kitu chochote muda huu tunavyoongea na wewe. Ila tukimaliza tutarudi Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuandikisha maelezo,” aliongeza Kicheere.

Dk Slaa anena
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema polisi walifika katika ofisi za chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuomba kuzungumza na Lwakatare.

 SOURSE: MWANANCHI


MUM NA CHUO KIKUU CHA OSMAN SOKOTO WAANZISHA USHIRIKIANO


Pichani; kutoka kushoto ni Ahmed Saggaf wa MUM, Sultan wa Sokoto, Alhaj Muhammad Sa’ad Abubakar III,     
 
Chuo Kikuu cha Kiislam Morogoro (Mum), kimeanzisha uhusiano wa kitaaluma na Chuo Kikuu cha Osman Dan Dodio Sokoto (Udus) cha Nigeria.

Makubaliano hayo yalifikiwa kati ya ujumbe wa Mum ulioongozwa na Kiongozi wa Baraza la Chuo, Ahmed Saggaf na Sultan wa Sokoto, Alhaji Muhammad Sa’ad Abubakar III. Pia, ujumbe wa Mum ulijumuisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Kassim Umba na Mhadhiri wa chuo hicho, Faraj Tamim.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Mum, inasema lengo la ziara hiyo ni kuanzisha uhusiano kati ya Chuo Kikuu cha Osman Dan Fodio Sokoto (UDUS) na Chuo Kikuu cha Kiislam Morogoro (Mum).

Inasema ushirikiano huo utahusisha programu kubadilisha wahadhiri na wanafunzi, kubadilishana uzoefu kwenye masomo ya Sharia, udaktari, jiolojia na utoaji nafasi za masomo. UDUS kina wanafunzi 35,000.

Vilevile uongozi wa MUM ulimuahidi Sultani wa Sokoto, Alhaj Muhammad Sa’ad Abubakar III kuendeleza ushirikiano huo, huku Sultan akielezea kufurahishwa kwake na mwaliko wa kutembelea Tanzania ambayo imekuwa ikisifiwa duniani kwa umoja na amani.

Pia, Sultan alishukurua uongozi huo kwa kutembelea Sokoto na kwamba, kutokana na juhudi hizo zimeweza kuunganisha vyuo hivyo

SOURSE: MWANANCHI

JAJI: DPP HANA MAMLAKA YA KUZUIA DHAMANA: VIONGOZI WA UAMSHO WAOMBE DHAMANA


 Photo: DPP hana mamlaka ya kumnyima mtu dhamana mahakamani

Salma Said,
Zanzibar: KESI ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) imeingia hatua mpya baada ya Mahakama Kuu jana kufuta maamuzi yote ya Mrajis wa Mahakama hiyo…

Viongozi hao wanakabiliwa na kesi ya madai ya uchochezi na kuhatarisha usalama wa taifa la Zanzibar.
“Maamuzi ya Mrajis yote yanafutwa kwani hayakuwa sahihi kwa vile Mrajis hana mamlaka ya kisheria ya kupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu,” alisema Jaji Abraham Mwampashi aliyesikiliza suala hilo jana katika Mahakama Kuu Vuga mjini hapa..

Moja ya mambo makuu yaliyofutwa ni zuio la dhamana ambalo Mrajis alilikubali kama lilivyokuwa limetolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP).
Jaji Mwampashi alitolea maamuzi baada ya pande mbili katika kesi hiyo za upande wa serikali na utetezi kubishana juu ya uwezo wa Mrajis katika kutoa maamuzi ya dhmana kwa washitakiwa hao.

Mawakili wa utetezi walidai kuwa Mrajis hana mamlaka hayo na upande wa waendesha mshitaka walidai kwamba anao uwezo huo.
Jaji Mwampashi alisema DPP anao uwezo wa kuizuia Polisi tu kumpa dhamana mtuhumiwa, lakini sio Mahakama kama ilivyotokea katika suala hili.

Jaji Mwampashi alisema DPP alitakiwa aeleze sababu za washitakiwa kutopewa dhamana na ni athari zipi za usalama wa taifa zitatokea iwapo watakuwa nje.
Alisema kama sheria ingekuwa hivyo kungekuwa hakuna haja ya kuwepo kwa Mahakama kama mtu mmoja anakuwa na haki hiyo na kusingeifanya Mahakama kuwa kimbilio la wanaoona wanapoteza haki zao.

Jaji Mwamapashe alisema hawezi kufuta kibali cha DPP cha kufunga dhamana kwa sababu hakupewa nafasi ya kuja mahakamani kutetea hoja yake.
Aliwaelekeza washitakiwa kuwasilisha upya ombi la dhamana ambalo litasikilizwa baada ya kesi yao ya msingi kupangiwa Jaji wa kuisikiliza.
Alisema Mrajis kisheria ana uwezo wa kusikiliza kesi za madai zinapokuwa katika hatua ya awali ya kutajwa, lakini akashangzwa na hatua kwamba Mrajis aliambiwa kwa mdomo na Jaji Mkuu kusikiliza kesi hiyo.

Washitakiwa hao ni Masheikh Farid Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, , Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmada Omar, Abdalla Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini, Azzan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman.

Washitakiwa hao wako rumande tangu kesi yao ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 25, mwaka jana. Wamerudishwa rumande wakisubiri kesi yao kupangiwa Jaji wa kuisikiliza na kujilikana itaanza kusikilizwa lini.


Salma Said,
Zanzibar: KESI ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) imeingia hatua mpya baada ya Mahakama Kuu jana kufuta maamuzi yote ya Mrajis wa Mahakama hiyo…

Viongozi hao wanakabiliwa na kesi ya madai ya uchochezi na kuhatarisha usalama wa taifa la Zanzibar.
“Maamuzi ya Mrajis yote yanafutwa kwani hayakuwa sahihi kwa vile Mrajis hana mamlaka ya kisheria ya kupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu,” alisema Jaji Abraham Mwampashi aliyesikiliza suala hilo jana katika Mahakama Kuu Vuga mjini hapa..

Moja ya mambo makuu yaliyofutwa ni zuio la dhamana ambalo Mrajis alilikubali kama lilivyokuwa limetolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP).
Jaji Mwampashi alitolea maamuzi baada ya pande mbili katika kesi hiyo za upande wa serikali na utetezi kubishana juu ya uwezo wa Mrajis katika kutoa maamuzi ya dhmana kwa washitakiwa hao.

Mawakili wa utetezi walidai kuwa Mrajis hana mamlaka hayo na upande wa waendesha mshitaka walidai kwamba anao uwezo huo.
Jaji Mwampashi alisema DPP anao uwezo wa kuizuia Polisi tu kumpa dhamana mtuhumiwa, lakini sio Mahakama kama ilivyotokea katika suala hili.

Jaji Mwampashi alisema DPP alitakiwa aeleze sababu za washitakiwa kutopewa dhamana na ni athari zipi za usalama wa taifa zitatokea iwapo watakuwa nje.
Alisema kama sheria ingekuwa hivyo kungekuwa hakuna haja ya kuwepo kwa Mahakama kama mtu mmoja anakuwa na haki hiyo na kusingeifanya Mahakama kuwa kimbilio la wanaoona wanapoteza haki zao.

Jaji Mwamapashe alisema hawezi kufuta kibali cha DPP cha kufunga dhamana kwa sababu hakupewa nafasi ya kuja mahakamani kutetea hoja yake.
Aliwaelekeza washitakiwa kuwasilisha upya ombi la dhamana ambalo litasikilizwa baada ya kesi yao ya msingi kupangiwa Jaji wa kuisikiliza.
Alisema Mrajis kisheria ana uwezo wa kusikiliza kesi za madai zinapokuwa katika hatua ya awali ya kutajwa, lakini akashangzwa na hatua kwamba Mrajis aliambiwa kwa mdomo na Jaji Mkuu kusikiliza kesi hiyo.

Washitakiwa hao ni Masheikh Farid Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, , Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmada Omar, Abdalla Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini, Azzan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman.

Washitakiwa hao wako rumande tangu kesi yao ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 25, mwaka jana. Wamerudishwa rumande wakisubiri kesi yao kupangiwa Jaji wa kuisikiliza na kujilikana itaanza kusikilizwa lini.
Swali linabaki Tanzania Bara DPP amepata mamlaka hayo wapi?


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU