Facebook Comments Box

Friday, July 19, 2013

AZAM TV WAINGIA MKATABA WA MILIONI 331 NA SIMBA SPORTS CLUB KWA AJILI YA KURUSHA SIMBA TV

 Kutoka kushoto Mwenyekiti wa Simba Aden Rage, Katibu mkuu wa Simba Evodius Mtawala, Meneja wa Azam Said Mohamed na Abubakar Bakhresa baada ya kuweka saini mkataba huo.


KAMPUNI ya mpya ya Habari nchini, Azam Media Group, leo imeingia Mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh. Milioni 331 na klabu ya Simba ya Dar es Salaam kwa ajili ya kurusha kipindi maalum cha klabu hiyo, kitakachojulikana kama Simba TV kupitia kituo kipya cha Televisheni, Azam TV.

Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage, kwa pamoja na Katibu, Evodius Mtawala na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini, Hamisi Kilomoni waliiwakilisha klabu hiyo katika utiaji saini wa Mkataba huo mnono kwenye ukumbi wa Kibo, jengo la PSPF, Dar es Salaam.


Upande wa Azam uliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Abubakar Bakhresa, Meneja Mkuu, Said Mohamed na Mwanasheria, Shani Christoms ambao waliikabidhi Simba SC hundi za fedha hizo kwenye hafla hiyo.

Meneja wa Azam Media, Mzee Said alisema kwamba Mkataba huo ni mwanzo tu, lakini kampuni hiyo imejipanga kusaidia zaidi soka ya Tanzania kwa kuingia mikataba mingi yenye manufaa kwa mchezo huo nchini.

Alhaj Rage, pamoja na kuwashukuru Azam Media kwa Mkataba huo mnono, alisema klabu inategemea kujikomboa zaidi kiuchumi kutokana na mikataba ya udhamini kama hiyo na muda si mrefu wataingia mikataba mingine itakayokuza zaidi pato la klabu.

“Nimesikia pia mnataka kununua haki za Televisheni za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, mimi nasema karibuni na katika hilo, natoa angalizo, mkinunua haki za TV za Ligi Kuu, naomba mtoe fungu sawa kwa kila klabu, hakuna kubagua eti huyu apate kidogo, yule apate zaidi, hapana,”.

“Lazima mpira wa miguu katika nchi hii maendeleo yafike kila sehemu na tuondoe ubinafsi wa kujifikiria eti sisi Simba ndiyo tupate zaidi, hapana. Hiyo si haki, lazima na zile klabu ndogo pia nazo zinufaike sawa na sisi kwa kuwa tunacheza ligi moja,”alisema Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM).
CHANZO:BIN ZUBEIRY


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU