Tarehe
27 Desemba maelfu ya wananchi wa Mtwara waliandamana kudai gesi ya
Mnazi Bay itumiwe kuendeleza viwanda katika mkoa wa Mtwara kabla ha
ijasafirishwa
kwenda kutumiwa maeneo mengine ya nchi. Kwa muda mrefu CUF Chama cha
wananchi kimekuwa kikisisitiza kuwa na sera zitakazohakikisha kuwa
maliasili na rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote kwa
ujumla na hususani wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo maliasili
hiyo imegunduliwa.
Katika nchi nyingi utajiri mkubwa wa gesi na
mafuta umeleta balaa badala ya kuleta neema. Nchini Nigeria katika delta
ya mto Niger ambako ndipo mafuta yanachimbwa kuna ghasia kubwa za
kisiasa kwa madai kuwa wananchi wa eneo hilo hawanufaiki na rasilimali
yao.
Wananchi wa mikoa ya kusini wana sababu za msingi za kulalamika kuwa kwa muda wa miaka 51 ya uhuru wa
Tanzania Bara bado hawajatendewa haki.
Serikali ya mkoloni wa Kiingereza ilijenga reli kuunganisha Nachingwea
na Mtwara ilipoanzisha mradi wa kilimo cha karanga. Mradi huu
haukufanukiwa. Badala ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo na kuendeleza
uzalishaji wa mazao mengine kama vile korosho, ufuta, alizeti, kunde na
mbaazi, Serikali ya TANU baada ya kupata uhuru ikaamua kun’goa reli ya
Nachingwea – Mtwara na kuihamishia Kilosa Mikumi.
Zambia
ilipokuwa inakabiliwa na tatizo la kusafirisha mizigo yake isipitie
Rhodesia iliyokuwa inatawaliwa na wazungu wachache, walipendekeza kwa
serikali ya Tanzania kujenga reli kwenda Mtwara kwani bandari ya Mtwara
ni nzuri, ina kina kirefu na haina msongamano. Shaba ya Zambia
ingepakuliwa kwa haraka na kusafirishwa kwenda nchi za nje. Vile vile
mizigo inayoagizwa kutoka nje ingepakuliwa haraka na kusafirishwa kwenda
Zambia. Serikali ya Tanzania haikuafiki pendekezo la Zambia na
ikasisitiza reli ya TAZARA iende Dar es Salaam.
Gesi
ya Songosongo ilikuwa itumiwe kama malighafi katika kiwanda cha mbolea
cha Kilwa Ammonium Company. Prof Cleophace Migiro alienda kusomea PhD ya
Chemical engineering kwa maandalizi ya kuja kufanya kazi KILAMCO. Ardhi
ya kujenga kiwanda ilinunuliwa Kilwa Masoko, kiwanja cha ndege
kikatengenezwa, mpango wa kuimarisha bandari ya masoko ukaandaliwa.
Mgogoro wa uchumi wa miaka ya 1980 ikatibua mambo.
Dr.
Shija waziri wa Nishati na Madini katika kipindi cha kwanza cha Rais
Mkapa alizungumzia umuhimu wa kufufua mradi wa KILAMCO lakini hakuna
kilichotendeka. Gesi ilipoanzwa kuchimbwa Songosongo likajengwa bomba
dogo la nchi 12 kusafirisha gesi chini ya bahari toka Songosongo hadi
Somanga. Bomba la nchi 14 lilijengwa toka Somanga hadi Dar es Salaam.
Uwezo
wa mabomba haya ni mdogo ukilinganisha na gesi inayopatikana Songosongo
na mahitaji yake kwa shughuli ya kufua umeme na kutumia viwandani.
Mkopo wa kujengea bomba la Songosongo hadi Dar es Salaam ulighubikwa na
tuhuma za ufisadi za ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha IPTL
kinachotumia mafuta mazito ambacho gharama zake za kufua umeme ni za juu
sana. Mkataba wa TANESCO na IPTL uliiwajibisha TANESCO kuilipa IPTL
dola milioni moja kila mwezi hata kama haijazalisha umeme wowote.
Mkataba huu ulidhoofisha sana hali ya fedha ya TANESCO.
Kampuni
ya Artumas iligundua kuwepo kwa gas Mnazi Bay, Mtwara na kuanza
utaratibu wa kuichimba mwaka 2006 na kuitumia kufua umeme wa Megawati
18. Kabla ya mtikisiko wa sekta ya fedha na uchumi wa dunia wa mwaka
2008, Artumas ilikuwa na mpango wa kuwekeza kwenye mtambo wa kufua umeme
Mtwara wa Megawati 300 na kuunganisha Mtwara kwenye gridi ya taifa.
Mpango huu ulikubaliwa na serikali na ukaingizwa katika Mpango Kabambe
wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme (National Power Development Master
Plan). Mradi huu wa kufua umeme MW 300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika
mwaka huu wa 2012.
Mtikisiko wa uchumi
na fedha duniani wa 2008 uliikumba kampuni ya Artumas. Thamani ya hisa
za Artumas iliporomoka katika soko la mitaji Canada na Norway. Artumas
iliiomba serikali dola milioni 7 kunusuru Mradi wa Nishati wa Mtwara
(Mtwara Energy Project). Uwezo wake wa kutekeleza mpango wa kufua umeme
Mtwara ukatetereka pamoja na kuwa mradi huo una faida ya muda mrefu.
Kampuni ya Artumas Group Inc. iliamua kubadilisha jina lake na kuwa
Wentworth Resources Limited.
Wananchi
wa Mtwara wanahitaji kujua kwa nini serikali haikutafuta njia mbadala ya
kugharamia mpango wa kufua umeme na kuiunganisha Mtwara na gridi ya
taifa?
Wentworth Resources wamefanya
upembuzi yakinifu (feasibility study) na kubaini kwamba njia nzuri ya
kibiashara na kiuchumi ya kutumia gas wanayoweza kuzalisha Mnazi bay
hivi sasa ni kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mbolea na kemikali
nyingine Mtwara. Hata hivyo serikali imewamrisha kupeleka gesi
watakayozalisha kwenye bomba la gesi la kwenda Dar es Salaam. Gazeti la
Financial Time la London la tarehe 6 Desemba 2012 linaeleza
“Bob
McBean, executive chairman of Wentworth Resources, which explores in
Mnazi Bay, had been planning to use any gas finds together with an
existing discovery to power a petrochemical plant to make Africa’s first
home-produced fertiliser. “We can supply 80[bcf] right away but we’d
have made more money with the plant,” anasema Bw.Mc Bean ambaye kampuni
yake imetakiwa kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam.
Kampuni
inayochimba gesi inaamini kuwa kujenga kiwanda cha kutengeneza mbolea
Mtwara kitakuwa na faida kubwa kwa kampuni yake. Isitoshe kiwanda hicho
kitaongeza ajira kwa vijana wa Mtwara. Kitaanza kuijenga Mtwara kama
kituo cha sekta ya gesi na viwanda vyake. Upatikanaji wa mbolea ya bei
inayotengenezwa hapa nchini utasaidia kuendeleza kilimo na kuifanya
kaulimbiu ya Kilimo Kwanza kutekelezwa kwa vitendo. Hatua ya serikali
kuilazimisha Wentworth Resources kuipeleka gas ya Mnazi Bay kwenye bomba
la gesi ili isafirishwe Dar es Salaam kunaathiri maendeleo ya Mtwara na
Tanzania kwa ujumla.
Ujenzi wa bomba
la Mtwara umeanza bila kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa kutakuwepo na
gesi ya kutosha kuisafirisha hadi Dar es Salaam. Bomba hili litakuwa na
uwezo wa kusafirisha futi za ujazo bilioni 200. Uwezo wa gesi ya Mnazi
Bay kwa hivi sasa ni futi za ujazo bilioni 80. Hakuna mpango unaoeleweka
wa kupata futi za ujazo bilioni 120 ili bomba la gesi liweze kutumiwa
kikamilifu. Mpaka hivi sasa gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 33
imegunduliwa hasa katika bahari yenye kina kirefu. Kuna uwezekano wa
kugundua mafuta. Uchimbaji wa gesi hii bado haujaanza. Inaweza
kuchukukua miaka 7 – 10 kabla ya shughuli ya uchimbaji wa gesi
kukamilika na kuanza kuitumia ndani ya nchi au kuiuza nje ya nchi.
Upatikanaji
wa mkopo wa masharti nafuu kutoka China wakujenga bomba la gesi ndiyo
umeishawishi serikali kutekeleza mradi huu haraka bila maandalizi ya
uzalishaji wa gesi ya kutosha.Ni vyema serikali ingetekeleza mradi wa
kufua umeme Mtwara na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa na kuruhusu
kiwanda cha mbolea kuanzishwa Mtwara.
CUF
Chama cha wananchi tunaitaka serikali kuzingatia kuwa, kwa kuwa mradi
wa kujenga bomba la gesi uko katika hatua za mwanzo ni vyema serikali
ikatathmini upya mantiki na faida za mradi huo. Mradi unaweza
kutekelezwa kwa awamu. Awamu ya kwanza iwe kujenga bomba la gesi had
Somanga Kilwa ili kuongeza uwezo wa kusafirisha gesi ya Songosongo kuja
Dar es Salaam.
Kama nchi bado tuna
udhaifu mkubwa wa kuandaa mipango na kusimamia utekelezaji wake.
Serikali itufahamishe utekelezaji wa National Power Development Master
Plan umefikia wapi? Vipi Mtwara development Corridor bado ipo?
Katika
kusimamia sekta ya gesi tujifunze toka nchi ya Norway, Ili kuendesha
shughuli za mafuta kwa ufanisi, Norway iliamua mapema kuwa makao makuu
ya shughuli za mafuta utakuwa Stavange na siyo mji mkuu wa Oslo. Uamuzi
huu umeufanya mji wa Stavange kukua na kuwa kituo cha biashara ya
mafuta. Mtwara uwe mji mkuu wa shughuli zote za mafuta na gesi kwa
sababu ina bandari asilia yenye kina kirefu na gesi imeanza kugunduliwa
kanda ya kusini ya bahari ya Tanzania.
CUF
tunasisitiza kwamba, malalamiko ya wananchi wa Mtwara ni ya msingi na
wala hayaathiri umoja wa kitaifa. Maoni yao ya kuwa na viwanda
vinavyotumia gesi Mtwara na maeneo mengine ya kusini yana mantiki ya
kiuchumi. Serikali iwasikilize isiwabeze. Msimamamo wa CUF wa Dira ya
Mabadiliko ni kuhakikisha kuwa maliasili na raslimali za nchi zinatumiwa
vizuri kuleta neema kwa wananchi wote. Wananchi wa Mtwara wana haki ya
kunufaika na neema ya gesi ya Mnazi Bay.
Mwisho Watanzania wote heri ya mwaka mpya – Happy New Year.
Imetolewa na
Mwenyekiti wa CUF-Chama cha wanachi, Taifa
Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba