Facebook Comments Box

Sunday, November 24, 2013

HATIMAE ZITTO KABWE AFUNGUKA


TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA
1. Utangulizi
Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu.
Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.
iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.
3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.
24 Novemba, 2013


KIBONZO: KINGEREZA HIKI MNASEMAJE



NILIKUWA NAOMBA MUNGU KILA SIKU AFUKUZWE CHADEMA - MAMA ZITTO

Siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa wa chama hicho, Zitto Kabwe, mama yake mzazi, Shida Salum ametoa ya moyoni akieleza kuwa kilichomkuta mwanaye kimefunika mabaya mengi yaliyopangwa afanyiwe.
“Kwa upande wangu naona kama ni ushindi kwa Zitto kutokana na jinsi ninavyojua hali ilivyo, mambo yalikuwa ni mengi mno na nikwambie tu, Zitto kuvuliwa uongozi kumefunika hayo yaliyokuwa yamekusudiwa kufanywa dhidi yake. Nilikuwa naomba Mungu  kila siku ili afukuzwe Chadema,” alisema mama huyo wakati akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Tabata, Dar es Salaam.
Shida Salum alisema kuwa Mungu amemnusuru mwanaye na kusisitiza, “Watu walikaa na kutengeneza ripoti ya siri kuhusu Zitto na kuiweka kwenye mtandao kisha kuituma kwa wanachama wa Chadema wanaowafahamu. Mpaka wanafikia hatua hiyo maana yake ni kwamba wamejaribu njia zote za kummaliza, lakini wameshindwa.”
Alisema kutokana na hali ilivyo hivi sasa amemnyang’anya mwanaye kwa muda simu zake zote za mkononi, kompyuta mpakato (Laptop) pamoja na iPad ili asiwasiliane na watu, kwa maelezo kuwa wapo wenye nia mbaya wanaomsaka kumpa pole za kinafiki. “Kwa sasa nataka mwanangu atulize akili.”
Shida Salum, mbali na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, pia ni  mwasisi wa  Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) na Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (Chawata).
Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo juzi walivuliwa uongozi kutokana na uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kilichokutana kwa siku mbili, kuanzia Novemba 20 mwaka huu katika Ukumbi wa Blue Pearl jijini Dar es Salaam, wakituhumiwa  kukisaliti chama.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto, Dk Mkumbo pamoja na  aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba, pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama.
Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Katika ufafanuzi wake wa jana, Shida aliwataka wanachama wa Chadema kuwa watulivu kwa maelezo kuwa Zitto hajafukuzwa uanachama, “Siku nyingi walikuwa wanamwinda na hata hilo jambo ambalo Chadema wanasema amefanya, hawana uhakika nalo.”
Juzi wakati akisoma uamuzi wa Kamati Kuu,  mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema wamebaini kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ambao umeandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.
Alisema kikundi hicho vinara wake wapo wanne,  Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu mwingine wa nne ambaye alieleza kuwa hajatambulika na anatumia jina la M2.
Mama Zitto ambaye wakati akizungumza na gazeti hili alikuwa amelala kutokana na kusumbuliwa na maradhi alisema, “Kutolewa katika uongozi ni jambo la kawaida.  Zitto hajafukuzwa chama ila anaweza akafukuzwa maana kapewa siku 14 tu za kujieleza.”
Alisema kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa, kwamba chama hicho walimwondoa Aman Kabourou (aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini-Chadema)  itakuwa Zitto, inaonyesha jinsi watu walivyo na chuki na mwanaye.
“Hayo ni maneno ya chuki, maana hata Zitto naye ana watu wake ambao wanaweza kutengeneza aina fulani ya chuki kwa viongozi wa chama na wanaweza kupata wakati mgumu kufanya safari au mikutano yao mikoani,” alisema.
Alisema tangu siku nyingi ndani ya Chadema kulikuwa na mpango wa kumng’oa Zitto, akifafanua kuwa hata katika kikao cha Kamati Kuu iliibuliwa hoja ya ruzuku za vyama, huku wajumbe wakimshutumu Zitto kwamba kwa nafasi yake na Naibu Katibu Mkuu alitakiwa kuitetea Chadema kuhusu ruzuku.
Katika vikao vya Kamati ya PAC, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku akitaka ruzuku kwenye vyama hivyo isimamishwe.
“Zitto alipoingia katika kikao cha Kamati Kuu alishikilia msimamo wake kwamba kama Chadema inachukia ufisadi, nacho lazima kihakikishe kinakaguliwa,” alisema na kuongeza;
“Wao wanaona ili waweze kusalimika katika suala hili la ruzuku ni lazima wamfukuze Zitto. Chadema hawako sawa, hesabu zao haziko sawa.”
Alisema kuwa tatizo lililopo ni kuwapo kwa mkakati wa watu fulani kuiyumbisha Chadema , hivyo kila juhudi zinafanywa ili kukitingisha chama hicho kipoteze mwelekeo.
“Siwezi kusema wamemwonea au hawajamwonea, wao wametumia waraka wa Mwigamba ambao Zitto amekiri katika Kamati Kuu kwamba hajawahi kuusikia wala kuuona, tofauti na Dk Kitila ambaye amesema amewahi kuuona,” alisema na kuongeza;
“Zitto anahusishwa na kitu ambacho Chadema hawana uhakika nacho, ukiusoma ule waraka katika aya ya mwisho umeandikwa hivi, ‘Huyu mtu tunayefikiria awe mwenyekiti hajaoa,
tumshauri aoe akikataa tutafute mtu mwingine’, maana yake ni kwamba waraka huo ulikuwa haujamfikia Zitto, kama ungekuwa umemfikia Zitto watu hao wasingemwomba Zitto agombee uenyekiti.” Alipoulizwa nafasi yake ndani ya Chadema kutokana na yaliyomkuta mwanaye alisema, “Mimi hawawezi kunitengenezea jambo. Hivi Zitto anaweza kuwa mbaya mimi nikawa mzuri.”
Mama huyo alieleza kuwa tangu alipovamiwa na majambazi nyumbani kwake, Aprili 19 mwaka huu hajawahi kuhudhuria kikao chochote cha Chadema. “Wale wanaodhani Zitto kaonewa wanatakiwa kuwa wavumilivu na wapole, wasubiri kwani kila kitu kinawezekana.”
Ushauri kwa mwanaye
Alisema kuwa mwanaye ana uamuzi wake na kwamba hata kama Chadema itamfukuza uanachama, haitaweza kumnyang’anya vyeti vyake vya elimu aliyoipata.
“Zitto anaweza kufanya kazi mahali popote duniani, lakini pia ni mwalimu anaweza kuamua kufundisha. Ubunge ni mgawanyo wa madaraka. Watu wote hatuwezi kuwa wabunge,” alisisitiza.
Alisema wakati Kikao cha Kamati Kuu kikifanyika Zitto alikuwa nje ya nchi na kwamba yeye alimshauri kuhakikisha kuwa anahudhuria kikao hicho.
“Alipotua tu na ndege aliniambia kuwa kuna foleni na alitaka kukodi pikipiki ili awahi kikao, aliniambia lazima aende ili kujua hatima yake.
Aliacha gari lake na kwenda na hata mimi nilimsisitizia kwamba ni lazima aende katika kikao,” alisema. Alisema kuwa Zitto alipofika katika kikao hicho aliweza kuzima hoja zote zilizomhusu ikiwamo ya ruzuku za vyama, kwamba baadhi ya wajumbe walipoona amebadili mwelekeo wa kikao, mjumbe mmoja (akamtaja kwa jina) aliibua waraka uliomng’oa Zitto katika wadhifa wake.
“Unajua Kamati Kuu ilijadili zaidi kuhusu ruzuku. Hata ule waraka uliongezwa maneno baada ya baadhi ya wanachama kumpora Mwigamba laptop yake alipokuwa mkoani Arusha katika kikao cha Chadema,” alisema.
Huku akiwataja wanachama wa Chadema walioongeza maneno katika waraka huo (wakiwamo wabunge wawili) na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema, mama Zitto alisema kilichomkuta mwanaye ni ushindi mkubwa, kwamba alipangiwa kufanyiwa makubwa zaidi ya yaliyomkuta.
“Hakuna amani maana ukisikia kengele inagongwa hapa nyumbani unasema hao ndiyo wamekuja kumuua Zitto nini, hivi sasa mpaka walinzi wanaolinda hapa wakisikia unakuja nyumbani kwa Zitto lazima wakuandike jina na kukufuatilia,” alisema mama huyo.
Dk Kitila alonga
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Mkumbo alisema kutokana na ushauri wa watu mbalimbali, yeye na Zitto  wamepanga kukutana na waandishi wa habari na kutoa tamko.
“Tumepanga mimi na Zitto tutatoa ufafanuzi kuhusu jambo hili, nadhani ni kesho (leo), tutawajulisha lakini,” alisema.
inShare
Related Stories
    Mtikisiko mkubwa Chadema, Zitto, Dk Kitila wavuliwa uongozi
Baada ya chama hicho kutangaza kuwaengua katika uongozi Zitto na Dk Kitila, saa mbili baadaye  Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chadema, Said Arfi aliandika barua  ya kujiuzulu.

CHANZO: MWANANCHI



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU