Facebook Comments Box

Monday, January 21, 2013

MWANACHUO WA ST JOHN UNIVERSITY DODOMA AUWAWA KINYAMA

 
 
JESHI la polisi mkoani Dodoma limeshutumiwa kwa kushindwa kuimarisha ulinzi katika baadhi ya maeneo mkoani humo hatua inayodaiwa kuchangia kuaawa kinyama kwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Saint John Lidya Leo Mzima na watu wasiojulikana.
Marehemu Lidya mwenye umri wa miaka 57 anadaiwa kuuawa siku ya jumapili hii majira ya saa nne za usiku pembezoni mwa maeneo ya chuo hicho chenye wanafunzi 5500
akiwa anarejea nyumbani baada ya masomo ya jioni.
Ni simanzi,vilio,huzuni na majonzi katika vyunga vya chuo hiki kufuatia tukio hili la kusikitisha ambalo linadaiwa kuyaweka katika mashaka na wasiwasi mkubwa maisha ya wanafunzi hawa.
Licha ya kulitupia lawama jeshi la polisi baadhi ya mashuhuda wanadai kuwa baada ya kufikwa na mkasa huo uliositisha safari ya maisha yake mwili wa marehemu Lidya uliharibiwa vibaya na mnyama asiyejulikana kwa kunyofolewa macho,masikio,pua,mguu na viuno vingine.
Prof.Gabriel Mwaluko ni makamu mkuu wa Chuo na Karimu Meshack ni afisa habari ambao kwa pamoja wanaelezea kilichorjiri.
Kutokana na shutuma za uzembe dhidi ya jeshi hilo Kamanda wa mkoa ACP David Misime anawataka wakazi wa mkoa huo kuimarisha ulinzi shirikishi kwa lengo la kuwabaini wahalifu.
Wakati huo huo Kamanda Misime anasema msako mkali umeanza wa kuwatia nguvuni waliohusika na ukatili huo ili waweze kufikishwa kwenye mikono ya sheria kwa ajili ya hukumu.



ATCL KUANZA SAFARI ZAKE ZA DAR KIGOMA KESHO



Wahandisi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakikamilisha kufunga kioo kipya ambacho kimenunuliwa kutoka nchini Marekani cha ndege yao aina ya Dash-8 Q300 yenye namba za usajili SH-MWF ambayo ilipata ufa (Wind shield crack) tarehe 11 Januari, 2013, muda mfupi baada ya ndege hiyo kuruka kutoka Kigoma kurudi Dar Es Salaam katika safari zake za kawaida. 
 
Matengenezo hayo yanafanyika katika uwanja wa ndege wa Kigoma yakisimamiwa na Mhandisi Righton Mwakipesile na Mhandisi Merkior Karwani.
 
Uongozi wa ATCL umedhibitisha kuwa safari za Dar-Kigoma-Dar zitaendelea kama ratiba yao inavyoonyesha punde kuanzia kesho tarehe 22/1/2013.


ANGALIA PICHA ZA MTOTO ALIEZIKWA MZIMA NA KUFUKULIWA NA KUKUTWA MZIMA

Mama mmoja nchini Nigeria ameamua kumzika mtoto wake akiwa hai. Baada ya taarifa kupatikana polisi walienda na kuamua kufukua. Baada ya kufukua walimkuta mtoto huyo na kumkimbiza hospitali aliposafishwa mtoto huyo alikutwa hai.

HALMASHAURI YA KIGOMA KUSOMESHA WATOTO WOTE WANAOSHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imeanza mchakato wa kuwakusanya watoto wadogo walemavu wanaoomba mitaani na kuwapeleka katika kituo cha walemavu Kabanga, wilayani Kasulu kwa ajili ya kuanza masomo ya shule ya msingi.
Ofisa Elimu Shule ya Msingi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Shaaban Bane aliyasema hayo wakati wa kuwasafirisha watoto wanane waliotambuliwa kwenda Kasulu kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mchakato huo.
Bane alisema baada ya kufika kwenye manispaa hiyo, aligundua tatizo la watoto wengi wadogo wenye ulemavu kutumika kama vitega uchumi na familia zao kwa kuomba fedha mitaani badala ya kwenda shuleni.
Kimsingi alisema kuwa hiyo inaonesha kuwa uduni wa kipato (umasikini) wa familia hizo ambazo haziwezi kuwapeleka watoto hao shuleni na kwamba wao kama Serikali wameona wachukue jukumu la kuhakikisha watoto hao wanapata haki yao ya kupata elimu.
Kwa sasa, Ofisa Elimu huyo alisema kuwa jumla ya watoto wanane wamepatikana kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa ya Kigoma Ujiji na mchakato wa kuwafanya wajiunge na shule maalumu ya Kabanga wilayani Kasulu umekamilika na jana walisafirishwa kuelekea huko.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Alfred Luanda alisema wazazi wanalo jukumu la kuhakikisha watoto wao wanapata elimu badala ya kuchukulia ulemavu wao kama kigezo cha kuwafanya wao ni masikini na kuanza kuzunguka mitaani kuomba fedha kwa wasamaria wema.


KIBONZO CHA LEO KINAHUSU MAPROFESA



UKUTA WA STENDI YA UBUNGO WAANGUKA NA KUHARIBU VIBAYA MAGARI YA WATU LEO HII

 Ukuta wa eneo la ndani ya kituo cha Mabasi ya Ubungo Bus Terminal
 umeangukia magari zaid ya 19 (baadhi kama uonavyo pichani) zikiwemo
bajaji  tatu,yaliyokuwa yamepaki
eneo  ambalo hutumika kupaki  wakiwa wanasindikiza abiria na ndugu zao,aidha chanzo cha ajali hiyo kimeeleza
kuwa ni Mkandarasi wa eneo hilo aliyekuwa  akibomoa ukuta huo,na pia imeripotiwa
kuwa kuna baadhi ya majeruhi ambao wamekimbizwa hospitali kwa matibabu.


 Baadhi ya Maofisa kutoka Jeshi la Polisi wakiangalia baadhi ya magari yaliyoathiriwa vibaya mara baada ya kuangukiwa na ukuta mapema leo asubuhi kwenye eneo la kupaki magari,ndani ya kituo kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani.Ukuta huo ulikuwa ukibomolewa na Mkandarasi ikiwa ni hatua za awali wa kituo hicho kuvunjwa kwa ajili ya kupisha mradi wa ujenzi wa mabasi yaendayo kasi.


Si Magari tu,hata bajaji pia zimeathiriwa vibaya kama uonavyo pichani

Pichani juu ni baadhi ya magari mbalimbali yalioyoathiriwa vibaya kufuatia kungukiwa na ukuta.


Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Afande Charles Kenyela akitoa maelekezo mafupi kwa baadhi ya maofisa wa Polisi waliokuwa wamefika kwenye eneo la tukio mapema leo asubuhi

ZITTO AITIKISA SERIKALI KUHUSU GESI

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA)

Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara. Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.
Ikumbukwe kwamba katiba ya nchi, ibara ya 9 katika mabano J inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d). Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.
Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu. Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.
Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika 19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na kuwasikiliza wananchi wanao dai haki yao ya kikatiba.
Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa mtwara ni kitendo kinacho weza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja wa taifa.”ibara ya 28, 1.
Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. Inawezekana Serikali na hasa watendaji wa Serikali waliojadili mkopo huu wameshapata chao na hivyo kuogopa kusikiliza madai halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.
Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate majawabu.
Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili. Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo Wizarani. Kwa nini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine 2, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi.
Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba imepandishwa maradufu. Wastan wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni sawa na kilomita 1.6).
Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na bwawa la Mtera linalo tegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5 katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.
Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayo pendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania hako yao. Hii ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.

Zitto Kabwe



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU