Facebook Comments Box

Sunday, February 24, 2013

AJALI MBAYA IMETOKEA MKOANI IRINGA




Ajali hii iliyohusisha magari mawili,Toyota Rav 4 na Toyota Cresta imetokea usiku wa kuamkia leo katika eneo la jirani na Maktaba ya mkoa, mjini Iringa,ambapo gari hiyo aina ya RAV 4  iliruka ukingo wa barabara  uliojengwa kwa sementi na kutua juu ya Gari hiyo aina ya Toyota Cresta (Taxi) na kushindwa kuendelea na safari.inasemekana kuwa isingesimama gari hiyo aina ya Toyota Cresta,basi dereva wa gari hiyo aina ya Rav 4 labda angekuwa katika wakati mgumu zaidi au kupoteza maisha kabisa. hakuna aliepoteza maisha kwenye ajali hiyo. 
(Picha na Meshack Maganga-Iringa)
HABARI ZAIDI INGIA HAPA 



MNYIKA: MH. SHUKURU KAWAMBWA AMEBAKIZA SIKU KUMI TU


KAULI ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kwamba hawezi kujiuzulu, imeamsha hasira ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kimesisitiza kwamba maandamano ya kumng’oa yako pale pale na sasa amebakiza siku kumi tu.

Kauli hiyo ilitolewa  na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika wakati alipotakiwa kueleza msimamo wa chama chao, hasa baada ya kauli ya Waziri Kawambwa  kwamba hawezi kujiuzulu.

Akizungumza na mdau wa Kitongoni Blog, Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, alisema kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe kwamba anampa siku 14 Waziri Kawambwa ajiuzulu, vinginevyo atang’olewa kwa maandamano bado ipo pale pale.

Alisema majibu ya Waziri Kawambwa yameonesha dharau kwa Watanzania, hasa walalahoi ambao ndio watoto wao wengi wamepata ziro katika mitihani yao ya kidato cha nne.

“CHADEMA tunaendelea kusisitiza kwamba Waziri Kawambwa ang’oke, awajibike, ameshindwa kazi na hili tunamaanisha,” alisisitiza Mnyika.

Alisema CHADEMA inaangalia namna ya kuitisha maandamano hayo kwa kuwashirikisha vijana waliofeli kwani wanaamini wamehujumiwa.

Mnyika aliwataka Watanzania na wengine wenye uchungu na udhaifu wa elimu ya Tanzania, hasa wazazi wajitokeze kwani fedha walizowekeza kwa watoto wao kwa ajili ya elimu, zimeteketea bure.


WAZIRI MKUU AUNDA TUME KUCHUNGUZA MATOKEO YA MTIHANI KIDATO CHA NNE

wpid-Prime-Minister-Mizengo-PindaWAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameunda Tume maalum itakayofanya uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambayo yalitangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa Februari 18, mwaka huu.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa Jumatatu wiki hii, asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne Oktoba, 2012 walifeli.
 
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Peniel Lyimo amesema Tume hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote wiki ijayo inajumuisha wadau kutoka Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tanzania Association of Managers and Owners of Non-Government Schools/Colleges (TAMONGSCO), Taasisi za Dini zinazotoa huduma ya elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) zinazoshughulikia masuala ya elimu.



Picture

MWAKYEMBE AFANIKIWA KUPANDISHA MAPATO BANDARI YA DAR ES SALAAM.




Meli zinapakua makontena katika bandari ya Dar es Salaam tarehe 29 Disemba, 2012. [Deodatus Balile/Sabahi]

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeongeza ukusanyaji wa mapato katika bandari ya Dar es Salaam kutoka shilingi bilioni 28 mwezi Novemba hadi shilingi bilioni 50 (dola milioni 18 hadi dola milioni 31) katika mwezi wa Disemba, kufuatia kusimamishwa kwa muda maofisa 16 wa bandari wanaotuhumiwa kwa mwenendo usiofaa.
 
Maofisa hao wa bandari, wakiwemo wakurugenzi wa ngazi za juu, walisimamishwa kwa muda mwezi Disemba baada ya Wizara ya Usafirishaji kuanzisha uchunguzi wa ndani kwa lengo la kutoa mwitikio wa malalamiko ya wateja kuhusu kucheleweshwa katika bandari hiyo, kwa mujibu wa Waziri wa Usafirishaji Harrison Mwakyembe.
Maofisa wa bandari wengine wasiopungua sita. Uchunguzi huo, ambao bado unaendelea, uligundua kuwa waajiriwa wa bandari walibadilisha mwelekeo wa biashara kutoka katika bandari kwenda kwa kampuni ndogo za usafirishaji na utoaji mizigo wanazomiliki, ukiukaji wa moja kwa moja wa mkataba wao wa ajira.
"Wateja wanakimbia bandari yetu kwa sababu ya ucheleshaji wa kukusudia unaofanywa na waajiriwa wasio na maadili ambao wanaongeza gharama za kufanya biashara," Mwakyembe aliiambia Sabahi. "Hii ni kinyume na mikataba yao ya ajira na wana mgongano wa maslahi na mwajiri wao ambae ni Serikali."
 
Miongoni mwa viongozi wa bandari wa ngazi ya juu waliosimamishwa ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA Ephraim Mgawe, Mkurugenzi wa Mipango Florence Nkya, Mkurugenzi wa Uhandisi Bakari Kilo, Mkurugenzi wa Mifumo ya Utawala Maimuna Mrisho, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Ayub Kamili, Naibu Mkurugenzi Mkuu Hamad Koshyuma, Naibu Mkurugenzi Mkuu Julius Fuko, na Meneja wa Bandari Cassian Ng'amilo.
Mashtaka rasmi bado hayajatolewa dhidi ya viongozi waliosimamishwa na bado hawajajibu tuhuma zozote hadharani. Mwakyembe alisema Bodi ya Wakurugenzi ya TPA itakutana hivi karibuni kutoa uamuzi wa mwisho kuhusiana na ajira yao.


IMAM APIGWA MAPANGA NA KUFA ZANZIBAR



Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Said Mwema (kulia) Waziri wa Mambo ya ndani Emmanuel Nchimbi na Kamnda wa Pilisi Zanzibar Ally Mussa kwenye moja ya mikutano na waandishi wa habari.          

SIKU chache baada ya kutokea kifo cha Padri Evarist Gabriel Mushi kupigwa risasi na watu wasiojulikana kichwani eneo la Beit el Raas, Jana Imamu wa Msikiti wa Mwakaje ameuawa baada ya kupigwa mapanga hadi kufa. Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo jana mchana majira ya saa 8 na kumtaja aliyefariki kuwa ni Sheikh Ali Khamis ambaye ameuawa na watu wasiojulikana.
  Kamanda Ahmada alisema Sheikh Khamis mbali ya kuwa ni Imamu wa Msikiti lakini pia ni mkulima na ameuliwa wakati akiwa katika mazingira ya kazi zake ndani ya shamba lake huko Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja. Akielezea mazingira ya tukio hilo Kamanda Ahmada alisema tukio hilo limetokea baada ya Sheikh Khamis kwenda shambani kwake katika shmba la minazi Kidoti ambapo wakati akiwa shambani hapo ndipo walipotokea watu kadhaa na kumpiga mapanga sehemu za shingoni mwake na kusababisha kifo chake muda mfupi baada ya kipigo hicho.
  Alisema baada ya tukio hilo, watu walimchukua na kumkimbiza hospitali lakini kutokana na kupoteza damu nyingi alifariki dunia wakati akiwa njiani na hivyo harakati za mazishi zinafanyika baada ya kuchukuliwa vipimo na wataalamu wa afya. Kamanda Ahmada ametoa wito kwa wananchi kutopuuzia taarifa za watu ambao wanawashuku na wenye kuleta maafa yakiwemo mauaji hapa nchini, kwani kuwaficha wahalifu ni kuendeleza utamaduni usiofaa katika jamii ambayo imeanza kuharibika kutokana na mauaji hayo yanayoendelea kila kukicha. Hili ni tukio la nne kwa viongozi wa dini kuhujumiwa ambapo tukio la kwanza Sheikh Fadhil Suleiman Soraga kumwagiwa tindi kali na watu wasiojulikana na kujeruhiwa vibaya wakati akifanya mazoezi nyakati za asubuhi karibu na nyumbani kwake Magomeni, tukio la pili ni lile la Padri Ambrose Mkenda aliyepigwa mapanga shingoni na kurejuhiwa vibaya na watu wasiojulikana wakati akitaka kuingia nyumbani kwake huko Tomondo Mjini Unguja. matukio hayo mawili yalitokea mwaka jana. Katika mwaka huu nako kumetokea matukio mawili kwa kuuawa kwa Pardi Evarist Mushi huko Beit El Raas wakati akitaka kuingia Kanisani na pia kuuawa kwa Sheikh Ali Khamis huko Kidoti shambani kwake Mkoa wa Kaskanizini Unguja.  Inna lillahi wainna ilayhi rajiiun.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU