MAELEZO NA HOJA BINAFSI YA KUPENDEKEZA BUNGE LIJADILI NA KUPITISHA
MAAZIMIO YA HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA
USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM KWA MUJIBU WA
KANUNI YA 54 FASILI YA (1) YA KANUNI ZA KUDUMU ZA BUNGE TOLEO LA MWAKA
2007
Mheshimiwa Spika; Awali ya yote niungane na wote wenye
mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza
wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania wa kuwawakilisha wananchi, kuisimamia serikali,
kuidhinisha mipango na kutunga sheria.
Mheshimiwa Spika; Aidha,
kwa namna ya pekee ni kushukuru wewe binafsi na uongozi mzima wa Bunge
kwa kunipa fursa hii adimu na adhimu ya kuwasilisha hoja binafsi kwa
mujibu wa kanuni ya 54 fasili ya (1) ya kupendekeza bunge lijadili na
kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa
maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.
Mheshimiwa Spika; Maji
ni uhai, hivyo matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji
wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na nchini kwa ujumla kama
hatua za haraka zisipochukuliwa yatageuka kuwa janga la taifa. Katika
kila watanzania katika Jiji la Dar es Salaam na nchini; kwa wastani
mmoja hapati huduma ya maji safi na salama na hali ni mbaya zaidi kuhusu
ushughulikiaji wa maji taka.
Wakati baadhi ya nchi duniani
zikielezwa kwenye kitabu cha hivi karibuni cha Mnukuzi Maalum wa Umoja
wa Mataifa (UN Special Rapporteur) kuwa katika mwelekeo unaostahili
kuhusu kuhakikisha haki ya maji na usafi wa mazingira (On the right
track; Good practices in realizing the rights to water and sanitation:
2012), hali ni kinyume kwa taifa letu.
Ripoti ya Taasisi ya
Kimataifa inayoshughulikia masuala ya maji (WaterAid: 2011) imeiweka
Tanzania katika kundi la nchi ambazo haziko katika mwelekeo unaostahili
wa kuboresha upatikanaji wa maji safi, ushughulikiaji wa maji taka na
usafi wa mazingira (Policy Report: Off Track, Off Target; why
investments in water, sanitation and hygiene is not reaching those who
need the most).
Mheshimiwa Spika;Hoja hii inalengo la
kuibua mjadala wa hatua za haraka. Kimsingi hatua hizi za haraka
hazitanufaisha Mkoa mmoja pekee kwa kuzingatia kuwa Mpango Maalum wa
kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam ni kwa ajili pia ya
maeneo mengine ya miradi iliyo sehemu ya mpango huo ya Morogoro mpaka
Pwani. Aidha, kujadiliwa na kupitishwa kwa mapendekezo ya hoja hii
kutaongeza pia msukumo wa miradi katika maeneo mengine ya mijini na
vijijini katika mikoa mbalimbali nchini.
Shukrani zangu za dhati
ziwafikie wabunge wenzangu wa vyama vya upinzani na wa chama tawala kwa
maoni na mapendekezo yenu yaliyoniwezesha kuirekebisha hoja hii pamoja
na ushauri wa Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashillilah na maafisa na
watendaji katika ofisi ya bunge, kambi rasmi ya upinzani na ofisi ya
mbunge wa Jimbo la Ubungo mlioboresha hoja hii kwa manufaa ya Jiji la
Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika;Nitumie
pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi
mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi
mnaoendelea kuniunga mkono kwa hali na mali katika kutimiza majukumu
yangu ya kibunge na nafasi nyingine ninazozitumikia.
Nawashukuru
sala zenu wakati wa kesi ya msingi na rufaa ya kupingwa kwa matokeo ya
ushindi wetu Jimbo la Uchaguzi la Ubungo; kwa pamoja tumeshinda,
tuendelee na kazi.
Aidha, pamoja na mjadala huu wa bungeni
natarajia kupokea maoni na mapendekezo yenu kuhusu hoja hii kwa njia
mbalimbali za mawasiliano ikiwemo kupitia mtandao wa
http://mnyika.blogspot.com kwa hatua zaidi. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.
MAELEZO YA HOJA:
Mheshimiwa Spika; Maji ni mojawapo ya mahitaji ya msingi
ya binadamu, maji ni uhai. Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama
ni sehemu ya muhimu ya maendeleo ya nchi na maisha ya wananchi. Maji ni
lazima kwa matumizi ya majumbani, maji ni muhimu ni moja ya malighafi
muhimu katika kazi za uzalishaji iwe ni za viwanda, kilimo, mifugo na
shughuli zingine za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika; Tanzania
ni nchi ambayo imejaliwa vyanzo vingi vya maji, vinavyohusisha mito,
mvua, maziwa na bahari; kuwepo kwa vyanzo hivi vya maji ni wazi kuwa
nchi yetu inaweza kuepukana na shida ya maji inayoikumba jamii ya
Tanzania iwapo tutaondoa udhaifu uliopo. Aidha, udhaifu huo unahusisha
pia kuziweka vyanzo vyenyewe pia mashakani kwa matendo ya binadamu yenye
kuathiri endelevu wa matumizi hali itayozua migogoro katika siku za
usoni iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mheshimiwa Spika;Upatikanaji
wa maji safi na salama kwa urahisi wa bei unachangia katika kupunguza
gharama za maisha; upatikanaji wa maji safi na salama karibu na makazi
husaidia jamii, hususan wanawake, kutumia nguvu na muda katika
uzalishaji na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini. Upatikanaji wa
maji safi na salama ni nyenzo ya kulinda utu na afya; kinyume chake
kuenea kwa magonjwa na maisha duni.
Ifahamike kuwa kadiri ya
Tathmini ya Hali ya watu na Afya ya mwaka 2010 (Demographic and Health
Survey 2010); ni asilimia 4.8 tu ya kaya zilizopo vijijini ndiyo
zinazopata maji katika eneo lao la kaya (water on premises) wakati ni
asilimia 19.4 tu ya kaya kwa mijini ndizo zenye maji katika kaya zao.
Hivyo kaya nyingi za Tanzania zinawekwa katika mazingira hatarishi kwa
magonjwa ya mlipuko na mengine ambayo si ya mlipuko kutokana na uhaba wa
maji, hali ikiwa tete zaidi katika maeneo yasiyopimwa yenye msongamano
mkubwa wa watu katika Jiji la Dar es Salaam (slums).
Mheshimiwa Spika;Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, toleo la mwaka 2005
haijataja haki ya kupata maji safi na salama; huu ni kati ya upungufu
ambao wananchi wa mijini na vijijini wanapaswa kuutolea maoni katika
mchakato wa katiba mpya kwa kurejea mfano wa Katiba ya Afrika Kusini,
Ghana na katiba mpya ya Kenya.
Katika hatua ya sasa haki hii
inapaswa kulindwa kupitia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi,
Kijamii na Kiutamaduni (“The International Covenant on Economic, Social
and Cultural Rights”, ICESCR) wa 1966. Mkataba huu unataja haki za
kijamii na hivi karibuni Umoja wa Mataifa (UN) umeutafsiri kuwa ni
pamoja na haki ya kupata maji safi na salama ambayo inapaswa kutiliwa
mkazo katika nchi yetu.
Suala la upatikanaji wa maji safi na
kuweza kushughulia maji taka ni sehemu ya makubaliano ya kimataifa
ambayo nchi yetu imeridhia kuingia mathalani Malengo ya Milenia (MDGs);
lengo namba saba (7) shabaha 10; la kupunguza nusu ya watu waoishi bila
maji na safi ya kunywa na usafi wa msingi. Hatua za haraka za kuboresha
upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka ni muhimu kama
sehemu ya haki za binadamu lakini lina tija pia katika uzalishaji na
uchumi wa nchi kwa kuwa tafiti zinaonyesha kwamba kudumu kwa matatizo
hayo kunazigharimu nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo wastani wa asilimia
sita (6) ya pato la taifa (Gross Domestic Product).
Utafiti
uliofanywa kwa Stockholm Environment Institute kwa kushirikiana na Benki
ya Maendeleo Afrika mwaka 2006 kuhusu uhusiano kati ya maji na umaskini
Afrika kwa kutumia mfano wa nchi yetu (Water and Poverty Linkages in
Africa: Tanzania Case Study) umebainisha namna ilivyo vigumu kupima
Tanzania inavyosonga mbele katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya
milenia yanayohusu maji. Aidha, utafiti huo umeeleza namna ambavyo bila
kushughulikia kwa haraka matatizo ya maji jitihada za kupambana na
umaskini zitakwama.
Mheshimiwa Spika; Jiji la Dar es
Salaam ni letu sote, ni mahali ambapo wabunge wote tunaishi kwa nyakati
mbalimbali hususan wakati wa vikao vya kamati za kudumu za Bunge hivyo
adha ya maji katika Jiji hili kila mmoja anaifahamu na anawajibu wa
kushiriki katika kuipatia ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu
na Makazi mwaka 2002 Mkoa wa Dar es salaam ulikuwa na jumla ya wakazi
2,497,940 huku ukikadiriwa kuwa na kasi ya ongezeko la watu ya asilimia 6
kwa mwaka; ikiwa ni juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.5, lakini
kasi ya upatikanaji wa maji na ushughulikiaji wa maji taka ikiwa ndogo.
Bunge ikiwa ni chombo cha juu cha kuisimamia Serikali linapaswa
kuitafakari hali hii kwa upekee wake kwa kuwa itakuwa na athari kwa
taifa kwa sasa na baadaye ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Hadi
kufikia mwaka 2011 Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na watu
zaidi milioni nne na laki tano likiwa na takribani nusu ya waajiriwa
wote wa viwandani nchini. Hivyo kwa kurejea takwimu za ujumla za sensa
zilizotolewa mwezi Desemba 2012 kwamba Tanzania kwa sasa ina watu zaidi
ya milioni 44.9; hoja hii inalenga kupendekeza kwa bunge kujadili kuhusu
mustakabali wa zaidi ya asilimia 10 ya Watanzania, lakini kwa kurejea
utangulizi wangu maazimio ninayopendekeza yapitishwe yatakuwa na maslahi
sio kwa wakazi wa Dar es salaam bali kwa taifa kwa ujumla mijini na
vijijini.
Mheshimiwa Spika; Upatikanaji wa maji
katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa
zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma
na upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.
Zipo
hisia kwamba Dar es salaam inapata huduma maji safi na maji taka kuliko
miji na mijiji mengine nchini, lakini uhalisia unaonyesha kwamba hali
ni bora kwa wachache wakati walio wengi hususan waoishi kwenye maeneo ya
wananchi wa kipato chini hali ya upatikanaji wa maji ni duni kuliko
miji na majiji mengine nchini.
Jiji la Dar es Salaam ni la
mwisho kwa kigezo cha wastani wa kitaifa wa upatikanaji wa maji
ukilinganisha na majiji mengine ambayo yanafikia asilimia 75; hivyo
hatua za haraka zinahitajika kurekebisha hali hiyo.
Hatua hizo
zitawezesha kupunguza kwa haraka tatizo hilo na kuelekeza nguvu zote
katika maeneo ya vijijini palipo na shida kubwa badala ya mfumo wa sasa
ambapo kwa miaka zaidi ya kumi, rasilimali zinatumika lakini
kunakosekana ufumbuzi endelevu maeneo yote.
Hatua za haraka
zinapaswa kuchukuliwa kuhusu hali hii kwa kuzingatia kuwa idadi ya watu
katika Jiji la Dar es salaam inaendelea kukua kwa kasi likiwa ni jiji la
tatu kwa ongezeko kubwa la watu barani Afrika na la tisa duniani;
matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka
katika jiji kutokana na msongamano wake wa watu ni bomu la wakati.
Mheshimiwa Spika; Mkoa
wa Dar es Salam unapata maji kutoka mito na visima kwa matumizi ya
nyumbani, viwanda, bustani, mifugo, usafi na Mazingira. Sehemu ya Jiji
inayopata maji inahudumiwa na Kampuni ya DAWASCO (Dar es salaam Water
Supply and Sewerage Company) ambayo imepewa mkataba na Mamlaka ya Maji
Safi na Maji taka Dar es Salaam, DAWASA (Dar es Salaam Water Supply and
Sewerage Authority) na maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji
kutoka visima vinavyoendeshwa na vyombo vya watumia maji, Taasisi na
watu binafsi.
Mheshimiwa Spika; Kwa upande wa Jimbo
la Ubungo kama sehemu ya Jiji la Dar es salaam katika kufuatilia masuala
ya maji nilianza kwa kufanya Kongamano la Maji mwanzoni mwa mwaka 2011
ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau wengine katika
kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi. Nikiri kwamba katika hatua za awali
ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ulikuwa mdogo kwa
kiwango cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia ‘maandamano ya maji’
kwenda DAWASCO. Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa upande wa
DAWASCO ambapo nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya
kutembelea maeneo yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo
zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza kutoka maji. Wakati wa hatua hizo
tumewaonyesha DAWASCO biashara haramu ya maji iliyokuwa ikiendelea na
baadhi ya maeneo wamechukua hatua ikiwemo kwa watendaji wao; hatua zaidi
zinahitajika.
Mheshimiwa Spika;Baada ya mwito wa
mara kadhaa hapa bungeni; nashukuru pia Waziri wa Maji Prof. Jumanne
Maghembe alifika Jimboni Oktoba 2012 kwa ajili ya uzinduzi wa visima
katika maeneo ya King’ongo, Kilungule na Mavurunza na kuona hali halisi
ya ugumu wa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es salaam.
Natambua
pia jitihada zinazofanywa na wadau wengine wa maendeleo Jimboni Ubungo
katika masuala ya maji hususani Shirika la Kibelgiji (BTC) katika maeneo
ya Kwembe na Kibamba. Hata hivyo, yapo bado maeneo mengi yenye matatizo
makubwa ya maji ikiwemo ya Msumi, Makabe, Msakuzi, Malambamawili,
Msingwa, Goba na mengineyo mengi katika Jiji la Dar es salaam. Na hata
yale yenye miundombinu ya maji kama Sinza, Manzese, Makurumla na mengine
nayo hali ni tete. Hali iko hivyo katika Manispaa zote tatu za Ilala,
Kinondoni na Temeke.
Mheshimiwa Spika; Hata katika
maeneo ya umma ya kuuzia maji, bei ipo juu kwa kuwa mamlaka zetu za
kuratibu na kusimamia masuala ya bei kama EWURA imekuwa na udhaifu
katika kusimamia na kuratibu bei elekezi wanazozitoa. Kwa mfano jiji la
Dar es Salaam: vituo vingi vya kutoa huduma za maji chini ya
DAWASCO/DAWASA maarufu kama “vioski vya maji” vimekuwa vikiongeza bei
tofauti na bei elekezi toka EWURA ya Tsh 1 kwa lita moja yaani ndoo ya
lita 20 kwa Sh 20 kinyume na waraka nambari 10-017 (Order No.10.017) wa
Juni 8, 2010, agizo lililopaswa kuanza kutekelezwa Juni 15, 2010.
Utafiti
wa Shirika lisilo la kiserikali la Twaweza uliofanywa katika maeneo
mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam uliopewa jina; “Bei ya maji Dar es
Salaam Je, wanaoendesha maghati ya maji wanazingatia bei walizopangiwa?”
uliweza kubainisha kukithiri kwa bei zilizoongezwa kinyume na taratibu
na agizo hilo la EWURA katika maghati ya maji. Hata baada ya
kurekebishwa kwa agizo hilo na bei kuongezwa kiasi bado maeneo hayo ya
kuuzia maji kwa umma yamekuwa yakipandisha bei kupindukia.
Mheshimiwa Spika; Kero
kubwa zaidi iko wa wauzaji binafsi ambapo mazingira ya upungufu na
ukubwa wa mahitaji umefanya maji yauzwe kama bidhaa ya anasa bila
mamlaka EWURA kutunga kanuni wala kudhibiti bei, na kuachia soko holela
yenye kuambana na hujuma za miundombinu katika baadhi ya maeneo ili
kuongeza uhaba.
Wananchi ambao wengi wao ni wa kipato cha chini
hupata huduma ya maji kwa gharama kubwa ambayo huuzwa kwa kati ya Tsh
300 hadi Tsh 500 kwa ndoo ya lita 20 kwa maeneo ya Dar es salaam.
Kuwapo
pia kwa watoa huduma wasio rasmi husababisha bei ya maji kuwa kubwa
ambapo inakadiriwa kuwa 68% ya wakazi wanaoishi maeneo ya mjini yenye
msongamano mkubwa hupata maji kutoka kwa wauzaji wasio rasmi.
Hatua
za haraka zinahitajika kudhibiti ongezeko kubwa la bei ya maji kwa
wananchi wa kipato cha chini wanaotegemea kupata maji kutoka sekta
binafsi ambapo wanaonunua maji kwa madumu hununua bei ambayo ni
takribani mara 15 ya bei ya mteja anayepata huduma ya maji ya bomba.
Mheshimiwa Spika; Kwa
nyakati mbalimbali katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 mpaka 2012
Serikali imekuwa ikitoa ahadi bungeni ya kumaliza tatizo la majisafi na
majitaka katika Jiji la Dar es Salaam bila utekelezaji sahihi, kamili na
wa haraka.
Malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa
Umaskini wa kwanza (MKUKUTA I) yaliyoingizwa pia katika ilani ya
Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2005-2010 hayakuweza kutekelezwa.
Malengo
mengine yameingizwa katika ilani ya CCM na Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kuondoa Umaskini awamu ya pili (MKUKUTA II) ya kuboresha upatikanaji wa
maji safi na usafi wa mazingira ifikapo mwaka 2015; nayo tukiwa mwaka
2013 mwelekeo unaonyesha kwamba hayatafikiwa iwapo hatua za haraka
zisipochukuliwa.
Mara baada ya kupitishwa kwa Mpango Maalum wa
Maji katika Jiji la Dar es salaam mwaka 2011, Rais alitangaza kwamba
tatizo la maji kuwa historia mwaka 2013; ambapo ni mwaka huu. Hata
hivyo, utekelezaji wa mipango hauashirii ahadi hiyo kutekelezeka na kwa
mwelekeo wa sasa tatizo litaendelea mpaka baada ya mwaka 2016 iwapo
hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mheshimiwa Spika;Mabomba ya ‘mchina’ bila maji na miradi hewa katika maeneo ya wananchi wa kipato cha chini Jijini Dar es Salaam: Kati
ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na
upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na
maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation
Project-DWSSP).
Mradi huo uliotumia dola milioni 164.6 hata
hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba
ya wachina hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji,
upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za
ufisadi katika matumizi.
Hali hii ni kati ya matatizo yanayokera
wananchi wa Jiji la Dar es salaam kwa kuwa na mabomba yasiyotoa maji
kwa muda mrefu hata kwa mgawo maarufu mitaani kama mabomba ya ‘mchina’.
Serikali
ilieleze bunge lako sababu ya mabomba hayo kutokutoa maji mpaka hivi
sasa, lini mabomba hayo yataanza kutoa maji katika maeneo ambayo maji
hayatoki mpaka sasa na hatua gani zimechukuliwa wa waliotekeleza mradi
huo bila kuzingatia maandalizi ya msingi.
Ni muhimu hatua
zikachukuliwa kwa wahusika kwa kuwa kitendo cha mabomba hayo kukaa muda
mrefu bila kutoa maji inafanya miundombinu hiyo kuanza kuharibika au
kuharibiwa ambayo ni hasara kwa taifa kwa kuwa pamoja na fedha
zilizotumika kuweka mabomba hayo kupotea, fedha nyingine zitatumika
katika hatua ya baadaye kufanya matengenezo kwenye maeneo
yaliyoharibika.
Aidha, yapo pia malalamiko ya kwamba yapo maeneo
ambayo yalitoa maji mara chache kati ya mwaka 2009 na 2010 lakini baada
ya hapo maeneo hayo hayajatoa maji tena mpaka sasa, Serikali itoe
maelezo ya kitaalamu kwa bunge na kwa wananchi kuhusu sababu za maji
hayo kutoka wakati huo na kutokutoka tena na hatua zinazochukuliwa
kurekebisha hali hiyo.
Mheshimiwa Spika; Kasoro
katika mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na
Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es
salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP); hazielezwi na
wananchi pekee bali pia hata watafiti mbalimbali.
Ripoti ya
karibuni kabisa mwaka 2012 ya Shirika la Kimataifa la Water Aid ya
utafiti uliofanywa ukihusisha wataalamu kutoka Overseas Development
Institute na Chuo kimoja cha nchini Uingereza (SOAS) iliyofuatilia
uwekezaji wa miradi ya maji mijini katika nchi za Ghana, Burkinafasso na
Tanzania ( Stregthening pro poor targeting of investments by African
utilities in urban water and Sanitation) ikiwemo namna miradi
ilivyoshindwa kuwajali maskini na maeneo na kiwango cha hali ya maji
kutokupatikana kinyume na malengo yaliyowekwa wakati wa kuanza kwa
mradi.
Mheshimiwa Spika; Matatizo ya kuwa na mabomba
yasiyotoa maji hayapo tu katika mabomba waliyofungiwa wananchi majumbani
bali pia kwenye visima na ‘vioski’/maghati ya jumuiya. Kuna udhaifu wa
kuanzisha miradi ya jamii na kuacha kusimamia uendelevu (sustainability)
wake na hatimaye baada ya muda mfupi miradi hiyo iliyotumia fedha za
umma inabaki kuwa ‘miradi hewa’.
Utafiti wa vituo vya maji
uliofanywa June 2009 na Overseas Development Institute (ODI) chini ya
udhamini wa shirika la Water Aid hapa nchini ulibainisha ni asilimia 54
tu ya vituo vya maji vilivyopo ndivyo vinatumika kwa kutoa huduma ya
maji.
Hivyo kwa wastani baada ya miaka miwili tu ya kujengwa
karibu nusu ya visima na vioski huwa haviendelei tena kufanya kazi.
Utaratibu wa kukimbilia kutumia fedha za miradi ya maji kwa mwaka wa
kibajeti mpya bila kuzingatia taarifa za utekelezaji na ufuatiliaji wa
miradi ya nyuma ni hatari kwa uendelevu wa kuwepo kwa huduma ya maji kwa
siku zijazo kama hatua za haraka hazitachukuliwa kuzingatia matatizo
yaliyojitokeza katika miradi iliyopita na kuzingatia ubora na ufanisi
katika miradi ya maji nchini.
Mheshimiwa Spika; Utafiti
uliofanywa na Economic and Social Research Foundation, umebaini
utofauti wa utekelezaji wa miradi ya serikali na mashirika binafsi
katika kauhakiki ubora wa matumizi ya fedha na huduma kwa jamii. Utafiti
ulibaini kuwa katika miradi iliyofadhiliwa na mashirika ya maendeleo,
wastani wa asilimia 67 ya vioski vilionekana kufanya kazi; wakati miradi
ambayo imefadhiliwa na Serikali ni wastani wa asilimia 45 ya vioski vya
maji vilikuwa vikifanya kazi katika maeneo hayo hayo. Utafiti huo
ulihusu Mikoa ya Singida na Dodoma.
Hali ni mbaya zaidi kwa
upande wa Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa utafiti mwingine wa Shirika
la Water Aid uliobainisha kuwa asilimia 85 ya vioski vilivyounganishwa
Jijini Dar es Salaam havitoi maji, Asilimia 10 vinatoa maji kwa kusuasua
na asilimia 5 tu ndivyo ambavyo vinatoa maji kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika;Kasoro katika utendaji na uwajibikaji wa mamlaka na vyombo vinavyohusika na utoaji na udhibiti wa huduma ya maji: Majukumu
ya utoaji wa huduma ya maji jijini Dar es salaam na baadhi ya maeneo ya
Kibaha na Bagamoyo yanafanywa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka
(DAWASA) ambayo ni mmiliki, mkodishaji na msimamizi wa utoaji wa huduma
ya majisafi na maji taka na ina wajibu wa kupanga na kugharamia
utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kuiendeleza na kugharamia
matengenezo ya dharura na makubwa.
Mwaka 2005 DAWASA iliingia
mkataba wa miaka kumi (10) wa uendeshaji na Shirika la Maji Safi na Maji
Taka Dar es Salaam (DAWASCO). Chini ya mkataba huo majumu ya DAWASCO ni
kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji na uondoshaji wa maji
taka, kuuza maji kwa wateja , kutoa ankara kwa wateja, kukusanya
maduhuli, kulipia gharama za uendeshaji, kutekeleza matengenezo makubwa
yanayogharamiwa na DAWASA na kutekeleza uunganishaji wa maji kwa wateja
wapya kwa kutumia mfuko wa maji.
Kisheria na kimkataba DAWASA
ina wajibu wa kuisimamia DAWASCO iliyoingia nayo mkataba; hata hivyo kwa
kuwa yote ni taasisi na mashirika ya umma ambayo bodi zake na watendaji
wake wakuu huteuliwa na mamlaka zile zile na kuripoti kwa watu wale
wale, hali ambayo ina athari kwenye utendaji na uwajibikaji.
Wakati
umefika sasa wa mkataba huo kati ya DAWASA na DAWASCO kuwekwa wazi kwa
umma; kufanyiwa tathmini ya miaka zaidi ya mitano iliyopita ya
utekelezaji; kufanyiwa marekebisho kwa ajili ya kipindi kilichobaki na
maandalizi kuanza ya mfumo bora unaopaswa kuanza kuandaliwa baada ya
kuisha kwa mkataba huo mwaka 2015.
Utoaji wa huduma ya maji
unamhusu pia mdhibiti ambaye ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati
na Maji (EWURA) yenye mamlaka ya kudhibiti utoaji wa huduma,
kuidhinisha bei ya huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka pamoja
na kutoa leseni za uendeshaji. Hata hivyo, EWURA imekuwa ikitoa
kipaumbele zaidi kwenye kutumia mamlaka yake kudhibiti kwa karibu sekta
ya nishati, huku udhibiti kwenye sekta muhimu ya maji hususan kwa upande
wa watoa huduma binafsi ukiachwa uwe katika mfumo wa soko holela na
kuchangia katika ongezeko la bei ya maji pamoja na ubovu wa huduma.
Wakati
umefika sasa wa Bunge kusimamia kwa karibu utekelezwaji wa The Energy
and Water Utilities Regulatory Authority Act (Sura ya 414) kifungu cha 6
ambayo inaelekeza bayana kwamba wajibu wa EWURA ni pamoja na kulinda
maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa huduma inazozidhibiti
ikiwemo maji wa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio
pembezoni au katika mazingira magumu (low income and disadvantaged
consumers).
Aidha kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha sheria hiyo
majukumu ya EWURA ni pamoja na kupanga viwango cha ubora, viwango vya
ugavi, kufuatilia utendaji ikiwemo uwekezaji na upatikanaji, kudhibiti
bei na tozo na kushughulikia malalamiko na migogoro.
EWURA
itumie mamlaka yake pia kwa kutumia vifungu vya 16, 17, 18 na 19
kuhakikisha kwamba masuala ya udhibiti wa bei hashaishii tu katika
mamlaka za umma na pia ianze yenye uchunguzi juu ya kuporomoka kwa kiasi
na kiwango cha huduma za maji katika Jiji la Dar es salaam na nchi kwa
ujumla na kupendekeza hatua za ziada za haraka zaidi kuweza kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika; Mwaka 2011 Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi wa ufanisi (performance audit) kuhusu
usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini ikiwemo Dar es
salaam, hata hivyo taarifa yake ya Januari 2012 baada ya kutajwa bungeni
miongoni mwa hati zilizowasilishwa; hatua za kutekeleza mapendekezo
yake hazikupata usimamizi wa kutosha wa kibunge.
Hivyo, ipo haja
kwa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa niaba ya Bunge ipokee
maelezo ya Serikali kuhusu utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo kwenye
ripoti hiyo ambayo yalilenga kuboresha utendaji wa DAWASA, DAWASCO na
Mamlaka zingine za maji katika mikoa yote nchini na hatimaye kamati hiyo
iwasilishe maoni na mapendekezo yake bungeni kwa ajili ya hatua zaidi.
Mfumo duni wa ushughulikiaji wa maji taka ni bomu la wakati katika Jiji la Dar es salaam: Mheshimiwa Spika;Hali
ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya asilimia
10 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na
hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa.
Hata katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam, mitandao ya maji
taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la
watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea
katika siku za usoni.
Kwa mujibu wa ripoti ya EWURA ya mwaka
2009, viwango vya huduma za uondoaji maji taka katika asilimia vimewekwa
katika mabano Mwanza (3.1%), Moshi (5.8%) Arusha (7.0%), Dodoma
(11.6%), Tabora (1.3%) na Tanga (9.3%).
Taarifa hiyo inaeleza
kuwa kwa upande wa Dar es salaam huduma za mtandao wa maji taka ni kwa
kiwango cha asilimia 4.8 katika Jiji lenye msongamano mkubwa wa watu
ambapo hata katika kata zilizopimwa kama ya Sinza na nyinginezo hali ni
tete.
Matokeo yake ni kuwawapo wakazi ambao hukiuka sheria na
kusubiri mvua zinyeshe na kutiririsha maji taka hali ambayo ni hatari
kwa afya za wananchi; kwa upande wa vijijini unafuu unapitakana katika
ukubwa wa maeneo ya kuweza kuchimba vyoo, kinyume na mijini ambapo
kadiri gharama za kukodi magari ya maji taka kwa sekta binafsi
zisizodhibitiwa zinavyozidi kuongezeka ndivyo hatari zinavyozidi katika
maeneo wanayoishi wananchi wa kipato cha chini.
Udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri, kamati na jumuiya za watumia maji: Katika
baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo za Jiji la Dar es salaam
yamekuwepo matumizi mabaya na udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya
maji inayosimamiwa na Halmashauri kwa kushirikiana na kamati za maji au
jumuiya za watumia maji.
Kushindwa kushughulikiwa kwa matatizo
ya kimfumo kuhusu uendeshaji wa miradi ya maji, kutokutekelezwa kwa
wakati kwa vipaumbele vya maji kwa mujibu wa bajeti za Halmashauri
iliyopitishwa na madai ya ufisadi katika miradi inayosimamiwa na kamati
za maji au jumuiya za watumiaji katika baadhi ya maeneo kumesababisha
wananchi kukosa huduma ya maji.
Hata hivyo, pamoja na wananchi
kuwasilisha malalamiko yao Wizara ya Maji na Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI) ili kutimiza wajibu wa
usimamizi na ufuatiliaji hatua za haraka zimekuwa hazichukuliwi hali
inayohitaji mjadala na usimamizi wa kibunge.
Katika mjadala
utakaotokana na hoja hii, naamini wabunge wenzangu mchangia uzoefu wenu
katika maeneo mnayotoka; naomba kwa upande wangu nitoe mfano wa Manispaa
ya Kinondoni kuhusu mradi wa maji kata ya Goba.
Tatizo la maji
katika kata ya Goba limedumu sasa kwa kipindi cha miaka zaidi ya
mitano, pamoja na kwamba serikali inaowajibu kulinda maslahi ya walaji
na kuhamasisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa watumiaji wakiwemo wa
kipato cha chini na walio pembezoni au katika mazingira magumu mamlaka
zinazohusika hazijaweza kutimiza wajibu ipasavyo kuhusu kata ya Goba.
Jitihada
nyingi zimefanywa zilizofanywa na wakazi wenyewe kama njia mbadala ya
kupata huduma hiyo muhimu kwa maisha ya Binadamu lakini zimekuwa
zikikwamishwa na baadhi ya watendaji wa Halmashauri kwa kushindwa
kusimamia kwa kurejesha na kupanua huduma hiyo muhimu kwa wananchi hata
baada ya kupokea malalamiko katika nyakati mbalimbali .
Mnaweza
mkajiuliza sababu za suala hili kuvuka mipaka ya Baraza la Madiwani wa
Manispaa ya Kinondoni, mpaka Bungeni; ni muhimu ifahamike mapema kwamba
jitihada katika ngazi hizo kwa miaka mingi hazijaweza kuleta ufumbuzi
hali inayohitaji chombo cha juu zaidi kwa niaba ya wananchi; yaani Bunge
kujadili kwa kuwa Wizara ya Maji nayo imeshindwa kuchukua hatua
zinazostahili kwa wakati.
Historia ya tatizo hili inaonesha
kuwa wakazi wa Goba wameshawahi kuandika barua kwa Waziri wa Maji barua
ya tarehe 15/10/2009 ikieleza kero ya maji kwa wananchi na wakimtaka
alipatie ufumbuzi tatizo hilo na nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa
mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, na mkuu wa wilaya ya Kinondoni pamoja na
hayo bado tatizo linaendelea kutopatiwa ufumbuzi huku wakazi wa Goba
wakiendelea kukosa haki yao ya msingi kwa kuwa hakuna maisha bila maji.
Kushindwa
kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kulipelekea wananchi pia kuandika barua
ya wazi kwa waziri mkuu mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda
wakilalamikia mradi wa maji wa muda mrefu, pamoja na barua hiyo hakuna
jitihada kamili zilizofanyika za makusudi kuondoa tatizo hilo.
Utendaji
mbovu na usimamizi mbovu wa miradi ya maji kwa manispaa ya Kinondoni
chini ya kamati za maji zilizosababisha maji kukatwa kwa nyakati
mbalimbali kati ya mwaka 2007 na 2011 ndiyo chanzo cha ukosefu wa maji
kwa kipindi chote hicho.
Katika kipindi cha karibuni, kamati ya
maji Goba baada ya kukatwa kwa maji ilimwandikia barua mkurugenzi wa
Manispaa ya Kinondoni tarehe 30/08/2011 yenye kumbukumbu namba
G/WP/GOBA/VOL013/11 ikimuarifu Mkurugenzi kuhusu kusitishwa kwa huduma
ya Maji kwa Wananchi wa Kata ya Goba.
Katika barua hiyo ambayo
mbunge nilipatiwa nakala yake, wananchi hao walimlalamikia mkurugenzi
kwa kutozifanya kazi barua zao wakionesha mfano barua ya tarehe
22/05/2011 na kumuomba Mkurugenzi kuchukua hatua za haraka ili huduma ya
maji irejeshwe hata hivyo Manispaa ilizembea kuchukua hatua
zinazostahili.
Mnamo tarehe 21/03/2011, nilimwandikia barua
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni yenye namba : KUMB:OMU/MJ/005/2011
yenye kichwa cha barua “Hatua za Haraka zinahitajika kuhusu mradi wa
Maji Goba” .
Kutokana na hatua stahili kutochukuliwa niliandika
barua nyingine kwa Mkurugenzi yenye kumb. OMU/MJ/008/2011 na
kupendekeza hatua za haraka kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
fedha kutoka mfuko wa Jimbo Tsh 3,000,000.00 zinapelekwa haraka katika
Akaunti ya maji Goba ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa
manispaa za kujenga uwezo wa mradi husika na kuhakikisha wananchi
wanapata huduma ya maji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa
ya Kinondoni alifanya ziara Goba tarehe 31/01/2012 katika ziara ile
mkurugenzi aliwaahidi wakazi wa Goba kurejesha huduma ya Maji ndani ya
wiki moja lakini hadi sasa ni zaidi ya mwaka wananchi bado hawajapata
huduma hiyo.
Tarehe 18/03/2012 niliwaandikia barua tena DAWASA
yenye kumbukumbu namba OMU/MJ/006/2012 kuhusu hatua ambazo DAWASA
imechukuakuhusu matatizo ya maji katika kata ya Goba, katika barua hiyo
nilitaka kujua hatua ambazo DAWASA imechukua kushughulikia matatizo ya
maji Goba hususani juu ya kufanya majadiliano na Manispaa ya Kinondoni
ili kuwa na mfumo endelevu zaidi wa utoaji wa huduma ya maji katika kata
ya Goba ambayo ina ongezeko kubwa la wakazi, makazi na mahitaji mengine
mengi kwa sasa.
Wizara ya Maji na mamlaka zingine za kiserikali
zinapaswa kuharakisha uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya wote
waliohusika kusababisha uvunjwaji wa haki za watumiaji wa huduma ya
maji, udhaifu wa usimamizi wa miradi ya maji na ukosefu wa huduma ya
maji katika kata ya Goba kwenye Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es
salaam ili kutoa fundisho kwa maeneo mengine.
Kwa kufanya
hivyo, Serikali ifuatilie mpaka Manispaa ya Kinondoni, DAWASA na DAWASCO
wawezeshe huduma ya maji kurejea kwa wananchi, kupanua kwa dharura wigo
wa upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kata ya Goba pamoja na kuboresha
mfumo mzima wa upangaji, utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maji
katika Manispaa ya Kinondoni, DAWASA na DAWASCO.
Aidha ili
kupata ufumbuzi wa kudumu Wizara ichukue hatua za ziada ili kata ya Goba
itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya Manispaa ya Kinondoni na
badala yake ihudumiwe na DAWASA pamoja na DAWASCO ili kuwezesha
uboreshaji mpana wa miundombinu.
Mheshimiwa Spika;Upungufu katika usimamizi wa Sheria za maji na haja ya kuharakisha utungaji wa kanuni na marekebisho ya sheria husika: Hatua
kuhusu uboreshaji wa huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka
katika Jiji la Dar es salaam zinasimamiwa na sheria mbalimbali
zilizotungwa na Bunge hili.
Baadhi ya Sheria hizo ni pamoja na
Sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji ya mwaka 2009, Sheria ya maji
safi na usafi wa mazingira ya mwaka 2009, sheria ya mamlaka ya udhibiti
wa nishati na maji ya mwaka 2001 na sheria ya mamlaka ya maji safi na
maji taka Dar es salaam ya mwaka 2001. Hata hivyo kumekuwa na upungufu
wa kusimamia utekelezaji wa sheria hizo ikiwemo katika kutunga kanuni na
kuchukua hatua kwa wakati.
Serikali inapaswa kutoa maelezo
bungeni ni kwanini mpaka mwezi Julai mwaka 2012 ilikuwa haijakamilisha
kutunga kanuni zinazohusu uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji wa
Maji (National Water Investment Fund) toka Sheria husika itungwe mwaka
2009. Bunge lijadili hoja hii ili pamoja na mambo mengine liisimamie
Serikali mfuko huu uweze kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi wote wenye
kuhitaji uwekezaji toka mfuko huu kuondoa matatizo ya maji nchini
ikiwemo Dar es salaam.
Mheshimiwa Spika; Aidha,
katika utekelezaji wa sheria umeonekana pia upungufu mwingine wa ziada
unaohitaji marekebisho ya sheria mbalimbali. Mfano, ukiondoa maeneo ya
mijini ambapo huduma za maji zinasimamiwa na mamlaka za maji safi na
maji taka kwa upande wa Dar es salaam ikiwa ni DAWASA; maeneo ya
vijijini kote nchini yanayohudumiwa na Halmashauri ikiwemo maeneo ya
pembezoni ya Dar es salaam yanayohudumiwa na Manispaa, mifumo ya
usimamizi ina udhaifu kutokana na upungufu wa kisheria.
Kutokana
na hali hiyo kwa nyakati mbalimbali limetolewa pendekezo na wabunge
kwamba paundwe Wakala wa Maji (TANWATER) kama ilivyo Wakala wa Barabara
(TANROADS) hata hivyo Serikali mpaka sasa haijatekeleza pendekezo hilo
ambalo utekelezaji wake utahusisha pia marekebisho ya sheria mbalimbali.
Mheshimiwa Spika; Sheria ya Mamlaka ya Maji Safi na
Maji Taka Dar es salaam ya mwaka 2001 nayo inahitaji kufanyiwa
marekebisho makubwa. Kati ya mambo yanayohitajika kufanyika ni pamoja na
kurekebisha ramani ya awali iliyopitishwa ikiwa ni sehemu ya sheria
husika kuhusu eneo ambalo kwa mujibu wa sheria linapaswa kuhudumiwa na
DAWASA (designed area) ili kuendana na ukuaji wa jiji pamoja na maeneo
jirani ya Kibaha na Bagamoyo.
Aidha, marekebisho mengine
yanahitajika katika utaratibu mzima wa DAWASA kutoa mikataba kwa
makampuni mengine kuendesha huduma ya maji kwa niaba yake ili kuepusha
kasoro zilizojitokeza wakati wa mkataba wa City Water na kasoro nyingine
zinazoendelea hivi sasa katika mkataba baina ya DAWASA na Kampuni ya
Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).
Marekebisho yanayohitajika
kufanyika ni pamoja na ya kubadili muundo wa Bodi ya DAWASCO ikiwemo
kuwezesha uwakilishi wa Halmashauri za Manispaa za Dar es salaam katika
bodi ya DAWASA.
Kwa upekee wa muundo wa Mkoa wa Dar es salaam,
Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inafanya kazi ya uratibu tu wakati
ambapo sehemu kubwa ya taratibu za ardhi, mipango miji na ujenzi ziko
katika Halmashauri. Halmashauri za Manispaa ndizo ambazo zinahusika kwa
kiwango kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji ukiondoa ya DAWASA
katika kata na mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam.
Hata
hivyo, wakati halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inawakilishwa kati
bodi ya DAWASA, Manispaa zote tatu hazina uwakilishi hali ambayo
inapunguza kiungo cha mawasiliano na kuathiri nguvu za Halmashauri
katika kufuatilia miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao na
wakati mwingine kuchelewesha miradi husika.
Marekebisho ya
sheria ya DAWASA yanapaswa kuhusisha pia kurekebisha adhabu zinazotokana
na makosa ya uharibifu wa miundombinu ya maji, wizi wa maji safi na
uunganishaji kinyemela wa mabomba ya maji taka; kwa kuwa adhabu zilizopo
kiwango chake kimepitwa na wakati na hakilingani na kukithiri kwa
makosa ya biashara haramu ya maji na hujuma katika miundombinu ya maji
katika jiji la Dar es salaam.
Kasoro katika upangaji na utekelezaji wa Mpango Maalum wa kutatua tatizo la Maji katika Jiji la Dar es salaam: Ikumbukwe
kuwa katika kutafuta ufumbuzi Mwezi Machi 2011 Baraza la Mawaziri
lilipitisha Mpango Maalum wa Maji Dar es salaam na Pwani wenye mgawanyo
wa fedha ufuatao:
Mahitaji ya fedha Mpango Maalum
Mahitaji ya fedha Mpango Maalum
|
Na.
|
Kazi
zitakazotekelezwa
|
Gharama
2010-2013
(SH.BILIONI)
|
Makadirio
kila mwaka wa fedha (sh. bilioni)
|
2010/11
|
2011/12
|
2012/13
|
2013/14
|
1
|
Upanuzi
wa mtambo wa Ruvu Juu
|
17.25
|
0.45
|
6.00
|
6.00
|
4.80
|
2
|
Upanuzi
wa mtambo wa Ruvu Chini
|
122.50
|
9.38
|
24.28
|
56.98
|
31.88
|
3
|
Kazi
ya visima vya Kimbiji na Mpera
|
133.15
|
10.35
|
70.90
|
29.25
|
22.65
|
4
|
Ujenzi
wa bwawa la Kidunda
|
174.75
|
3.00
|
7.80
|
83.70
|
80.25
|
5
|
Upanuzi
wa mtandao wa mabomba ya maji safi
|
82.40
|
-
|
24.05
|
37.15
|
21.20
|
6
|
Uchimbaji
na ukarabati wa visima katika maeneo yasiyo na maji.
|
4.00
|
1.50
|
2.50
|
-
|
-
|
7
|
Kuimarisha
utoaji wa huduma ya maji
|
18.00
|
-
|
5.00
|
6.00
|
7.00
|
8
|
Kuboresha
uondoaji wa majitaka (upanuzi wa mtandao na ujenzi wa mitambo mitatu ya maji
taka)
|
100.60
|
-
|
-
|
50.30
|
50.30
|
9
|
Miradi
mingine
|
0.20
|
0.20
|
-
|
-
|
-
|
10
|
Elimu
kwa umma
|
1.00
|
0.50
|
0.20
|
0.20
|
0.10
|
|
Jumla Kuu
|
653.85
|
25.38
|
140.73
|
269.58
|
218.18
|
Katika kutekeleza mpango huu maalum, natambua kwamba upanuzi wa
mfumo wa maji wa Ruvu Juu ikiwemo ujenzi wa wa Tanki la Kibamba na Bomba
mpaka Kimara utafanyika na fedha za ujenzi huo kiasi cha dola milioni
132 zimepatikana ikiwa sehemu ya mkopo wa dola milioni 178 kutoka
Serikali ya India. Nafahamu pia kwamba ujenzi wa kupanua intake na
machujio mapya ya maji unaendelea kwa udhamini wa Shirika la Milenia
(MCC) wa kiasi cha dola za kimarekani milioni 36.8. Naelewa pia kuwa
ujenzi wa bomba kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam utakaogharimu
shilingi bilioni 122.5 za walipa kodi wa Tanzania umeanza.
Hata
hivyo, kiwango cha uwekezaji huo hakijaweza kufikisha malengo
yaliyopitishwa na Baraza la Mawaziri na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano
uliopitishwa na Bunge hili; kwa kuwa jumla mpaka mwaka wa fedha
2012/2013, zilipaswa kuwa zimetumika au walau zimetengwa kiasi cha
shilingi bilioni 435.67 ikiwa ni hatua ya haraka ya kuboresha
upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es
salaam na mikoa mingine inayoguswa na miradi hiyo ikiwemo ya Morogoro na
Pwani.
Mheshimiwa Spika; Hivyo, pengo hilo linapaswa
kuzibwa kwa haraka kupitia nyongeza ya fedha katika Mpango wa Maendeleo
na Bajeti ya mwaka 2013/2014 kwa kuchukua hatua za haraka. Serikali
ieleze bungeni imefikia wapi katika kupata fedha za kulipa fidia ya
maeneo ya hifadhi ya maji ya Kimbiji na Mpera kiasi cha shilingi bilioni
27 ambayo ilipaswa kuwa imelipwa tangu mwaka 2011 na lini hasa ujenzi
utaanza.
Serikali ieleze iwapo ujenzi wa Bwawa la Kidunda Mkoani
Morogoro unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 175 utaingizwa katika
vipaumbele vya taifa kwa mwaka 2013/2014 kwa kuzingatia umuhimu wa bwawa
hilo katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo
yenye kufanya upatikanaji wa maji kutokuwa na uhakika katika mto Ruvu
kipindi chote cha mwaka na kusababisha uhaba wa maji kwa wananchi wa
Pwani na Dar es Salaam.
Hatua hizi zote zitakuwa na tija kwa
wananchi wengi zaidi iwapo zitaambatana na ujenzi wa mfumo wa usambazaji
wa maji katika maeneo ambayo hayakufikiwa katika awamu iliyopita;
maeneo ambayo wananchi huyaita ‘yaliyorukwa katika uwekezaji wa mabomba
ya mchina’ na ukarabati wa mifumo chakavu ya usambazaji wa maji.
Serikali inapaswa kueleza ni lini maeneo hayo yatawekewa mtandao wa
mabomba ambayo yanakisiwa kuhitaji jumla ya shilingi bilioni 82.4.
Mheshimiwa Spika; Kwa
upande mwingine, ili kuondokana na ‘bomu la wakati’ serikali ione
umuhimu wa kutafuta fedha kwa haraka kiasi cha shilingi bilioni 100.6
kwa ajili ya kuboresha huduma za maji taka kama ilivyoahidi kwa nyakati
mbalimbali.
Fedha hizi zinaonekana ni nyingi lakini ni matokeo
ya udhaifu wa miaka mingi katika mipango miji katika Jiji la Dar es
salaam hali inayosababisha gharama za usambazaji wa huduma ya maji safi
na uondoaji wa maji taka kuwa kubwa. Upo umuhimu wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutambua kwamba ongezeko la zaidi ya
asilimia 70 ya maeneo ya makazi ambayo hayajapimwa katika Jiji la Dar es
Salaam ikilinganishwa na wastani wa asilimia 30 wa miji mingine mikuu
ya mikoa ni hali yenye kuathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi na
maisha kwa wananchi kwa ujumla.
Ujenzi wa miundombinu hiyo mipya
na ukarabati wa ile chakavu ya usafirishaji hautakuwa na maslahi tu kwa
wananchi kwa kuwawezesha kupata huduma bali pia utakuwa na tija kwa
nchi kwa kupunguza upotevu wa maji mpaka asilimia 25 na hivyo kudhibiti
hasara ambayo inalikumba taifa hivi sasa kutokana na kiwango cha maji
kinachopotea kwa Jiji la Dar es Salaam pekee.
Bajeti ndogo ya sekta ya maji na utegemezi wa fedha kutoka nje:
Mheshimiwa Spika; Fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi
ya maendeleo kwenye sekta ya maji ni kidogo na hata hizo zinazotengwa
utegemezi wa wahisani kutoka nje ni mkubwa kwa kiwango cha kuathiri
miradi katika Jiji la Dar es salaam na nchi kwa ujumla.
Kujibu
wa ripoti ya Hali ya Umaskini na Maendeleo ya Watu mwaka 20112 (PHDR)
Fedha za ndani za kutekeleza bajeti ya Sekta ya Maji imekuwa ikishuka
mwaka hadi mwaka toka 57% katika mwaka wa fedha 2005/06 hadi 10% kwa
mwaka wa fedha 2011/12.
Hali hii imesabababisha kukithiri kwa
utegemezi katika vyanzo vya mapato toka nje na kwa wabia wa maendeleo
kuwezesha miradi ya maji; fedha ambazo hazipatikani kwa wakati na kwa
kiwango kinachokidhi mahitaji.
Kwa mwaka 2011/12 tumeshuhudia
kutokutimizwa kwa azimio la serikali la kutenga kiasi cha Dola za
Kimarekani 128 milioni kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Maji
(WSDP) huku bajeti pangwa ikiwa ni dola za kimarekani 28 milioni tu kwa
mwaka huo 2011/12.
Tufahamu kwamba kupungua huku kwa kiwango cha
bajeti katika sekta ya maji kunapingana hata na azimio la Sharm el
Sheikh la nchi za Umoja wa Afrika la mwaka 2008 la kutaka dhamira na
azma ya kuongeza kipaumbele cha kisiasa katika utengwaji na kuwekwa wazi
kwa bajeti kwa ajili ya sekta ya maji safi na maji taka.
Mheshimiwa Spika; Utekelezaji
wa bajeti ya mwaka 2012/2013 umeendelea kuonesha upungufu katika utoaji
wa fedha za miradi ya maendeleo katika sekta ya maji, taarifa
zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miezi sita ya kwanza Jumla ya
Shilingi Bilioni 29 tu ndizo zilitolewa ikiwa ni sawa na asilimia 36
katika fedha za ndani. Hali hii ni kidogo ikizingatiwa kiwango
kilichoidhinishwa na tume ya mipango kikiwa ni shilingi 48,326,792,184
kwa kipindi cha robo ya kwanza pekee.
Mheshimiwa Spika, Mapungufu
yanayojitokeza katika utekelezaji wa mipango ya serikali hususani
katika ugawaji wa rasilimali fedha ambazo zimeidhinishwa na bunge katika
huduma muhimu za jamii kama maji, matokeo yake ni kuwa na huduma mbovu,
hivyo napendekeza bunge lijadili hali hiyo na kupitisha hatua za haraka
ambazo zitanufaisha nchi kwa ujumla ikiwemo Jiji la Dar es Salaam.
Hatua
hizo zitawezesha fedha za miradi ya maendeleo ya maji kutolewa kwa
wakati katika miezi iliyobaki ya mwaka wa fedha 2012/2013 na kupewa
kipaumbele katika Mpango wa Mwaka wa Maendeleo na Bajeti kwa mwaka
2013/2014.
Mheshimiwa Spika;
Udhaifu katika utekelezaji wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini: Tangu
mwaka 2000 Bunge hili limekuwa likipewa ahadi za utekelezaji wa
Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RWSSP). Wakati maelezo
ya kuanza kwa mpango huo yalipoletwa bungeni mwaka 2003, wakati huo
ukiitwa mpango wa vijiji kumi (quick wins), yapo maeneo katika Jiji la
Dar es salaam ambayo yalikuwa na vijiji na yaliingizwa katika mpango
huo. Hata hivyo, mpaka leo miaka takribani kumi baadaye mwaka 2013
maeneo hayo yakiwa yameshapanda hadhi na kuwa mitaa miradi hiyo
haijatekelezwa kwa ukamilifu wake.
Maeneo hayo yamekosa maji kwa
pande zote, hayajahudumiwa na DAWASA na DAWASCO kwa kuwa yapo kwenye
vijiji kumi; na mradi huo wa vijiji kumi haujaweza kuwafanya wananchi
hao wapate huduma ya maji.
Hali hii haihusu Halmashauri za
Manispaa za Jiji la Dar es Salaam za Ilala, Kinondoni na Temeke; inahusu
halmashauri zote nchini ambazo mpango huo ulipaswa kutekelezwa. Naamini
kujadiliwa kwa hoja hii kutawezesha wabunge wenzangu kueleza pia uzoefu
katika maeneo yenu ya vijijini na mijini hatimaye kutokana na
mapendekezo ya hoja hii; Bunge likapitisha maazimio ambayo yataweza
kuchangia katika kurekebisha hali hii.
Mheshimiwa Spika; Programu
hii ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ilipaswa kutekelezwa kwa
awamu nne, ambapo utekelezaji wa awamu ya kwanza baada ya kucheleweshwa
toka mwaka 2003 ulipaswa kuanza mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka
2010/2011. Kwa maneno rahisi ni kwamba hadi kufikia hivi sasa ilipaswa
tayari maji yawe yameshapatikana katika vijiji kumi vya kila halmashauri
nchini, hata hivyo ukomo wa muda wa awali ukiwa umeshapita kwa zaidi ya
mwaka mmoja; utekelezaji katika maeneo mbalimbali nchini haukufanyika
hata robo.
Hali iko hivyo, wakati ambapo fedha zimetumika bila
maji kupatikana; katika hatua hiyo ya kwanza jumla ya shilingi bilioni
96.4 zimetumika kwenye “quick wins” hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 2012
huku maji kwa sehemu kubwa kukiwa hakuna; hali ambayo ni matumizi
mabaya ya rasilimali za umma.
Mheshimiwa Spika; Katika
ufuatiliaji wangu kuhusu masuala ya maji katika Manispaa za Jiji la Dar
es salaam, katika halmashauri zingine na katika Wizara ya Maji
nimebaini kwamba hali hiyo ilisababishwa na mikataba mibovu yenye dalili
za ufisadi, kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa makampuni
yaliyopewa zabuni katika mazingira ya utata na udhaifu katika mchakato
mzima wa zabuni na usimamizi wa miradi.
Matokeo yake watafiti na
wachimbaji binafsi wengi wao wakiwa hawana uwezo wa vifaa na wataalamu
walipewa kazi na kulipwa fedha bila hata ya mchakato kukamilika; badala
ya kuwekwa mfumo wa watafiti kuhusika pia na uchimbaji na kulipwa kwa
kadiri na matokeo na hatua iliyofikiwa. Anafanya utafiti mwingine,
anachukua fedha zake anakwenda; anayekwenda kufanya uchunguzi ni
mwingine naye anachukua fedha zake anakwenda; anayejenga miundombinu ni
mwingine, naye anaelekezwa eneo na baadaye kueleza kwamba hakuna maji
huku hasara ikiwa imeshapatikana.
Ripoti ya Tathmini (Appraisal
Report) ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Rural Water
Supply and Sanitation Program) ya mwaka 2010 inaonyesha namna ambavyo
awamu ya kwanza katika ya mwaka 2007 mpaka 2010 ilivyoshindwa
kutekelezwa kwa ufanisi. Usimamizi wa kutosha wa kibunge unahitajika
kuhakikisha awamu ya pili (RSSWP Phase II), ambayo awali ilipangwa
ifanyike kuanzia mwaka 2011 mpaka 2014 inafanyika kwa kuanzia na kufanya
ukaguzi wa awamu iliyopita.
Bunge lako lijadili hali hii na
kupitisha maazimio yenye kuwezesha ukaguzi maalum ufanyike kwenye
matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini
katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zote nchini ili kasoro hizo
zisijirudie katika awamu ya pili ya programu hiyo inayotarajiwa kuanza
mwezi Juni mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika; Baada ya
maelezo hayo sasa naomba kuwasilisha hoja kwa mujibu wa kanuni ya 54
fasili ya (1) (2) na (3) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha
maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi
na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.
MABADILIKO
KATIKA HOJA KUHUSU HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI
SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM (Kwa mujibu wa Kanuni 55 (10) ya Kanuni za Kudumu za Bunge)
Kwa
kuondoa maneno kuanzia “KWA KUWA, kati ya mwaka 2003….. (yaliyo kuanzia
katika ukurasa wa 42 na kuendelea mpaka ukurasa wa 45 yanapoishia
maneno maneno)…….. mapendekezo ya mpango wa taifa”
Na kuingiza maneno: “
KWA KUWA,
Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini ikiwemo katika Manispaa za
Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na
kukamilika mwaka 2010/2011 kwa kugharimu dola za kimarekani milioni 292
hata hivyo tathmini ya miaka miwili na nusu ya utekelezaji (mid term
review) imebanisha kasoro nyingi katika utekelezaji.
KWA KUWA,
Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati
na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam
na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and
Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka
sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina
hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa
usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika
matumizi.
NA KWA KUWA, Wizara ya Maji iliandaa waraka
maalum wa kuiomba Serikali kutenga kiasi cha shilingi bilioni 653.85
Mpango Maalum 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondaji wa
majitaka katika Jiji la Dar es salaam na kupitishwa na Baraza la
Mawaziri mwezi Machi 2011 lakini utekelezaji wake unaelekea
kucheleweshwa mpaka mwaka 2016.
NA KWA KUWA, katika mwaka
wa fedha 2011/2012 na 2012/13 Serikali haikutenga kiwango kamili cha
fedha kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
ulioidhinishwa na Bunge na kwa kuzingatia mgawanyo wa Mpango Maalum wa
Maji Safi na Maji Taka katika Jiji la Dar Es Salaam na kauli ya Serikali
ya tarehe 7 Novemba 2012.
NA KWA KUWA, kwa mujibu wa
ibara ya 62 (2) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 , Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka, kwa niaba ya
wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika
utekelezaji wa majukumu.
NA KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara
ya 63(3) katika utekelezaji wa madaraka yake bunge laweza kujadili na
kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa
kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutunga sheria
pale utekelezaji unapohitaji kuwapo sheria.
NA KWA KUWA,
Malengo ya Kitaifa yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa Mjini maji kwa
asilimia 90 ifikapo mwaka 2010 na kwamba malengo hayo kwa Jiji la Dar es
Salaam yamesogezwa mbele na kuwekwa malengo mapya ya upatikanaji wa
huduma ya maji safi kufikia asilimia 90 na uondoaji wa maji taka kufikia
asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.
KWA HIYO BASI, Bunge
linaazimia kwamba Serikali ichukue hatua za haraka zaidi za kuboresha
upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la
Dar es salaam:
NA KWAMBA, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalum wa matumuzi ya fedha matumizi ya
bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la
Dar es salaam na Halmashauri zingine na kuwezesha hatua za ziada
kuchukuliwa.
NA KWAMBA, Kufuatia kauli iliyotolewa
bungeni tarehe 7 Novemba 2012 kuhusu Mpango Maalum wa kutatua tatizo la
maji katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 Serikali
izingatie makisio ya awali ya gharama za mpango huo na kuingiza
mahitaji yaliyobaki kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka
2013/2014 na Bajeti ya mwaka 2013/2014.
NA KWAMBA, Mpango
wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya
Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji
wa visima 29 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa
kukamilika kwa dharura katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka
hivi sasa ikiwemo iliyozinduliwa Oktoba 2012 yenye kuhitaji miundombinu
ya ziada kufikia wananchi zaidi.
NA KWAMBA, Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa thamani ukilinganisha na
ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa
miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya
Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation
Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit)
uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
NA KWAMBA,
EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya
visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na
kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali
lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali.
NA KWAMBA,
EWURA iharakishe kukamilisha mchakato ulioanza wa kutunga kanuni za
udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi
katika Jiji la Dar es salaam.
NA KWAMBA, Kamati husika ya
Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa
usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on
the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 ili
maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa kujadili na kushauri kuhusu
mapendekezo ya mpango wa taifa na bajeti ya nchi.
NA KWAMBA,
Serikali iwasilishe bungeni haraka iwezekanavyo muswada wa sheria ya
marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply
and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu
uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo
thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.”
Naomba kuwasilisha.
…………………
John John Mnyika(Mb)
Jimbo la Uchaguzi-Ubungo