Facebook Comments Box

Monday, September 30, 2013

NGASSA AOMBA WAPENZI NA WANACHAMA WA YANGA KUMCHANGIA ILI AWEZE KURUDISHA PESA ALIZO ILIPA SIMBA


Mshambuliaji nyota Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa ameonekana akifanya mazoezi mara mbili, baada ya kumaliza awamu ya pamoja na wenzake Yanga SC chini ya kocha wake, Mholanzi Ernie Brandts akaenda katika ufukwe wa Coco kufanya mazoezi binafasi. 

Ngassa ambae ameanza kucheza juzi katika mechi kati ya Yanga na timu ya Ruvu Shooting ya RUVU, Mkoani Pwani baada ya kutumikia kifungo cha michezo 6 pamoja na kuilipa timu ya Simba pesa zake shilingi milioni 45 baada ya kuamuriwa kufanya hivyo na TFF ikiwa ni adhabu baada ya kuingia mkataba na Simba huku akijua kuwa bado ana mkataba na timu ya Azam.

Mchanganuo wa pesa hizo ni kwamba shilingi 30 milioni ni fungu alilolipwa na Simba na shilingi milioni 15 ni fidia. Mchezaji huyo alilazimika kulipa pesa hizo kutoka katika akaunti yake mwenyewe ambazo alilipa siku ya Ijumaa na siku ya Jumamosi alicheza mchezo kati ya Ruvu na Yanga ambapo timu yake ilipata ushindi wa bao 1-0 huku yeye akitoa pasi ya goli hilo kwa mfungaji Hamis Kiiza 'Diego'.


Katika hali ya kushangaza Ngassa ameomba wanachama na wapenzi wa Yanga walioguswa na kitendo cha kulazimika kujilipia mwenyewe fedha za Simba SC, Sh. Milioni 45 kumchangia katika akaunti namba 01J2095037800 katika benki ya CRDB kwa jina la Mrisho Halfan Ngasa. “Naomba wanachama na wapenzi wa Yanga SC walioguswa kunichangia fedha katika akaunti hiyo ili tuwe tumesaidiana kulipa deni hilo,” alisema.
Ngassa akijifua peke yake Coco Beach




Ngassa alipoulizwa kuhusu kufanya mazoezi ya ziada, alisema ni kwa sababu pia anakabiliwa na kazi ya ziada kuisaidia timu yake katika Ligi Kuu, hivi sasa ikiwa inazidiwa na wapinzani wa jadi, Simba SC kwa pointi tano kileleni.  

Ngassa anadai Simba SC ilimwambia kuwa anasaini kucheza kwa mkopo kumalizia Mkataba wake wa Azam, lakini kumbe ni Mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo baada ya ule wa mkopo kumalizika.

“Nawashauri wachezaji wenzangu kwamba, wanapoingia mikataba na klabu, wahakikishe wanakuwa na mawakili, ili wawasaidie kujua kilichomo ndani yake na wasaini mikataba ambayo wanaielewa,”
Chanzo:http://tinyurl.com/k6td4pn


TAARIFA MPYA KUHUSU UJENZI WA UWANJA WA KISASA WA YANGA


[Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Francis Kifukwe (katikati) ambaye pia ni mwenyekiti wa mradi wa ujenzi wa uwanja eneo la jangwani akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu leo, kushoto ni mzee Jabir Katundu (mwenyekiti wa baraza la wazee) na kulia Lawrence Mwalusako katibu mkuu wa Yanga SC ]

LEO tungependa kupitia kwenu kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi wetu wa Uwanja wa kisasa wa mpira katika Jiji la Jangwani kama itakavyojulikana mara ya mwisho tuliongea na kuonana ilikuwa mwezi wa tatu wakati Ndugu zetu wa BCEG walipokabidhi Concept design ama Usanifu wa awali na kuanzia sasa tutakuwa tunatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mradi huu. 

Wahenga walisema UKICHA KUSEMA HUTATENDA JAMBO lakini pia KUKAA KIMYA SANA kunajenga hisia mbaya na kutoa nafasi ya upotoshwaji wa habari. 

Kwa kifupi napenda kuwakumbusha kuwa Makubalino ya Awali (Memorandum of Understanding) yalisainiwa 23 Novemba 2012. Pamoja na mengineyo YANGA inatakiwa:-
• Kupata na kuwa na eneo la kutosheleza malengo ya mradi
• Kupata ushauri mzuri, michoro mizuri na mkandarasi mzuri wa mradi
• Kupata na kutenga fedha za kukamilisha usanifu na ujenzi wa mradi
Kwa upande wa BCEG wajibu wao ni kuwa na utaalamu na uzoefu wa kutosha. BCEG wameandaa na kukabidhi michoro ya usanifu wa awali kukidhi matakwa ya YANGA. YANGA tunatakiwa kutoa maoni yetu na na kuingia RASMI mkataba wa ujenzi.
Kutokana na kukua kwa Jiji la Dar es Salaam, na katika hali ya kutaka klabu iwe na vitega uchumi klabu imeonelea ni vyema kama ingekuwa na uwanja wa mpira wa karne ya sasa na baadaye ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na mioundombinu ifuatayo:-
1. Uwanja wa mpira wenye viti 40,000
2. Hostel ya wachezaji na football academy ya vijana
3. Viwanja vya mazoezi
4. Uwanja wa kutosha kuegesha magari
5. Hoteli na sehemu ya makazi
6. Ukumbi wa mikutano
7. Sehemu ya maofisi, benki, zahanati (sports clinic)
8. Maduka, supermarket na sinema
9. Sehemu za kubarizi, kupumzikia (Recretional and Open spaces)

Mara baada ya azma yetu kukamilika eneo hili litaitwa “Jangwani City” na kufanya wakazi wa maeneo ya Jangwani na sehemu za jirani wasiende maeneo ya mbali kutafuta huduma muhimu za kijamii. Eneo hili litaboresha mandhari nzima ya Jangwani kwa kukuza mazingira na miundombinu. Hii itahusu pamoja na mambo mengine ujazaji udongo (tuta kubwa), upandaji miti, bustani za kubarizi, kuboresha mifereji ya majitaka na kudhibiti mafuriko ya eneo la Jangwani na hivyo kulipatia sura ya kibiashara na kitalii.
Ili kukamilisha azma ya kuwa na Jangwani City itakayo kuwa na miundombinu yote hiyo, Uongozi ulipeleka maombi ya eneo la nyongeza Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa barua zenye kumbukumbu namba YASC/ARDHI/MWK/YM/46/2012 na YASC/ARDHI/MWK/YM/47/2012 za 12 Desemba 2012, na mpaka sasa bado maombi yetu hayajajibiwa.
Mwezi wa saba, Wadhamini/Uongozi wa YANGA walimwandikia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuomba msaada wake kufanikisha maombi ya nyongeza ya kiwanja yaliyowasilishwa Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Klabu ya Yanga ina kiwanja chenye ukubwa wa hekta 3.59 eneo la Jangwani. Kiwanja hiki kina hati miliki kwa miaka 99 toka mwaka 1972 na katika eneo hilo, klabu ilifanikiwa kujenga uwanja wa mpira wa Kaunda na Jengo la klabu la ghorofa tatu. Jengo hili lilijengwa kwa ufadhili mkubwa sana wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) na michango ya wanachama na wapenzi wa klabu ambao kila siku wamekuwa wakiamini kuwa haba na haba hujaza kibaba.
Ndugu Wandishi wa habari kwa kifupi tumefikia hapo, zoezi la kutoa maoni yetu kuhusu michoro ya usanifu wa awali na kuingia rasmi mkataba wa ujenzi na BCEG limesimama, likisubiri majibu ya nyongeza la eneo.  Ni matumaini yetu zoezi hili litakamilika hivi karibuni na kuendelea na mradi.
YANGA DAIMA MBELE NYUMA MWIKO
Dar es Salaam, 30 September 2013
Francis Mponjoli Kifukwe


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU