KATIBU Mkuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad Slaa, amemvaa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye akisema madai aliyoyatoa dhidi yake ni ya kipuuzi na yasiyokuwa na tija kwa Watanzania waliopigika na umasikini.
KATIBU Mkuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad Slaa, amemvaa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye akisema madai aliyoyatoa dhidi yake ni ya kipuuzi na yasiyokuwa na tija kwa Watanzania waliopigika na umasikini.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Nape kudai kuwa katibu huyo ni CCM damu ndiyo maana hata kadi yao ameendelea kuwa nayo hadi leo licha ya kuhamia CHADEMA.
Akifungua mkutano wa NEC Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza juzi, Nape alidai kuwa Dk. Slaa tangu aikimbie CCM na kuhamia CHADEMA hajarudisha kadi yao.
Hata hivyo, Dk. Slaa licha ya kukiri kuwa na kadi hiyo ya CCM hadi leo, alifafanua kuwa hiyo ni mali yake halali na ameihifadhi kwenye makumbusho kwa ajili ya kumbukumbu kwa ajili ya wajukuu zake na vizazi vijazo.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Dk. Slaa alisema madai ya Nape ni hoja ya kipuuzi isiyokuwa na tija kwa wananchi na kwamba hazina mashiko, bali zimelenga kupoteza muda na wananchi.
"Kadi ni mali yangu, na nimeihifadhi kwenye makumbusho kwa ajili ya historia ya wajukuu. CCM wanaweweseka kutokana na kushindwa kwake kuisimamia Serikali yao ili kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema.
Dk. Slaa alitamba kuwa Nape na wenzake waachwe wapige mayowe, lakini mwaka 2015 ndiyo wataisoma namba. Kwamba huo utakuwa mwisho wa CCM maana CHADEMA wanaandaa mipango bora zaidi ya kuwasaidia Watanzania kimaendeleo.
“Na Tanzania itakuwa mfano mkubwa wa kimaendeleo katika utawala wa CHADEMA," alisema Dk. Slaa huku akisisitiza kwamba umasikini uliowagubika Watanzania mwisho wake ni 2015.
CCM wavurugana
Jijini Arusha vita ya makundi ya urais 2015 ndani ya CCM, imeanza kujitokeza upya baada ya kuibuka mvutano mkali kati ya Mwenyekiti wa Jumiuya ya Wanawake (UWT) mkoani hapa, Florah Zelote na mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige.
Licha ya Magige kutoka mkoa huo akipitia kundi la vijana, mwenyekiti wa UWT anadai kuwa mbunge huyo anajipitisha na kutoa misaada kwa lengo la kusaka ubunge kupitia jumuiya hiyo mwaka 2015.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili, zinasema kuwa Zalote alitoa madai hayo kwenye kikao cha baraza la UWT wilaya ya Arumeru Novemba 30, mwaka huu, ambapo anadaiwa kuwaeleza wajumbe kuwa Magige hana jipya kwani misaada anayotoa ni ya kutaka kujijenga ili apate ubunge kupitia jumuiya hiyo.
Kwamba Mwenyekiti huyo aliweka wazi kuwa UWT mkoani Arusha inawakilishwa bungeni mmoja tu, Namelok Sokoine ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Sokoine.
Habari za ndani zinadai kuwa Zalote, alitumia kikao hicho kuwahamasisha wanawake kutohudhuria hafla ya uzinduzi wa taasisi ya Magige, iliyokuwa ikifanyika siku hiyo akidai kuwa kuhudhuria ni ‘kumpa ujiko’ mbunge huyo wa kuwania ubunge wa UWT 2015.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Zelote alikiri kutohudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa na Magige kutokana na kuwa na majukumu mengine ya kiofisi.
Hata hivyo alikanusha madai ya kumzungumzia Magige kwenye kikao hicho ingawa alikiri kuwa alikuwa na mwaliko wa hafla ya uzinduzi wa taasisi yake maendeleo lakini alishindwa kuhudhuria.
Alisema kuwa alitoa udhuru kupitia katibu wake ambaye alijibu barua ya mwaliko iliyofika ofisini kwake kwa kuwaarifu kuwa hataweza kuhudhuria kwani atakuwa wilayani Arumeru.
“Ninajua utawala bora na ninauheshimu sana, sijamtaja Magige popote, hata wakati wa kikao changu, nilimuongelea mwakilishi wetu wa UWT bungeni, Namelok Sokoine yeye ndiye nilimsemea kwa wajumbe kuwa kwa sasa hawamuoni kwani yuko nje ya nchi anamuuguza mama yake, lakini akirudi tutapita naye kwenye maeneo yao,” alisema.
Aliongeza kuwa ni vema Magige kama ana malalamiko afuate taratibu za chama badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari.
Naye Magige aliliambia gazeti hili kuwa ameamua kuzindua taasisi hiyo kwa ajili ya kusaidia jamii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.
Alisema kuwa akiwa ni mbunge anayetokana na CCM ana wajibu wa kutekeleza Ilani ya chama hicho jambo alilodai kuwa anaamini hata mwenyekiti huyo wa UWT anatakiwa kulifanya.
Kuhusu kugombea ubunge kupitia UWT mwaka 2015, Magige alisema hiyo ni haki yake kikatiba na akitaka hakuna wa kumzuia.