Rais
 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema 
hatagombea tena wadhifa huo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika 
Februari 24 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF leo, Rais 
Tenga amesema wakati anaingia kwenye uongozi mwaka 2004 ajenda ilikuwa 
na kuijenga TFF kama taasisi kwa kuweka mifumo ya uendeshaji ikiwemo 
kutengeneza katiba na kanuni, jambo ambalo limefanyika.
“Wajumbe wamekuwa wakiniuliza Rais vipi? Mimi hapana. Nilishafika 
pale pa kufika. Tulipoanza wakati ule ilikuwa ni kujenga taasisi. Na 
kazi hiyo tumeifanya. Tulipoingia mwaka 2004 hiyo ndiyo ilikuwa ajenda,”
 amesema Rais Tenga.
Amesema walitengeneza Katiba, vyombo huru vya kufanya uamuzi, 
kuongeza wigo wa wapiga kura ambapo hivi sasa kwenye mpira wa miguu 
hakuwezi kutokea migogoro, hata ikitokea kuna mfumo wa kuidhibiti.
Rais Tenga ameishukuru Sekretarieti ya TFF, Kamati ya Uchaguzi ya 
TFF, kamati za uchaguzi za wanachama wa TFF na vyama wanachama wa TFF 
kwa hatua iliyofikiwa katika uchaguzi ambapo mikoa yote imekamilisha 
uchaguzi na kubaki vyama shiriki pekee.
Ametoa mwito kwa wadau kujitokeza kugombea uongozi TFF, kwani baada 
ya kujenga taasisi ajenda iliyobaki ni mpira wa miguu wenyewe ikiwemo 
nini kifanyika ili mpira uchezwe katika maeneo mbalimbali.
“Tumeshatengeza mfumo, sasa ni kuangalia jinsi ya kuendeleza mpira. 
Changamoto ni tufanye nini ili mpira uendelee. Tunataka watu wengine 
wabebe hiyo ajenda ili tuangalie tunakwendaje mbele,” amesema.
Pia amesema ushirikiano ambao amepata kwa wapenzi na wadau wa mpira 
wa miguu ni wa ajabu. Vilevile ameishukuru vyombo vya habari, Serikali, 
klabu, wadhamini na wafadhili kwa mchango wao katika uendeshaji wa mpira
 wa miguu nchini.