Facebook Comments Box

Friday, January 11, 2013

LISSU: HAKUNA SABABU YA BAADHI YA WATU KUWA JUU YA SHERIA

Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu akiwaeleza waandishi wa habari kuwa Chama chake kimependekeza kuwepo kwa utawala wa majimbo utakaorahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi Picha na Salhim Shao 
Kwa ufupi
“Pia kinga ya Rais inatakiwa kuondolewa ili kuleta nidhamu ya utendaji katika ofisi hii ya umma. Akifanya makosa ya jinai ashtakiwe kama mhalifu mwingine, hakuna sababu ya baadhi ya watu kuwa juu ya sheria, kila mtu awe chini ya sheria,”


MCHAKATO wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi yatakayosaidia katika uundwaji wa Katiba Mpya unaendelea na safari hii ni zamu ya makundi maalumu vikiwemo vyama vya siasa ambavyo vimeanza kutoa maoni yao mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mikutano hiyo kati ya Tume na wawakilishi wa vyama vya siasa inafanyika katika Ofisi Kuu za Tume pamoja na Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Vyama vyote vimepewa fursa ya  kushiriki katika utoaji maoni na baadhi ya mambo ambayo wameyapendekeza kuwamo katika Katiba Mpya ni pamoja na utawala wa majimbo na kuwapo kwa mgombea binafsi.
Kimsingi hoja hizi zimekuwa zikitolewa maoni mara nyingi na wananchi katika mikutano mbalimbali ya Tume iliyokuwa ikifanyika nchi nzima kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, tofauti na sasa ni kwamba wanasiasa wamezieleza kwa undani zaidi na kuzifafanua namna gani zinavyoweza kuingia katika Katiba ijayo.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimejikita zaidi katika muundo wa Muungano na utawala wa majimbo, wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejielekeza kwenye hoja ya mgombea binafsi.
Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu anasema kuwa chama chake kinataka kuona Katiba Mpya inakuja na mfumo mpya ambao utaleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali zikiwamo utawala, rasilimali, ulinzi wa mali za umma, haki za binadamu, uwajibikaji serikalini na muundo wa Jamhuri ya Muungano ambao utasaidia kuunusuru usivunjike.
Lissu anasema kuwa kuna kila sababu ya Katiba Mpya kuleta mabadiliko katika muundo wa Muungano ambao Chadema wanapendekeza uwe Muungano wa Shirikisho wa Serikali tatu, yaani Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ndogo ya Jamhuri ya Muungano.
“Hatuwezi kuendelea na mfumo uliopo wa Muungano kwani una upungufu mwingi. Ni fursa nzuri ambayo tumeipata ya kutengeneza Katiba Mpya ya nchi ambayo kimsingi inapaswa kuleta mabadiliko yatakayounusuru au kuuokoa Muungano usivunjike. Tukikosea tunaweza kujikuta tunatengana kama ilivyo kwa Ethiopia na Eritrea, Sudan na Sudan Kusini, Yugoslavia na Czechoslovakia,” anasema Lissu.
Pia anasema kwa kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa hiari kunatakiwa kuwe na haki ya kujitoa kwa upande usioridhika kuendelea kuwa kwenye Muungano.
Anasema utaratibu wa kujitoa uwe kwa njia ya kura ya maoni itakayopigwa na wananchi wa upande mmojawapo wa Muungano na ikiwa theluthi mbili ya wananchi wakikubali kujitoa basi iruhusiwe wajitoe kwa sababu Muungano huu haukuwa wa lazima.
Lissu anaongeza kuwa kwenye mambo ya Muungano wamependekeza yawemo mambo saba tu ambayo ni ulinzi na usalama, wizara zisizozidi 18, Bunge lisilozidi wawakilishi 300, mamlaka ya uteuzi ya Rais ambayo yanapaswa kupunguzwa, Rais ashtakiwe akifanya makosa ya jinai, pamoja na kuweka bayana suala la umilikaji wa rasilimali za nchi.
Kuhusu mamlaka ya uteuzi ya Rais anaeleza kuwa ni lazima yapunguzwe ili kuiondoa nchi kwenye mfumo wa urais wa kifalme.


POLISI WAKAMATWA WAKISAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA



Picha hii na Maktaba.

ASKARI polisi wawili wa wilayani Bunda, mkoani Mara, wanashikiliwa na jeshi la polisi katika mkoa wa Simiyu, kwa tuhuma ya kusafirisha madawa ya kulevya aina ya mirungi.

Kamanda wa polisi mkoani Simiyu Salum Msangi, amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 7:30 mchana, katika kizuizi cha polisi kilichoko katika eneo la wilaya ya Busega, karibu na mji mdogo wa Lamadi, kwenye barabara kuu ya Mwanza-Musoma.

Kamanda Msangi amewataja asakari polisi hao kuwa ni pamoja na mwenye namba E. 4640 koplo Daniel na E. 6224 Koplo Mwinyihaji, na kwamba walikamatwa wakiwa na mirungi yenye uzito wa kilo 72 iliyokuwa imewekwa kwenye mabegi mawili.

Alisema kuwa askari hao walikuwa na gari binafsi yenye namba T. 168 DWB, aina ya Noah, ambapo pia walikuwa na wanawake wawili, Achien Aoko (30) na Penina Samson (20), ambao wote ni wakazi wa wilayani Tarime.

Aidha, alisema kuwa baada ya askari hao ambao walikuwa wamevaa kiraia kufika katika kizuizi hicho, gari yao ilipekuliwa na askari, na ndipo ikagundulika kwamba kulikuwa na mabegi mawili ya mirungi.

Kamanda Msangi alisema kuwa askari hao tayari wanaendelea na mashitaka ya kijeshi, ambapo wanawake waliokuwa nao jana wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bariadi ambayo kwa sasa inafanya kazi kama mahakama ya mkoa wa Simiyu.




KESI YA DK. ULIMBOKA: MTUHUMIWA J. MULUNDI AMTAKA BALOZI WA KENYA KORTINI




Dk. Stephen Ulimboka baada ya kipigo kikali kutoka kwa J. Mulundi


Raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21) anayekabiliwa na mashitaka ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka, ameiomba Mahakama kumleta Balozi wa nchi yake mahakamani.

Mulundi alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu Agnes Mchome wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya upande wa mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi yake bado haujakamilika. Alihoji kwa nini upelelezi wa kesi hiyo unachelewa kukamilika na kwa nini upande wa mashitaka hawaleti mashahidi mahakamani ili kesi hiyo iishe?

Hakimu Mchome alisema jambo hilo liko nje ya uwezo wa Mahakama hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.

Mulundi aliiomba Mahakama kushinikiza Balozi wa Kenya aende mahakamani, huku akidai ameshaanza mgomo mahabusu na ataendelea nao. Hakimu Mchome alisema Mahakama hiyo haina uwezo wa kumshinikiza balozi wa nchi yake kufika mahakamani, lakini anaweza kufuata utaratibu kwa yeye kumuandikia Balozi wake barua.

Hata hivyo Mulundi hakuridhika na majibu hayo na kuomba apelekwe kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta ili akawasilishe malalamiko. Alitolewa katika chumba cha Hakimu Mchome na kupelekwa ofisini kwa Hakimu Mugeta ambako alidai upelelezi wa kesi yake unacheleweshwa.

Hata hivyo Hakimu Mugeta alisema Mahakama haina uwezo wa kuharakisha Polisi kukamilisha upelelezi kwa sababu kesi hiyo iko chini ya Polisi.

Hakimu Mchome ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 23 mwaka huu itakapotajwa tena. Upande wa mashitaka uliwasilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka.

Alipotoka mahakamani, Mulundi alikuwa anachechemea hasa mguu wa kushoto kitu ambacho kilisababisha ashuke kwa taabu katika ngazi za Mahakama. Pia alionesha sura ya huzuni, lakini Ofisa Magereza waliokuwa naye walishangaa na kudai alitoka mahabusu akitembea vizuri.

Inadaiwa kuwa, Juni 26 mwaka jana, katika eneo la Leaders Club, Mulundi alimteka Dk Ulimboka. Katika shitaka la pili anadaiwa Juni 26 mwaka jana, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha sheria inadaiwa alijaribu kumsababishia kifo Dk Ulimboka. Kwa mara ya kwanza mshitakiwa huyo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Julai 13 mwaka jana.







 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU