Baada ya kufuatilia kwa undani, na kwa upana kuhusu swala la gesi ambalo linaendelea kuwa ni mgongano au, ni mgogoro kati ya Serikali na wananchi wa Mkoa wa Mtwara/Lindi kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwenda kinyerezi Dar- es–Salaam, tumebaini yafuatayo:-
1. Hakuna Sera ya gesi ambayo husababisha kupatikana Sheria baada ya kupelekwa Bungeni na kuidhinishwa bali kilichopo ni rasimu ya sera ambayo haina ushirikishwaji wa mawazo ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi, ambako vyanzo vya gesi hiyo ipo.
2. Elimu kuhusu gesi na manufaa yake kwa wananchi haikutolewa ili kujua haki zao kwa madhara yatokanayo na (Uvunaji) uzalishaji wa gesi hiyo, na jinsi watakavyonufaika.
Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 inatamka wazi katika Ibara ya 63 kifungu cha H na K juu ya gesi ya Mnazibay Mtwara na Songo songo Kilwa, Lindi kuhusu umeme wa (240 MW) Kinyerezi na (300MW) Umeme wa Mnazi bay Mtwara.
-Vifungu hivi vinafafanua:
• Gesi ya Mnazi bay itakuwa kwa ajili ya Mitambo ya kuzalisha umeme ambayo itajengwa Mtwara (300MW)
• Mitambo ya kuchakata gesi kujengwa Mtwara
• Ujenzi wa viwanda Mtwara ili malighafi itokanayo na gesi itumike kutengeneza mbolea, plastic vikiwemo na viwanda vya Cementi
3. Gesi ya Songo songo inafafanua wazi kuwa gesi hiyo itapelekwa Kinyerezi . Dar –es –Salaam kwa madhumuni hayo hayo.
• Kuendeleza viwanda mbali mbali
• Kuzalisha umeme (240 MW)
• Kuchakata gesi kwa kujenga mitambo
Katika ahadi ya Rais wa Jahuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa wakati wa Kampeni za uchaguzi katika hotuba yake ya tarehe 29/10/2010 alitamka wazi kuwa Mkoa wa Mtwara uwe tayari kwa maendeleo makubwa ambayo yanakuja kutokana na gesi iliyogunduliwa katika Mkoa wa Mtwara huko Mnazi bay
Alimainisha/aliainisha juu ya viwanda mbalimbali vitakavyojengwa hapa mkoani vya mbolea,cement, plastic n.k na kuwataka wananchi wajiandae kupokea maendeleo hayo kwa kujenga nyumba nzuri zenye sifa kwa ajili ya wageni. Pia wawasomeshe watoto wao ili wawe na elimu ya juu na kupata ajira katika Makampuni yanayokuja.
Hata baada ya uchaguzi Rais wetu alipokuja kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kumchagua, alitamka tena katika hotuba yake akisisitiza ahadi yake ya kujenga viwanda ambavyo vitaleta maendeleo kwa Mikoa ya Kusini na kusababisha ajira kwa wana kusini, na kuagiza kwa Meya wa Manispaa Mtwara/Mikindani kuwapa maeneo ya kujenga viwanda hivyo, kwa kile kilichoonekana kukosa maeneo ya ujenzi huo kwa makampuni hayo. Ahadi hizi alizozitoa kwa wananchi kwa ujumla wao wamezipokea na kuendelea kuzifanyia kazi.
Chanzo cha Matatizo:
Mara baada ya kuonekana kile walichokitarajia wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kutumia gesi ya Mnazi bay kuleta maendeleo yao kuwa imeamriwa kusafirishwa kwa bomba na kupelekwa Kinyerezi Dar –Es –Salaam ili kuzalisha umeme na kuchakata gesi na mitambo hiyo iwe huko.(Mgeuko wa Ilani ya Uchaguzi, na kutozingatia ahadi zake mwenyewe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa kinyume na kauli za usemi wake mwenyewe kwa kukitangaza kituo cha Kinyerezi kuwa ni sehemu ya mitambo ya gesi ya Mnazi bay-Mtwara na Songosongo-Lindi na kwamba bomba hilo litachukua miezi (18) mpaka kukamilika kwake, kwa matamshi haya ndiyo yaliyoleta hasira na chuki kwa wananchi wa Mtwara/Lindi kwa ujumla.
Hali hii imewafanya wananchi wa Kusini kutokuwa na Imani na Serikali na viongozi wake wahusika na sakata hili la gesi kwa semi mbalimbali za viongozi hawa
-Mfano.
(1) Kwa hali yoyote gesi lazima itoke Mtwara (Kwa gharama yoyote ile) kwa kukubali ama kutokubali itakwenda Kinyerezi kwa bomba
(2) Kuitwa wahaini wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kuandamana
(3) Kuitwa wajinga, hawakusoma na kuwa watu wa vijiweni wasio na elimu ya gesi
(4) Nitafanya lolote hata kama nitalaumika na Mataifa mengine lakini wapo watakaochekea yatakayotokea na kauli zinazobadilika kila kunapokucha.
(5) Usemi wa kuigawa nchi vipande vipande
Viongozi hawa hawajui kuwa chanzo kipo kwao wenyewe, kwa kutozingatia kuwa wananchi hao ambao hawana elimu kama yao wanao upeo mkubwa wa kufikiri na kutoa maamuzi kama wanavyotoa wao….
Mfano.
(1) Gesi haitoki Mtwara
(2) Tupo tayari kufa wote kwa ajili ya gesi
(3) Haiwezekan mitambo ya aina zote
-Kufua umeme
-Kuchakata gesi
-Kunufaisha viwanda vya Dar-es-Salaam kwa gesi yetu
-Mikataba ya gesi ya Mnazibay kufutwa ili kuanzisha mikataba iliyo na manufaa kwa Mkoa wa Mtwara na wananchi wake.
(4) Kwa nini bomba la gesi kujengwa kwa muda wa miezi 18 na bara bara kwa miaka 51 ya uhuru haimalizwi kujengwa. Je kwenye gesi kuna nini nyuma yake.?
Hiki ni kiini cha matatizo yote kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara kuandamana na mikutano mbalimbali ya kuhamasisha kutokubali gesi kuondoka Mtwara
Nukuu za Wananchi wa Mkoa wa Mtwara/Lindi
1-Kung’olewa kwa Reli
2-Kung’olewa kwa mashine za maji Newala na kupelekwa Dodoma.
3-Kung’olewa kwa taa za kuongoza ndege uwanja wa Mtwara na kupelekwa Uwanja wa KIA Moshi
4-Kuondolewa kwa Mtwara Korido
5-Kuwekezwa kwa bandari ya Mtwara kwa muda usiojulikana inaonyesha jinsi Serikali na viongozi wake wanavyohujumu Mikoa ya Kusini na wananchi wake kwa ujumla.
-Wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi wamefikia ukomo sasa wa kutengwa kimaendeleo, kimazingira na kutendewa uonevu wa makusudi na kilio chao cha mwisho ni hiyo gesi ambayo kauli mbiu yao ni GESI HAITOKI MTWARA KWA BOMBA KWENDA KINYEREZI DAR-ES-SALAAM
.
-Wananchi wote wameungana juu ya kuitetea gesi kutoka Mtwara, badala yake Serikali ifuate mikataba ya kwanza inayohusu gesi ya Mtwara pamoja na Ilani ya uchaguzi ya CCM ifuatwe na Rais atekeleze ahadi zote alizotoa hapo kwanza na afute kauli yake ya kupeleka gesi Kinyerezi, na wala Serikali isitumie nguvu katika swala zima la gesi ya Mnazibay Mtwara.
TAMKO LA UMOJA WA MAKANISA YA KIPENTEKOSTE –P.C.T MKOA WA MTWARA
P.C.T
kwa kuzingatia mwono uliopo wa hali tete yenye mwelekeo wa kumwagika damu na kuigawa nchi vipande vipande na kuondokewa amani, yafuatayo yafanyike
• Serikali isitishe mpango wake wa kuondoa gesi kutoka Mnazi bay Mtwara kwa kuisafirisha kwenda Kinyerezi Dar –es Salaam kwa bomba.
• Mitambo ya kuchakata gesi ijengwe Mtwara ili gesi isafirishwe kama mazao ya gesi na mabaki yake kutumiwa katika viwanda vya mbolea na plastic.
• Mitambo ya kuzalisha umeme ijengwe Mtwara na kusafirisha umeme na kuunganisha gridi ya Taifa.
• Viwanda vilivyoahidiwa vya mbolea,plastic,cemet n.k vianze kujengwa sasa na isiwe propaganda tu ya kisiasa toka kwa viongozi kwa kuondoa dhana iliyotokea huko nyuma ya kuonekana Kusini ni ukanda wa vita usiendelezwe.
Mfano kule Kilwa Lindi ambako ahadi ya kujenga kiwanda cha mbolea kwa gesi ya Songo songo mpaka leo hakijajengwa kwa kuwapatia nafasi ya ajira na kujiajiri kutokana na viwanda hivyo
• Serikali iwe sikivu kwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi ambako vyanzo vya uchumi wa gesi vipo kwa kutekeleza madai yao, kwa kuwa hawapingi kupelekwa umeme gridi ya Taifa na kuuza gesi iliyochakatwa tayari kwa kuliingizia Taifa mapato.
• Serikali ikamilishe sera za gesi na mafuta na kupatikana sheria ambayo italinda mikataba yote inayofanywa na serikali juu ya gesi na kulinda wananchi wa eneo husika mikoa ya Mtwara na Lindi kwa madhara yanayotokana na gesi kwa kuwashirikisha kutoa mawazo yao.
• Mazungumzo yafanyike kati ya Serikali na wananchi katika kupata ufumbuzi wa swala la gesi kwa njia ya Amani na wala isitumie nguvu zilizonazo kwani kufanya hivyo ni kuleta maafa yasiyo ya lazima kwa Taifa.
• -Serikali isisikilize wabunge wadanganyifu ambao hawana makubaliano na wananchi katika majimbo yao wanayotoka, ambao huchochea mgogoro huu kwa lengo lao binafsi.
• Viongozi ambao wametoa matusi kwa wananchi wafute usemi wao kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara ambao wamewaita wahaini kwa kuwaomba radhi bila masharti yeyote kwani semi hizo huleta chuki, uhasama, na matengano katika nchi, na kusababisha nchi isitawalike.
• Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2010 Ibara 63 Kifungu H na K ambavyo vipo wazi, hasa kwa kuzingatia kuwa sera zinazotekelezwa sasa na Serikali ni zile zote zilizoandikwa kwenye Ilani ya uchaguzi.
• Serikali irudishe tumaini kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na amani inayoonekana kutoweka kwa matamshi yanayoashiria kumwagika kwa damu bila kujali kuwa nchi ilipatikana bila kuwaga damu.
• Serikali iwatambue wananchi wa Mikoa ya Kusini kuwa wana haki ya kutimiziwa matakwa yao kama wananchi wa mikoa mingine kwa kupata maendeleo kutokana na vyanzo vya uchumi vilivyopo katika maeneo yao.
-Sisi viongozi wa dini tunamwomba Mungu awape hekima viongozi wetu wa Serikali kwa sababu wamepewa dhamana na Mungu kuliongoza Taifa.
-Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza, bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza Methali 11:3
-Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake, bali wenye haki watapona kwa maarifa. Methali 11:9
Imesainiwa na
BISHOP C. CHILUMBA
MWENYEKITI MKOA
PAMOJA
NA:-
PASTOR SELEKWA
KATIBU PCT- MKOA WA MTWARA
Nakala:
• Mwenyekiti PCT Taifa-Dar –es –Salaam
• Maaskofu na Wachungaji wote wa PCT Mkoa wa Mtwara.