Habari za mwaka mpya wote natumaini mmekesha salama na nitoe pole kwa wale ambao mkesha huu umekuwa mbaya kwa kuwaletea majeruhi na nitoe pole kwa familia ambazo zimepoteza baadhi ya watu wa familia zao kutokana na mkesha huo wa mwaka mpya.
Nianze kwa kusema nafurahi kwa kuwajua wasanii baadhi tokea wakiwa na umri mdogo kama wangu kama George Alex maarufu kwa jina la Squeezer akiwa anasoma Highland high School pale Iringa, Mike Mwakatundu maarufu kama Mike T tukiwa tunasoma wote pale Lugalo sekondary School Iringa hapo nikapata nafasi ya kumuona Ambwene Yesaya maarufu kama AY hapo akiwa mwanafunzi wa Ifunda Tech School kwa mara ya kwanza katika mashindano ya Don Bosco baada ya hapo Disco pale ruaha, R.O.M.A Mkatoliki pale Old Moshi High School nikiwa nimemtangulia.
Nirudi katika mada moja kwa moja kwa jina na heshima waliojijengea ndani na nje ya Tanzania naweza kusema hawaishi maisha ambayo wanapaswa kuishi. Rais Jakaya Kikwete Jana amezindua majibu ya sensa na kusema watanzania tupo milioni 44 sitaki kuamini na siwezi kuamini kuwa mtu kama R.O.M.A hana washabiki milioni 4 ambao wanaweza kununua Albam yake au wimbo wake huu ambao anauza elfu 3. Kwa hii elfu 3 akipata watu milioni 4 hapa nazungumzia 12,000,000,000 kijana wa kitanzania anakuwa katoka na anawaajiri watanzania wengine wengi katika matamasha "show" zake.
Leo hii baada ya kutoa wimbo wake wa 2030 ambao kila mtu kaupenda watanzania wengi tulikuwa tukisubiri zile tovuti zetu ziandike DOWNLOAD FREE WIMBO WA R.O.M.A MKATOLIKI 2030 HAPA halafu tuuchukue na kujiburudisha kwa bure na ikifika siku ambayo kuna matamasha tukaingie kwa elfu 7 ambayo sidhani kama katika hiyo elfu 7 anapata hata elfu kwa kila kichwa. Watanzania tumekuwa washabiki wanafiki. Tuna shusha kwenye tovuti nyimbo za wasanii badala ya kununua na kuwaacha wasanii masikini tukisubiri waumwe ili tuwachangie.
Hongera sana R.O.M.A kwa hatua ya kishujaa ya kuamua kujikwamua na mimi napenda niite hatua ya Kininja. Hilo ni jasho lako naomba ulisimamie ipasavyo. Shime watanzania tuwaunge mkono wasanii wetu ili wapate matokeo ya jasho lao.